Friday, 19 February 2016

MAGUFULI NI MATEKA WA CHAMA KWA ZANZIBAR

Kama unafuatilia jinsi maamuzi na matendo ya siku kwa siku ya Rais John Pombe Magufuli wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ‘yanavyoiumba’ Tanzania aitakayo kwa kuiumbua Tanzania aliyowachiwa na mtangulizi wake, Jakaya Khalfani Mrisho Kikwete, unatoka na jawabu moja tu – kwamba Rais Magufuli anaamini kuwa Kikwete alikuwa amekosea kwa kila jambo kwa muda wa miaka kumi ya utawala wake, isipokuwa kwenye suala la Zanzibar tu.

Uamuzi wa mwisho kabisa wa Rais Magufuli ni wa Alkhamis (Februari 18), ambapo aliamuru kufutwa kwa vibali vyote vya kuingiza sukari nchini akisema uingizaji huo unaathiri viwanda vya ndani na uzalishaji ambao ungelikuwa na manufaa zaidi kwa taifa. Kwamba sukari imekuwa ikiingizwa kutoka mataifa ya nje na hivyo kuligharimu taifa fedha za kigeni, ilhali nchi ina uwezo wa kutosha wa kuzalisha na kusambaza sukari na pengine hata nje ya mipaka yake, kilikuwa kilio cha muda mrefu cha kambi ya upinzani, hasa kupitia kwa aliyekuwa Mwenyekiti ya Udhibiti wa Hisabu za Serikali Bungeni, Zitto Kabwe.

Haina haja ya kuyataja yale yanayoitwa majipu yaliyotumbuliwa na yanayoendelea kutumbuliwa kwenye maeneo mengine – bandarini, nishati, reli, elimu, afya na kadhalika na kadhalika. Kuanzia Waziri Mkuu hadi mawaziri wengine na manaibu wake, wote wamejifunga vibwebwe kwa ziara ya kushitukizia (lakini zinazoandamana na mkururo wa wapigapicha na maripota), orodha isiyosomeka ya fukuzafukuza na maamuzi yasiyo idadi ya zimamoto. Nasikia hilo limeshuka hata kwa wakuu wa mikoa na wilaya.
Mkuu wa wilaya ya Iringa akimbeba mwandishi ili apate kupigwa picha ziwekwe mitandaoni.

Akijitetea juu ya staili hii ya utawala, mwenyewe Rais Magufuli aliwaonya wakosoaji wake kuwa wasimuone mwendawazimu, bali yeye yuko timamu, ila ameikuta nchi ikiwa imeoza naye anataka lazima iende mbele “na itakwenda tu.”


Kwamba Tanzania imeoza (au kwa usahihi zaidi, watendaji kwenye serikali ya Tanzania wameoza) kwa ufisadi wa kila aina, ni jambo linalofahamika na hata kuzoeleka, kiasi cha kwamba ndiyo mtindo wa kawaida. Jinsi ufisadi ulivyozama kwenye damu, basi afisa wa shirika la umma au idara ya serikali huonekana mzembe sana machoni pa wenziwe ikiwa kwa muda mfupi anaokaa kwenye ofisi hiyo ya umma hajaweza kujijengea himaya ya kiuchumi na ukwasi wa kifedha. Mwizi, kwa hivyo, ndiye shujaa, na muadilifu ndiye bwege, na bado ikawa inaaminishwa kuwa “nchi inakwenda mbele tu.”

Chama cha Mapinduzi (CCM), ambacho kimeitawala nchi kwa zaidi ya nusu karne (kikianzia na kuwa TANU kwa Tanganyika na ASP kwa Zanzibar), kimejenga jamii inayoishi na kuogelea kwenye ufisadi. Jamii inayoabudu mafanikio kwa njia ya mkato na inayochukia misingi ya uadilifu, uwajibikaji na haki. Matokeo yake, Tanzania iliyojaaliwa kila neema ya ardhini na baharini, ni miongoni mwa nchi masikini kabisa duniani. Magufuli anasema umasikini huu hauna maelezo yoyote zaidi ya ukorofi wa walio kwenye nafasi za kutengeneza uchumi wa nchi, na hivyo ameamua kupambana nao “na nchi itakwenda tu.”

Miradi na mirija mingi ambayo utawala wake inadhani kwamba inavujisha fedha za walipakodi na kuziingiza kwenye makasha ya matajiri wachache sasa inakaguliwa upya na mengine kuahirishwa, kufungwa au kuhamishiwa. Miongoni mwao ni bandari ya Bagamoyo, nyumbani kwa mtangulizi wake, Jakaya Kikwete. Wateule kwenye nafasi za utendaji na uwakilishi, ambao wengine walijipatia nafasi hizo miezi michache kabla ya Kikwete kuondoka madarakani, wamejikuta ama wakipoteza kabisa nafasi kwenye utawala wa Magufuli au wakipelekwa maeneo tafauti na waliyokuwa nayo. Na nchi lazima iende tu.

Kwa hivyo, japokuwa Magufuli amechukuwa takribani nusu na robo ya wanajeshi aliowakuta kwenye kikosi chake – maana hata yeye mwenyewe alikuwa sehemu ya wanajeshi hao hao – staili yake ya kutawala imewaambukiza alioingia nao mstari wa mbele wa mapambano. Mawaziri wale wale ambao chini ya Kikwete walikuwa wenyewe “mizigo”, kwa mujibu wa tathmini ya Katibu Mkuu wa CCM Abdulrahman Kinana, hivi leo wamegeuka kuwa “watumbuaji majipu” wakubwa, akiwemo Waziri Mkuu Kassim Majaaliwa. Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue, ambaye daima alikuwa mwanadiplomasia tu wa Ikulu akifunikwa hata na Salva Rweyemamu, ghafla moja amegeuka kuwa sauti kali ya kutisha ambaye akitokeza mbele ya waandishi wa habari (na hujitokeza mara kwa mara), basi ujuwe kuna “jipu” limeshatumbuliwa.

Kwa ujumla, hadi sasa picha unayoipata ni kuwa katika mengi, Magufuli anajaribu kuchora mstari mwekundu baina ya pale utawala wa mtangulizi wake ulipoishia na pale wake yeye unapoanzia, au angalau anapotaka uanzie. Lakini sio kwenye suala la Zanzibar, ambako mtumbua majipu huyu anayeota kuwa akifika kwa Mungu atachaguliwa kuwa amiri jeshi mkuu wa malaika, ameshindwa kujipambanuwa utafauti wake na watangulizi wake, Kikwete na Benjamin Mkapa.

Kwa la Zanzibar, Magufuli ni mwana-CCM kama walivyo wana-CCM wengine hasa wanapokuwa viongozi wakuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kama ilivyo Marekani, ambapo kubadilisha rais kunaweza kusihusikane kabisa na kubadilika kwa sera ya nje ya taifa hilo, ndivyo ilivyo kwa Tanzania na sera yake ya Muungano kuelekea Zanzibar. Kutoka Mwalimu Julius Nyerere hadi John Pombe Magufuli, Zanzibar ni sehemu inayopaswa kuchukuliwa kama koloni na mshindani ambaye lau panakuwa na nafasi, basi angelizamishwa kwenye Bahari ya Hindi asionekane tena. Lakini kwa kuwa hakuna uwezekano huo, basi kinachopaswa kufanyika ni kuidhibiti kwa nguvu zote za kijeshi na kisiasa kusudi isifurukute, isitukutike.

Kama alivyofanya Mkapa kwa kumimina majeshi na vifaru mwaka 2000 na baadaye 2005 kuwazuwia Wazanzibari kufanya maamuzi juu ya khatima ya nchi yao, ndivyo alivyofanya Kikwete mwaka 2015 na anavyofanya Magufuli hivi leo. Hoja kuu ni kulinda Mapinduzi na kuimarisha Muungano dhidi ya wanaoleta ‘fyokofyoko’, neno ambalo kwa Kiswahili cha Kizanzibari ni matusi ya kitandani (Waswahili husema fyokonyoko). Kwa watawala wa Tanganyika, maana halisi ya kulinda Mapinduzi na kuimarisha Muungano ni kuzuia haki ya Zanzibar kujitawala na kujiamulia mambo yake yenyewe.

Kwao wao, Zanzibar inapaswa kuwa chini ya miguu yao milele, maana kinyume chake ni kuhatarisha siasa za mtawala, ambacho ni kitu kinachowaunganisha wote waliokikalia kiti cha enzi cha Magogoni kwenye kapu moja. Hivyo, Rais Magufuli anaweza kumuona Kikwete alikosea kwenye mradi wa Bandari ya Bagamoyo, anaweza kumuona hakuwa makini kwenye vibali vya sukari, akamuumbua kwenye usimamizi wa bandari, na mengine kadhaa wa kadha yaliyopo na yajayo, lakini kamwe hataweza kumuona alivurunda kwenye “Zanzibar Project”.  Na kwenye hilo, atamsitiri uso wake daima milele.

No comments: