Wednesday, 8 January 2014

TANGANYIKA HAKUNA WAKUIZUIA TENA !

SASA tunayajua yaliyomo ndani ya Rasimu ya Pili ya Katiba ya Tanzania inayopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba inayoongozwa na Jaji (mstaafu) Joseph Warioba.  Yote yako bayana.
Kupatikana kwa rasimu hiyo ya pili ambayo Jumatatu wiki hii alikabidhiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Jakaya Kikwete pamoja na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, kunahitimisha kazi za Tume ya Katiba zilizoanza Mei 3, 2012 kwa ukusanyaji wa maoni ya wananchi na kufikia kilele cha mwanzo ilipotolewa Rasimu ya Kwanza Juni 4, 2013.
Tume hiyo sasa inavunjwa ingawa mwenyekiti wake atabakiwa na jukumu moja la kulitekeleza: Februari mwakani ataiwasilisha kwa kuisoma Rasimu ya Pili ya Katiba mbele ya Bunge Maalumu la Katiba ili ijadiliwe na kupitishwa au kutopitishwa na Bunge hilo.
Rasimu hiyo ikipitishwa basi hatua itakayofuatia hapo itakuwa ni kuiwasilisha kwa wananchi watoe uamuzi wao kupitia kura ya maoni itayopigwa mwakani.
Warioba ameona mbali. Amesimama imara licha ya kupakwa kila aina ya matope na kutukanwa hasa kwa sababu ya pendekezo la Tume yake katika Rasimu ya Kwanza kuhusu muundo wa Muungano. Ameonyesha uadilifu wa kusimamia haki bila ya kuyumbishwa ijapokuwa yeye ni mkereketwa wa chama kinachotawala.

La muhimu alilofanya Warioba ni kuifufua Tanganyika katika utaratibu mpya wa kuufanya Muungano wa Tanzania uwe na muundo wa Shirikisho baina ya Nchi Washirika, yaani Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, nchi ambazo wakati zilipokuwa zinaungana kila moja yao ilikuwa ni dola huru yenye mamlaka yake kamili.
Katika hotuba aliyoitoa wakati wa kuikabidhi Rasimu ya Pili kwa Kikwete na Shein, Warioba alikiri kwamba suala la Muungano, na hasa muundo wa Muungano, lilikuwa suala lililojadiliwa kwa hamasa kubwa na wananchi.
Warioba aliongeza kusema kwamba asilimia 13 ya wananchi wa Tanzania Bara walitaka pawepo serikali moja, asilimia 24 walipendekeza serikali mbili na asilimia 61 walipendekeza muundo wa Muungano wenye serikali tatu. 
Hii takwimu ya mwisho ni kinyume kabisa na baadhi ya wenye midomo mirefu walivyokuwa wakitwambia na walivyotaka tuamini kwamba watu wengi wa Bara wanapendelea mfumo wa serikali moja. Ukweli ndio huo ulioibuliwa na Tume ya Katiba.
Ama kwa upande wa Zanzibar asilimia 34 walipendekeza serikali mbili, asilimia 0.1 walitaka serikali moja na asilimia 60 walitaka Muungano wa Mkataba. 
Hii takwimu ya mwisho inawasuta waliokuwa wakitubeza tulipokuwa tukisema kwamba wengi wa Wazanzibari wanataka pawepo Muungano wa Mkataba.  Tulibandikwa kila aina ya majina na tukavurumishiwa kila aina ya matusi ilhali tulikuwa tukiyabaini kwa usahihi kabisa maoni ya Wazanzibari.
Warioba alisema pia kwamba Wazanzibari wana malalamiko matatu makubwa. Kwanza, kwamba serikali ya Tanganyika imevalishwa koti la serikali ya Muungano na hivyo nguvu za Zanzibar zimepungua.  Pili, ongezeko la ‘mambo ya Muungano’ na tatu, kuondolewa Rais wa Zanzibar kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano.
Rasimu hii ya Pili imeyapatia ufumbuzi malalamiko hayo. Kwanza, kwa kufufuliwa Tanganyika na serikali yake; pili, kwa kupunguzwa ‘mambo ya Muungano’ na kuwa saba.  Nayo ni:
  • Katiba na Mamlaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
  • Ulinzi na Usalama wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
  • Uraia na Uhamiaji.
  • Sarafu na Benki Kuu.
  • Mambo ya Nje.
  • Usajili wa Vyama vya Siasa.
  • Ushuru wa Bidhaa na Mapato yasiyo ya kodi yatokanayo na Mambo ya Muungano.
Tatizo la tatu limetanzuliwa kwa kuweka kanuni ya kwamba Rais wa Muungano akitoka Nchi moja Mshirika basi Makamu wake atoke Nchi ya pili Mshirika.
Rasimu hii ya Pili ya Katiba bado ina madosari, bado inahitaji kunyoshwa na kupigwa msasa lakini lazima tukiri kwamba ina mambo kadhaa yaliyo mazuri. Kati yao ni tume zilizopendekezwa, kwa mfano, Tume ya Maadili ya Uongozi na Uwajibikaji; Tume ya Haki  za Binadamu na Tume Huru ya Uchaguzi. Sasa kutakuwa na wagombea huru wa uchaguzi, hata wa urais.
Kadhalika Rasimu hiyo inasema: “Kila Nchi Mshirika wa Muungano itakuwa na mamlaka na haki zote juu ya mambo yote yasiyo ya Muungano, na katika utekelezaji wa mamlaka hayo, kila Nchi Mshirika wa Muungano itazingatia misingi ya ushirikiano na mshirika mwingine kwa kuzingatia haki na usawa kwa ajili ya ustawi ulio bora wa wananchi wa pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano.”
Ingawa Mambo ya Nje ni moja ya ‘Mambo ya Muungano’ hata hivyo, kwa mujibu wa Rasimu hii, “kila Nchi Mshirika wa Muungano itakuwa na uwezo na uhuru wa kuanzisha mahusiano au ushirikiano na jumuiya au taasisi yoyote ya kikanda au kimataifa kwa mambo yaliyo chini ya mamlaka yake kwa mujibu wa Katiba ya Nchi Mshirika wa Muungano.”
Mwengine anayestahili kumwagiwa sifa ni Kikwete. Bila ya shaka historia itamwangalia kwa jicho la rehema kwa uamuzi wake wa kuweka kando misimamo ya chama chake akizingatia badala yake maslahi ya taifa.
Kikwete alionyesha ujasiri mkubwa alipowapa mgongo wabunge wa Chama cha Mapinduzi(CCM) waliokuwa na nia, na walioanza hasa hatua, za kutaka kuitia munda Rasimu ya Kwanza ya Katiba kwa kuuweka mbele ukereketwa wao wa kichama na maslahi yao ya binafsi.
Rasimu hii imewasuta wengi kuanzia wanasiasa wahafidhina wa CCM hadi wasomi na wale wenye kujiona kuwa ndio watetezi wa msimamo wa Mwalimu Julius Nyerere kuhusu Muungano. 
Hawa wamesahau kuwa wakati umebadilika na kwamba mifumo yote ya Miungano duniani imebadilishwa na nyakati kwa matakwa ya umma. Ile iliyosita kufanya hivyo imejikuta ama ikivunjika au ikisambaratika, kama kwa mfano Yugoslavia ya zamani au Muungano wa Jamhuri za Kisoshalisti za Kisovieti.
Jambo lenye utata mkubwa sasa ni namna Bunge la Katiba litavyoundwa. Hatari iliyopo ni kwamba iwapo Bunge hilo litaundwa kama inavyopendekezwa basi muundo huo utakuwa ni kichekesho kwa demokrasia kwani utakipa chama CCM usemi mkubwa katika Bunge hilo.
Hii ni kwa sababu kwa ilivyo sasa wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano pamoja na wajumbe wote wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar watakuwa wajumbe wa Bunge la Katiba.  Hivyo asilimia 71 ya wajumbe 640 wa Bunge hilo watatoka CCM; hiyo ni idadi kubwa mno. Isitoshe CCM inaweza pia ikawaweka watu wake katika nafasi 201 za wawakilishi wa kawaida katika Bunge hilo.
Kwa ufupi, Katiba itayopitishwa na itayowasilishwa kwa wananchi kwenye kura ya maoni itakuwa ni ile inayotakiwa na CCM. Hiyo ni kasoro kubwa katika mchakato wa kulipatia taifa Katiba mpya.  Profesa Chris Peter Maina, mwanasheria maarufu na Mwenyekiti wa Huduma za Sheria Zanzibar, anasema kwamba kasoro hiyo imesababishwa na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba iliyofanyiwa marekebisho kidogo na kupitishwa hivi karibuni na wabunge.
Jukumu moja la Bunge la Katiba litakuwa kuhakikisha kwamba yale mambo ambayo Zanzibar haijawahi kuyapata katika kipindi cha miaka 50 iliyopita ya Muungano hivi sasa inayapata. Kwa mfano, ile kanuni itayotumika kwa Rais wa Muungano na Makamu wake kwamba mmoja akitoka upande mmoja wa Muungano makamu wake atoke upande mwingine utumike pia kwa mkuu wa majeshi na makamu wake. Na iwe vivyo hivyo kwa upande wa polisi, uhamiaji na usalama wa taifa. Na pawepo na uwiano kwa upande wa uteuzi wa mabalozi.
Bado panahitajika ufafanuzi kuhusu sheria ya uhamiaji katika kipengele cha uraia.  Ingawa uraia ni mmoja panahitajika pawepo na utaratibu wa kuweza kutambua raia wa Jamhuri ya Muungano ametoka Nchi gani Mshirika. Hilo halitokuwa tatizo kwa Zanzibar ambayo tayari ina kitambulisho cha ukaazi kwa Mzanzibari.
La kukumbukwa ni kwamba katika mchakato huu mzima wa kutafuta Katiba ifaayo kwa Tanzania ushindi mkubwa ni wa umma ulioshirikishwa na uliotekeleza wajibu wake wa kuiongoza Tume kwa kutoa maoni yake.  Kwa hilo tunapaswa tumpe heko tena Kikwete kwa ujasiri wake wa kuuamini umma wa Tanganyika na Zanzibar. 
Kilichobakia ni kwa Bunge la Katiba kuhakikisha kwamba uchaguzi wa 2015 utafanyika chini ya Katiba mpya. Changamoto iliyopo hapo ni kwa Tanganyika kuweza nayo kuwa na Katiba yake kabla ya wakati huo.
- See more at: http://www.raiamwema.co.tz/hatimaye-warioba-aifufua-tanganyika#sthash.CGcrkDoJ.dpuf

No comments: