Friday, 3 July 2020

WATANZANIA WANAISHI NCHI YA UCHUMI WA KATI?

Watanzania wanaishi Nchi ya Uchumi wa Kati? - Zitto Kabwe

Tangu jana nimeona shamrashamra kubwa kuhusu kinachoitwa mafanikio ya Tanzania kuwa nchi ya Uchumi wa Kati. Kuingia Uchumi wa Kati ni hatua nzuri lakini inayohitaji ufafanuzi wa kiuongozi. Hatua hii ikifanyiwa  propaganda itaonekana kuwa Serikali ya Awamu ya Tano wana uhaba wa mafanikio au hawajui wanachoshangilia. Ni muhimu sana kutambua kuwa kufikia hatua  hii ni mchango wa awamu zote zilizotangulia na wananchi wa Tanzania na si matokeo ya awamu moja au miaka 5 tu.

Benki ya Dunia inaitambua nchi kuwa ya Uchumi wa Kati pale ambapo Pato la Wastani la Wananchi wake lipo kati ya Dola za Marekani 1,090  hadi 12,235 kwa mwaka. Katika kundi hili kuna Uchumi wa kati wa chini kabisa, Uchumi wa kati wa chini, Uchumi wa kati kati na Uchumi wa kati wa Juu. Kwa kimombo zinaitwa Lower Middle Income, Low Middle Income, Middle Income, Upper Middle Income.
Hiki kinachoshangiliwa hapa kwetu ni ile hatua ya kwanza, yaani tupo Getini kabisa. Pato la Wastani la kila Mtanzania limevuka Dola za Marekani 1,090 ( taarifa pia zinaonyesha kuwa Benki ya Dunia imeshusha vigezo na hivyo kupanua Goli ).

Hichi kipimo kinachotumika ni nini ?

Pato la Wastani (income per capita) ni jumla ya Pato la Taifa (GDP) ukiligawa kwa kila Mtanzania mpaka mtoto mdogo aliyezaliwa leo.
Yaani unachukua mapato ya Watanzania matajiri kama kina Bakhresa, Rostam Aziz, Mohamed Dewji na kadhalika, pamoja na Mapato ya vijana waendesha bodaboda, wakulima wa nyanya Ilula-Iringa na watu wasio na kipato kabisa kisha ugawe kwa kila Mtanzania kwa sawa. Kinachopatikana ndio wastani wa Pato la kila Mtu.
Ni hesabu za nadharia tu. Ni muhimu sana kuelewa nadharia hii kwamba wastani wa Pato la mtu ni Hesabu tu ya kujumlisha na kugawanya lakini sio uhalisia wa Pato la Mtu.

Pato la Taifa la Tanzania kwa bei za mwaka 2019 lilikuwa shilingi Trilioni 139. Mwaka 2019, Tanzania Bara ilikadiriwa kuwa na Watu Milioni 54 ambapo Pato la wastani la kila mtu lilifikia shilingi 2,577,967. Kiasi hicho cha pato la wastani kwa kila mtu kwa mwaka 2019 ni sawa na dola za Marekani 1,096 hivyo kuwa tumevuka kiwango cha Benki ya Dunia cha kuwa na Uchumi wa Kati.

Mwaka 2015, Pato la wastani la Mtanzania lilikuwa limefikia wastani Dola za Marekani 1,060. Kwa hiyo tulikuwa tumepungukiwa Dola za Marekani 30 tu ili kufikia ‘Lower Middle Income’ ambayo ndio tumeifikia sasa. Imetuchukua miaka 5 kuongeza $30 kwa kila Mtanzania kama wastani wa Pato lao.
Kwa wastani kila Mwaka Serikali imeweza kuongeza wastani wa Dola 6 tu kwa Mwaka kwa kila Mtanzania, yaani shilingi 14,000 tu kwa fedha za kitanzania.

Hatujafikia Lengo

Maendeleo ya Tanzania yanaongozwa na Mpango wa Maendeleo ya Taifa. Lengo letu kwenye Mpango huo ni “Tanzania kuwa nchi ya Uchumi wa kati wa wastani wa Pato la mtu kufika Dola za Marekani 3,000 ifikapo 2025. Kuvuka mpaka na kufikia hatua tuliyofikia ni hatua muhimu na ya kufurahisha lakini bado hatujafika safari yetu.

Kama imetuchukua miaka 5 kuongeza Dola 30, itatuchukua miaka mingapi kuongeza Dola 2,100? Hii maana yake ili kufikia Wastani wa Pato la Mtanzania la Dola za Marekani 3,000 kwa Mwaka, katika miaka 5 ijayo, tunapaswa kuongeza pato letu maradufu. Bado tuna mwendo mrefu kufikia lengo letu la kuwa na Uchumi wa Kati.

Nimeshangaa sana kuona Kuwa Baadhi yetu wakiwemo viongozi wanatamka kuwa Tanzania imefikia lengo la uchumi wa Kati miaka 5 kabla ya muda uliopangwa. Sio kweli kwani lengo tulilojiwekea ni Dola za Marekani angalau 3,000 kama Pato la Wastani la kila Mtu kwa Mwaka. Kusema kuwa tumefikia lengo ni dalili kuwa tuna uhaba wa mafanikio, tena uhaba mkubwa. Lakini pia kuna hatari kubwa ya kutoka kwenye mstari wa utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa kujidanganya kuwa tayari tumefikia lengo.

Hata kama tungekuwa tumefikia lengo tulilojiwekea bado tunapaswa kupokea habari ya nyongeza ya wastani wa pato kwa kila mtu kwa tahadhari kubwa sana. Kuna faida na hasara ya kupanda daraja hili. Ukiwa ‘under developed low income country’, faida yake ni kupata misaada na mikopo yenye unafuu mkubwa. Ni sawa na mtoto mdogo anayepewa vyakula vya kupondwa pondwa. Hii inatoa ahueni kubwa kwa nchi kujijenga kiuchumi. Ukifaulu na kuingia kwenye kundi la uchumi wa kati hii mbeleko inaondoka. Sasa utapaswa kukopa mikopo ya kibiashara zaidi ambayo riba yake ni kubwa. Kwa lugha nyingine, mikopo inakuwa ghali na misaada inapungua sana.  Yaani matarajio ni kuwa sasa umekuwa mkubwa ujitafunie. Mikopo ya Biashara ambayo tayari tumeanza kuchukua kiasi cha kuwa 34% ya Deni la Taifa. Benki ya Dunia imetoa mwanya wa Deni letu la Taifa kuwa kubwa na lenye gharama kubwa kulihudumia.

Faida ya kuwa uchumi wa kati ni kwamba ukomo wa Nchi wa kukopa katika masoko ya Fedha na mitaji inapanuka kuliko sasa. Hivyo unaweza kufanya mambo makubwa zaidi. Hasara yake ni gharama ya mikopo hiyo inaumiza uchumi ambapo mara nyingi sana unakuwa si imara sana kwa kuwa mara nyingi, uchumi huo hubebwa  na takwimu tu ambazo zinaweza zisiakisi maisha halisi ya watu.

Mathalan, nchi zenye madini na mafuta, pato la Taifa linaweza kuonekana kubwa lakini vigezo vya hali ya maisha ya watu (Human Development Index) ikawa chini sana. Nchi nyingi za Low Middle Income zinalalamika sana kuomba zifikiriwe upya na mashirika ya kifedha. Baadhi ya Nchi zinaomba kwa Benki ya Dunia zishushwe daraja ili kukwepa hasara hizi. Sisi tunashangilia sana. Nadhani hatujui tunachoshangilia ni nini.

Kwa Nchi kama yetu ni muhimu sana Viongozi kuwa na uwezo mkubwa wa kutofautisha kati ya Uchumi wa Takwimu na Uchumi Halisi wa Wananchi. Uhalisia ni kuwa uchumi wa wananchi ni goi goi sana. Hali ya maisha ya wananchi imeanguka kutokana na kupungua kwa shughuli za uchumi za uzalishaji mali. Katika miaka 5 Serikali ya Awamu ya Tano imetumia Bajeti ya Shilingi Trilioni 162 sawa na wastani wa Dola za Marekani 1,173 ukizigawa kwa kila Mtanzania. Hata hivyo katika miaka hiyo 5 Pato la Mtanzania limeongezeka kwa Dola za Marekani 30 tu. Hii maana yake ni kuwa Matumizi yetu ya Bajeti hayaongezi shughuli za Uchumi za Wananchi wengi.

Kwa mfano, wakati tumetumia Shilingi 1.8 Trilioni kwenye matumizi ya kununua Ndege 11 zinazotumiwa na 5% ya Watanzania, katika miaka 5 tumetumia Shilingi Trilioni Moja tu kwenye matumizi ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi zinazotegemewa na 67% ya Watanzania. Bajeti hii ya Kilimo ni 0.6% ya Bajeti yote ya Tanzania kwa miaka 5.

Kutokana na Hali hiyo ya matumizi yasiyozingatia shughuli za uchumi za wananchi, taarifa ya Benki ya Dunia (Tanzania Economic Upadte number 11 ) inaonyesha kuwa jumla ya Watanzania 2.7 milioni wameingia kwenye dimbwi la umasikini Kati ya Mwaka 2017-2019. Unakuwaje Nchi ya Uchumi wa Kati wakati mamilioni ya Wananchi wanakuwa masikini kila mwaka ?

Nimalizie kwa kusema kuwa, kwa kasi tuliyokuwa nayo kwa miaka 5 iliyopita inatia mashaka ikiwa tutafika lengo letu la Uchumi wa Kati miaka 5 ijayo  iwapo tukiendelea na maono haya, fikra hizi na matendo haya. Kuvuka mpaka ni hatua muhimu na ya kufurahisha lakini bado hatujafika safari yetu. Mpango wa Taifa unatutaka tufikia Pato la Kila Mtu la walau Dola za Marekani 3,000 kwa Mwaka ifikapo 2025.

Kufikia lengo hili inakuja na wajibu mkubwa kwa kila mmoja wetu kama Taifa na tunahitaji Uongozi na maono mapya. Tunahitaji Wananchi wawe na Raha na Furaha, wakifanya Kazi kwa bidii na kufurahia matunda ya jasho lao ( #KaziNaBata ).

Lindi, Tanzania
3/7/2020

No comments: