Monday 15 August 2016

Kwaheri Jumbe, tunalo la kukumbuka

Mwaka 1975, wakati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere akisusia kushiriki katika mkutano wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) uliokuwa unafanyika nchini Uganda kwa sababu ya tafauti zake na Rais Iddi Amin Dada, Mzee Aboud Jumbe Mwinyi ndiye aliyekuwa mkuu wa nchi ya Zanzibar. Mzee Jumbe hakufurahishea kuingizwa kwa Zanzibar katika mgogoro wa Mwalimu Nyerere na Idd Amin. Hivyo alituma ujumbe maalum kuelekea Uganda na kushiriki katika mkutano huo wa kilele. Miongoni mwa waliokuwa wajumbe ni Mzee Hassan Nassor Moyo. Mwalimu Nyerere alikasirika sana na kitendo cha Zanzibar kutuma ujumbe wakati Tanzania kama taifa ilishasusia. Hapa ni kabla ya kufutwa kwa chama cha Afro-Shiraz Party (ASP) kilichokuwa kikitawala Zanzibar na kabla ya kuzaliwa kwa Chama cha Mapinduzi (CCM) mwaka 1977. Ushahidi huu upo katika mtandao wa WikiLeaks ikionyesha taarifa ya balozi wa wakati huo wa Marekani kwa Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi yake.
Tayari tulikuwa na muungano, lakini wa mambo yake 11 tena katika hatamu za vyama vilivyoongoza Zanzibar na Tanganyika katika mfumo unaofanana na utatu. Maana hapo tulikuwa na serikali mama ya muungano, vyama ndivyo vilivyoshika hatamu, kwa bara TANU na kwa Zanzibar ASP. Mfumo ni ule ule wa serikali mbili lakini katika uangalizi wa vyama tafauti bara na visiwani. Ni mfumo wa utatu, kwa vile hatamu za nchi zilibebwa na ASP na TANU. Uwepo wa muungano ulikuwa chini ya uangalizi na makubaliano ya vyama hivyo. Na ndio maana Mzee Jumbe kwa kipindi hiki akawa na uwezo wa kufanya lile ambalo lilikuwa na maslahi ya Zanzibar kwa muongozo wa ASP. Serikali ya Zanzibar chini ya hatamu za ASP na Tanganyika kwa TANU, huku ya muungano ikitegemea ridhaa ya vyama husika, utatu ulioakisi umbili wakati ule.
Na Foum Kimara
Na Foum Kimara
Tulipofuta ASP, na hatamu za uongozi zikabebwa na chama kipya CCM, hapo ndipo koti liliposhonewa vifungo. Maana nidham sasa ikafuata kwanza utukufu wa chama, na huko kulikuwa na mkuu mmoja, nae ni Mwalim. Ilimchukuwa miaka 13 mpaka alipoweza kwa njia ya mzunguko kuhakikisha kiongozi wa Zanzibar hatakuja kwa ridhaa ya wazanzibari bali kwa maslahi mapana ya chama chake. Tulipoimba kwaheri ASP mama, tukaiaga pia Zanzibar ikiwa mshirika sawa katika muungano, ikiwa nchi ya kiafrika ilioamua kubeba uafrika kwa nia njema na zaidi ikawa ndio mwanzo wa istifham kubwa na madai ya mabadiliko ya mfumo wa muungano.

Mwalim ndipo alipothubutu kutamka kwa uwazi dira ya Chama tawala katika mfumo wa chama kimoja kwamba “Dira ya CCM ni mbili kuelekea moja” kwa vile hakukuwa na ASP iliopima mengi kwa maslahi ya Zanzibar kama mshirika wa muungano. Ilibaki minong’ono kutoka Kisiwandui, kwa vile kulikuwa na fundisho tosha la Mzee Jumbe unapopingana na azma ya Mwalim pale maslahi yake kwa Zanzibar unapoyapindua. Ilichukuwa miaka 28 mpaka kwa uwazi kabisa ikatoka kauli ya “usitikise kibiriti kilichojaa”. Kauli hii ilikuja kwa sababu ya miaka 27 ya kubururwa na umwalimu katika mfumo wa muungano uliokuwa hauna usawa, haki na heshima.
Isitoshe kwamba bado Rais wa Zanzibar aliweza kupokea ujumbe wa viongozi tafauti kwa ile kofia ya umakamo wa Rais wa muungano, hili nalo likaanza kuwa tatizo katika dira ya mwalim ya mbili kuelekea moja. Ikatafutwa sababu kwamba ati upinzani unaweza kushika madaraka Zanzibar na kujengewa khofu ikafika hadi tukakubali kuifuta heshima ya mwisho ya Rais wa Zanzibar kimataifa, tukaiondosha kofia ya umakamo wa Rais, na matokeo yake ndio adhara iliotufika Comoro, Anaejitambulisha kuwa mkuu wa nchi, akaweka nyuma na mabalozi wa nchi nyengine badala safu ya marais wenzake.
Katika tamthilia hii tunaona mtitiriko wa azma ya muda mrefu ya kauli mbiu ya mbili kuenda moja. Kwanza kwa hadaa ya kuiondosha “buffer” ya ASP katika kulinda maslahi ya Zanzibar. Pili kwa kuyaongeza mambo ya muungano kutoka 11 mpaka zaidi ya 30 kwa kupitia mkono wa chuma wa chama na nidham iliojengwa na Mwenyekiti na Rais mwenye jeshi. Tatu kwa kuizamisha hadhi na heshima ya Rais wa Zanzibar kimataifa ili kumnyima uwezo wa kusema na kusikika, kumzidisha utegemezi na unyenyekevu kwa Rais wa Muungano na kuhakikisha Baraza lake la Mawaziri halitambulikani nje ya mipaka yetu. Kilichobaki katika hatua ya mwisho ni vyombo viwili. Kwanza Baraza la Wawakilishi, na pili mahakama kuu Zanzibar.
Kwa hili linaakisi tahtim ya azma ya Mwalim kwa kupitia hii rasimu ya Sita na Chenge. Kutaka kutuaminisha kwamba ni yenye maslahi mapana kwa Zanzibar wakati yale madai ya muda wote yamevishwa tu kilemba. Kwa mfano nafasi ya makamo wa Rais wa Muungano kubebwa na Rais wa Zanzibar, tumepewa makamo wa pili, alienyuma ya Waziri Mkuu wa Tanganyika katika kila nyenzo isipokuwa heshima tu ya nambari, tulichodai ni namba au heshima tu? Katika masuala ya muungano, mhusika si Rais wa Zanzibar, bali Makamo wake aliemchagua kama mgombea mwenza, ambae daima kwa sasa atakuwa mzanzibari, utaratibu wa nyuma sasa umefutika.
Pili ni kuiwekea utukufu katiba ya muungano iwe juu ya katiba ya Zanzibar, kiasi kwamba BLW halitakuwa na nguvu kama hii ilioakisi mabadiliko ya katiba ya Zanzibar ya 2010, iliorejesha utulivu, mafahamiano na siasa za ujasiri visiwani. Lazima kwanza tukapate idhni kwa mtawala Bara. Na hata mahakama kuu Zanzibar, katika rasimu hii ya Sita, kutakuwa na mahakama kubwa zaidi Bara ambayo hata mfumo wake na uteuzi wa wajumbe wake umesimikwa na nguvu za Rais wa Muungano. Hivyo lolote la Zanzibar linaweza kupingwa kwa maslahi tu ya Rais wa muungano kwa kupitia vyombo hivi muhimu vya kisheria. Ndio yale yale ya mwaka 1977 ya nia njema ya Mzee Jumbe, ya kuifuta ASP na matokeo yake tumeyaona hadi leo.
Rasimu hii itahitimisha azma ya kuidogoza Serikal ya Zanzibar kuwa kama tu ya mikoa bara, inakwenda sambamba na kelele za kina Kesi wa Nkasi, kwamba sisi ni sawa na tarafa moja tu ya Dar. Kwa vile nje ya mipaka mkuu wetu kwa ushahidi sasa amefutiwa heshima anayostahili, sasa mradi uko katika kuvunja utukufu wa ndani. Na ndio maana katika Baraza la Mawaziri la muungano, ukimuondoa Rais, na makamo wa kwanza, basi mwenye nguvu za kusimamia Baraza ni Waziri Mkuu, ambae ni Makamo wa tatu, huyu wa pili ambae ni Rais wa Zanzibar ni kivuli tu.
Moja katika rambi rambi za Mzee Jumbe, ni kutoka katika msikiti wa Maamur, upanga Dar Es Salam. Msikiti ule ulijengwa baada ya Makamo wa Rais wa Muungano wakati huo Mzee Jumbe kuingilia kati mgogoro uliokuwapo na kutoa sehemu hio kwa waislam waliokuwa na makaburi yao miaka ya nyuma. Leo hii hakutatokea suala kama hili ambalo Rais wa Zanzibar kwa heshima ya umakamo wa Jamhuri hii ataweza kufuatwa. Sio kwamba limevunja misingi ya kuungana, bali limevunja hata heshima ya kiongozi wetu kwa jamii nzima upande wa pili. Ndio maana hakuna kwa sasa lolote lililo kubwa kwa wazanzibari zaidi ya kudai mamlaka kamili.
Tunaposema mamlaka kamili basi ni kiu ya kuona heshima, haki na usawa na unasimama kama ulivyokuwa baada ya kuungana. Tunadai mamlaka kamili yenye heshima kwa Rais wa Zanzibar, tunadai mamlaka kamili ya Baraza letu la Wawakilishi, mahakama zetu, katiba yetu na uwezo wetu wa kujiendesha sio wa kutegemea na kuomba kufikiriwa kama ambavyo Shamsi Nahodha na genge lake wanavyotutia aibu Bungeni. Tunadai mamlaka yatayoheshimiwa kivitendo na kurejesha nafasi yetu katika muungano wa haki, heshima na usawa.
Kama ambavyo nia ya mbili kwenda moja na dhamira ya Mwalim ilivyokuwa miaka ya uongozi wake na uhai wake na leo hii kuwa ni urithi wa baadhi ya viongozi wakuu upande wa pili, kwa Zanzibar nako “defiance” inazidi na madai yanazidi, nguvu za madai zinazidi. Nimnukuu Mzee Warioba kwamba katika suala la muungano wazanzibari ni wamoja kwa lililo moyoni, na ndio khofu kubwa kuendelea kupuuza ndoto ya wazanzibari walio wengi bila ya unafik na tamaa ya tumbo. Tulianza na madai machache ya Mzee Karume na Mwalim kumnasihi wakati kuwa bado, tukaja na jaribio la Mzee Jumbe, tukaja na msisitizo wa kibiriti kichojaa, tafsiri yake ni kubwa hasa kwa wazanzibari na kiu ya mabadiliko.
Tukaja na mabadiliko ya katiba ya mwaka 2010, na leo tuna msisitizo wa madai ya mamlaka kamili. Tusiwafikishe wazanzibari kubaya zaidi na kuja kuondosha stahamala, na imani ya kuweza kurejesha haki wakiwa bado katika muungano, wenye undugu na umoja wa kupigiwa mfano. Wakati umefika wa woga huu wa kupandikizwa, sijui uislam, sijui uarabu na upuuzi mwengine kumalizika, ili muungano usongre mbele kwa haki heshima na usawa badala ya maslahi ya chama kilichojidhatiti kwa kuhakikisha kinawatia khofu na kuwaadhibu wale wenye muono tafauti.
Tuachieni tuitajenge Tanzania mpya ya ridhaa ya washirika wake, si ya kiini macho cha vuguvugu la vita ya baridi na tamaa ya kumeza kisiwa kwa sababu ya udogo wake. Tuachieni tujenge muungano wa haki, usawa na heshima kwa kila upande hasa kwa sisi “generation” tuliozaliwa tukiwa katika muungano. Tuweze kuuona urithi kuwa wa maana na wa kujivunia badala ya kuutazama kama ukoloni wa muafrika mkubwa kwa muafrika mdogo. Kwetu muungano ni zaidi ya hamasa za kimajui, ni kurasa mpya kuhakikisha haki, heshima na usawa inakwenda sambamba na nia njema ya kuungana kwa hiyari na kwa maslahi mema ya pande zote mbili.

No comments: