Thursday 31 March 2016

Hoja ya Kitila Mkumbo haina mashiko.

Upinzani wa aina ya prof Kitila   Unapodhihaki demokrasia kwa goli la mkono.

Hoja ya msingi ipo hapa, wenzetu hutoa misaada kutokana na mapato ya walipa kodi wao. Na msingi mkubwa wa misaada ni uwajibikaji wa serikali husika kwa wananchi wao kwamba misaada inayotolewa inaendana na misingi ya haki na demokrasia. Sawa ni utu unaowaongoza katika kuchagua nani wa kuwapa lakini tusisahau kwa serjkali yoyote ya nje tathmini zao kwanza zikidhi haja ya utoaji wa fedha hizo za walipa kodi wao. Sasa leo serikali katili kwa wananchi wake, isio jali haki, inayoendeleza ubabe na kutothamini demokrasia itazuiwa kwa kuendelea kupatiwa fedha za kujikimu na kuongeza matumizi ya nguvu kwa wanyonge? Hivi unafikiri kamati zao za bunge zinazopitia misaada hii itaziweka vipi serikali husika katika uwajibikaji hasa kwa matumizi ya fedha za walipa kodi wao kwa kuzigawa kama misaada kwa nchi zinazoelekea katika majokho ya uimla?

Mimi nashangaa sana wenzetu wanapopiga kelele kwa kukosa misaada kwa jambo la msingi ambalo watawala ndio wa kulaumiwa. Wamefuta uchaguzi halali na kupanga uchaguzi mpya wenye ushahidi mkubwa wa matokeo ya kupanga panga, wakapiga watu na kuwaweka ndani, wakawatia wananchi kiwewe na kuwatishia kwa nguvu za vifaru ambavyo ni sehemu pia ya misaada kutoka kwa wafadhili, wakafuja misingi ya haki kama mahakama na vyombo vya usalama, wakateka waandishi wa habari na kuwahujumu,halafu bado nchi wafadhili zitazitama tawala kama hizi kuwa na utu wa kupokea misaada inayowapa nguvu zaidi ya kuumiza wananchi wao wenyewe? Fikiri pesa za uchaguzi wa marudio zilitoka wapi? Au yale magari yenye namba za mashirika ya wahisani yaliotumika kumbeba Makamo Mwenyekiti wa Tume kuzuia kutangazwa kwa mshindi wa October zinabeba jukumu gani kwa wahisani katika ubakwaji wa demokrasia?

Nakubaliana kabisa kwamba hili si jambo jema hasa kwa wanyonge, lakini kwa serikali husika utu pekee hautoshi hasa ikiwa kuna ushahidi mkubwa wa fedha hizo kutumika kuendeleza utawala wa mabavu kwa wenye mawazo tafauti na kutokuwa na faida kwa wanyonge waliowengi. Hivi jitazame mwenyewe jee utaweza kutoa fedha za msaada kwa mlevi alie nje ya maduka akiomba omba ukijuwa hasa kwamba msaada wako utakwenda kinyume na principle za utoaji?

Sasa tujiulize lengo la kujitegemea ni lipi? Kwamba tujitegemee ili tuwe na nguvu zaidi za kuwanyima wanyonge haki ya kuchaguwa kiongozi wao? Au tujitegemee kwa mantiki ya kuwasaidia wanyonge waweze kusimama na haki zao ikiwamo haki ya kufanya mabadiliko katika uongozi wenye maslahi nao? Katika yote haya tusiwalaumu wanaotoa misaada wakiwajibika kwa wananchi wao na fedha za walipa kodi wao kwa kuwa tu sisi hatuna utamaduni wa kuthamini fedha za walipa kodi wetu. Bali tuzilaumu tawala zetu wenyewe ziliokosa insaf kiasi kwamba kwa wazi wazi hutamka kushinda hata kwa goli la mkono.

Tawala zetu zimefurutu ada, hasa katika masuala ya haki. Niliuliza laiti hizi sheria kandamizi kama sheria ya mitandao ingelitungwa na wakoloni tungekuwa na uzalendo wa kutetea kama tulio na sasa? Au hizi chaguzi ambazo mshindi anapokonywa wazi wazi kwa ubabe huku watawala wakidhihaki demokrasia kwa goli la mkono na kutotoa serikali kwa karatasi tuseme zinabeba huo umoja na uzalendo wa kitaifa?

Nimalizie kwa kuuliza jee uzalendo wa kitaifa ulikuwa wapi kukemea uvunjwaji wa haki za binaadamu visiwani katika kipindi cha uchaguzi wa marudio kutoka kwa amri ya mkuu wa nchi kwa aliowaita wapenda haki "fyokofyoko"? Au huo umoja wa kizalendo hauwezi kuwa na maslahi mapana zaidi kwa wananchi kwa kuungana pamoja kupinga dhulma ya watawala katika misingi ya haki? Iweje hii kuwa ni vita ya nchi dhidi ya wahisani na isiwe ni vita ya umoja wa wananchi na wahisani dhidi ya tawala za kibabe hasa Zanzibar ambako demokrasia ilichezewa na haki za wananchi zikawekwa kapuni? Hivi tunajuwa wangapi hadi hii leo wanyonge wako ndani? Kiongozi anaejisifia wanyonge kunyia ndooni kweli anakidhi haja ya kupewa fedha za misaada katika uongozi wa mabavu? Kiongozi anaewaita wengine mabwege kwa kuwapora haki yao ya kuchagua anaingia katika gurupu la utu na umoja wa kizalendo? Hivi hatuoni haya au kwa sababu yanaathari kwa koloni Zanzibar pekee?

Sikubaliani na Profesa Mkumbo anapotaka kuamsha hamasa ya wananchi dhidi ya wahisani ambao wanawajibika kwanza kwa wananchi wao katika matumizi ya pesa za walipa kodi wao. Sikubaliani kabisa na dhana ya kujitegemea ili tuweze kuzidisha ubabe kwa wanyonge, na wala haiingii akilini kusema hii ni vita ya nchi nzima katika mantik ya kunyimwa misaada na wahisani bali ni vita ya wananchi dhidi ya watawala wababe wasiothamini misingi ya demokrasia na haki za binaadamu.

Haya yasiamshe ari tu ya uzalendo na fikra ya kujitegemea bali pia iamshe hamasa ya kusimamisha haki katika uhuru usioingiliwa kwa vile lengo la kuzuiwa kwa misaada ni kushurtisha misingi ya demokrasia sio kuwakomoa wanyonge. Hivi tunafikiri kuzuiwa kwa viza kwa viongozi ndio njia pekee ya kuhamasisha ukuaji wa demokrasia? Tukumbuke mbaya wa haya ni watawala waliofuta chaguzi, wakapiga watu, wakapanga chaguzi na kupika matokeo ya kuwaweka madarakani milele. Dhambi ya dhulma hii ni kubwa kwa wanyonge kwa kukosa imani kabisa na misingi ya haki ya kuchagua viongozi wenye ridhaa zao wananchi. Na baya zaidi kuendelea kwa ubabe wa aina hii ni machafuko siku za mbele na vifo kwa wanyonge kwa kutazama mabadiliko nje ya misigi ya kidemokrasia.

Tatizo si kuzuia kwa misaada bali sababu za kuzuiwa kwake. Kiburi cha viongozi wa Zanzibar ni kwa sababu ya vifaru na mizinga kutoka upande wa pili. Kama tulivyopinga ukoloni wa makaburu kwa waafrika kusini basi tupinge kwa nguvu zote ukoloni wa CCM kwa Zanzibar.

No comments: