Saturday, 30 May 2020

ZANZIBAR KUMEKUCHA

Zanzibar 2020: CCM itayaepuka makosa haya manne ya kimkakati?
May 30, 2020|Habari, Makala, Siasa


Oktoba mwaka huu wa 2020 Zanzibar inaingia katika Uchaguzi Mkuu wa Wawakilishi, Wabunge na Rais. Vyama viwili vinatarajiwa kuwa na nguvu kubwa katika uchaguzi huu, kwa maana ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na chama cha ACT Wazalendo.

Katika kila chaguzi Jumuiya ya Kimataifa imekuwa ikiinyoshea kidole Zanzibar kutokana na mapungufu makubwa yanayoweka demokrasia na haki za binadamu hatarini. Mbali na hilo, kinara wa siasa za upinzani Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad kila wakati ameeleza bayana kwamba upinzani umeshinda na kuporwa chaguzi zote za Rais visiwani Zanzibar toka mwaka 1995 mpaka 2015.

CCM inaingia katika Uchaguzi Zanzibar 2020 ikiwa na majeraha mengi ya mishale mgongoni kutokana na kulazimika kila mara toka mwaka 1995 hadi 2015 kutumia nguvu nyingi ya dola kuhalalisha ushindi wake na wakati mwingi hadi kuwepo kwa umwagaji damu.

Swali wanalojiuliza wachambuzi wengi wa siasa za Zanzibar, Tanzania na Afrika kwa ujumla ni je namna gani mwaka huu CCM itaweza tena kushinda visiwani humo na kuonekana imeshinda kihalali? Ikumbukwe kwamba kadiri kila miaka inavyosogea imezidi kuwa ngumu kwa CCM kuhalalisha ushidi wake Zanzibar mpaka kufikia wakati kulazimishwa kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (GNU), ambayo ilifanya mabadiliko kwenye Katiba ya Zanzibar na CCM na CUF kuwa wabia katika SMZ, ubia ambao ulivunjika baadaye.

Wajuzi wa siasa za Zanzibar wanataja mambo makubwa manne yanayoweza kuipa CCM walau nafasi ndogo ya kuhalalisha (legitimize) ushindi wake Zanzibar 2020, iwapo wataupata.

Jambo la kwanza ni kuteua Mgombea atakayekubalika ndani ya CCM Zanzibar wenyewe, walau kwa asilimia 80. Historia inaonyesha kufeli kwa CCM Zanzibar kuanzia kura za Wawakilishi, Wabunge hadi Rais hutokana na kulazimishiwa wagombea wasopendwa na wanachama hivyo kuigawa CCM hata kabla haijakwenda uwanja wa mapambano dhidi ya wapinzani. Kosa hili la kimkamkati (strategic blunder) hutoa goli la kwanza kwa upinzani kabla hata ya kupulizwa kwa kipenga cha kampeni. Hesabu ya kawaida ya siasa, kadiri kundi la wanachama wasompenda mgombea fulani linavyokuwa kubwa ndivyo kura zake zinavyozidi kupungua kwani sasa anakosa kura za CCM wenyewe ambazo kwa siasa za Zanzibar na uchache wa kura, anguko linakuwa dhahiri. Makosa ya namna hii yameonekana katika takwimu za kura za majimbo mengi Zanzibar na muhanga mmojawapo ni Profesa Makame Mbarawa aliyekosa Ubunge mara mbili (Mkanyageni 2010 na Mkoani 2015) kutokana na uteuzi wake kupokelewa kwa shingo upande ndani ya chama chake mwenyewe.

Jambo la pili ni wapi anatoka Mgombea wa Urais kati ya Unguja na Pemba. Siasa za unasaba Zanzibar zina mizizi imara na moja ya sheria isiyoandikwa (unwritten rule) ya miaka ya karibuni ndani ya CCM ni ile ya kupokezana kwenye Urais kwamba akitoka Muunguja basi aingie Mpemba, ama akitoka Mpemba afate Muunguja. Rais wa sasa Dkt Shein ni mzaliwa wa Chokocho Pemba, aliyemtangulia (Amani Karume) ni kutoka Unguja. Kihesabu, wahafidhina wa Unguja ambako ndiko kwenye ngome imara ya CCM visiwani Zanzibar lazima watataka mgombea atoke kwao 2020. Katibu Mkuu wa CCM na mwanazuoni mbobezi kwenye Sayansi ya Siasa Dkt Bashiru Ally amewahi kukiri hadharani kwamba, CCM haiendeshwi tu kwa Katiba yake bali pia ina kanuni zisizoandikwa na mapokea na iwapo hilo ni sahihi tunaweza kuona ikafuata njia hiyo ya kupokezana kati ya Unguja na Pemba.

Jambo la tatu ni namna ya CCM kupata kura Pemba. Iwapo Rais wa Zanzibar atatoka Unguja, Makamu wa pili atatoka Pemba lakini kimkakati hii peke yake haitoshi kuhakikisha CCM wanapata kura (hata hizo chache) Pemba. Katika hili CCM itabidi iwape nafasi zaidi Pemba katika ushiriki kwenye meza ya uongozi (quid pro quo/nipe kitu, nikupe kitu) na hii huenda ikawa nafasi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa takribani miaka 10 sasa Pemba haijawa na kiongozi yeyote mwandamizi (Waziri Mkuu, Rais au Makamu) katika Serikali ya Muungano hivyo basi iwapo CCM itafanya hilo inaweza kujihakikishia walau kura chache Pemba kujipa na kujipa uhalali.

Jambo la nne ni haki kutendeka katika uchaguzi na kuonekana kwamba imetendeka. Hili nalo lina sura mbili. Moja CCM haiwezi kuanza kampeni ikiwa na Mgombea asiyekubalika na kundi kubwa hata ndani ya CCM yenyewe, halafu ioenekane kushinda uchaguzi. Pili CCM lazima ijenge mtandao wa ushawishi kiitikadi na uenezi Zanzibar wenye nguvu si tu ndani ya Zanzibar bali kimataifa kama wenzao ACT. Mkakati wa kutambua na kutenda kabla ya jambo (pro-active), na sio wa kukaa kujitetea yanapowafika huku ikipokea masumbwi toka upinzani kitaifa na kimataifa. Katika eneo hili la uenezi kimataifa na kitaifa ACT Wazalendo wanaonekana kujipanga zaidi, na CCM lazima kufanya hivyo iwapo inataka kuonyesha dunia kwamba safari hii itashinda Zanzibar na itashinda katika haki.

Kitatokea nini iwapo CCM itafanya makosa ya kimkakati katika mambo hayo manne?

Iwapo CCM itaboronga kwenye mambo haya manne ya kimkakati japo wengi wanaamini ni jambo gumu kutokea, basi CCM ijiandae kuingia tena katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar kati yake na ACT Wazalendo. Iwapo ACT itafanikiwa kuingia katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa basi kwa namna ya mwelekeo wa mikakati yake, ushawishi nyumbani, umataifa, mabadiliko ya kizazi, siasa na aina ya uongozi (generational shift) na oganaizesheni yake inaweza kuwa mwanzo wa CCM kuondoka madarakani Zanzibar miaka michache mbele.

Maalim Seif Sharif Hamad bado ana nguvu kubwa ya ushawishi ndani ya Zanzibar na bado anao uwezo wa kwenda pasu kwa pasu au hata kuwazidi CCM katika sanduku la kura. Kitu ambacho Maalim na timu yake walikosa ni taasisi imara yenye mtandao wa kimataifa na mikakati bora ya kupigia kelele wizi wa chaguzi kimataifa kwa kiwango cha juu na kushinikiza haki kupatikana. Upungufu huo ndio ACT Wazalendo wanakwenda kuuziba na kuifanya hali ya CCM Zanzibar kuwa tete hasa wakifanya makosa hayo manne ya kimkakati. Kiongozi wa ACT Wazalendo Zitto Kabwe ni kijana, msomi mwenye mapungufu yake lakini mwenye uwezo mkubwa wa kuzifikia na kushawishi taasisi na jumuiya ya kimataifa kuhusu mambo ya kidemokrasia na haki za binadamu. Hili amelionesha mara nyingi, mfano hapa majuzi kupelekea hadi mkopo wa Benki ya dunia kwa Tanzania wa dola milioni 500 kusitishwa, kitendo ambacho CCM walitumia kila silaha waliyo nayo kupambana naye. Wakati wa uchaguzi utete wa hali utakuwa maradufu.

Mwandishi wetu Zanzibar

No comments: