Ukisoma makala ya ZZK utakuta swahiba wangu anataka tuamini kwamba upinzani hautatoka kwengine kokote isipokuwa kutoka safu ya wajamaa pekee. Ima ndani ya safu ya watawala hawa dhidi ya JPM au katika safu ya mtandao wa wajamaa wenyewe na hasa wanaouamini mfumo wa Umwalimu. Lakini ushahidi mkubwa duniani unaonyesha kabisa anachokifanya JPM kama muendelezo wa uongozi wake ni mnasaba kabisa na ujamaa na wajamaa wengi wanaofukuta katika maendeleo kwa misingi ya uimla na kubana haki. Fikra yote nzima kwangu naitafsiri katika ile ile taswira potofu ya mwalimu dhidi ya mabeberu na wengine aliowaita majina ya ajabu na kuzitukuza asasi za kijamaa kuwa ndio zenye uthubutu wa kuongoza.
Utakuta katika makala ile imekuja kipindi kizuri cha kuuweka upinzani hasa bara kuwa kama uliokosa ajenda, lakini hapo hapo anakubali kwamba uimla uliopo ni hatari kwa taifa na kusahau kwamba watu walimpinga mwalimu kwa sababu hii hii ya kuitafsiri haki kwa misingi ya kiimla ya kijamaa. Naamini hakuna ajenda kubwa ya kusimama nayo kama ajenda ya kusimamia uhuru na demokrasia pana yenye tija kwa wananchi. Zaidi katika mqzingira ya siasa za bara ni vigumu sana kuwa na ajenda kama ambavyo upinzani ulivyo kwa Zanzibar lakini ajenda za kisiasa ni sawa na "evolution" kwamba zinaendana na msukumo wa mazingira ulivyo. Binafsi nathubutu kusema upinzani wa sasa utaweza kuibuka na ajenda kubwa zaidi kuliko kipindi chote cha siasa za vyama vingi nchini Tanzania kwa sababu ya uimla unaoinyemelea nchi ilioweza kujisukuma zaidi katika demokrasia baada ya miaka ya giza kutoka hatamu tafauti za viongozi.
Nilivyomsoma zaidi ni kwamba anaonekana kuwa na "soft touch" kwa JPM katika makala ile kwa dhana ya kwamba wanyonge wanamfahamu na kumkubali kwa anayoyafanya, na kwamba dhana iliojengewa ni kuwa upinzani ujenge ajenda katika umasikini na namna gani watawavusha wanyonge kutoka katika umasikini wakati huwezi kujenga kisima cha mawazo ya aina hii huku hio haki ya kusambaza ajenda za namna hio zikiwa zimekaliwa na amri kuu ya kuzuia shughuli za kisiasa kwa vyama badala ya wale waliochaguliwa tu. Utasikika wapi ikiwa ndani ya bunge ni amri ya bwana mkubwa, mahakama ndio hivyo na serikali ikizidi kupima nguvu ya demokrasia baina ya ile ilio huru na nguvu ya haki na ile ya tafsiri ya Kagame na maendeleo ya kiuchumi bila ya haki? Hivi kuna ajenda tukufu zaidi ya kusimama na haki, uhuru na demokrasia hasa katika uongozi unaonukia uimla na utawala wa amri? Wengi wa wanyonge wamejengewa taswira za propaganda na kukata tamaa na hata kwa wengine wenye muamko ni sababu ya baadhi kumuona JPM kama malaika. Kwamba huko nyuma ni wao pekee waliokosa haki, leo wote tuko katika msukumo mmoja wa matumizi ya amri, badala ya haki na uhuru wake tumebaki kuzomeana kwa sote kuwa katika tafsiri ya haki ya mtawala.
Zaidi ni mapema mno kupima umaarufu wa mtu anaetumia joho la kupambana na rushwa huku akijidhatiti katika uimla tena bila ya woga wa kusimamia maneno ya ajabu ya kupotea kwa watakaompinga huku akijificha katika maombi ya kupewa subira, au kuwahamasisha polisi na mauaji badala ya hekima kiasi kwamba anathubutu kusema hata ikiwa ni ndugu yake katika mazingira haya angelishukuru kapumzika kwa salama kama ni miongoni mwa wale watakaoukumbwa na alichokiita "lazima raia walale". Hivi ni sawa kuusemea upinzani kukosa ajenda katika tasiwra hii iliopo ya ubabe, nguvu na msukumo wa wazi wazi wa kudharau haki?
Yaliotokea Zanzibar pekee ni ajenda kwa upinzani mzima kwa sababu ikiwa leo utawala na uongozi wa huyu Masiah mpya unapinga hata uwapo wa demokrasia katika visiwa vidogo tu kweli upinzani utaweza kufanikiwa kwa ajenda alizozitaja yeye kuwa tukufu wakati mtawala akiendelea kujidhatiti katika uimla na nguvu zisizopingika? Nafikiri umefika wakati wa haya majaraha kati ya CDM na ZZK yakae pembeni na kutazama uhalisia wa tunapoelekea badala ya hizi "theory" za vitabuni ya namna ya kuuendesha upinzani katika mazingira ya nchi tulivu wakati tulipo ni katika "maturity" ya uimla utakaoturudisha nyuma katika kipindi cha khofu kwa sababu tu ya kuhakikisha chama kinandelea kushika hatamu wa miaka 50 mengine.
Hakuna ajenda tukufu kama haki, uhuru na utawala wa demokrasia, na sehemu pekee ambapo ajenda ya maendeleo inaweza kukuwa zaidi ni pale ambapo utulivu wa kweli wa demokrasia utasimama. Ikiwa JK alionekana kuwa na imani ya hadaa ya demokrasia, alishindwa kusimama na haki ndani ya chama chake, na hata kwa Zanzibar ndogo ambayo ingelimpa heshima kubwa duniani kama angeliruhusu haki ya uchaguzi kusimama, tena kwa siasa zilizoonyesha utulivu na faida kwa wananchi na kashindwa kuukubali ukweli wa kukataliwa kwa chama chake itakuwa huyu anaethubutu wazi wazi kuutukuza uimla, mauaji na matumizi ya nguvu kwa wananchi?
Wala tusijidanganyane kwamba wananchi wataendelea kuukubali uhuru wao kuminywa, demokrasia na haki kuzuiwa kwa muda mrefu na kuendelea kuukubali ufalme wa chama na uongozi wake. Ukitazama hata nchi zilizoendelea kiuchumi zimekumbana na mashaka makubwa ya wananchi kwa sababu ya kushindwa kuiendeleza haki, uhuru na demokrasia. Kwa sasa nchi inanyemelewa na giza zito la haki na uhuru wake kuliko kipindi chote cha uhai wa "generation" hii ya vijana. Na ajenda kubwa ni kututoa katika shimo la udikteta na kuifahamisha jamii athari za mmoja kushika hatamu za nchi kwa ubabe pamoja na kusukuma uhuru wa haki badala ya tamthilia za upinzani kugawiwa kwa sababu ndogo ndogo na ushindani usio na tija. Wakati tunanyosheana vidole, uimla unazidi kushamiri na tukiacha ukamea na kuzaliana tutakuja kuyakuta ya Sani Abacha ndani ya ardhi ya Afrika Mashariki. Wanaofikiri wanyarwanda wako katika furaha wasubiri anguko la Kagame na miji itavyoshamiri furaha kwa ndoto ya uhuru. Sawa na Ghadafi, Zenawi na wengine wengi, kinachowasukuma kuonekana na kupendwa na wengi ni propaganda si uhuru wa kupima kukubalika kwao na wananchi.
Wanaoitwa polisi kwa mahojiano kama si Lisu, ni Zito, kama si Mbowe na Mbatia ni Maalim Hamad. Kwa hili la upinzani uimla katika kulinda maslahi yake hauchagui ila katika kuwagawa ndio utawasikia kiongozi pekee wa upinzani mwenye ajenda ni mjamaa mwezao. Ukweli hasa tusome ya Umma party na jinsi gani majuto ni mjukuu kwa kukubali kuwekeza katika ndoto iliotoweka na kuwasukuma katika maisha nje ya ardhi yao kwa sababu tu ya kusahau adui mkubwa zaidi, nayo ni jamii iliolelewa katika ujinga na kukuzwa katika misingi ya utukufu kwa binaadamu aliumbwa na nafsi ya kutenda dhambi. Hakuna adui zaidi ya adui wa haki, hakuna fisadi mkubwa zaidi ya fisadi wa demokrasia na uhuru wa kuishi kwa haki. Tusiyumbe katika maadili ya kutafsiriwa fisadi halali na fisadi haramu, tutazame athari za fisadi wa haki asie na utu na anaeamini katika matumizi ya nguvu kwa maslahi ya ndoto na "ego" zake.
No comments:
Post a Comment