Saturday 1 June 2013

Dr Shein Uwe Mkweli Kwa Vitendo sio maneno tu ! Action speak Louder !

Dk Shein : Hatima ya Katiba ya Muungano itaamuliwa na wananchi wenyewe





Na Said Ameir, Nanjing China

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amewahakikishia watanzania wanaoishi katika Jimbo la Jiangsu nchini China kuwa hatima ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaamuliwa na wananchi wenyewe na si vinginevyo.


Dk. Shein amesema mchakato wa mabadiliko ya Katiba unaosimamiwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba unaendelea vyema na umefikia hatua nzuri ya uchambuzi wa maoni ya wananchi ambapo rasimu ya maoni hayo yatawasilishwa kwenye mabaraza ya katiba kwa majadiliano zaidi.


Dk. Shein amesema hayo wakati wa mkutano na watanzania ambao wengi wao wanafunzi wanaosoma katika vyuo vikuu vilivyoko katika Jimbo la Jiangsu uliofanyika katika hoteli ya Sofitel mjini Nanjing jana katika siku yake ya pili ya ziara yake ya siku tatu katika jimbo hilo.


“Tume imakamilisha awamu ya kukusanya maoni ya wananchi na sasa iko katika hatua ya uchambuzi wa maoni hayo ili kuandika rasimu ya kwanza ambayo nayo itapelekwa katika mabaraza ya Katiba kujadiliwa” Dk. Shein alieleza.


Alifafanua kuwa mchakato huo ni wa uwazi, hakuna uficho wa aina ye yote na unafanyika kwa kufuata njia za kidemokrasia hali ambayo umepata sifa kutoka nje kwa kuwa nchi nyingine zimeshindwa kufanya mabadiliko ya katiba zao kwa mfumo huo.
Dk. Shein amesema wananchi hawapaswi kuwa na mashaka au kuleta sintofahamu katika jamii kwa kuwa kila mmoja amepewa fursa ya kushiriki katika mchakato huo hatua kwa hatua hadi kufikia kupata katiba mpya kama ilivyopangwa.


“Mchakato umewashirikisha wananchi kutoka hatua ya kwanza ya kutoa maoni, mijadala katika mabaraza ya katiba, Bunge na Baraza la Wawakilishi hadi kuipigia kura rasimu ya mwisho”aliwaeleza wanafunzi hao.

Alifafanua kuwa rasimu ya mwisho itakayopitishwa na Bunge itapigiwa kura kupitishwa kwake kunahitaji kuungwa mkono na pande zote mbili za muungano.


Dk. Shein amewaambia wanafunzi hao kuwa amefanya ziara nchini humu kwa lengo la kuimarisha uhusiano kati ya Tanzania na China na kwamba hilo si jambo la bahati mbaya kwa sababu ushirikiano huo ni muda mrefu.

“Nchi zetu zimekuwa na ushirikiano kwa miaka mingi na sasa tumekuwa ndugu ambao tunasaidia kwa hali na mali ”alisema na kuongeza kuwa Mpango wa Ushirikiano kati ya China na Afrika ambao umepangiwa dola za kimarekani bilioni 20 Tanzania nayo itafaidika.

Rais wa Zanzibar amewaeleza wananfunzi hao kuwa hali ya mipaka ya Tanzania ni salama na hakuna migogoro na majirani na kuongeza kuwa hivi sasa mchakato wa utekelezaji wa ushirikiano katika Jumuiya ya Afrika Masjhariki unaendelea vizuri.

“Haja ya viongozi waanzilishi wa Bara la Afrika ni kutaka shirikisho la kisiasa Afrika lakini hilo ni vigumu kulitekeleza lakini sisi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki lengo letu ni kuwa na serikali moja ya shirikisho lakini ili kupata ufanisi mchakato wake unakwenda hatua kwa hatua kufikia huko ” alifafanua.

Katika mkutano huo wanafunzi walipendekeza wataalamu watanzania walioko nje washirikishwe katika mipango ya serikali ya kubadilishana wataalamu katika nchi waliko kwa kuwa mara nyingine wako wataalamu wageni wangependa kwenda Tanzania lakini hawajulikani au hakuna mtu wa kuwasaidia kutimiza azma yao.

Hii ni mara ya pili kwa Dk. Shein kukutana na watanzania wanaoko nchini wakati wa ziara yake inayoendelea hivi sasa nchini humo. Mara ya kwanza alikutana na watanzania wanaoishi katika jiji la Beijing.

No comments: