Thursday, 30 January 2014

MZIMU WA ABOUD JUMBE UNAWATAFUNA CCM

Wiki hii umefanyika uzinduzi wa maadhimisho ya kutimia miaka 37 ya Chama Cha Mapinduzi  katika Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Makamu na kuongozwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM (Zanzibar), Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein.Mengi yamesemwa, tumesikia tambo za viongozi wa CCM akiwamo Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana kuhusu uimara wa chama, umakini wake huku akiviponda vyama vingine vya siasa.Kinana amesema kazi ya CCM ni kuwaletea maendeleo wananchi.  Kazi ya kuzua wameviachia vyama vya upinzani. Ni miaka 37 sasa imetimia tangu Afro Shiraz Party (ASP) na Tanganyika African National Union (TANU) vilipoungana na kuzaliwa CCM. Kwa sasa CCM sio tena chama kipya, ni kikongwe ukilinganisha na vyama vingine katika Afrika na hata sehemu nyingine duniani. Je, malengo ya kuunganishwa kwa ASP na TANU yamefanikiwa kwa kiasi gani?
Iko wapi misingi ya CCM ya mwaka 1977?  Nakumbuka miongoni mwa mambo ambayo yalikuwa yakielezwa ni pamoja na kupinga dhuluma ya aina yoyote, uonevu, ukoloni mamboleo, ukandamizaji na unyanyasaji, huku ujamaa na kujitegemea vikipigiwa chapuo.Uzinduzi wa sherehe za CCM uliambatana na hotuba zenye kuwakejeli wanaotaka mageuzi, wanaotaka mamlaka kamili au serikali tatu katika muundo wa Muungano kuwa wanaopoteza muda, hakuna liwalo. Tumewasikia viongozi wa CCM wakiwahakikishia wanachama wao wasiwe na wasiwasi, kwamba muundo wa Muungano utabakia wa serikali mbili.Hawa viongozi wanapata uhalali wa kuongoza kutokana na maamuzi ya wananchi. Katika hili la Katiba Mpya baada ya kazi zote, hatua ya mwisho ni ya wananchi kuamua kama wanaitaka au hawaitaki kupitia kura ya maoni.
Suala la mabadiliko ya muundo wa Muungano limo katika rasimu ya katiba ambayo itawasilishwa kwenye Bunge Maalumu la Katiba. Ikiwa rasimu hiyo itakwenda kwa wananchi ikiwa na mapendekezo ya serikali tatu na wananchi wengi wakasema ndio kwa Katiba Mpya, hao wanaosema hakuna serikali tatu watakaa upande upi? Watafanya nini ikiwa wananchi walio wengi kupitia kura ya maoni wamekubali kubadili muundo wa Muungano? Watapuuza matakwa ya umma kwa kuamua watakavyo? Miaka 37 ya CCM kuelekea miaka 50 ya Muungano Aprili 26, ni zaidi ya vizazi viwili, huu ni wakati tafauti kabisa. Uamuzi wowote utakaofanyika uzingatie mahitaji ya wakati wa leo, kesho pengine miaka hamsini ijayo.Kuna mambo mengi yamebadilika, wananchi wanahitaji mabadiliko ili kuendana na hali halisi ya Tanzania ya leo ambayo ni tofauti na ile ya mwaka 1977. Hali ya kisiasa nayo imebadilika sio tu katika Afrika hata katika nchi za Ulaya na Marekani.Tukielekea kwenye kilele cha miaka 37 ya kuzaliwa kwa CCM kuna mengi ya kujiuliza; je, kama si mapinduzi, Muungano ungekuwapo, au waasisi wa Mapinduzi walitaka hivi ilivyo kwenye Muungano?
Kuna mengi ya kuuliza na kwa sababu mbalimbali kuendelea kudhani kuwa kuujadili Muungano ni uhaini tutakuwa tunajidanganya, kwani kuficha au kudharau maradhi ni ugonjwa hatari, na ipo siku mauti itatuumbua.Walichokuwa wakikifanya ni ubabaishaji mtupu wa kisiasa na kuwapumbaza baadhi ya watu. Nakumbuka baada ya Makamu Mwenyekiti mstaafu wa CCM (Zanzibar), Amani Abeid Karume kutoa hotuba ya kuwahimiza wananchi kuvumiliana kisiasa kule Dodoma alipokuwa akiwaaga wanachama wenzake, walijitokeza watu ndani ya CCM kuanza kumbeza na kumkejeli.Kosa la Karume kwao lilikuwa kuwaeleza umuhimu wa kuvumiliana, kuendesha siasa za kistaarabu, kiungwana na kushindana kwa hoja katika majukwaa huku akitaka kustahamiliana wakati wa mchakato wa utoaji maoni kuhusu Katiba Mpya.
Baadhi ya watu wakaanza kumjia juu, kisa kueleza umuhimu wa kuvumiliana kwenye tofauti ya maoni kwa  wanaotaka mabadiliko na wale wasiotaka, lakini cha ajabu ni kuwa baada ya matamshi yote ya kumkejeli Karume, kesho yake na wao wanakuja na mawazo yale yale ya wanamageuzi ni dhahiri kuwa unafiki wao umejidhirisha kwa njia hii.Mosi, kwenye mikutano yao waliwaeleza watu kwamba wanatetea sera ya CCM, pia wanalinda historia ya ASP na TANU, kisha wakawasimanga wale wanachama wenzao waliokuwa wakitoa mawazo ya kutaka mabadiliko katika Muungano.Wanabeza kwanza, lakini wamalizapo mikutano utawasikia wakisema wanataka jambo fulani libadilishwe, liondolewe katika Muungano au baadhi ya mambo waliyosema yalikuwa ni magumu kutekelezwa katika mfumo uliopo.
Pili, Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilipokuwa ikipita, tuliwasikia wakitoa maoni ya kutaka mamlaka kamili ya Zanzibar, orodha ya mambo ya Muungano ipunguzwe, marais wawili wawe na nguvu sawa kimadaraka mwisho Zanzibar iwe na uwezo wa kujiunga na mashirika la kimataifa! Hao ndio aina ya wanasiasa tulionao katika miaka 37 ya CCM. Wale viongozi shupavu ya aina ya  Mzee Aboud Jumbe Mwinyi hawapo tena. Mzee Jumbe na Waziri Kiongozi wake, Ramadhan Haji Faki hawakupindisha maneno, walisimama imara hadi dakika ya mwisho.Mzee Jumbe atabaki kuwa alama ya wanasiasa wasiuyumbishwa kwa maslahi ya cheo, atabaki katika kumbukumbu za kizazi hiki na kijacho katika utetezi wa mageuzi ya muundo wa Muungano na hata siasa kwa kukubali kuunganisha ASP na TANU.Ni Jumbe aliyesimama wakati ule katika kuona kwamba ASP na TANU vinaungana na kuzaliwa CCM, lakini pia ni yeye aliesimama mwaka 1984 kuona kwamba mfumo wa muundo wa Muungano unabadilika na kuwa wa serikali tatu, je, miaka 37 ya kuzaliwa kwa CCM, chama hicho kitaweza kuvuka salama katika mchakato wa kupata katiba? 

No comments: