Friday 29 September 2017

NGUVU YA LISSU NI KUBWA KULIKO YA RISASI

Posted on September 23, 2017 by Zanzibar Daima in KALAMU YA GHASSANI 

Sisi wengine tangu siku ya mwanzo akina Nape Nnauye walipokuwa wakitetea uamuzi wa serikali ya awamu ya tano kuzuia matangazo ya moja kwa moja ya bunge kupitia televisheni ya taifa kwa madai ya kubana matumizi, tulijuwa wameshachelewa. Si katika zama hizi za mawasiliano ya mitandao ya kijamii, ambapo nguvuhasa za mawasiliano zimo viganjani mwa watu! Kwamba huu si wakati tena wa kuwapangia watu cha kusikia, kuona, kusoma na kusikiliza, hata kama una sheria kali kama ya Uhalifu wa Mitandaoni iliyokimbizwa mbio mbio kupitishwa bungeni na utawala wa awamu ya nne wa Jakaya Kikwete kuuwahi uchaguzi wa 2015! Huwezi. Wengine tulishasema kuwa ukilizima ‘Bunge Live’ kupitia televisheni ya TBC, utakuja kukumbana na ‘Bunge la Wananchi’ kupitia televisheni nyingi zaidi za mitandaoni. Ki vipi? Likawa ndilo swali.
Nimetaja neno ‘nguvu’ hapo juu na hapa nitalifafanuwa. Watu wenye nguvu – na sio wenye maguvu – huwa wana mambo matatu yanayofanana. Kwanza, huwa wako wazi, hawajifichi na sio wale watu wasiojulikana; pili, huwa hawafi hata wakiuliwa na hubaki milele na, tatu, wanawafanya wengine kunena ama kutenda kwa niaba yao, wawepo ama wasiwepo. Na hao ni pamoja  na hata maadui zao.

Na Mohammed Ghassani
Sababu ni kuwa maana ya nguvu halisi ni ushawishi. Ule uwezo wa kumuathiri mtu nafsini na akilini mwake. Akawaza kama utakavyo wewe awaze na, hatimaye, akatenda kama utakavyo wewe atende – ama kinyume chake. Wanafalsafa husema: “Niwazavyo ndivyo nilivyo!”
Wakati naandika makala hii, bado mbunge wa Singida Mashariki na Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika, Tundu Lissu, anaendelea kupigania maisha yake kwenye chumba cha wagonjwa mahututi jijini Nairobi, Kenya – umbali wa kilomita 682, mwendo wa masaa 10 na dakika 16 kwa gari itembeayo kilomita 112 kwa saa kutoka mjini Dodoma, Tanzania, alikoshambuliwa Alhamis ya tarehe 7 Septemba.
Lissu yuko mbali kwelikweli kifizikia na kidhahania, maana hata huko Nairobi aliko, nako ananing’inia baina ya uhai na umauti. Lakini kiuhalisia, mwanasiasa na mwanaharakati huyu yupo ndani ya ardhi ya Tanzania, nchi anayoipigania ambayo kwayo akamwagwa damu yake. Mwangwi wa sauti yake unaakisika kwenye miji yote mikubwa na midogo, vyombo vyote vya habari vilivyo rasmi na visivyo rasmi, vikao vilivyo rasmi na visivyo rasmi vya wanasiasa, wanaharakati, na raia wa kawaida. Mote ni Lissu, Lissu, Lissu!
Nguvu ya Lissu ni kubwa kuliko inavyotazamwa
Ndio ujuwe namna msomi huyu wa sheria alivyo na nguvu za kweli. Hana mabavu ya kulazimisha watu kusema na kutenda, lakini ana ushawishi wa kuwafanya wengine wamuone shujaa wao. Bali hata kwa maadui zake, nguvu yake inawafanya waitikie mdundo wa ngoma inayopigwa naye. Maana yake ni kusema kuwa kumbe zile risasi zaidi ya 32 alizomiminiwa nyumbani kwake Dodoma, hazikuweza kuzivunja nguvu za Lissu, bali kinyume chake ni kuwa zimeziongeza mno kufikia umbali wa kuwapatia Watanzania kile kitu adimu ambacho walikuwa wanakililia tangu utawala wa awamu ya tano uanze. Matangazo ya moja kwa moja ya bunge – ‘Bunge Live’.
Ukisikia namna ambavyo uongozi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, hasa kupitia Spika Job Ndugai, unavyojitahidi kupapatua na kujibizana na wabunge wa upinzani kuhusu kadhia hii ya Lissu, unaweza kukiona ninachokusudia hapa. Kwanza alianza Mbunge Saeed Kubenea wa Ubungo, ambaye alizungumza kwenye ibada ya Jumapili ya Kanisa la Uzima na Ufufuo la Mchungaji Josephat Gwajima, akitaja mkasa mzima wa tukio la kushambuliwa Lissu na kutaja idadi tafauti ya risasi na zile alizozitaja Spika Ndugai hapo kabla. Matangazo ya ibada hiyo yalikuwa yakirushwa moja kwa moja na mitandao ya YouTube na Facebook.
Muda mchache, Spika Ndugai akaamuru Kubenea aitwe mbele za Kamati ya Maadili na Usalama za Bunge kuhojiwa eti kwa kukikashifu kiti kuwa kimesema uongo kwenye tukio la kushambuliwa Lissu. Kisha akaja Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, ambaye vidio yake ilisambaa pia mitandaoni akiwa Nairobi anakomuuguza Lissu akimkosoa Spika Ndugai kwa kutumia muda mwingi kupambana na Kubenea badala ya kushughulika na hali ya Lissu aliye kitandani.
Siku ya pili asubuhi, Spika Ndugai akasimama tena bungeni kutumia kiti cha uspika kumjibu Lema, akienda mbali zaidi ‘kusumbulia’ kuwa serikali na wabunge wa Chama chake cha Mapinduzi (CCM) ndio waliochangia kumsafirisha Lissu hadi Nairobi.
Dakika chache tu baada ya Spika Ndugai kuyasema hayo akiwa kwenye kiti cha enzi cha uspika makao makuu ya nchi, Dodoma, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, anapanda hewani kupitia ukurasa wa Facebook na mtandao wa YouTube akimsuta Ndugai juu ya anachokisema. Mchana wake, Mbunge wa Mpendae, Salim Turki, ambaye ndiye aliyetajwa na Spika Ndugai kuwa alilipia ndege ya kumpeleka Lissu jijini Nairobi kwa matibabu, akakanusha kuwa hakulipa, isipokuwa alidhamini na kwamba malipo yalifanywa na CHADEMA yenyewe. Vidio yake ikasambazwa mitandaoni – Facebook na YouTube.
Kufikia jioni, ofisi ya bunge ikaonekana kusalimu amri kwa kutoa taarifa ya kimaandishi kuweka sawa kauli ya Spika Ndugai juu ya utata huo wa malipo ya ndege ya Lissu. Tena nayo ikasambazwa kupitia ukurasa wa Facebook. Kwa hivyo, unapouangalia huu mtiririko wa mawasiliano ya moja kwa moja (mubashara) kati ya wabunge wa upinzani na kiti cha spika ndani ya kipindi hiki cha kushambuliwa Lissu, unapata picha kwamba kumbe bunge lilikuwa ‘live’.
Kwamba kumbe Lissu akiwa kitandani jijini Nairobi amelifanya bunge la Tanzania liruke moja kwa moja kupitia mitandao ya kijamii. Kubenea anasema kanisani, YouTube inarusha; Ndugai anaipata Dodoma, anajibu kwenye kiti cha spika.
Lema anaingilia kati kupitia Facebook na YouTube akiwa Nairobi hospitali; Spika Ndugai anarudi tena kitini pake kujibu. Msigwa anayaona majibu ya Spika hayafai, anashuka tena kwenye YouTube na Facebook; Ofisi ya Bunge inatoa waraka wa kimaandishi inausambaza mitandaoni kuweka mambo sawa.
Yote hayo, mote humo, kila kitu tunakipata mubashara, bila chenga, moja kwa moja kutoka Nairobi na Dodoma. Hata tunaoishi maelfu ya maili kutoka Dodoma, tunajuwa mapigo ya moyo ya bunge yanadundaje. Tunaweza kusoma kupitia uso wa Spika Ndugai, ile fadhaa iliyolikumba bunge  na, hapana shaka, nchi nzima kwa sababu ya mtu mmoja tu – Tundu Lissu.
Hivi ndivyo nguvu hasa inavyofanya kazi. Ndipo unapojuwa kuwa, kama ilivyosemwa awali, kumbe pana tafauti baina ya kuwa na nguvu na kutumia mabavu. Wakati waliotaka kumuua Lissu walitumia mabavu kuizima nguvu yake, yeye anatumia nguvu yake kuyazima mabavu yao.
Walidhani kwamba kama jaribio la tarehe 7 Septemba lingefanikiwa, hivi sasa Lissu angelikuwa ameshalala pima sita chini ya ardhi. Wamemzima na kumnyamazisha. Kama alivyosema mwenyewe: “Tutanyamaza tukiwa makaburini mwetu!”
Lakini uhalisia wa nguvu umenena vyengine. Sio tu kwamba risasi hazikuweza hapo hapo kuondoka na roho yake, bali pia akiwa anapigania uhai wake huko Nairobi aliko, Lissu amekuwa kama kwamba yumo ndani ya viunga vya – kama si kwenye ukumbi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano – Dodoma.
Hakuna siku ilipita bila kutajwa. Hakuna gazeti limewahi kuchapishwa bila habari yake ya moja kwa moja au isiyo ya moja kwa moja. Hakuna televisheni wala redio imewahi kumaliza matangazo yake bila kuonesha picha yake. Hakuna mtandao wa kijamii hata mmoja – iwe Facebook, Twitter, YouTube, Instagram ama hata makundi ya WhatsApp – unaweza kupitisha siku bila Lissu kuwamo ndani yake.
Katika uzima wake na katika ugonjwa wake, nguvu za Lissu ni kubwa mno kuweza kuzuilika kwa mabavu yoyote yawayo. Ndiyo thamani ya kuwa upande wa ukweli. Unakuwa huzami chini. Wakupendao watakuhusudu, wakuchukiao watakuhishimu!
Ndio maana hata akiwa katikati ya uhai na umauti, Lissu amesimama imara na kuwapatia Watanzania kile wakitakacho. Ukweli na ujasiri na uthubutu.
Baadhi ya wakati, kheri yaweza kuzaliwa kutoka matumboni mwa shari na hakuna kipindi ambacho hayo yamedhihirika wazi kuliko juma hili moja tangu Lissu apigwe risasi!
TANBIHI: Makala hii ilichapishwa mara ya kwanza na gazeti la Mwelekeo la tarehe 19 Septemba 2017 chini ya kichwa cha habari “Lissu katupa Bunge Live”.

No comments: