MKUTANO Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) umeahirishwa baada ya vurugu kuibuka ukumbini,anaandika Charles William.
Wafuasi wanaoaminika kuwa, ni wale wanaomuhitaji Profesa Ibrahim Lipumba, aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho walivamia ukumbi wa mkutano huo na kusababisha hali tete kwa muda. Hali ililazimu mkutano huo kuahirishwa.
Wafuasi hao waliokuwa nje ya hoteli ya Blue Pearl, mahali uchaguzi ulipokuwa ukiendelea, waliingia kwa nguvu ndani ya ukumbi huo, wakipinga kutangazwa kwa matokeo ya kura zilizodaiwa kupigwa ili kuridhia kujiuzulu kwa Prof. Lipumba.
Hapo awali, mkutano huo uliingia katika mvutano baada ya kuwasili kwa Prof. Lipumba na wafuasi wake kutaka apewe nafasi ya kujieleza na kuulizwa maswali na wajumbe wa mkutano.
Taarifa kutoka ndani ya ukumbi huo zimeeleza kuwa, Julius Mtatiro, Mwenyekiti wa kikao cha uchaguzi huo aliwadhibiti wafuasi hao na kutompa nafasi ya kujieleza Lipumba kwa hoja kuwa, hakuna kipengele cha katiba kinachompa nafasi ya kuhojiwa maswali wala kuzungumza katika mkutano mkuu zaidi ya kusomwa kwa barua yake ya kujiuzulu.
Wajumbe waliotaka Prof. Lipumba kupewa nafasi ya kujieleza na kuulizwa maswali wanadaiwa kukasirishwa na uamuzi huo na hivyo baadhi kususia kupiga kura na kutoka nje.
Wakati wajumbe hao wakitoka wengine walibaki ukumbini na kupiga kura. Masumbuko Joseph Katibu wa CUF wilaya ya Bukombe ni mmoja kati ya wajumbe waliotoka nje na kuvua nguo za CUF na kuzitupa huku akiwambia wanahabari, “sikubaliani na kinachoendelea ukumbini”.
Saa 19:30 usiku ikiwa ni baada ya kura kupigwa, na wajumbe kupewa muda wa mapumziko, Mkutano huo wa CUF ulipaswa kuendelea na matokeo ya kura za uamuzi wa kuridhia kujiuzulu kwa Lipumba au la kutangazwa.
Taarifa kutoka ndani ya ukumbi wa mkutano mkuu zimedai Julius Mtatiro, Mwenyekiti wa kikao cha uchaguzi huo alitangaza matokeo ya kura 476 zilizoridhia kujiuzulu kwa Lipumba na kura 14 zikitaka asijiuzulu na aendelee kukiongoza chama hicho.
Baada ya matokeo haya kutolewa, ndipo wafuasi wa Lipumba waliokuwa nje ya ukumbi walivamia ukumbini na kufanya vurugu kubwa na hatimaye kumlazimu Mtatiro kutangaza kuahirishwa kwa mkutano huo.
“Kwa kuwa kuna kundi la watu ambao siyo wajumbe wa mkutano huu wameingia ukumbini, na wanafanya vurugu. Natangaza kuahirisha mkutano huu mpaka pale tutakapowatangazia tena,” alisema Mtatiro huku wafuasi wa Lipumba waliokuwepo ukumbini hapo wakishangilia.
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, baadhi ya wafuasi hao wa Lipumba walirusha viti na kuwashambulia wajumbe wa mkutano huo hususani wale wa Zanzibar waliokuwa karibu na mlango wa kuingilia na kutokea.
Jeshi la Polisi licha kuwepo katika eneo hilo kwa lengo la kulinda amani na, licha ya baadhi ya askari wake wasio na sare kuingia ndani, hata hivyo hawakudhibiti vurugu hizo mpaka zilipomalizika kwa Lipumba kutoka ukumbini na kusindikizwa kwa kushangiliwa na wafuasi wake.
Baada ya Lipumba kuondoka, magari zaidi ya Jeshi la Polisi yenye askari yaliwasili na hatimaye askari mmoja mwanamama ambaye hakutambulika mara moja, kutoa tangazo la kuwataka watu watawanyike katika eneo hilo.
Mmoja wa viongozi wa CUF makao Makuu, ambaye jina lake limehifadhiwa kwa madai kuwa hana mamlaka ya kuzungumzia uchaguzi huo, ameiambia Mwanahalisi Online kuwa; “wajumbe wanaomuunga mkono Lipumba ni wengi zaidi na siyo 14 kama walivyotangazwa.”
“Usisikilize propaganda, Mtatiro hana uhalali wa kuongoza kikao cha uchaguzi kwa kuwa yeye tu baraza kuu limemjadili kwa kumchafua Prof. Lipumba. Kesho tutatangaza majina ya wajumbe wote wa Mkutano Mkuu wnaomuunga mkono Lipumba na tutataja majina na maeneo wanapotoka na tutaonyesha saini zao za kumtaka Lipumba arejee,” amesema.
No comments:
Post a Comment