Tuesday, 7 July 2020

KARIBU MEMBE: TAMKO LA VIONGOZI WA ACT WAZALENDO MIKOA YA LINDI, MTWARA, MKOA WA KICHAMA SELOU NA PWANI KUMUOMBA WAZIRI WA MAMBO YA NJE MSTAAFU NDUGU BERNARD MEMBE KUJIUNGA NA CHAMA CHA ACT WAZALENDO.



KARIBU MEMBE: TAMKO LA VIONGOZI WA ACT WAZALENDO MIKOA YA LINDI, MTWARA, MKOA WA KICHAMA SELOU NA PWANI KUMUOMBA WAZIRI WA MAMBO YA NJE MSTAAFU NDUGU BERNARD MEMBE KUJIUNGA NA CHAMA CHA ACT WAZALENDO.

Jana tarehe 6/7/2020, aliyekuwa  Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania na kada wa muda mrefu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)  Ndugu Bernard Kamilius Membe alitangaza rasmi kuacha jitihada za kupigania uanachama wake ndani ya CCM baada ya kufukuzwa na Kamati Kuu ya CCM kinyume hata na Katiba ya Chama hicho.

Leo tarehe 7/7/2020 sisi viongozi wa Chama cha ACT Wazalendo wa Mikoa ya Lindi, Mtwara, Mkoa wa Kichama Selou na Pwani tumekuja hapa Kijijini Rondo anapoishi kumletea ombi maalumu la kujiunga na Chama chetu.
Siku ya tarehe 30/6/2020 Kiongozi wa Chama Ndugu Zito Kabwe  akihutubia wanachama  katika mkutano wa ndani uliofanyika Kilwa Kivinje, alimualika Ndugu Bernard Membe kujiunga na vyama vya upinzani ili  kuja kuongeza mshikamano kuhami demokrasia na kuleta mabadiliko ya utawala nchini. Kwetu sisi wito huu ulikuwa ni hatua muhimu kuelekea mageuzi makubwa ya kisiasa hapa nchini.

Uamuzi wa Ndugu Bernard Membe kurudisha kadi ya CCM tumeupokea kwa matarajio makubwa. Hii ni kwa sababu uamuzi huu unafungua milango kwa yeye kuchagua kujiunga na vyama vya siasa vya upinzani nchini ikiwa ataona inafaa.

Ndugu Bernard Membe, sisi kama viongozi wa kisiasa tumekuwa tukifuatilia kwa umakini, misimamo, muelekeo na mtazamo wako kuhusu demokrasia, haki na utawala wa sheria. Kwa hakika tunaamini kuwa hayo ndiyo yaliyokufanya ufukuzwe CCM. Hata hivyo mambo haya uliyoyapigania ukiwa ndani ya CCM ni hitajio kubwa la taifa letu.

Utawala wa awamu ya tano umeshitadi katika ukandamizaji wa haki, demokrasia, uhuru wa mawazo  na utawala wa sheria. Ili kukabiliana na tatizo hili tunaamini nguvu ya pamoja, uzoefu wa kiuongozi na utawala  vinahitajika.

Ni kwa msingi huo ndiyo maana sisi viongozi wa ACT Wazalendo   mikoa ya Lindi, Mtwara, Selou na Pwani  tumekuja hapa kukuomba  ujiunge na chama chetu cha ACT Wazalendo. Chama chetu kimejipambanua kwa kupigania haki, demokrasia, utawala wa sheria , mashirikiano ya vyama vya siasa na wadau wengine ili kuleta mabadiliko ya kiutawala na kuhami demokrasia nchini.

Kwa nini sisi? Pamoja na ukweli kuwa wewe ni kiongozi wa  kitaifa na siku zote umepigania maslahi ya kitaifa, lakini pia unatokea kusini.
Mwenyekiti wa CCM Taifa Rais john Pombe Magufuli amewahi kutamka wazi mara baada ya wabunge wa Kusini na Pwani pamoja na Chama chetu kupigania fedha za wakulima wa korosho zaidi ya shilingi bilioni 221 kuwa, yuko tayari kupoteza  majimbo yote ya CCM kusini ikiwemo la Waziri Mkuu lakini Serikali haitarudisha fedha za wakulima wa korosho. Aidha alienda mbali kwa kueleza kuwa ikiwa tutaandamana kudai haki yetu hiyo basi tutapigwa akianza na shangazi zetu.

Tunaona fahari ikiwa sisi tutawaongoza wengine  kukuomba uje kujiunga na Chama hiki ili ushiriki mapambano ya kujikomboa ili kurejesha utawala wa sheria, haki na demokrasia nchini.
Ni matarajio yetu kuwa utatukubalia na kujiunga na ACT  - Wazalendo.

Tamko hili limesomwa na  Isihaka Rashid Mchinjita, Mwenyekiti Mkoa wa Lindi na Mjumbe wa kamati kuu. Limeandaliwa na,

1. Isihaka Rashid Mchinjita – Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Mkoa wa Lindi na Mjumbe wa Kamati Kuu 
       
2. Abdallah saidi Mtalika  -   Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Mkoa wa Kichama wa Selou       
                                                       
3. Alphonce Andrea Hitu -   Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Mkoa wa Mtwara     
                                                   
4. Mrisho  Khalfani  Swagara-Mwenyekiti Mkoa wa Pwani                                                     

Asanteni.

No comments: