Kijijini kwetu alikuwepo mzee mmoja ambaye alikuwa maarufu sana. Miongoni mwa mambo yaliyompa umaarufu ni jinsi alivyokuwa mweledi katika elimu ya dini ya Kiislamu kiasi cha kuwafundisha baadhi ya aalim wakubwa katika kijiji hicho. Pamoja na taaluma aliyokuwa nayo, alikuwa mpenzi mkubwa wa pombe. Kwa ufupi alikuwa mlevi, unaweza kusema wa kupindukia.
Katika sikukuu moja ya Eid-ul-Fitri majira ya laasiri akiwa ameshauchapa ulevi hajiwezi, akitembea kwa shida, alikutana na watu wakiwa wamebeba jeneza wakielekea makaburini kuzika. Aliwaangalia kama vile ni jambo geni kwake, kisha akasema: “Jamani watu wengine nao hawachagui hata siku ya kufa? Inakuwaje leo siku ya sikukuu mtu unakwenda kujifia? Siku ya furaha unaigeuza ya msiba.” Maneno yake hayo yakawa gumzo kubwa kijijini.
Siku ya pili watu kadhaa walimfuata kumuwaidhi kwamba sasa pombe inampeleka kubaya mpaka anafanya utani na kudura za Allah. Miongoni wa waliomfuata ni sahibu yake wa karibu sana ambaye alimueleza: “Sahibu yangu sasa pombe inakumaliza. Mimi ninajua miaka yote unalewa, lakini hivi vituko vyako vya jana naona ulevi unakumaliza!” Na yeye mwenyewe akamjibu kwa upole: “Ni kweli unayosema. Hata mimi najiuliza sijui jana nililewa pombe gani. Lakini kila lenye mwanzo lina mwisho. Mimi kuanzia leo nnaweka nia ya kuacha ulevi!” Na kweli, baada ya muda aliwacha kabisa pombe, akafanya kazi ya ualimu na mtu wa kushikamana na dini.
Maelezo aliyoyatoa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Hamad Masauni wiki chache zilizopita katika Bunge la Jamhuri ya Muungano kuhusiana, pamoja na mambo mengine, masheikh wa Zanzibar waliopo mahabusu katika gereza la Ukonga Dar es Salaam yamenikumbusha kisa hicho nilichokieleza hapo juu. Nimejiuliza peke yangu, nikaona haitoshi, niulize na wenzangu akiwemo na yeye mwenyewe, hivi amelewa pombe gani iliyompelekea aeleze mambo ambayo hata mtoto mdogo anaweza kubaini kwamba ni ya kuhandisiwa?
Napenda nieleze kwa ufupi kwa nini nimejiuliza Masauni amelewa pombe gani. Ndani ya bunge kumekuwa kukitolewa maelezo kuhusiana na kadhia ya masheikh hao na baadhi ya mawaziri ambayo ni ya kusikitisha; mengine ya uongo wa wazi na mengine ya ubabaishaji wa kupindukia. Nimewahi kuona Mwigulu Nchemba akitoa maelezo ya ubabaishaji Bungeni kuhusiana na kadhia ya masheikh wakati akijibu suali la Mheshimiwa Dkt. Suleiman Ali Yussuf. Aidha, nimewahi kushuhudia mwalimu wangu, Profesa Palamagamba Kabudi, akifanya siasa bungeni kwa kupitia haki za raia hao ambao hadi sasa hawana hatia. Lakini, maelezo ya Masauni kwa hakika yaliniuma sana kiasi cha kunisukuma kuandika ukweli ninaoufahamu katika kadhia hiyo. Imeniuma kwa vile alitoa maelezo akiwa amejitanda kilemba cha uumini na kupenda uadilifu. Kupenda uadilifu ni kitu chema sana, lakini kuna msemo wa wanafalsafa unaosema “The principle of being principled is to be principled.” Kwa ufupi huwezi kuwa muadilifu nusu nusu. Ukiamua kujinasibisha na uadilifu, lazima uonekane au angalau ufanane na uadilifu.
Masheikh Kukamatwa na Kusafirishwa Tanzania Bara
Wakati masheikh hao walipokamatwa, Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein alikuwa katika safari ya kikazi katika visiwa vya Samoa. Dkt. John Pombe Magufuli, nadhani, wakati huo hakuwa ameanza hata mchakato wa kugombea urais au hata fikra ya kugombea nafasi hiyo. Mhandisi Hamad Masauni yeye alikuwa mbunge wa kawaida, sidhani kama alishaanza kuwa na ndoto ya kuwa naibu waziri. Mimi wakati huo nilikua Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Zanzibar.
Siku ya pili tu tokea kukamatwa masheikh hao usiku mkubwa na asubuhi wakasafirishwa kupelekwa Dar es Salaam, baadhi ya wazazi na jamaa wa masheikh hao walinifuata ofisini; wake kwa waume. Kilikuwa kikundi kikubwa kwa kweli. Mmoja kati ya hao alikuwa mke wa mmoja wa wahusika na mmoja ni mama mzazi wa mmoja wa wahusika. Maelezo yao jinsi ya walivyokamatwa yalikuwa ya kusikitisha sana. Niliwaahidi kwamba nitafuatilia kwa haraka suala la kusafirishwa kwao kupelekwa Dar es Salaam, kwani ninahisi haikuwa sawa kisheria. Siku hiyo hiyo niliomba kuonana na Makamo wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi, na nilipata miadi ya kuonana naye siku ya pili asubuhi.
Nilipokutana na Makamo wa Pili wa Rais nilimweleza kwamba, suala la watu kukamatwa ni jambo la kawaida na ndio kazi ya polisi kama wanatuhumu mtu ametenda kosa la jinai. Hata hivyo, sababu ya kuonana naye ni kueleza maoni yangu ya kisheria juu ya uharamu wa kitendo cha kuwasafirisha kwenda Dar es Salaam chini ya Katiba ya Zanzibar na Sheria. Nilimpa mfano wa kadhia ya watu waliokamatwa Zanzibar kwa tuhuma za uchochezi kwa kutangaza kutaka Pemba ijitenge. Wahusika hao walipokamatwa, Rais Amani Karume alikuwa katika ziara ya kikazi nchini Marekani, lakini aliporudi tu siku ya pili akamuita Mwanasheria Mkuu, Mheshimiwa Idi Pandu, na mimi binafisi nikiwa Mkurugenzi wa Mashtaka, na kutuhoji kwa nini tuliruhusu watu hao wasafirishwe kupelekwa Dar es Salaam kwa tuhuma za kosa lililotokea Zanzibar. Nakumbuka alihoji: “Hivi hao watu kama wamesema, si wajibiwe tu? Na kama ni lazima wakamatwe na kuhojiwa, hivi Zanzibar hapana Serikali, hapana Mwendesha Mashtaka, hapana Mahkama?” Baada ya kumjibu kwamba watu wamekamatwa na kusafirishwa bila ya sisi kushauriwa, alimwita Kamishna wa Polisi naye baada ya kumhoji akampa amri watu hao warejeshwe Zanzibar haraka na kama wana tuhuma zozote waje washtakiwe Zanzibar. Baada ya siku mbili watu hao wakarejeshwa Zanzibar.
Aidha, nilimweleza Makamo wa Pili wa Rais msimamo wa kisheria uliotolewa na Mahkama Kuu ya Zanzibar chini ya wakati huo Jaji Mkuu Augustino Ramadhani na pia Mahkama ya Rufaa ya Tanzania ambapo Mahkama hiyo ilielekeza wazi kuwa mtu anapotuhumiwa kwa kosa lolote lililotendeka Zanzibar, hata kama kosa hilo ni chini ya Sheria ya Muungano, basi lazima ashtakiwe na mamlaka ya mashtaka ya Zanzibar, katika Mahkama ya Zanzibar na kwa kutumia sheria za nyendo za jinai za Zanzibar. Baada ya kumueleza hivyo aliahidi atalifatilia kwa Kamishna wa Polisi Zanzibar.
Kilichonishangaza sana ni kwamba wakati Dkt. Shein aliporudi kutoka safari, alituita mimi nikiwa Mwanasheria Mkuu na Mkurugenzi wa Mashtaka, Bwana Ibrahim Mzee, tukiwa pamoja na Makamo wa Pili wa Rais. Miongoni mwa mambo aliyotuarifu ni kwamba Jeshi la Polisi wanataka tutowe wanasheria wa Serikali kutoka ofisi zetu mbili waende Dar es Salaam wakashirikiane nao kuwahoji watuhumiwa kwa vile wanasheria wa Zanzibar wanazielewa vizuri zaidi sheria za Zanzibar.
Mimi nilitangulia kumueleza kwamba: “Kabla hujarudi safari, nilionana na Makamo wa Pili na kumpa ushauri wangu wa kisheria kuhusu kadhia hiyo na nilimueleza kwa kina msimamo wa kisheria na kwamba kusafirishwa watu hao na kwenda kuhojiwa na kushitakiwa Dar es Salaam ni haramu!” Ilionesha dhahiri kwamba hakuwa amearifiwa kabla juu ya ushauri huo. Nilimalizia kwa kumwambia kwamba: “Kwa vile suala hilo si halali, nikitowa wanasheria kufanya kazi hiyo, nitakuwa ninabariki kitu batili!” Naye Mkurugenzi wa Mashtaka akatoa maelezo nadhani fasaha zaidi ya kuunga mkono kwamba suala hilo lilikuwa batili na si vyema kwa wanasheria wa Serikali kutumika kubariki batili hiyo.
Rai iliyotolewa ni kuwa Makamo wa Pili aitishe kikao cha vyombo vya ulinzi vinavyohusika na kadhia hiyo ili kupata muafaka. Siku ya pili tukaonana na vyombo husika chini ya uenyekiti wa Makamo wa Pili wa Rais. Si vyema kueleza kwa urefu yaliyojiri katika kikao kile lakini inatosha kusema kwamba hatimaye angalau mmoja wa maofisa waandamizi wa Tanzania Bara aliyepigiwa simu tukiwa katika kikao kile alikiri kwamba hata wao wanafahamu kwamba hilo jambo lina matatizo ya kisheria, lakini kwa sasa wanachotaka ni kupata ukweli wa tuhuma hizo na ndio maana wakaomba msaada wa wanasheria wa Serikali kutoka Zanzibar. Baada ya maelezo hayo, busara iliyotoka ni kuwa wanasheria wa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka waende Dar es Salaam kama ilivyoombwa kwa vile Ofisi hiyo ndiyo inayohusika na mashtaka na sio Ofisi ya Mwanasheria Mkuu. Siwezi kuyasema yale wanasheria hao walioenda Dar waliyoeleza baada ya kurudi safari hiyo, lakini naamini Bwana Masauni kama ana nia ya dhati ya kutafuta ukweli atawatafuta wanasheria hao kwa vile bado wapo.
Katika maelezo yake, Bwana Masauni anasema kwamba amejiridhisha kuwa Serikali imesimamia suala hili kwa uadilifu na kama angelihisi haisimamii kwa uadilifu, angejiuzulu na akaungana na wale wanaohoji kadhia hiyo. Suala langu ni kwamba hivi Serikali inaposhauriwa na Mwanasheria Mkuu ambaye, chini ya Kifungu cha 20(1) cha Sheria Namba 6 ya 2013, ushauri wake wa kisheria ndio msimamo rasmi wa kisheria wa Serikali isipokuwa kama Rais atatoa maelekezo tofauti au utenguliwe na Mahkama, na ikaenda kinyume na ushauri huo, huo ndio uadilifu? Mbali ya ushauri wa Mwanasheria Mkuu, katika masuala ya kesi za jinai, Serikali inapokwenda kinyume na ushauri wa Mkurugenzi wa Mashtaka, nao huo ndio uadilifu anaouzungumzia Bwana Masauni?
Msimamo wa Kisheria
Katika mfumo wa kikatiba wa Jamhuri ya Muungano, masuala ya Mahkama na usimamizi wa sheria si suala la Muungano. Kilichokuwa cha Muungano ni Mahkama ya Rufaa pekee. Kwa hivyo, hadi katika ngazi ya Mahkama Kuu, hakuna Mahkama ya Jamhuri ya Muungano bali Mahkama ya Tanzania Bara au Mahkama ya Zanzibar. Na katika hilo, ndio maana Mahkama Kuu ya Zanzibar na Mahkama Kuu ya Tanzania Bara zina mamlaka sawa [concurrent jurisdiction].
Katika Sheria ya Jinai, jambo moja lililowekewa ufafanuzi mzuri ni juu ya upeo wa mashtaka na mamlaka ya kushtaki. Tulizoea kukariri kwa moyo kutokana na umuhimu wake kifungu kinachoeleza ni wapi mtu atashtakiwa kwa kosa alilotenda. Kwa upande wa Zanzibar, kwa mfano, mtu atashtakiwa katika Mahkama za Zanzibar endapo viini vyote vya kosa [elements of the offence] vimefanyika Zanzibar au katika bahari kuu ambayo Zanzibar ina mamlaka nayo chini ya sheria za kimataifa. Aidha, anaweza kushtakiwa Zanzibar endapo baadhi ya viini vya kosa vimetokea nje ya Zanzibar lakini baadhi ya viini vya kosa vimetokea ndani ya Zanzibar. Kwa ufupi, ili mtu ashtakiwe Zanzibar ni lazima kuwe na uhusiano wa kosa hilo na Zanzibar. Hali ni hivyo hivyo kwa sheria za jinai za Tanzania Bara.
Hata hivyo, suala ambalo muda mrefu lilikuwa na utatanishi ni: jee, Mahkama Kuu ya Zanzibar inao uwezo wa kusimamia sheria zilizotungwa na Bunge la Muungano? Mahkama Kuu ya Zanzibar katika kesi kadhaa imewahi kutowa ufafanuzi wa suala hilo. Katika kesi ya Himid Mbaye v. The Brigade Commander of Nyuki Brigade ya 1982, Mahkama Kuu ilieleza kwamba pamoja na kwamba Kamanda huyo ni ofisa wa Muungano, lakini kwa vile amefunguliwa madai Zanzibar lazima ashtakiwe Zanzibar kwa kufuata sheria ya Nyendo za Madai Zanzibar na hivyo haihitajiki kupata ridhaa ya Waziri wa Sheria wa Serikali ya Muungano bali Waziri huyo apewe taarifa ya siku 60 kama inavyoeleza sheria ya Zanzibar ya nyendo za madai. Mahakama Kuu pia iliwahi kutoa msimamo unaofanana na huo katika kesi ya Shaaban Khamis v. Samson Goa and the Commissioner of Police ya 1983.
Mbali ya maamuzi hayo ya Mahkama Kuu ya Zanzibar, Mahkama ya Rufaa ya Tanzania katika kesi ya Seif Sharif Hamad v. SMZ ya 1992 ilitoa ufafanuzi bayana zaidi hasa kuhusiana na kesi za jinai. Katika kesi hiyo Bwana Seif Sharif Hamad alishtakiwa kwa tuhuma za kupatikana na nyaraka za siri za Serikali kinyume na Sheria ya Usalama wa Taifa [National Security Act]ambayo ilitungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano. Hati ya mashtaka [Information] ilitiwa saini na Mkurugenzi Wa Mashtaka wa Tanzania Bara kwa vile ndiye aliyetajwa chini ya Sheria hiyo ya Usalama wa Taifa kwamba ndiye mwenye mamlaka ya kufungua mashtaka.
Mahkama ya Rufaa ilieleza: “Since the High Court of Zanzibar is not a Union matter, then its procedures and officers too are not Union matters. So if legislation of the Union Parliament which applies to both parts of the Union is silent as to the procedure to be followed in case of litigation or prosecution in the High Court of Zanzibar for purposes either of consent or instituting or conducting prosecution it is the Attorney General of Zanzibar or such officers appointed by him. The DPP [of the Mainland Tanzania] is not such an officer and as such officer and therefore he could not give his consent nor file information in the High Court of Zanzibar. So the proceedings were and are hereby declared to be a nullity.”
Kwa ufupi, Mahkama ya Rufaa ilibatilisha mashtaka na mwenendo mzima wa kesi kwa sababu DPP wa Tanzania Bara hakuwa na mamlaka ya kufunguwa kesi Zanzibar na aliyepaswa kufungua kesi ni Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, ambaye kwa wakati huo ndiye aliyekuwa na mamlaka ya mashtaka kwa vile ofisi ya DPP Zanzibar ilikuwa bado haijaanzishwa.
Ukichanganya yale niliyoeleza hapo awali na msimamo huu wa Mahkama ya Rufaa, ndio mana hata vyombo husika vya Tanzania Bara walijuwa na bado wanaelewa kwamba kuwasafirisha masheikh na kwenda kuwashtaki Tanzania Bara ni kinyume na Katiba zote mbili na ni kinyume na sheria za pande zote mbili za Muungano. Kama Bwana Masauni alikuwa na nia ya dhati ya kutafuta ukweli na kujiridhisha uadilifu katika suala hili, asingeliacha kutafuta wataalamu wa Sheria ambao wanalifahamu vizuri suala hili wakampa ufafanuzi.
Kiini cha Masheikh Kusafirishwa Kupelekwa Dar
Inahitaji weledi na kumbukumbu kidogo tu kufahamu kiini cha njama hiyo.
Baada ya vyama kuanzishwa Tume ya Muafaka ya Zanzibar chini ya Sheria Namba 10 ya Mwaka 2001, miongoni mwa mambo waliyoyafanya ni kutafuta wataalamu kufanya mapitio ya mfumo wa kisheria wa Zanzibar. Moja ya jopo la wataalamu hao alilokuwemo Profesa Issa Shivji lilibaini kwamba mashtaka yanatumika vibaya sana kwa malengo ya kisiasa. Na hivyo, wakapendekeza ianzishwe Ofisi huru ya Mkurugenzi wa Mashtaka badala ya mashtaka kuendeshwa na Mwanasheria Mkuu ambaye ana nasaba ya karibu na siasa.
Ilipoanzishwa Ofisi hiyo mwaka 2002 chini ya Katiba ya Zanzibar kupitia Marekebisho ya Nane ya Katiba, nilipata heshima ya kuteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka mwanzilishi wa Ofisi hiyo, ambapo niliitumikia kwa miaka 9 kabla ya kuteuliwa kuwa Mwanasheria Mkuu. Miongoni mwa mambo ambayo yalifanyika ni kuondoa Polisi katika uendeshaji wa mashtaka ili wabaki na kazi ya upelelezi na badala yake mashtaka yaendeshwe na wanasheria wa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka [civilianization of prosecution service]. Aidha, sheria za jinai, ile ya Jinai, Sura ya 13 [Penal Decree] na ile ya Nyendo za Jinai, Sura ya 14 [Criminal Procedure Decree] zilifanyiwa mapitio makubwa na kutungwa sheria mpya ya Jinai Namba 6 ya 2004 na ya Nyendo za Jinai, Namba 7 ya 2004.
Miongoni mwa mambo yaliyozingatiwa katika sheria hizo mpya ni pamoja na kuharakisha mashtaka kwa kuondoa utaratibu wa Uchunguzi wa Awali [Preliminary Inquiry], kuweka ukomo wa upelelezi ambapo muda maalum wa upelelezi uliwekwa kwa makosa mbalimbali na utaratibu wa kuomba kuongezwa muda wa upelelezi na Mahkama. Aidha, suala la dhamana liliwekwa bayana zaidi. Tokea wakati wa Sheria ya Jinai ya zamani [Penal Decree],hakukuwa na kosa ambalo halina dhamana chini ya sheria za Zanzibar. Isipokuwa tu kwa makosa makubwa kama vile mauaji, Mahkama Kuu pekee ndio yenye uwezo wa kutoa dhamana. Ilikuwa mazoea kwamba Mahkama Kuu nayo haikuwa ikitoa dhamana. Hivyo, sheria mpya iliweka bayana zaidi tu utaratibu wa kuomba dhamana Mahkama Kuu hata kwa makosa makubwa endapo mtu amekaa mahabusu muda mrefu na hakuna dalili kwamba upande wa mashtaka unafanya juhudi za kuridhisha katika upelelezi. Mfumo mpya wa mashtaka ulisisitiza sana upelelezi ufanyike kwanza kabla ya kufunguwa mashtaka. Hatua hizo zilipunguza sana mahabusu, kesi za kubambikiwa na kesi za kisiasa.
Rais Karume, kwa juhudi zake binafsi alihimiza kufanya kila aina ya mageuzi ambayo yataleta ustaarabu katika kusimamia mashtaka.
Mfumo huo wa uendeshaji wa sheria za jinai ulionekana kikwazo kwa baadhi ya maofisa wa polisi, hasa wale waliotoka Tanzania Bara. Na kwa hakika kutokana na kauli mbalimbali za walioandaa mpango wa kuwasafirisha masheikh hao kwenda Dar es Salaam, hilo ndio ilikuwa kiini cha masheikh hao kufanyiwa dhulma waliyofanyiwa na wanayoendelea kufanyiwa sasa.
Ninachojiuliza tu ni kwamba hivi Bwana Masauni hata akipata ukweli juu ya hili, bado ataona masheikh wanafanyiwa uadilifu? Pengine ni vibaya kutangulia kumhukumu, lakini naamini kama angekuwa na dhamira ya kweli ya kutafuta ukweli asingeshindwa kulijua hili.
Tathmini ya Masauni
Katika maelezo yake, Masauni anasema kwamba alienda kuwaona masheikh hao na wakamuhakikishia kwamba hawana tatizo lolote isipokuwa la kesi yao kuchelewa. Aidha, walimuahidi kwamba hawatokubali kutumika tena katika siasa. Alienda mbali zaidi kutuhumu kwamba inawezekana walihusika, kwa namna moja au nyengine, katika kadhia za watu kumwagiwa tindi kali na Padri mmoja kuuliwa Zanzibar. Na huyu ni mtu anayejinasibu na kutafuta ukweli na anayeamini kwamba yanayofanywa ni ya uadilifu.
Hili limenishangaza na kunikumbusha mmoja wa watu waadilifu sana naye ni Seyyidna Omar Ibnul Khattab. Katika kitabu chake cha MAISHA NA NYAKATI ZA SEYYIDNA OMAR, Dr Ali Mohammad as-Sallabi, miongoni mwa visa vingi vinavyofafanuwa misingi ya uadilifu iliyosimamiwa na Seyyidna Omar, ameeleza kisa cha Gavana wa Misri, Amr ibn Al-As. Siku mojawapo vijana walikunywa kinywaji ambacho hawakujua kama ni kilevi. Baada ya kinywaji hicho kuwalewesha walifikishwa mbele ya Gavana wa Misri ili wapewe adhabu kwa kulewa. Ingawa mwanzoni alisita, lakini alitekeleza adhabu [hadd] kwa kuwachapa bakora na kuwanyoa nywele zao hadharani. Lakini aliitekeleza adhabu hiyo hiyo kwa mmoja wa vijana hao kwa faragha akiwa ndani ya nyumba yake. Alifanya hivyo kwa sababu kijana huyo alikuwa mtoto wa Seyyidna Omar, ambaye ndiye aliyekuwa Khalifa wa Dola ya Kiislamu wakati huo na ambaye ndiye aliyemteua Amr kuwa Gavana wa Misri. Alipopata habari hiyo, Seyyidna Omar alimpelekea Amr barua kali ya kumuonya kwa kufanya upendeleo huo na akamtanabahisha kwamba yeye Omar kama kiongozi hampendelei yeyote katika kutimiza wajibu wake.
Kisa chengine chenye mafunzo makubwa ni pale mtoto wa Gavana huyo alipompiga kijana mmoja wa Kimisri lakini Amr hakuchukuwa hatua yoyote dhidi ya mtoto wake. Seyyidna Omar alimuita yeye na mtoto wake na baada ya kumkanya akamtaka afanye suluhu na aliyefanyiwa kitendo hicho. Mbali ya hayo, alimwambia maneno ambayo huwa yananukuliwa sana na wapenda uadilifu. Alimwambia: “Hivi wewe ni nani wa kuwafanya watumwa watu waliozaliwa na mama zao wakiwa huru!?”
Masauni yeye hajakerwa na masheikh hao kuwekwa ndani muda mrefu kwa kisingizio cha upelelezi kutokamilika. Na bado anajinasibisha na uadilifu na uumini. Uadilifu unahitaji ukerwe na kila chenye harufu ya dhulma, harufu ya uonevu na harufu ya upendeleo. Ndio viongozi waadilifu wa kweli kama Seyyidna Omar walivyotufunza kwa vitendo.
Inawezekana Masauni hafahamu kwa sababu hakuwepo, kwamba masheikh hao hawajawahi kuhusishwa wala kutuhumiwa kisheria kwa makosa aliyoyataja ya kumwagiwa watu tindikali wala kuuawa kwa Padri. Majalada ya kesi hizo yapo na angeweza kujiridhisha. Ni vyema kumtanabahisha kwamba kumsingizia mtu iwe moja kwa moja au vyenginevyo kwa madhumuni tu ya kuonyesha kwamba ni mbaya ni kiwango cha juu cha kukosa uadilifu ambao Masauni anapenda kujinasibisha nao. Ndio maana Allah [SW] katika Surat Al-Furqan [Sura ya 25], alipotaja sifa za watu wema amesema kwamba watu wema ni pamoja na wale ambao sio mashuhuda wa uongo na wanapokutana na mambo ya kipuuzi huyapita huku wakibaki na heshima. Allah ameliunganisha hili la ushuhuda wa uongo na mambo ya upuuzi [laghwa] kwa sababu mara nyingi ni katika mambo hayo ya laghwa ambapo shetani huipamba starehe ya kupita, dhulma na haramu mpaka watu wakafika kuwa shuhuda wa uongo. Ni wazi na shetani naye amempambia Masauni laghwa katika jukwaa la siasa.
Hivi Masauni hafahamu kwamba masheikh hao kukaa ndani kwa miaka sita sasa ni adhabu ya kudhiisha na kudhalilisha? Masheikh hao ni watu wenye familia, wenye ndugu, wenye watoto, wenye wanafunzi, wafuasi, majirani na wahisani. Wapo ambao ndoa zao na familia zimeparaganyika kwa sababu tu ya wenyewe kuwa mahabusu. Wapo ambao familia zao zinaishi kwa dhiki kubwa kwa sababu ya wao kutokuwepo. Wapo ambao wazee wao wanaumwa kwa sababu ya fikra juu ya watoto wao. Fikiria pia afya na siha za watu hao ambao wapo kizuizini huku wao wakiwa na yakini kwamba wapo kizuizini sio kwa tuhuma za jinai, bali kwa dhulma ya dhahiri. Bado unapata sura, mdomo na maneno ya kujinasibisha na uadilifu katika kulishughulikia suala lao?
Nini Hasa Kosa la Masheikh?
Hakuna asiyejuwa, hata wale wanaojitowa fahamu, kwamba masheikh hao wapo ndani ikiwa sehemu ya uwekezaji unaofanywa kuwanyamazisha wote wanaodai haki zao kama wananchi wa Zanzibar ndani ya Muungano. Na wanafanya hivyo kwa njia ya amani, kwa njia zinazokubaliwa kisheria, njia ya kusema na kutoa mawazo yao. Uwekezaji huo umeanza siku nyingi na bado unaendelea. Hilo ndio kosa walilolifanya na kukamatwa chambilecho Wazungu “red-handed”. Lakini naomba nimtanabahishe Masauni maneno ya mwanasiasa mahiri wa Uingereza Bwana William Pitt [Earl of Catham] aliyoyasema katika Bunge la Uingereza tarehe 14 Januari 1766 wakati akiwatetea na kuwaunga mkono Wamarekani kwa kudai haki zao kutoka kwa Waingereza: “Gentlemen have been charged with giving birth to sedition in America. They have spoken their sentiments with freedom against the unhappy act, and that freedom has become their crime. Sorry I am to hear the liberty of speech in this House imputed as a crime…I rejoice that America has resisted.”
Nadhani Bwana William Pitt anastahiki kujinasibisha na uadilifu kwa kuisema Serikali yake ndani ya Bunge akiwatetea wale ambao wanaoshtakiwa kwa makosa ya uchochezi kwa kudai haki zao huku akionesha wazi kuwa anawaunga mkono katika harakati zao.
Aidha, ni vyema Masauni akakumbuka kwamba historia ya dunia imethibitisha kuwa huwezi kutumia nguvu na vitisho kunyamazisha watu wanaodai haki zao. Wenye busara kama vile mbunge mwengine maarufu wa Uingereza, Bwana Edmund Burke, naye katika hotuba yake katika Bunge la Uingereza aliyoitoa Machi 1775 aliitanabahisha Serikali yake kwamba matumizi ya nguvu hayajawahi kusaidia katika kunyamazisha harakati za binadamu kudai haki yake. Yeye alisema: “The use of force is but temporary, it may subdue for a moment, but it does not remove the necessity of subduing again; and a nation is not governed which is to be perpetually conquered.”
Hoja ya Masauni ya Siasa za Kuligawa Taifa
Miongoni mwa maneno mazuri sana aliyoyasema Bwana Masauni ni yale ya kukemea siasa za kuligawa taifa. Jinsi ya alivyosema yale maneno kwa hisia, binafsi natamani sana ingekuwa kauli yake ya dhati kabisa. Kutokana na ushawishi wake wa kisiasa, angeisaidia sana Zanzibar kuondokana na maradhi ya ubaguzi na mifarakano inayopandikizwa kila uchao hata kwa kizazi cha kesho.
Lakini hivi Masauni hajui nani walioko mstari wa mbele kupandikiza fitna hiyo? Wanasema hata hofu ya Mungu hawana. Wanasema hadharani, kwa mabango na matangazo kauli za kupandikiza chuki na kukigawa hata chama chao kwa misingi ya rangi, asili na kabila. Wapo waliokwenda mbali zaidi na kusema katika mikutano ya hadhara na vyombo vikuu vya nchi kwamba Serikali ya Zanzibar haiwezi kutolewa kwa njia ya kura kwa vile imepatikana kwa mapinduzi. Ndio tuseme Masauni anataka tuamini kwamba hajawahi kuyasikia au kuyaona hayo yote? Tumuulize ni lini ameyakemea hata kwa faragha? Na yapo mengine mabaya zaidi ya hayo ambayo yanajenga mizizi ya chuki ya muda mrefu zaidi kwa vizazi vyetu na ambayo tunaamini kama Masauni hakushiriki kuyaandaa, basi angalau anayajuwa vizuri lakini hayajawahi hata kumuuma kwamba ni mabaya kwa mustakbali wa taifa.
Hitimisho
Inasikitisha sana kwamba katika karne hii ya maendeleo makubwa sana ya binaadamu, katika taifa letu bado wapo viongozi wanaotumia rasilimali na nguvu nyingi kushughulikia mambo ambayo hayaongezi tija wala sifa yoyote kwa taifa. Kama angekuwa na dhamira ya dhati ,Masauni angeisaidia sana Serikali kupata ukweli na ufumbuzi wa suala la masheikh wale wanaoteseka kwa sababu tu ya hakuna aliyepo tayari kuwa mkweli. Watu wote niliowataja na wengine ambao sikuwataja wanaolijuwa suala la masheikh kwa undani wapo na ni wazima wa afya. Mimi naamini kwamba wanaweza kusaidia sana kuueleza ukweli. Baadhi yao wamestaafu na hiyo inawapa fursa ya kuwa wawazi zaidi.
Mimi naamini viongozi wetu wa sasa walibebeshwa tu suala la masheikh. Ukizingatia kwa makini kauli ya Mwigulu Nchemba, kauli ya Profesa Kabudi na kauli ya Masauni zinavyopishana ni dhahiri kwamba yapo mambo viongozi hawaelezwi ukweli.
Kama nilivyotangulia kueleza kwamba lilipotokea suala hili,Rais Magufuli hakuwa ameanza hata mchakato wa Urais na Dkt Shein naye hakuwepo hata nchini. Ni busara wakachukuwa nafasi yao kama viongozi waliobebeshwa tu suala hili na kulipatia ufumbuzi wa haraka. Kwa Dkt Shein, itamsaidia sana kama atatanabahi ule msemo wa Kiswahili unaosema: “Ukishapata Mlango wa Kuingia basi Tafuta na wa Kutokea”. Rais Dkt Amani Karume nadhani aliukumbuka msemo huu na leo kwa hakika anafaidika nao.
Mwandishi wa makala hii aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Ofisi ya Mwendesha Mashitaka na kisha Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar.
credit:ZANZIBAR DAIMA
Kijijini kwetu alikuwepo mzee mmoja ambaye alikuwa maarufu sana. Miongoni mwa mambo yaliyompa umaarufu ni jinsi alivyokuwa mweledi katika elimu ya dini ya Kiislamu kiasi cha kuwafundisha baadhi ya aalim wakubwa katika kijiji hicho. Pamoja na taaluma aliyokuwa nayo, alikuwa mpenzi mkubwa wa pombe. Kwa ufupi alikuwa mlevi, unaweza kusema wa kupindukia.
credit:ZANZIBAR DAIMA
No comments:
Post a Comment