::Rais wangu JPM,Pemba haiitaji "mikwara" na "vitisho",bali mashauriano na mapatano::
Ulikuwa Pemba...ile Pemba ya pwani ya Tanzania!!Pemba isiyo rafiki kwa chama chako na wala sidhani kama iliwahi na itakuja kuwa rafiki kwa chama unachokiongoza.Pwani ya Kiwangwa..Mkondo wa Nungwi!!Wao hujuana kwa vilemba
Hata ulivyokuwa unahutubia,waliona huna kilemba kama chao,ndio maana wale wenyeji wako wakakuletea wenyeji wa Unguja na sio Wapemba wenye mji.Leo ulihutubia na kukemea wale "waliosombwa",toka bara na Visiwani...Hadhira uliokusudia haikuwepo...Hawawezi kuwepo sbb hawakukupigia kura.
Hiyo uliyoiona leo walaaa sio Pemba atiii!!Ile ilikuwa "nkusanyiko" wa waliotoka bara na sehemu ya Unguja.Tazama boti za leo na kesho zitakazovyojaa "maruani".Huku Pemba ilishazoeleka,kupiga na kupigwa wasio wa huku.
Leo haikuwa siku ya visasi na vitisho,ilikuwa siku ya mapatano na mashauriano.Vitisho na mikwara inaongeza mpasuko.Vijembe na kejeli haviwaweki walio na tofauti pamoja..bali vinajenga ufa kuchimbua uhasama.
Huku hawazikani,hawasabahiani,hawaswali pamoja,hawakai barazani na jamvini kwa umoja.Hata vipandio wanyimana.Hawahitaji vitisho na mikwara.Wanahitaji mapatano na mashauriano.Kwanini mashauriano...Ndiyo!! Kwanini?Kwa sbb hawakukuchagua wewe na chama chako...Sio wewe tu,hata wenzako waliopita hawakuwahi kukubalika huku Pemba,toka 1995,2000,2005 na 2010 ndiyo kabisaa,mpaka wakaamua kuunda Umoja wa Kitaifa.2015 siijadili...maana leo umempongeza Jecha mbele yao.Jecha Salum Jecha umeagiza apewe tuzo!Loooh!!
Aliwahi kusema Mwanafalsafa wa Uyunani "Ex Africa semper aliquid novi" i.e "There is always something new (coming) from Africa.Hili la Jecha kutangazwa kupewa tuzo katikati ya Viwanja vya Gombani ya Kale pale Pemba,linathibitisha msemo huu wa Zenobius
Ni nani anatupa kibri hiki?Ni haya madaraka ya mwili yasiyoweza kuangamiza roho!?Ni majeshi na vifaru?au ni pesa na mamlaka?Heri walio wapatanishi...Maana hao watauona Ufalme wa Mungu.Watendeeni haki...Umajenga chuki kwa vizazi na vizazi!Hawa wanarithishana kutu ya chuki hizi...Zitadumu miaka na miaka.
Msingi wa kuyamaliza haya sio mikwara,wala sio vitisho kwa yule ambaye wao "wanamuheshimu".Kumtolea lugha za kejeli yule ambaye wao wanamuamini..ni kwahuzunisha na kuwasononesha hao walio na imani nae.Kwanini lugha hizi za kuudhi na kejeli kwa watu wenye heshima ya kiungozi kwa ngazi ya Taifa?kumfananisha kiongozi wao,tena Makamu wa kwanza wa Rais mstaafu kama "mjinga" na mtu asiyejielewa ni kujenga chuki nyingine,hapa hatujengi bali tunabomoa.Ni lini tutakumbuka kuwa kudondoka kwa ukuta huanza na nyufa??!!.
Alikuwepo Komandoo!!Alivuruga na kuvunja miguu...alibetua kuanzia mtoto mpaka babu!Hakika ulikuwa ni wakati wa mateso na taabu.Vyeo vilikuwa havivuki mkondo wa Nungwi bila kadi ya chama.Hali hiyo imerudi na sasa imekuwa zaidi.Hatupeani kazi kwa kutazama nasaba,itikadi na ukaazi.Hili ndio sharti lilikuwa sharti kumkimbiza Sultan?Moshi wa mabomu na ghasia za uchaguzi zimelemaza watoto na watu wazima,Wapo walioingiwa na moshi wa mabomu wakiwa watoto wadogo,mpaka leo wanaugulia matatizo ya macho!Ni Mungu gani tunaomba kila siku?Huyu huyu mwingi wa rehma mwenye kuogofya na kukataa visasi na manyanyaso kwa wasio na hatia?
Afisi nyingi ni huyu wa Kuvuka Nungwi na huyu ni jirani wa Chumbe.Loooh...ama hakika wale wa Pemba hujuana kwa vilemba,kumbe na wao hujulikana kwa vilemba na watu wasio na jamii zao.
Silaha yao ni moja...Lakh'aa na du'waa!!Hakuna wa kumshtakia.Walipojazana eneo la darajani Znz wakiuza bidhaa zao,wakatambulika kwa vilemba vyao.Na sasa wamevunjiwa na kuhamishwa kwa amri ya wa pili kwa madaraka baada ya Rais wa Znz.Pale si wa Wete wala Chakechake anafanya yake kupata riziki.
Ndio!!Walimuita Komandoo...na alikuwa komandoo kweli kweli!
Sasa hana nuru tena...bila mkongojo hafiki hatua mbili mbele ya uso wake.Wapo walioponywa na Nabii Issa,na wakapata uwezo wa kuona tena,na walipoona wakaambiwa wasiwaambie watu kuwa ni yeye ndiye aliyewaponya.Lkn hawa hawakuwa na upofu wa ukubwani...hawa walizaliwa nao.Pengine wangekuwa na ule wa ukubwani Nabii Issa angaliwauliza..."Mbona mlizaliwa na nuru,nini kimepoteza nuru yenu?"...Kama swali hilo lingeulizwa kwa "mzee mzima" Yamkini jibu lingekuwa zito.
Mwingine kazunguka Cuba,China na India.Saratani ya mkono wa kushoto...Sasa panaoza na kutoa maji na ungaunga!!Angalikuwa ni "mashoto" tungesema ndio mkono uliodhinisha idadi za delaya ma washawasha.Lkn sio hivyo...labda ni maamuzi tu ya mgawaji raabuka.Yeye hawasikiliza walio na kilio cha sala kuliko kilio cha furaha!!Sala hujenga na kuleta ukaribu na Mungu...Sisi tutaendelea kusali,ili wote wanaoamini ktk ubabe na kejeli warudi kwenye meza ya duara.
Haijakuwepo suluhu ya mikwara na vitisho!Unatisha nini kwa mahali ambapo kura zako hazijazi kiganja cha mwana wa kaya?Mapenzi ya kweli hayapimwi kwa uwingi wa maruani,bali hiyari.Maana hiyari hushinda utumwa.Kama ilivyo Dodoma ya wagogo na makao makuu ya chama na serikali...Pwani ya Nungwi nao ina waja wake...Wakikohoa,watu wanaitika.Meza ya duara ndio mahali pake...Aliliona Aman Abeid Karume.
Walisema Wakoloni, "Zanzibar ipigapo ngoma,Maziwa Makuu yote hucheza"....Hatuitaki ngoma ya Znz!!
No comments:
Post a Comment