Sunday 7 February 2016

POLISI ZANZIBAR WAFUMBUIA MACHO UWEPO NA HUJUMA ZA MAZOMBI SASA KUTUNGULIWA KWA MISHALE YA KIMASAI ILI UTAMBULISHO WAO UPATIKANE.

Watu wasiojulikana wanaoingia mitaani na kupiga wananchi katika maeneo mbalimbali ya Unguja, Zanzibar maarufu kama ‘mazombi’, wameendelea kuvitesa Visiwa vya Unguja, huku Jeshi la Polisi likisema halina taarifa zao.

Watu hao wanaojifunika soksi usoni, wanadaiwa kutumia silaha za moto na jadi kujeruhi, kupiga watu mbalimbali hasa katika maeneo ya Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja.

Mitaa inayotajwa kuathiriwa na mazombi hao ni Tomondo, Sarayevo, Darajabovu, Msumbiji, Magogoni, Amani Kwa -Mabata, Mtoni, Bububu, Sharifu Msa, Kihinani, Kinuni na Welezo.

Hata hivyo, Kamishna wa Polisi Zanzibar, Hamdan Omari alisema suala hilo pia linawapa tabu kwa sababu wanasikia tu kupitia watu na vyombo vya habari lakini hawajawahi kupata taarifa rasmi.

Kuhusu watu kuumizwa na kupigwa na mazombi hao, alisema wanasikia na wanatamani mmoja wao aende kutoa taarifa ili iwe rahisi kwao kulifanyia kazi kuliko kusikia juujuu bila kuwa na cha kushika.

“Kama kuna suala linatusumbua ni hili la mazombi. Mwananchi mtusaidie kufikisha ujumbe huu, yeyote atakayedhuriwa na hao watu aje kutoa taarifa polisi au apige simu namba za usalama akiwa eneo la tukio ili iwe rahisi kuanza kazi ya kuwasaka wahalifu hao, hatuwezi kushughulikia kesi bila kuwa na ushahidi,” alisema Kamishna Omari.

Wakati kamishna huyo wa polisi akisema hayo, mkazi wa Bububu, Maalimu Rashid Abdalla alisema mwanzoni waliwachukulia mazombi kama mamluki hasa katika chaguzi tofauti na sehemu zao wanakoishi, kumbe hali ni tofauti.

“Mimi nilishuhudia mamluki hao katika uchaguzi mdogo wa Mwakilishi wa Jimbo la Bububu Agosti 16, 2012 walipokuja na gari aina ya pick-up na kupiga risasi ovyo hewani kuwatawanya watu waliokuwa wakipiga kura wakiwa wamefunika nyuso kwa vitambaa ili wasionekane,” alisema.

Mkazi wa Sharifu Msa, Bakari Juma alisema amewahi kuwaona mazombi akisema ni makundi ya vijana wapatao 80 ambao hufunika nyuso kwa soksi, wanatumia magari yanayobandikwa namba baadhi ya vikosi vya SMZ ‘pick-up’, wana bunduki, mapanga, mikuki, mashoka na kila aina ya silaha.

“Mnaona kazi hii, mimi nimeponea chupuchupu siku ile ya uchaguzi, mazombi walipoingia mitaani pale Mtoni tukiwa tumekaa ofisini wakatuvamia,” alisema kijana huyo, huku akionyesha gamba la risasi alilodai ni miongoni mwa yaliyotawanywa na mazombi mtaani kwao Oktoba 25, mwaka jana.

Mapema mwaka huu, Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano wa CUF, Ismail Jussa Ladhu alilaani vitendo vinavyodaiwa kufanywa na mazombi hao ikiwamo kuvunja maskani ya ‘Commonwealth’ iliyopo Michenzani na kung’oa bendera ya chama chake iliyokuwa eneo hilo.

‘Mazombi’ wanadaiwa pia kuvamia Kituo cha Redio cha Hits FM cha Migombani, Unguja mwishoni mwa mwaka jana na kusababisha uharibifu mkubwa wa mali na kutishia maisha ya watu waliokuwa studio.

Akisimulia madhara aliyoyapata kutoka kwa watu hao, Juma Yassin anayekaanga chipsi katika eneo la Kibweni, Unguja, alisema alipigwa na kuporwa fedha zaidi ya Sh100,000.

“Walipomaliza kufanya waliyodhamiria walinichukua na kunitupa vichakani kule karibu na kiwanja cha mpira cha Meli Nane (Kihinani, Wilaya ya Magharibi) mpaka nikapoteza fahamu, nilipojitambua nikajiburuza, nikaomba msaada usiku wa manane nikarudishwa,” alisema Yassin.

Watu wengine walioripotiwa kukabiliwa na mazombi usiku wa kuamkia Jumatano ya wiki hii ni waziri mstaafu ambaye pia alikuwa Kamishna wa Mapato Zanzibar, Mohamed Hashim Ismail ambaye katika uchaguzi uliopita, aligombea uwakilishi katika Jimbo la Dimani kupitia CUF.

“Hawa ni maharamia na walaaniwe kwa nguvu zote kwani wanatumiwa kuleta vurugu na hawaitakii mema nchi hii,” alisema Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano wa Umma wa CUF, Salim Bimani.

Suala la mazombi lilitinga pia bungeni na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni alisema Serikali haiyaelewi makundi hayo lakini itafuatilia kwa kina taarifa zao.

Aliyekuwa mgombea mwenza wa urais kwa tiketi ya Chadema na Ukawa, Juma Duni Haji alisema kila siku mazombi hao wanapiga watu, wanatumia magari ya Serikali na hawachukuliwi hatua.

“Waziri wa Mambo ya Ndani anajibu bungeni kwamba hakuna kitu kama hicho, wakati kimekuwa kikiendelea Visiwani, ” alisema Duni.  

Chanzo : Mwananchi

No comments: