Friday, 10 July 2020
UCHAMBUZI WA UTEUZI WA HUSSEIN MWINYI
Wafuatiliaji wa Mambo ya siasa hapa Zanzibar wametuletea tathmini hii fupi mara baada ya NEC ya CCM kumteua Dkt Hussein Mwinyi.
Kwanza baadhi ya wana CCM wamenuna wakilalamika kwamba wazanzibari hawana tena chaguo lao kwenye CCM, isipokuwa Upande wa Bara ndio unamuweka Mtu mwenye Maslahi yao.
Kuingizwa Dkt Khalid na Shamsi kwenye tatu bora kulilenga kuzigawa kura za Zanzibar hasa Unguja ambapo kura zimeelekea zaidi kwenye maeneo ya watu wanakotoka. Shamsi kaungwa mkono kwa kura 16 ikiaminiwa zaidi ni wajumbe wa NEC kutoka Kusini Unguja na Khalid kura 19 kutoka Kaskazini Unguja ambapo anatoka. Dkt Hussein kanufaika na kura za NEC bara na baadhi ya kura za mijini Magharibi ambazo zinanasibishwa na watu kutoka Tanzania Bara ambao ni wazanzibari wenye maslahi na Bara.
Kelele za kumkataa Mnyaa ambae inasemekana alikuwa chaguo la Watawala zilipindisha maamuzi mapenma ili kuepuka chuki ya wazi ambayo ingekigawa chama. Mwenyekiti na Timu yake walishtuka mapema. Taarifa zinabainisha ndio sababu ya kupelekwa Shamsi na Khalid ili kutuliza mpasuko wa kura za Unguja za mkoa wa Kaskazini na kusini.
Waliopanga mchezo walitegesha ilimradi maslahi ya Bara yamezingatiwa. Acha Mbarawa atote lakini Mwinyi apite na Bara ipete huo ndio msemo wa Mwisho ' Acha Mbarawa atote, Mwinyi apite na bara ipete"
KWA NINI MNYAA alilazimika kuachwa?
Nimeeleza kidogo. Huyu alihesabika mtu asiyewafaa wana CCM wahafidhina na wale maslahi. Ukweli ni kwamba Rais MAGUFULI anaogopwa na hata CCM wenzake. Zanzibar kuna utamaduni wa ulaji na kupendeleana sana . Ufisadi ndani ya serikali ni mkubwa na huwa wanalindana.
Prof Alihatarisha maslahi ya wana CCM waliozowea kudekezwa. Lakini upepo wa Upemba na kuwa mtu wa Mwenyekiti anaeogopwa ulilazimisha watu kushikamana wasikose yote. Walau Dkt Mwinyi angetosha na kweli ametosha baada ya kura za Kusini na Kaskazini Unguja kugawiwa.
Kwa kiasi kupitishwa kwa Dkt Mwinyi kuna usalama wa wastani kwa CCM kuliko angepitishwa Mnyaa. Mwenyekiti ameruka mtego kiasi.
"NGUVU YA MFUMO ULIOKWISHWA KUMUANDAA DKT MWINYI NA USALAMA WA CHAMA UMEPINDISHA MSIMAMO WA MWENYEKITI KWENYE DAKIKA 15 KIPINDI CHA KWANZA". Nguvu hiyo imemtoa Prof kwenye reli.
Siasa ni hesabu.
Almuradi CCM kindaki kindaki na wana ASP asili wamenuna. Ila kwa wahafidhina wasioitakia mema Zanzibar kidogo wameshusha pumzi kuliko angepita Mnyaa.
Watu wamenuna kiasi na picha nyengine ya kudharauliwa chaguo halisi la Zanzibar kwa wana CCM limedhihiri tena.
KUHUSU DKT MWINYI.
Huyu aliandaliwa mapema kuja kushika nafasi ya urais wa Zanzibar na tetesi zinasema hata urais wa JMT huko mbele.
Ana aminiwa kuwa ametengenezwa kuulinda Muungano kuliko CCM wengine ambao mara kadhaa huzusha zogo pale maslahi yao yanapohojiwa ndani ya CCM Zanzibar . Alitengenezwa sana huyu LAKINI Utawala uliopo haukumpa kipaumbele kwa kuepuka makambi yaliyoko Bara.
Utawala uliopo unamuona ni zao la wale wale waliozoea kubweteka na wasiosimamia maamuzi ya hapa kazi tu lakini mfumo ndio uliokwisha kumuandaa.
Bye bye Zanzibar. Usiniulize kwa nini.
Kwa hisani ya wanachimbo walioko Field Zanzibar
Kishada
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment