Friday 2 December 2016

Zanzibar umevunja katiba ya Muungano kutunga,sheria ya Mafuta?

Zanzibar kunyakua mafuta na gesi imevunja katiba ya muungano?
DEC 01, 2016by JOSEPH MIHANGWAin MAKALA
HIVI karibuni, Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, ametia saini kuwa sheria, Muswada wa Mafuta na Gesi Asilia kuwa chini ya mamlaka na usimamizi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).  Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977, ibara ya 4 (3), mafuta na gesi ni mambo yaliyo chini ya mamlaka ya Serikali ya Muungano.

Akitia saini muswada huo, Shein alisema taratibu zote za kutungwa sheria hiyo zimefuatwa kikamilifu, na kwamba wanaomtuhumu kuvunja Katiba ya Jamhuri ya Muungano kwa kufanya hivyo ni walegevu wa akili, wachochezi, waropokaji wasiojua wasemalo.

Umma ulitarajia kupata mrejesho kutoka kwa wasomi wa sheria za Katiba na wa Sayansi ya Siasa juu ya jambo ambalo sasa linaelekea kuzua utata wa kisiasa na kikatiba; lakini ukimya umetawala badala yake, pengine kwa kuchoshwa na “kero” za Muungano za milipuko ya mara kwa mara ambapo mawazo wanayotoa hayasikilizwi kwa sababu za kisiasa, ushabiki na ubabe kutawala kufikia kuitwa “wasaliti” wa Muungano.

Je, manung’uniko yanayoendelea chini kwa chini kwamba Katiba imevunjwa yana msingi wowote?. Je, Baraza la Wawakilishi na Rais wa Zanzibar wana mamlaka ya kutunga sheria juu ya mafuta na gesi kama walivyofanya?.

Majibu kwa maswali haya hayawezi kupatikana ila kwa njia ya rejea ya misingi na matakwa ya Muungano wetu kama tutakavyoona katika makala haya, japo kwa ufupi.

Asubuhi ya tarehe 22 Aprili 1964, mjini Unguja, waasisi wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Rais Julius Kambarage Nyerere wa iliyokuwa Jamhuri ya Tanganyika, na Rais Abeid Amani Karume, wa iliyokuwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar; walitia saini Hati ya Makubaliano kuunganisha nchi zao kuwa nchi moja kwa jina la “Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar”, na hati iliyotumika kuunganisha nchi hizo kujulikana kama “Hati ya Muungano”, au kwa lugha ya kigeni, “Articles of Union”.

Chini ya Mkataba huo, Tanganyika na Zanzibar ziliungana kwa mambo 11 tu na mengine yote kuachwa kushughulikiwa na kila nchi husika katika himaya yake kama inavyobainishwa na ibara ya 3 (a) na ya 5 ya Mkataba pamoja na Sheria za Muungano katika ujumla wake; kwamba kutakuwa na mamlaka mbili tofauti za Bunge (Legislature) na za kiutawala (Executive) zenye kujitegemea, kati ya Jamhuri ya Muungano na Zanzibar; na kwa sababu hiyo (ibara 5) “Sheria za Tanganyika na zile za Zanzibar zitaendelea kuwa na nguvu katika nchi hizo kwa mambo yasiyo ya Muungano”.

Mambo hayo 11 ya Muungano yalikuwa ni: (1) Katiba na Serikali ya Jamhuri ya Muungano (2) Mambo ya Nchi za Nje (3) Ulinzi (4) Polisi (5) Mamlaka juu ya hali ya hatari kwa nchi (6) Uraia (7) Uhamiaji (8) Biashara ya Nje na Mikopo (9) Utumishi katika Jamhuri ya Muungano (10) Kodi ya Mapato inayolipwa na watu binafsi na Mashirika, ushuru wa forodha na ushuru wa bidhaa zinazotengenezwa nchini unaosimamiwa na Idara ya Forodha na (11) Bandari, Usafiri wa Anga wa Kiraia, Posta na Simu.

Ni matakwa ya sheria za kimataifa, kwamba, ili Mkataba unaofikiwa kati ya nchi huru mbili au zaidi uwe na nguvu ya kisheria kuweza kutekelezeka katika nchi, lazima uridhiwe na Bunge la nchi husika kwa kutungiwa sheria.  Kwa hiyo, tarehe 25 Aprili 1964, Bunge la Tanganyika lilikaa na kuridhia Mkataba huo kwa Sheria Namba 22 ya 1964; na kwa Zanzibar (japo bado kuna utata kuhusu hilo kama lilifanyika) inasemekana Baraza la Mapinduzi liliketi na kuridhia siku hiyohiyo Bunge la Tanganyika liliporidhia.

Sheria hizi mbili; yaani Sheria ya Tanganyika na ile ya Zanzibar ya kuridhia Mkataba wa Muungano, zinajulikana kwa pamoja kama “Sheria za Muungano” (Acts of Union) 1964;, bila hivyo Muungano usingetangazwa na kuanza kufanya kazi kuanzia 26 Aprili 1964.

Hadi sasa, mambo ya Muungano yameongezeka kufikia 23, likiwamo la “Maliasili ya mafuta, pamoja na mafuta yasiyochujwa ya motokaa na mafuta ya aina ya petrol na aina nyinginezo za mafuta au bidhaa, na gesi asilia” na ambayo ndilo chimbuko la makala haya.

Jina “Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar” lililotumika katika Mkataba wa Muungano na sheria za Muungano, lilikoma kutumika Desemba 1965 kufuatia sheria ya Bunge Namba 61 ya 1964 (United Republic Declaration of Name) iliyopitishwa kwa theluthi mbili ya wabunge kubadili jina kuwa “Jamhuri ya Muungano wa Tanzania”; ambapo Sheria ya Bunge Namba 24 ya 1967 ilimpa Rais mamlaka na uwezo wa kubadili jina “Tanganyika” kwenye hati za taasisi zote za kisheria na kuingiza jina “Tanzania”.

Kuongezeka kwa mambo ya Muungano tofauti na yale ya asilia na namna kulivyofanyika, kumekumbana na hisia mbalimbali chanya na hasi, hasa kutoka upande wa Visiwani ikidaiwa kwamba kuna lengo la “kuimeza Zanzibar”; huku wengine wakiona kwamba utaratibu uliotumika ni wa kidikteta, batili na haramu, wenye kukiuka Katiba na Mkataba wa Muungano.

Hisia chanya ni pamoja na zile kwamba, hatua ya kuongeza mambo ya Muungano kutoka 11 asilia, ina lengo la kuimarisha zaidi Muungano (kuelekea Serikali moja ya kitaifa) na mfano wa kuigwa na nchi zingine kuelekea Muungano wa Afrika.

Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulifikiwa kwa njia ya dharura kwa shinikizo la mazingira ya kipindi hicho cha “vita baridi” kati ya nchi za ubepari na ubeberu wa  kimagharibi na nchi za kambi ya kisoshalisti za Mashariki, hivi kwamba hapakuwa na muda wa kutosha kuweza kuandaliwa Katiba ya Muungano.

Kwa sababu hiyo, Mkataba wa Muungano uliweka wazi (ibara ya tano) kuwa, katika kipindi cha mpito kisichozidi miezi 12 ambapo Muungano ungekuwa umepata Katiba yake chini ya utaratibu uliowekwa kwenye Mkataba huo, “Katiba ya Tanganyika itakuwa ndiyo Katiba ya Mpito ya Muungano kwa kufanyiwa marekebisho” kuingiza mambo yote 11.

Kwa bahati mbaya na kwa sababu ya uhusiano wa pande mbili za Muungano kuanza kuingia nyongo, mazingira hayakuruhusu kuundwa kwa Tume ya Kupendekeza Katiba na (ili hatimaye) kuitishwa kwa Bunge la Katiba, hadi miaka 12 baadaye ilipopatikana Katiba ya kudumu iliyopo sasa, yaani ile ya mwaka 1977.

Tuharakishe kutamka hapa kwamba, japo Kisheria Katiba ya nchi ndiyo sheria mama wa Sheria zote nchini, na kwamba sheria yoyote inayokinzana na Katiba ni batili; lakini kwa Katiba ya Muungano wa Tanzania na ile ya Zanzibar, Msingi na Kanuni kuu [grand norm] ya katiba zote, kuanzia na ile ya Mpito [1964, 1965] hadi hii ya sasa, ni Mkataba wa Muungano unaofafanua mambo yaliyokubaliwa na aina [muundo] ya Muungano uliofikiwa.  Bila Mkataba wa Muungano, hakuna Sheria wala Katiba ya Muungano au ile ya Zanzibar, na si kinyume chake.

Ndiyo kusema, Mkataba wa Muungano, kama ulivyoridhiwa kupitia sheria ya Muungano (1964) ni sheria kuu inayoweka msingi wa Muungano na ukomo wa uhuru wa Katiba ya Muungano.

Ni kwamba, Katiba ya Muungano na ile ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, hazina budi kuitika bila kupenda mwangwi wa Mkataba wa Muungano ambapo kwa mantiki hiyo (Mkataba/Sheria ya Muungano) sio sheria za kawaida kama sheria zingine. Kinyume chake Katiba inayokinzana au kukiuka misingi ya Mkataba au sheria za Muungano itakuwa batili tangu mwanzo wa kutungwa kwake (void ab initio).  Na kwa mantiki hiyo pia, Mkataba wa Muungano ni sehemu kuu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano.

Katiba zote mbili za Muungano, yaani Katiba ya Mpito na Katiba ya Kudumu ya mwaka 1977, zilitoa utaratibu wa kufanyiwa marekebisho ukijumuisha kuongeza, kupunguza au kuboresha mambo ya Muungano kwa njia ya miswada ya Bunge la kawaida.

Ibara ya 62 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano, 1977, inaunda Bunge ambalo wajumbe wake ni wabunge wote pamoja na Rais (National Assembly). Ukimwondoa Rais, Bunge linaundwa na wabunge wa majimbo wa kuchaguliwa kutoka Bara na Visiwani na wengine wa kuteuliwa kwa mujibu wa ibara ya 66 ya Katiba.  Bunge hili ndilo lenye “Mamlaka” ya kutunga (pamoja na kurekebisha) sheria kwa mambo yote ya Muungano na pia kuhusiana na mambo yote yanayohusu Tanzania Bara.

Katiba ya Muungano imeorodhesha mambo ya Muungano 23 ambayo ni Bunge pekee la Muungano lina mamlaka juu yake kwa ajili ya Jamhuri ya Muungano, likiwamo la mafuta na gesi ambalo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeamua kulinyofoa ki-imla kutoka kwenye orodha ya mambo ya Muungano, kazi ambayo ilipaswa kupitishwa kwa kura na angalau theluthi mbili ya idadi ya wabunge wa Bunge la Muungano.

Aidha, kwa mujibu wa ibara ya 98 (1) (b) ya Katiba, mambo manane ya Muungano ambayo marekebisho yake yanahitaji kuungwa mkono na angalau theluthi mbili ya Wabunge kutoka Bara na theluthi mbili kutoka Visiwani; mafuta na gesi asilia ni mojawapo, hivi kwamba, ilivyotokea halikupaswa kushughulikiwa na Baraza la Wawakilishi Zanzibar kwa sababu, kama tulivyoona, liko nje ya mamlaka ya Baraza hilo.

Kwa yote haya, kuhusiana na sheria iliyopitishwa na Baraza la Wawakilishi Zanzibar, kuna kila ishara na kwa vigezo vyote,  kuonesha kwamba Katiba ya Muungano imevunjwa, ila tu kama tutathibitishiwa vinginevyo.  Hakuna Muswada wa Bunge, wala Bunge la Jamhuri ya Muungano lililokaa kujadili na kuupitisha kwa utaratibu tuliokwishauelezea.  Haitoshi tu kuwaita wenye “kuhoji” hatua hii “walegevu wa akili” au wachochezi katika zama hizi za demokrasia na utawala wa sheria. Yanatakiwa majibu makini na yenye kujitosheleza.

Tangu kuasisiwa kwake kwa njia ya dharura mwaka 1964 hadi leo, Muungano wa Tanganyika na Zanzibar umepitia na unaendelea kupitia, misukosuko na mitafaruku mingi iliyokuja kupewa jina “Kero za Muungano”,

Moja ya mitafaruku hiyo ni madai ya Wazanzibari kwamba “nchi” yao inamezwa na “Tanganyika” ambayo wanadai ndiyo imejigeuza kuwa Muungano, kutokana na kuzidi kuongezeka kwa mambo ya Muungano ki-imla bila ridhaa ya Wazanzibari.

Ni mambo kama haya yaliyofanya Rais wa awamu ya pili, Aboud Jumbe Mwinyi, arubunike kutaka ufafanuzi mahakamani juu ya aina ya Muundo wa Muungano uliokusudiwa, na kwa kutaka kufanya hivyo, alivuliwa nyadhifa zote za uongozi, Visiwani na Bara.  Kabla ya hapo, Nyerere na Karume waligongana juu ya kero hii kufikia Karume kutaka kuvunja Muungano akisema, “koti likikubana unalivua”.

Na miaka ya karibuni, Zanzibar imefanyia marekebisho ya Katiba yake na kujitambua kama “Nchi” ya “Wazanzibari”, na kwamba sheria yoyote itakayopitishwa na Bunge la Muungano ambayo itatumika Zanzibar kwa mambo ya Muungano, lazima ipelekwe mbele ya Baraza la Wawakilishi, bila shaka kama tahadhari kwa kudhibiti sheria zenye lengo la “kuimeza Zanzibar”.  Huu ni “ujasiri” mpya ambao haukufikirika kabla ya hapo kwa hofu ya “kibano” cha Muungano.

Yaliyotokea Zanzibar ni mwendelezo wa masahibu yanayousibu Muungano tangu kale hadi leo kuonesha kwamba “kero” za Muungano zingali hai, mbichi na zenye macho makavu. Je, tuamini kwamba Zanzibar imenyakua mafuta na gesi kwa hasira kutoka Muungano bila hofu ya “kibano” kwa sababu halikuwa jambo la Muungano asilia tangu mwanzo, hivi kwamba imefuatilia haki  yake iliyoporwa na Muungano?.

Ikitokea kwamba Baraza la Wawakilishi limetunga sheria kuondoa “Mambo ya Nchi za Nje” katika orodha ya Mambo ya Muungano, kama lilivyofanya kwa mafuta na gesi; tutanyamaza pia kama tulivyonyamazia hili la mwisho?.

Kama ni hivyo, Muungano wendapi?.

jmihangwa@yahoo.com/0713-526972

http://www.raiamwema.co.tz/zanzibar-kunyakua-mafuta-na-gesi-imevunja-katiba-ya-muungano/

No comments: