Monday 1 February 2016

Zahma ya magufuli Zanzibar

WIKI hii napenda kujadili suala linalohusu zahma ya kisiasa iliyozuka kwa mara nyingine tena Visiwani Zanzibar, baada ya kufanyika uchaguzi uliokosa tamati mwezi Oktoba mwaka jana.
Uchaguzi huo ulinyimwa tamati na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Salim Jecha pale alipotangaza kwamba anaufuta kutokana na kuwapo kwa vitendo vya kukosa uaminifu katika baadhi ya maeneo ya visiwa hivyo, lakini hususan akielekea kuwalaumu viongozi na wafuasi wa Chama Cha wananchi (CUF).
Jecha sasa ametangaza tarehe ya uchaguzi mpya, Machi 20, na kusema kwamba wagombea watakuwa ni wale wale waliogombea mwezi Oktoba. CUF, kwa upande wao wamekwisha kutangaza kwamba hawatashiriki uchaguzi huo kwa maelezo kwamba uchaguzi ulikwisha kufanyika na kilichobaki sasa ni kwa ZEC kutangaza matokeo.
Na Jenerali Ulimwengu
Na Jenerali Ulimwengu
Ugumu wa hali ya kisiasa visiwani unazidi kujionyesha dhahiri kutokana na CUF kudai kwamba inavyo vielelezo vya matokeo kutoka katika vituo vyote vya kupiga kura, na kwamba ni maelezo hayo hayo yaliyomsaidia mgombea wake, Seif Sharif Hamad, kufanya ankara na kutangaza kwamba alishinda uchaguzi huo.
Hali hii ndiyo huitwa kwa Kiingereza ‘impasse’ au ‘deadlock’. Kwa Kiswahili kisichokuwa rasmi naweza kuuita ‘mkwamo’. Mkwamo huu ni mkubwa na wala haufai kupuuzwa na wakuu wa kisiasa na kiutawala nchini, hususan Rais John Pombe Magufuli. Alipokuwa akiomba kura za Watanzania aliwaahidi kwamba angeshughulikia matatizo ya Jamhuri nzima, na si ya upande mmoja wa Jamhuri.
Dk. Magufuli ni Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, kazi ambayo ameianza kwa ari kubwa na kwa kuchukua hatua ambazo zimewapa Watanzania wengi matumaini makubwa na imani kwake. Binafsi nimekwisha kumpongeza kupitia safu hii, na namuomba asitetereke katika hatua zake anazozichukua dhidi ya maadui wa maendeleo ya nchi yetu.

Lakini kuna jambo ambalo sitachoka kumkumbusha Rais Magufuli iwapo ananisoma, nalo ni kwamba amerithishwa nchi iliyooza kuzidi kuoza. Kwa bahati mbaya katika mambo yote anayofanya tangu achukue madaraka, hakuna jipya alilobuni. Amekuwa akishughulikia viporo vya wenzake waliomtangulia na waliokuwa wamezembea katika wajibu wao kiasi kwamba katika maeneo mengi serikali ilikuwa imefutika.
Hatua za kuwakamata wakwepaji wa kodi si dhana mpya, lakini ilikuwa imesahauliwa kabisa kwa sababu walikuwapo wakubwa walionufaika na ukwepaji huo wa kodi. Kukataza misafara kama ya mahujaji katika safari za kiserikali si jambo geni.
Niliwahi kufanya kazi katika Serikali ya Mheshimiwa Rais A.H Mwinyi, nikiwa ofisa wa ngazi ya juu wizarani, na nakumbuka jinsi Waziri Mkuu Joseph Warioba alivyokuwa akifyeka majina ya watu wasio muhimu katika safari za serikali, ikiwa ni pamoja na majina ya mawaziri. Nakumbuka angalau siku moja Warioba alipokata jina la waziri aliyetaka kuongoza kikundi cha Taarab kwenda Ngazija. Si kazi ya waziri.
Lakini katika utawala wakuruhusu ukwepaji wa kodi na safari za “Masantula” haya mambo yalionekana kama ya kawaida. Miezi michache iliyopita niliandika juu ya misafara ya makumi ya mahujaji wazururaji wa kiserikali ninayokutana nayo ughaibuni wakati ambapo wajumbe wanne au watano wangetosha. Ninapoandika makala hii niko Addis Ababa na ninaona mabadiliko.
Niliandika pia kwamba madaraja ya usafiri wa mahujaji hawa ni ghali mno, na kwamba hata pale Umoja wa Mataifa uko tayari kuwasafirisha, maofisa wa Tanzania wanakataa ufadhili huo.
Yote haya yanadhihirisha ukweli kwamba hata pale wakuu serikalini wanapozijua sheria, kanuni na taratibu, iwapo watapewa mwanya hata kidogo, watazivunja na halafu wataufanya uvunjaji huo wa sheria uwe ndio utaratibu mpya. Hatimaye watadai hizo anasa walizojipangia kana kwamba ni haki yao.Ukiwasema wanajibu kwamba ni watu wenye wivu. Mimi sina wivu katika hili. Nimesafiri kabla baadhi ya hawa maofisa hawajazaliwa (na naendelea), na nimekwenda karibu kila kona ya dunia, tena nikiwa kijana mdogo na mwenye uwezo, si tu wa kuburudika ipasavyo, bali pia uwezo mkubwa wa kujifunza kutoka kwa wenzetu. Mojawapo nililojifunza ni kwamba hata serikali za nchi za matajiri hazifanyi anasa kama serikali yetu.Ndiyo maana napenda kusisitiza kwamba kila kinachofanyika kisifanyike kwa kukurupuka ama kwa kutegemea nishati binafsi ya utendaji kazi ya mkuu wa nchi. Nina maana kwamba kila jambo ovu tunalolitambua kama ovu halina budi kuwekewa utaratibu wa kulishughulikia, utaratibu utakaotumika katika ngazi zote za utawala bila kuwaruhusu mawaziri, wakuu wa wilaya au wakuu wa mikoa kujifanyia kila mtu anavyojihisi. Na jambo jema sawia.
Kufanya kazi kwa kufuata taratibu katika maeneo yote kutaleta ufanisi wa kudumu kwa sababu hata pale walipoanzisha utaratibu wakiwa wamekwisha kuondoka, bado misingi yao inabakia ikiongoza matendo ya wakuu wapya wanaowarithi.Pasi na shaka, hilo linatupeleka moja kwa moja katika hoja yangu kuhusu katiba ya nchi, ambayo ndiyo sheria mama inayotawala sheria zote pamoja na taratibu na kanuni. Katiba ikiandikwa kwa weledi na uaminifu (na si kwa uhuni tulioushuhudia Dodoma mwaka jana), itaweka mambo makuu yote wazi, na hatutakuwa na haja ya kukurupuka kila linapotokea jambo kama hili la Zanzibar.Hapa tulipo tumekwama kwa sababu tumezoea kuendesha mambo yetu kienyeji, hata pale ambapo tunajua kwamba tungekuwa na taratibu zinazoeleweka na zilizo wazi, tungepata faida zaidi. Kwa sababu hilo limetushinda, sisi ni watu wa kukurupuka na jipya linaloelekea kutufaa kwa leo lakini hatujui kesho nini kitatokea.
Kwa mfano,miaka mitano iliyopita tulishitukizwa na kitu kilichoitwa “maridhiano” kati ya Rais wa Zanzibar, Amani Karume, na mpinzani wake mkuu Seif Sharif Hamad wa CUF. Hakuna aliyewahi kuona hati ya maridhiano hayo, isipokuwa hao wawili, na pengine Ismail Jussa. Rais Kikwete aliishia kutoa pongezi kwa makubaliano ambayo hakuwa kayasoma.Leo hii inaelekea “maridhiano” hayo hayana maana tena, na hayawezi kuepuka kutokuwa na maana iwapo kati ya watia saini wawili kabakia mmoja na huyo mmoja anasema kashinda uchaguzi na anatakiwa apewe mikoba ya serikali. Hayo ndiyo madhara ya kuendelea na utaratibu wa kutokuwa na utaratibu, na kuwaruhsu watu wazue mizungu inayoonekana kama itawafaa kwa wakati uliopo lakini punde inageuka kuwa mizungu isiyomsaidia yeyote bali inachochea chokochoko kubwa zaidi.
Zanzibar iko ndani ya zahma, na Magufuli hawezi kuikwepa kwa sababu ni jukumu lake, na hilo jukumu aliwaomba Watanzania wamkabidhi yeye ahangaike nalo, na wao wakamwambia “Hilo!” Sasa anatakiwa ahangaike nalo kweli kweli, na asitulie na wala asichoke.Hawezi kuchoka kwa sababu iko mantiki isiyokuwa na huruma kwa yoyote: Tanzania = Tanganyika+Zanzibar. Tanzania—Zanzibar= Tanganyika .Uchaguzi umekamilika Tanganyika katika sehemu zake zote. Serikali imeundwa na inafanya kazi. Uchaguzi wa Zanzibar umekwama. Serikali haijaundwa ingawa kuna watu wanaosema kwamba ile serikali iliyomaliza muda wake mwezi Oktoba ndiyo “serikali halali.”
Hatuna ushahidi wa kisheria kwamba serikali iliyokuwapo mwaka jana bado ni halali, na ikitokea kwamba si halali, basi itakuwa imetenda mambo mengi ambayo kisheria ni batili.TANBIHI: Makala hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza na gazeti la Raia Tanzania, Toleo Na. 442 la tarehe 27 Januari 2016. Jenerali Ulimwengu anapatikana kwa anwani ya barua-pepe: ulimwengu@jenerali.com au kwenye mtandao wake: www.jenerali.com

No comments: