Wednesday, 26 April 2017

Muungano, Zanzibar na miaka 53 ya ukaliwaji wa kimyakimya

MTAZAMO WA MZANZIBARI



Zanzibar ina bahati mbaya ya kukaliwa na tawala za kigeni kwenye historia yake, zikibadilishana moja baada ya nyengine, lakini haijawahi kuacha kuzipinga tawala hizo kwenye historia yake yote.Huu ni mwaka wa 53 huu tangu Zanzibar iwekwe kwenye himaya na nchi jirani ya Tanganyika kupitia mkataba uliopewa jina la “Hati ya Muungano” ambao umezaa hiki ambacho kinaitwa leo kuwa ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.Mengi yameandikwa na kusemwa katika kuelezea chimbuko na dhamira hasa ya Muungano huu, na mengi yanathibitisha kutokuwepo kwa uwazi na ukweli huu unasababisha kiwango kikubwa cha kutokuridhika, hasa kwa upande wa Zanzibar, ambayo ndiyo muathirika mkubwa wa huo unaoitwa Muungano.Wanaowakosoa wakosoaji wa Muungano huu hujenga hoja juu ya kudumu kwa Muungano wenyewe, wakisema: “Kama Muungano huu ni mbaya na hautakiwi, basi usingelidumu hadi leo!”


Wanachokisahau ni kwamba kudumu kwa mahusiano kati ya pande husika kwa miaka mingi si lazima kutokane na uzuri wa mahusiano yenyewe, bali mara nyengine ni mbinu, mikakati na hila kati ya wale waliomo kwenye mahusiano hao, hasa za mwenye nguvu kubwa zaidi.Alisema kweli Rais Mstaafu Benjamin Mkapa mwaka 2004 kuwa “asilimia kubwa ya kizazi cha sasa cha pande zote mbili ni kile kilichozaliwa baada ya 1964”, lakini hakuwa sahihi alipodai kuwa kwa hao wote “utambulisho pekee wanaoujuwa na kujivunia nao ni Utanzania wao tu!”

Hakuwa sahihi kwa wengi miongoni mwa Wazanzibari, ambao wanauchukulia Muungano wenyewe kuwa ni utawala wa kigeni kwenye ardhi yao unaowalazimisha na kuwaamulia wao jinsi ya kuyaishi maisha yao ya kisiasa, kiuchumi na hata kijamii.Kwa Wazanzibari walio wengi, utambulisho wao umebakia kuwa Uzanzibari tu na utiifu wao umekuwa kwenye utambulisho huo. Hata pale ambapo sheria zinazohusiana na Muungano wenyewe zinawanyima nafasi ya kujitambulisha na Uzanzibari wao – kwa mfano, wanapolazimika kutembea na paspoti za Tanzania – bado wao wanajitambua na kujitambulisha kama Wazanzibari.

Kama kuna kitu ambacho Muungano huu umekithibitisha kwa Zanzibar ndani ya miaka hii 53, ni kwamba taifa kubwa la Kiafrika – licha ya umasikini na udhaifu wake wa kiuchumi – linaweza kutumia nguvu na umasikini wake huo kulikalia taifa jengine dogo na kulitendea kadiri lipendavyo.
Katika hayo ambayo Tanganyika yenye koti la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania huitendea Zanzibar ni kuiamulia vipi uchumi wake uwe, kwa kuwa imejipa madaraka ya kumiliki nyenzo kuu zote za uchumi huo – kodi, sarafu, mikataba ya kimataifa kwenye masuala ya uchumi.

Tanganyika pia kupitia chama chake, CCM, inaamua nani ashike nafasi ya uongozi wa juu ndani ya Zanzibar. Tukio la mwisho kabisa linalothibitisha hayo, ni uchaguzi wa Oktob 2015, ambao ulifutwa siku tatu baada ya kufanyika na siku moja baada ya kituo cha kutangazia matokeo kuvamiwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania lililo chini ya amri ya Amiri Jeshi Mkuu, kwa wakati huo Rais Jakaya Kikwete.Sababu ya hayo ni ukweli kwamba katika uchaguzi huo, mbinu za wizi wa kura ambazo zilitumika chaguzi za nyuma zilikuwa zimeshindwa na ushindi ulishakuwa mikononi mwa upinzani, ambao Tanganyika inauchukulia kuwa ni adui wa maslahi yake visiwani Zanzibar.

Chini ya Muungano huu pia, Zanzibar haiwezi kusemwa kuwa ni mahala salama, maana ingawa suala la ulinzi na usalama wa raia na mali zao limewekwa chini ya mikono ya Muungano, kwa makusudi kabisa mara kadhaa hali yake huchafuka mbele ya macho na wakati mwengine usimamizi wa taasisi zile zile za Muungano ambazo zina jukumu la kusimamia ulinzi huo.Katika mifano hiyo, makundi ambayo yanasaidia kuendelea kuwapo kwa madaraka ya Tanganyika visiwani Zanzibar kwa kuwakandamiza wale wanaoonekana kutishia madaraka hayo, huachiwa kufanya yatakavyo. Ndizo hadithi za makundi ya Janjawidi, Mazombi na Vikosi vya SMZ.

Ni hivi majuzi tu ndipo rikodi mbaya ya uvunjaji wa haki za binaadamu dhidi ya wanaoupinga utawala imehamia Tanganyika, lakini miaka nenda miaka rudi huo umekuwa ni utamaduni wa kudumu visiwani Zanzibar, mbele ya macho ya taasisi zinazoitwa za Muungano.

Kwa kuulinda ukaliaji wake visiwani Zanzibar, Tanganyika aidha huunga mkono waziwazi au hunyamazia kabisa kabisa ukandamizaji wowote dhidi ya yeyote anayeonekana kuhatarisha maslahi yake visiwani humo.Ni bahati mbaya sana kwamba wakati Mzanzibari anaadhimisha miaka 53 ya Muungano, haya yaliyotajwa hapa yanakuja kichwani mwake kama uhalisia wa hicho kinachoitwa Muungano na, kwa hivyo, kwake huwa si kumbukumbu ya siku ambayo nchi yake iliungana na nchi nyengine, bali msiba wa siku nchi yake ilipochukuliwa moja kwa moja na jirani yake.

Lakini bahati mbaya zaidi ni kuwa nguvu za Tanganyika kuichukuwa Zanzibar zimewezeshwa kwa kiasi kikubwa pia na baadhi ya Wazanzibari wenyewe. Wakati tunazungumzia kuwa sehemu kubwa ya Wazanzibari wanaouchukulia vibaya Muungano huu, ukweli ni kuwa pia ipo sehemu ya Wazanzibari ambayo inaamini kuwa ndiyo njia pekee salama ya wao kubakia madarakani.Kwao wao, hata kama wanajuwa kuwa Zanzibar imepoteza pakubwa kuwamo kwenye mikono ya Tanganyika, jambo hilo ni aula zaidi kwao madhali tu ni wao ndio ambao wanapata fursa na nafasi ya kufaidika na kuwamo mikononi humo, kuliko kuwa na Zanzibar yenye nguvu kama Zanzibar lakini isiyokuwa mikononi mwao.

Kwao wao, ni bora kuwa na Zanzibar dhaifu, masikini, dhalili, isiyokwenda mbele daima lakini ambayo iko mikononi mwa himaya inayowatambua wao kuwa ndio pekee wanaoweza kuyalinda maslahi ya himaya hiyo, kuliko kuwa na Zanzibar yenye nguvu, imara na inayosonga mbele, lakini ambayo wao sio wenye hatamu.

TANBIHI: Makala ilichapishwa kwa mara ya kwanza kwenye gazeti la Mwelekeo la tarehe 25 Aprili 2017.
ZANZIBAR DAIMA.

No comments: