Monday, 29 August 2016

Baraza Kuu la CUF Limewasimamisha Uwanachama Wanachama 11.


 Naibu Katibu Mkuu wa CUF Nassor Ahmed Mazurui akizungumza na wandishi wa Habari  katika Ofisi ya Chama hicho iliyopo Vuga Mjini Zanzibar wa kwanza (kushoto) Mkurugenzi Habari na Mawasiliano wa Chama Salum Bimani na wapili (kulia) Shaweji Mketo, Naibu Mkurugenzi Mipango na Uchaguzi.
Baadhi ya Waandishi wa Habari waliohudhuria mkutano wa Chama cha Wananchi CUF  wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho Nassor Ahmed Mazrui.
Naibu Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa CUF Shaweji Mketo akijibu maswali ya waandishi wa habari katika mkutano wa chama hicho  uliofanyika Ofisini kwao Vuga Mjini Zanzibar.(Picha na Makame Mshenga-Maelezo Zanazibar)
Na.Rahma.Khamis/Kijakazi.Abdallah Maelezo Zanzibar 
Chama cha Wananchi (CUF) kimemfukuza uwanachama Kaimu Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Wazee Shashu Legeye na kuwasimamisha uwanachama wanachama 11  kufukuzwa  baada ya kusababisha vurugu la Mkutano Mkuu uliofanyika  Agost 21 katika Ukumbi wa Ubungo Plaza Dar-essalam.

Akizungumza na waandishi wa habari huko Ofisini kwake Vuga Naibu Katibu Mkuu wa CUF Nassor Ahmed Mazurui amesema Baraza kuu la Uongozi la Taifa la Chama kimeamua kuchukua hatua za kinidhamu kwa Viongozi na wanachama waliohusika kuchochea vurugu hizo.

Amesema kuwa hatua hiyo imekuja baada ya wanachama hao kutokuwa na uaminifu kwa chama na kukubali kurubuniwa na baadhi ya vyama vya siasa na kutumiliwa kufanya vurugu.

Aliwataja wanachama  waliosimamishwa  kuwa ni  Prof. Ibrahim  Haruna Lipumba, Magdalena Sakaya, Abdul Kambaya, Ashura Mustafa, Omar Muhina Masoud,Thomas Malima, Kapasha  H. Kapasha, Maftaha Nachuma,Mohammed  Habibu Mnyaa, Haroub Shamis na Mussa Haji Kombo.  Rukiya Kassim Ahmed na Athumani Henku  wamepewa karipio kali.

Mazrui amesema Baraza Kuu la Taifa la CUF limewateuwa wajumbe wengine wa Kamati  ya Uongozi  wakiwemo  Julius Mtatiro kuwa Mwenyekiti wa CUF,  Katani Ahmed Katani  na Severina Mwijage kuwa Wajumbe .

Aidha Baraza Kuu limewateua  Joran Basange kuwa  Kaimu Naibu Katibu  Mkuu  kwa upande wa Tanzania Bara, Mbarala Maharagande kuwa Kaimu Naibu Mkurugenzi wa Habari Uenezi na Mawasiliano kwa Umma hadi nafasi zitakapojazwa rasmi kwa mujibu wa sheria  ya CUF.

Hata hivyo Naibu Katibu Mkuu  amewahakikishia wanachama na wapenzi wa CUF kuwa  chama bado kipo imara na makini na hakitoyumbishwa kwa hila na njama za wasaliti.

Nae Naibu Mkurugenzi  Mipango na Uchaguzi Sheweji Mketo amesema kuwa wao wanafanyakazi ya siasa kwa kuwakomboa Watanzania  na wamejipanga kuhakikisha  wanachukua Dola uchaguzi wa 2020.

IMETOLEWA NA HABARI MAELEZO ZANZIBAR.

No comments: