Thursday, 5 May 2016

Makamba anachekesha na hoja dhaifu. Akumbuke ni tume ya Warioba ndio iliopunguza viti vya wabunge wa muungano lakini ni yeye na genge lake lililong'ang'ania wingi wa wabunge wa sasa. Miongoni mwa wajumbe walioidhinisha udogo wa wabunge wa muungano kufikia ishirini kutoka zanzibar ni Kamishna Ali Saleh ambae sasa ni mbunge wa Malindi. Kama anauchukia muungano na kuupenda ubunge basi asingeridhia kupunguzwa wabunge wa Zanzibar kufikia ishirini. Hoja ya kitoto.

Mfano mzuri atazame Scotland na SNP, ambayo kwa uwazi kabisa inataka kujitenga katika muungano wa UK kiasi kwamba wabunge wote wa Scotland 59 kasoro mmoja ni wa chama cha SNP wanaoshiriki katika House of Common. Tuseme nao wanaupenda ubunge huku wakiuchukia muungano? Hoja ya kitoto na iliojengwa kifitina, atazame wabunge wa UKIP katika EU parliament ambao wako huko kuupinga kabisa kwa uwazi muungano wa ulaya, jee tuseme wanaupenda ubunge na kuukata muungano au wamefika kuwakilisha maoni ya wananchi wao waliowachagua wakijuwa ajenda walioipiga debe na kuchaguliwa nayo? Atazame Sinn Feinn waliozuia wabunge wao kushiriki bunge la muungano, jee wamefanikiwa ajenda ya kujiunga na Jamhuri ya Ireland Au SNP ilioweza hata kufikia kuitisha referendum wakiwa na wabunge?

Logic ya kitoto kabisa ya Makamba yenye msingi tu wa kufitini na kufurahisha barza. Tuje kwenye historia hata ASP ilikuwa na uwakilishi katika baraza la sheria la Mkoloni huku wakiipinga serikali ya kikoloni, jee tuseme nao waliupenda uwakilishi katika serikali ya mkoloni? Mwalimu na Tanu jee? Atazame "struggle" dhidi ya ukoloni na ushiriki wa upinzani katika vyombo vya utungaji sheria na madhumuni ya ushiriki wao. Leo hii wananchi wanaelewa na hata mkuu wa nchi anafanya kazi kwa sababu ya upinzani imara bungeni unavyofanya kazi ya kuyaonyesha madudu ya serikali ikiwamo wizara yake Makamba. Ajibu hoja badala ya kutafuna ulimi na dharau, tuna haki katika kushiriki katika bunge linaloweza kubadili mfumo wa muungano badala huu butu usio na dira.

Ushiriki wa wazanzibari (wenye muono tafauti na mfumo huu butu wa muungano) kwenye bunge ni haki yetu kama ulivyo ushiriki wa SNP katika bunge la UK, au la UKIP katika EU au hata ushiriki wa marehem Mtikila katika bunge la Katiba alieupinga muungano wazi wazi, jee yeye ana haki zaidi ya ubunge kuliko mzanzibari? Makamba ajibu hoja ya namna gani jeshi la muungano limekuwa likitumika katika kukandamiza demokrasia badala ya "cheap politics" kwa msema kweli aliechaguliwa na wananchi kupinga udhalimu wa mfumo butu kuwa ni mpenda ubunge asiependa muungano. Ajibu  hoja za khofu ya wingi wa waislam Zanzibar kama ambavyo Lukuvi na Sita walivyotoka wazi kujieleza.

Ni huyu huyu Makamba aliekuwa mbele kuwaomba CUF kushiriki chaguzi hata wa 299999, leo anauliza inakuwaje kuupenda ubunge unaopatikana kwa chaguzi na kuukata mfumo wa muungano unaolindwa kwa jeshi? Ubunge wa hiyari dhidi ya mfumo wa muungano wa nguvu za jeshi? Asiishie katika ushiriki wetu katika bunge tu, atazame urais wa muungano, jee atathubutu kuuliza tunashiriki vipi wakati tuna muono tafauti katika mfumo wa muungano? Ajibu hoja za msingi, badala ya kujikita katika utoto na upotoshaji.

Akumbuke nafasi ya Mwalim akiwa mtetezi wa uhuru, nafasi ya Mzee Karume akiwa mpinga ukoloni, na atazame historia za wapinga ukoloni katika mabunge ya serikali za kikoloni, atazame nchi tunazofanana nazo na namna gani ushiriki wa wapinzani katika bunge unavyosukuma mbele dhana nzima ya ajenda zao. Turudi katika hoja, haki kwanza na mabadiliko ya mfumo wa muungano wa haki, heshima, usawa na ridhaa ya wananchi badala ya vifaru, mizinga na vitisho vya jeshi.By Farrel Jn

No comments: