Friday 26 February 2016

Baina Sahrawi, Timor ya Mashariki na Zanzibar pana njia nyembamba

Umoja wa Mataifa nao una wajibu wake kwa Zanzibar, ambayo ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mwanachama wa Umoja huo. Ndio maana, kupitia shirika lake la maendeleo (UNDP), umekuwa mdau mkubwa wa uchaguzi visiwani Zanzibar kwa kipindi kirefu sasa, ukiwemo uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba 2015. Hivyo unaujuwa kwa kina mgogoro ambao umezushwa na uhuni wa Jecha Salim Jecha, lakini huenda Umoja huo haukuwa na macho ya kuuangalia mgogoro huu katika uhalisia wake – yaani mahusiano kati ya Tanganyika na Zanzibar. Bali pale viongozi wa taasisi zinazoitwa za Muungano wanapobariki uhuni huo, jicho la mwenye akili linapaswa haraka sana kuuona moja kwa moja mkono wa mkaliaji dhidi ya mkaliwaji. Na ni jicho hilo ambalo sasa jumuiya ya kimataifa inapaswa kuwa nalo.
Mwaka 2005 nilialikwa na Shirika la Utamaduni na Sayansi la Umoja wa Mataifa (UNESCO) kuwa sehemu ya timu ya vijana wanaokaribia 20 kutoka maeneo yanayofanana duniani kote, kushiriki semina juu ya “Vijana na Ujenzi wa Amani Ulimwenguni” iliyofanyika kwenye mji mkuu wa mkoa wa Comarca, katikati ya jimbo la Catalonia, Uhispania. Miongoni mwa vijana wenzangu walikuwa ni kutoka Macau, Palestina, Timor ya Mashariki, Sahrawi (Sahara ya Magharibi) na Lebanon. Mji wenyewe wa Manresa ni mkongwe kama ulivyo Mji Mkongwe wa Zanzibar na yote miwili ni sehemu ya Turathi za Kimataifa zilizo chini ya UNESCO.

Ilinichukuwa muda mrefu kidogo kuja kuzingatia kuwa pana huo mfanano nilioutaja baina yetu washiriki wa semina hiyo, maana hatukuwahi kuambiwa na mwezeshaji yeyote yule ndani ya wiki mbili za kuwapo hapo. Kwenye makala hii, nitauzungumzia mshabaha huu kwa kuziangalia namna Timor ya Mashariki na Sahrawi zinafavyonana na Zanzibar kwa muktadha wa kinachoendelea sasa kwenye siasa za visiwa vyetu ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, baada ya uamuzi wa kihuni wa Jecha Salim Jecha kuufuta uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba 2015 na kisha kuutangaza mwengine wa tarehe 20 Machi 2016.
Ingawa kuna wengi ambao wanataka kuuona na kuuonesha mgogoro uliozuka baada ya uhuni huo kuwa ni baina ya demokrasia na udikteta tu visiwani Zanzibar lakini, kama alivyonukuliwa aliyekuwa waziri wa mambo ya nje wa Tanzania, Benard Membe, “kuna swali kubwa zaidi ya kurejea na kutorejea uchaguzi”. Kwa hakika, uhuni huu umeiibua hadharani ile picha pana ya mgogoro baina ya Tanganyika, kwa upande mmoja, na Zanzibar, kwa upande mwengine, kuliko ilivyo baina ya CCM na CUF. Hili tunaweza kulifahamu kwa kuangalia muktadha unaofanana na kadhia yetu, na hapa naziona Timor ya Mashariki na Sahrawi zina mengi ya kutufunza.
Timor ya Mashariki ya leo siyo ilivyokuwa miaka 15 iliyopita. Leo ni taifa, dola na nchi kamili inayojitawala wenyewe, lakini ina historia yake kufika hapo na kwa muktadha wa makala hii, turejee tarehe 28 Novemba 1975 ilipojitangazia uhuru kwa mara ya kwanza kutoka Ureno, chini ya chama cha wanamapinduzi kiitwacho FRETILIN. Siku tisa tu baadaye, ikavamiwa na kukaliwa na taifa la jirani, Indonesia, na kuitangaza kuwa jimbo lake la 27 kwa jina la Timor Timur.
Wakati Indonesia inapeleka wanajeshi wake kuivamia na kuikalia nchi hiyo, ilidai ilikuwa imeombwa kufanya hivyo na viongozi wa Timor ya Mashariki, madai ambayo kamwe hayakuwa ya kweli wala hayakutambuliwa na Umoja wa Mataifa. Hata hivyo, kuanzia hapo, Timor ya Mashariki ikawa chini ya ukoloni mpya wa jirani yake uliodumu kwa robo karne, huku Watimori wakipambana kijeshi na kisiasa, maelfu yao wakiuawa, kuteswa na kupotea, hadi pale Umoja wa Mataifa ulipoingilia kati rasmi na kuitisha kura ya maoni mwaka 1999 iliyopelekea kukoma kwa udhibiti wa Indonesia dhidi yake na tamko rasmi la uhuru kamili la tarehe 20 Mei 2002.
Sahrawi nayo, au Sahara ya Magharibi, ilivamiwa na majirani zake wawili kupitia kile kinachoitwa Mkataba wa Madrid wa tarehe 14 Novemba 1975, ambapo mkoloni Uhispania alikubaliana na majirani Morocco na Mauritania kujiingiza punde yeye anapoondoka. Ingawa mkataba huo haukutambuliwa na Umoja wa Mataifa na hivyo Uhispania ikaendelea kutambulika kama “mlezi halali” wa watu wa Sahrawi, lakini ndio njia iliyotumiwa na Morocco kuendelea kuikalia ardhi ya Sahara ya Magharibi hadi hivi leo.
Kama walivyofanya Watimori, nao Wasahrawi waliupinga uvamizi huo dhidi ya nchi yao na chini ya cha chama chao cha ukombozi, Polisario, walijitangazia uhuru tarehe 27 Februari 1976, wakiiita nchi yao Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kiarabu ya Sahrawi. Umoja wa Afrika unaitambua jamhuri hii na ina kiti chake kwenye makao makuu ya Umoja huo, Addis Ababa, lakini ukweli ni kuwa serikali yake iliyo uhamishoni inatawala robo moja tu ya eneo ambalo inalichukulia kuwa ardhi ya Sahrawi yenyewe na sehemu iliyobakia ikiendelea kukaliwa na Morocco.
Umoja wa Mataifa hauitambuwi rasmi serikali hiyo, lakini kufikia mwaka huu wa 2016, imeshatambuliwa na mataifa 85, nayo ikiwa na balozi zake kwenye mataifa 18 duniani.
Kadhia za Timor ya Mashariki na Sahrawi hazina tafauti sana na ya visiwa vya Zanzibar, ambavyo vilikuwa chini ya Himaya ya Uingereza tangu mwaka 1890 hadi Disemba 1963. Mwezi mmoja baada ya Uingereza kuondoa mkono wake, yalifanyika mapinduzi ya tarehe 12 Januari 1964 na siku 100 baadaye ukaundwa Muungano na jirani yake, Tanganyika.
Jinsi mapinduzi yenyewe yalivyofanyika na kufuatiwa na kitendo cha kuungana tarehe 26 Aprili 1964, muna uhusiano mkubwa wa kile ambacho Indonesia ilikuja kukifanya dhidi ya Timor ya Mashariki na Morocco dhidi ya Sahrawi muongo mmoja baadaye.
Morocco na Mauritania zilitumia kisingizio cha Mkataba wa Madrid kati yao na mkoloni, Uhispania, kuingia na kuikalia ardhi ya Sahrawi, Indonesia ikatumia kisingizio cha ‘kualikwa’ na viongozi wa Timor ya Mashariki kuivamia na kuikalia nchi hiyo, ilhali  Tanganyika ilitumia kisingizio cha, kwanza, maombi ya baadhi ya viongozi wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Afro Shirazi (YASU) kuingia Zanzibar kufanya Mapinduzi ya Januari 1964 na, kisha, cha Mkataba wa Muungano wa Aprili 1964 kuikalia Zanzibar kwa zaidi ya nusu karne sasa.
Tangu Morocco iitwaye Sahrawi mara baada ya mkoloni wa Kizungu (Uhispania) kutangaza kuondoka, inaiita sehemu hiyo Jimbo la Kusini la Morocco, Indonesia iliita Timor ya Mashariki kuwa ni mkoa wake wa Timor Timur na Tanganyika inaiita Zanzibar kuwa ni Tanzania Zanzibar. Kuna wengi sana tunaokhofia – tena tukiwa na ushahidi kabisa – kuwa safari ya Zanzibar kuwa mmoja wa mikoa ya Tanganyika imekuwa ndilo lengo la muda mrefu la CCM.
Lakini lazima kitu kimoja kisemwe kwa uwazi kabisa katika kuutafautisha, kwa mfano, ukaliaji wa Indonesia dhidi ya Timor ya Mashariki na huu wetu wa Tanganyika dhidi ya Zanzibar. Kitabu cha Kwaheri Ukoloni Kwaheri Uhuru cha Dk. Harith Ghassany na kile cha Pan-Africanism or Pragmatism. Lessons of the Tanganyika-Zanzibar Union kilichoandikwa na Prof. Issa Shivji vinaelezea kwa undani namna dhana za Mapinduzi na Muungano zilivyofanikiwa kuificha hatua ya Tanganyika visiwani Zanzibar kwenye guo la “dhamira njema”.
Dhana hizo zimetumiwa kuuendeleza na “kuulainisha” ukaliwaji wetu kwa njia tafauti. Kwa mfano, jina la asili la mkaliaji limebadilishwa kutoka Tanganyika na kuwa Tanzania Bara ili kulijengea uwiano na lile la Tanzania Zanzibar analolitumia kumuita mkaliwaji wake. Kuna hata hekaya ya uongo na kweli kuwa jina lenyewe la Tanzania limetokana na kuchanganywa kwa majina ya nchi hizo mbili, yaani “Tan-” kutokana na Tanganyika na “-zan-” kutokana na Zanzibar. Serikali inayoundwa na mkaliaji daima imekuwa ikijumuisha baadhi ya watu kutoka upande wa mkaliwaji ingawa kutoka chama kile kile ambacho kinaratibu mchakato mzima wa ukaliaji wenyewe.
Katika ngazi ya kijamii, raia wanaotoka ardhi iliyokaliwa wana haki zote za kiraia kwenye ardhi ya mkaliaji, ikiwemo elimu, ardhi, afya na huduma zote za kijamii kiasi cha kwamba wengi wanajihisi wana maisha mazuri zaidi wakiwa huko kuliko wakiwa kwenye ardhi yao ya asili.
Katika suala la kiusalama, ndani ya kipindi cha nusu karne ya ukaliwaji huu, mauaji ya moja kwa moja yanayoweza kuhusishwa na ukaliwaji wenyewe ni yale ya mwaka Januari 2001 ambapo watu zaidi ya 60 waliuawa na vyombo vya dola katika kile kinachoelezewa na shirika la haki za binaadamu la Human Rights Watch kwenye ripoti yake “Risasi Zilinyesha kama Mvua” kama mauaji ya makusudi dhidi ya waandamanaji wasio silaha.
Lakini kando ya hapo, ukaliwaji huu umeratibiwa kwenye kiwango cha juu kabisa cha kisiasa, na hata wanaoupinga wanafanya hivyo kwa tahadhari ya hali ya juu sana, diplomasia, maridhiano na mualaka, ndio maama ukiulinganisha na ukaliaji wa Indonesia dhidi ya Timor ya Mashariki, utaukuta huu wetu kuwa una afadhali. Wa Indonesia ulitandwa na mateso na mauaji ya maangamizi, yakiwemo yale ya mwaka 1991 ambapo Watimori 250 waliuawa katika eneo la Santa Cruz kwa wakati mmoja. Inakisiwa kuwa ndani ya kipindi cha ukaliaji huu, Indonesia ilihusika na asilimia 70 ya vifo vipatavyo 200,000 vya Watimori. Hadi mwaka 1999, Timori ya Mashariki ilikuwa na raia 823,386 tu, na hivyo unaweza kuona kuwa takribani robo nzima walikuwa wameuawa na jeshi la Indonesia na makundi ya wanamgambo wanaoungwa mkono na serikali ya Jakarta.
Vile vile, kinyume na jaala iliyozikumba Sahrawi na Timor ya Mashariki, ambazo uvamizi wa mataifa jirani dhidi yao ulilaaniwa haraka na Umoja wa Mataifa, kukaliwa Zanzibar na jirani yake Tanganyika hakukulaaniwa na Umoja wa Mataifa, bali kulikubalika na kupongezwa kwa kuwa mfano bora wa namna nchi za Kiafrika zinavyoweza kuihuisha ndoto ya “Afrika Moja”. Moja ya sababu ni kwamba kilichofanywa na Tanganyika kilipata baraka za wajumbe wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ambao walikuwa na maslahi yao kwa ukaliaji huo na pia kulipitia mikononi mwa kiongozi ambaye alikuwa na uwezo mkubwa wa kiakili, Julius Nyerere, kuliko wenzake wa Mauritania, Morocco na Indonesia za wakati huo.
Lakini siku zimepita na uhalisia umebadilika ndani ya mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama zinavyobadilika kwenye siasa za kilimwengu. Sasa dunia imeamua kuwa njia za kuupata uongozi wa ofisi za umma ni uchaguzi unaokidhi vigezo vya uhuru, haki na usawa miongoni mwa wanaowania nafasi hizo, kwani umma ndio muamuzi halisi wa nani aongoze mataifa yao, ikiwemo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo ni mwanachama wa Umoja wa Mataifa. Zanzibar ni sehemu ya Jamhuri hiyo, bila ya kujali ilikujaje kuwa sehemu hiyo na, kwa hivyo, Tanzania ina wajibu wa kimataifa kwenye suala hili kwa sababu zote mbili: kama mkaliaji (kama inavyohoji makala hii) na kama mwakilishi wa dola iitwayo Tanzania (kama wanavyohoji wale wanaouona huu kuwa ni muungano wa kawaida na wa hiari wa madola mawili yaliyokuwa huru).
Na kwa hivyo, Umoja wa Mataifa nao una wajibu wake kwa Zanzibar, kama sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo ni mwanachama wake. Ndio maana, kupitia shirika lake la maendeleo (UNDP), Umoja huu umekuwa mdau mkubwa wa uchaguzi visiwani Zanzibar kwa kipindi kirefu sasa, ukiwemo uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba 2015. Hivyo unaujuwa kwa kina mgogoro ambao umezushwa na uhuni wa Jecha Salim Jecha, lakini huenda Umoja huo haukuwa na macho ya kuuangalia mgogoro huu katika uhalisia wake – yaani mahusiano kati ya Tanganyika na Zanzibar. Bali pale viongozi wa taasisi zinazoitwa za Muungano wanapobariki uhuni huo, jicho la mwenye akili linapaswa haraka sana kuuona moja kwa moja mkono wa mkaliaji dhidi ya mkaliwaji. Na ni jicho hilo ambalo sasa jumuiya ya kimataifa inapaswa kuwa nalo.
Zanzibar Daima.

No comments: