Wednesday 24 February 2016

KONA YA ALLY SALEH


Mbunge wa jimbo la Malindi Muheshimiwa Ally Saleh Makala yangu ya leo kwenye MTANZANIA
Kwa jicho langu la kisanii natamani sana kadhia ya Uchaguzi wa Marejeo niitungie hadithi fupi. Naamini itakuwa tamu sana na hapana shaka mhusika wake mkuu atakuwa ni Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ZEC jecha Salum Jecha. Ni mkasa ambao kama haukutungiwa hadithi kiasi chochote cha kuelezewa katika mfululilizo wa makala za magazetini, hakitatosha kuuonogesha na kuufanya usisahaulike. Maana hapo ndipo panapokuwa na tofauti baina ya habari na sanaa.
Lakini naona wakati wake bado. Tuone kituko hiki kitavyoishia kisha ndipo wasanii kama mimi na wengine waingie kazini. Ila hakika kama vile alivyokuwa akisema Dk. Salmin Amour aliyekuwa Rais wa Zanzibar na kujipa jina la Komandoo au Karume Mdogo alivyokuwa akisema katika hali kama hizi kuwa “ Hapa inalekea patakuwa na mchuzi wa Kigoa.”

Mchuzi wa Kigoa Dk Salmin alikuwa akisema ni ule ambao mwisho utakuwa hauliki kwa wingi wa pilipili maana hauna udhibiti kwa sababu kila mmoja anaongeza pilipili yake bila ya kujali kuwa wenzake nao pia wametia pilipili chunguni. Haya, Uchaguzi wa Okotba 25 umefutwa. Tukaambiwa kuwa tarehe ya kurudiwa itatangazwa. Kimya kimya ghafla ikatangazwa kuwa ni Machi 20 na sasa kila mtu anasubiri kweli itakuwa hiyo kama isemwavyo na kweli utakuwa ni Uchaguzi Mkuu wa Marudio au ni mfano tu?
Maana sharti kuu la kwanza la kuwepo Uchaguzi Mkuu katika nchi ni kupatikana muwafaka wa kitaifa. Muwe mmetoka vitani au muwe katika hali ya amani Uchaguzi Mkuu unanoga pale vyama vinaporidhia na kushiriki katika kila hali kuona kuwa jambo hilo linafanikiwa na sio kulipiga vita.


Pili ni umma kuitikia. Uchaguzi Mkuu unatakiwa uvume kwa uhakika wake na sio kuvia kwa mikasa yake na wananchi wakijua kuwa njia kuu na moja pekee ya kubadilisha uongozi ni kufanyika kwa uchaguzi na kila mwenye haki ya kuandikishwa anandikishwa bila ghalat wala hila.
Tatu Uchaguzi Mkuu unatakiwa ufanywe au usimamiwe na chombo chenye kukubalika na kinachosimama pamoja katika kila hali na kama kupapurana ni ndani kwa ndani wenyewe kwa wenyewe na mbele ya umma wao ni wamoja.Nne Uchaguzi Mkuu wenye sifa ya kuwa ni Uchaguzi Mkuu ni ule ambao vyama na wananchi wanakuwa na imani ya hali ya juu kuwa kura zitaheshimiwa na walioshinda watatangaziwa kuwa ni washindi hata kama ni kuwaudhi na kuwakera watawala. Kinyume cha hapo ni kudanganyana tu.

Kwa wengi tunaona Machi 20 hapatakuwa na uchaguzi ambao una sifa za hapo juu. Umma ulishiriki kwa dhati uchaguzi wa Oktoba 20 kwa kuwa kulikuwa na uwezekano wa sifa hizo kutimizwa hadi ZEC ilipofanya hiana na kwa hivyo kupoteza imani mbele za watu au wapiga kura.
Ni nani ambae ataamini tena kuwa kutakuwa na ushindani wa haki na mshindi atatangazwa? Kipi kinaweza kuifanya ZEC, iwapo vyama vyote vitashiriki, vitangaze chama halali kilichoshinda? CUF waliiamini Tume 1995,2000,2005,2010 na dhihirisho la mwisho likawa ni 2015. Ni kipi cha kurudisha imani ya wapiga kura kwa Tume? Tunaambiwa kuwa vyama vitakavyoshiriki ndio hivyo hivyo na uchaguzi wa marejeo utaendelea kwa vitakavyo kuwepo. Jee hapo ndio kuna muwafaka wa kitaifa? Hivi kweli Tume inaamini kuwa inatenda haki kuendelea na uchaguzi na matokeo hayo ya uchaguzi yataiweka Zanzibar katika hali ya amani na kutawalika?

Hivi Tume pale ambapo chama kikubwa chenye wafuasi wanaoweza kufanya maamuzi kama ilivyoonekana Oktoba 25 kinapokataa kushiriki kinajihisi kina uhalali wa kuendelea na vyama vyengine kama hakuna kilichotokea? Yaani CCM mgombea wake wa Urais aliyepata kura kama 182,000 hivi ashindanishwe na vyama ambavyo hata kura 500 hawakufikisha kimoja kimoja, ndivyo ni sawa tu?
Au Tume kuendelea na Uchaguzi ilhali ikijua kuwa hakuna chama hata kimoja chenye uwezo wa kuchukua kiti chochote cha Uwakilishi isipokuwa CUF na CCM ambavyo hata hivyo viligawana viti 27-27 kwa ushahidi wa vyeti vilivyotolewa na Tume yenyewe, kura iendelee tu kama kwamba hakuna kitu?
Na udiwani jee? Yaani CCM haina uwezo wa kupata hata diwani moja Pemba na kuzisalimisha diwani 15 Unguja, basi uchaguzi huo nao uendelee ilhali tunajua hakuna chama chengine chochote katika vinavyoshawishiwa kushiriki vyenye uwezo wa kushinda, kisha hali iwe ya kawaida tu?

Hivi viongozi wa Tume wanataka kweli wakumbukwe na watiwe kwenye historia kwa hili? Huwa mimi wallahi najiuliza ni kutanzwa au kweli hii ni hiari? Unapata hisia ngumu kuona undani wa jambo hili na kweli ni Mungu tu ndio ajueae.Msajili wa Vyama vya Siasa anaacha ofisi yake ya kiyoyozi Dar es salaama kushuka Zanzibar kuvishawishi vyama vya siasa vishiriki uchaguzi huu. Mimi nimekuwa nikijiuliza jee hili linakuza au lina viza demokrasia jamani? Kukishawishi chama kishiriki katika hali kama hii ndiko kutatufikisha kweli tuendako?
Kisha kwa Tume kuwashawishi wetu wapige kura nimekuwa nikijiuliza ili iwe nini? Kwani kupiga kura kwa sheria zetu ni lazima si ni hiari? Isipokuwa kubwa tu mtu atatupa demokrasia yake, ambayo kwa wengine tayari imo katika debe la taka tokea Oktoba 25 na walioitia humo ni Tume yenyewe.
Nafikiria siku ya kupiga kura itakuwaje na siku ya pili yake kwa wafanyakazi wa Serikali ambao tunaambiwa wanashuritishwa itakuwaje? Nafikiria bararani ukionekana huna wino kwenye kidole alama kuu ya kupiga kura itakuaje?
Nafikiria uchaguzi ambao hauna waangalizi wala mawakala hasa kwa vyama ambavyo vinasema havitaki kushiriki uchaguzi huo hali itakuwaje? Nani atasadikisha kura zao, ambazo hata hivyo itakuwa wapenzi wao hawaendi kupiga, na zile zitazoonekana zimepigwa kwao zinakuwaje?
Na katika hali hiyo yote, ili tu matokeo ya Urais yapatikane nchi kutumia tshs billion 7.5 ikiwa ni miezi minne tu tokea kutumia tshs bilioni 7.4 ni kwa faida hiyo tu? Kutumia billion 15 shillingi karibu ili upatikane Urais kwa mgombea wa CCM ni jambo la maana na adilifu kwa Zanzibar?
Naamini tutaingia katika rekodi za dunia kama nchi, lakini pia Tume nayo itaingia katika rekodi ya dunia kwa yanapitikana nchini mwetu mwetu wakati huu. Kubwa najiuliza na bado sijapata jawabu baada ya Tume kusema hakuna chama ambacho kitaruhusiwa kujitoa hata baada ya CUF kusema wazi hakitashiriki.
Najiuliza CUF itapata diwani ngapi Unguja na majimbo mangapi Unguja? Pia CUF itapata majimbo mangapi Pemba na diwani ngapi? Lakini kubwa lao Mgombea wa CCM Dk Ali Muhammed Shein atapata kura ngapi ili awe mshindi wa marudio dhidi ya Mgombea wa CUF Maalim Seif Shariff Hamad.
Pengine hesabu ya CCM si ngumu kujua. Ni idadi itayotosha kupata ushindi diwani, Barazani na Urais kwa raha zao, kama watu wasemavyo. Lakini bila ya shaka kwa kupitia kisanduku cha kura ambacho pamoja na yote haya kitakuwa halali, kwa kufanywa.
Jarida moja maarufu la nje lilitwalo Readers Digest liliwahi kuandika “ Anything that is not happening in the world can happen in Zanzibar” yaani kwa maana ya “Jambo lolote ambalo haliwezi kutokea duniani kwengine linaweza kutokea Zanzibar” na hili ni mojawapo

No comments: