Wednesday 1 June 2016

Maalim Seif asema yeye ndio Rais wa Zanzibar na Dk Shein ni Rais wa Jecha


KATIBU Mkuu Wa Chama Cha Wananchi wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad alimeliyambia jeshi la polisi kuwa yeye ndie Rais wa wananchi wa Zanzibar aliyechaguliwa Octoba 25 katika Uchaguzi Mkuu na Dk Ali Mohamed Shein ni rais wa Tume ya uchaguzi Zanzibar. Maalim Seif aliyasema hayo wakati alipohojiwa na jeshi la polisi jana na kutaka ajieleze kwa nini hamtambui Dk Shein kuwa ndio rais na badala yake anajitangaza kuwa yeye ndio Rais wa Zanzibar. Katika Mahojiano hayo yaliyochukuwa muda wa masaa matatu kuanzia saa 3:30 hadi saa 6:20 baina yake na jopo la maafisa wa upelelezi wa jeshi hilo, Maalim Seif bila ya hofu wala woga aliliambia jeshi hilo kuwa yeye ndie rais wa Zanzibar na Dk Shein ni Dikteta.
Mwanasheria wake Awadhi  Ali Said aliyeambatana na Maalim Seif katika mahojiano hayo, alisema hicho ndicho alichokiongea Maalim Seif mbele ya maafisa 12 wa upelelzi wa jeshi hilo .
Mahojiano hayo ambayo yalifanyika Makao makuu ya jeshi hilo, huku askari polisi wakiimarisha ulinzi maeneo mbalimbali ya mji wa Zanzibar na kusababisha baadhi ya huduma kusimama kwa muda haswa maeneo ya Mtendeni ambapo ndio makao makuu ya CUF. Awadhi alisema ,Maalim Seif aliulizwa na jeshi la polisi kwanini  hakemei  kitendo cha baadhi ya wananchi na wafuasi wa CUF kumtambua kuwa yeye ndie rais badala ya Dk Shein, aliwajibu kuwa ndio yeye ndie rais na wananchi ndio wanaoamini hivyo kwani  walimchaguwa katika uchaguzi wa octoba 25 mwaka jana na sio Dk Shein.
Alisema pia aliulizwa kuwa amemuita Dk Shein ni Dikteta,Maalim Seif alikiri kuwa ni kweli ni Diktete kwa sababu uchaguzi wa huru na haki uliendeshwa octoba 25 na waangalizi wa ndani na nje wa Uchaguzi huo walithibitsha kuwa uchaguzi, ulikuwa ni huru na haki na yeye ndie aliyekuwa akiongoza katika uchaguzi huo kwa kupata kura nyingi na kumshinda Dk Shein. Awadhi alimnukuu  Maalim Seif alivyokuwa akihojiwa na jeshi hilo katika mahojiano hayo”mimi kama kiongozi wa CUF nasimamia maamuzi ya baraza kuu la chama changu ambayo kutoutambuwa uchaguzi wa marudio wa machi 20 mwaka huu na kuutambuwa uchaguzi wa octoba 25 mwaka jana na kuhakikisha kuwa tunafanya  harakati za kisiasa ili serikali hii iliyopo ambayo imebaka demokrasia haimalizi muda wa miaka mitano”alisema Maalim Seif katika mahojiano hayo.

Aidha Awadhi alisema mahojiano hayo yalichukuiliwa maelezo ya kipolisi yaliyorikodiwa chini ya onyo la kisheria na Maalim Seif kutuhumiwa kwwa makosa ya kufanya uchochezi chini ya kifungu cha 45 sheria ya jinai ya Zanzibar.
Awadhi alieleza kuwa Maalim Seif alitakiwa ajieleze kwanni alifanya  mikutano na maandamano kisiwani Pemba na kuoneshwa  ushahidi wa picha za video za watu waliyojipanga barabarani lakini katibu mkuu huyo, alikanusha na kusema kuwa alikuwa akisherehekewa kama ni kiongozi wa kisiasa na hayakuwa maandamano na baadae alifanya mikutano ya ndani ya kuimarisha chama.
Pia Jeshi hilo lilimtaka ajieleze kutokana na matamshi aliyoyatoa katika mikutano hiyo kwa kutoa matamshi ya  uchechezi ikiwemo kusema DK  Shein hatomaliza muda wake, na alijibu kuwa ni kweli alisema DK Shein aliyoko katika mamlaka ambayo amewekwa na tume ya Uchaguzi hatomaliza miaka mitano ya uongozi .
Maalim Seif aliwahakikishia Maafisa hao wa jeshi la Polisi kuwa yeye  na chama chake cha CUF, hakina dhamira ya kumdhuru  DK Shein wala kuendesha taratibu nyengine zozote nje ya ulingo wa kisiasa bali watahakikisha kuwa Dk Shein atang’oka kupitia harakati za kisiasa.
Naibu Mkurugenzi wa upelelezi na Makosa ya jinai Salum Msangi akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na mahojiano hayo hakutaka kueleza kwa undani mahojiano hayo kati yao na Maalim Seif lakini alisema kuwa wamekamilisha mahojiano hayo na wamemuachia huru kwa dhamana ya watu wawili.
“tumemaliza mahojiano yetu kwa leo na tutakapomuhitaji tena tutamuita tena Maalim Seif na jeshi la polisi tunaendelea na upelelezi wetu na wote tuliowahoji watakaobainika kuwa wanahatia tutawapeleka mahakamani”alisema Msangi.

No comments: