Friday 25 April 2014

WAHAFIDHINA WA CCM!

Dkt. Mwinyihaji Makame Mwadini, Waziri wa nchi Afisi ya Rais, Zanzibar
Dkt. Mwinyihaji Makame Mwadini, Waziri wa nchi Afisi ya Rais, Zanzibar
Na Jabir Idrissa
BAADA ya wahafidhina kuamini kukanushakanusha hainufaishi dhamira zao mbaya, wameamua kupotosha. Wanavitumia vyombo vya dola maana mabunge ya sheria hayatoshi. Wanatumia makanisa kutisha na kupakazia ubaya wasiokuwepo kwenye Bunge Maalum la Katiba. Wanatumia hongo kulazimisha ujinga wao utambuliwe na kuzingatiwa. Bungeni matusi, masimango, kejeli; nje makongamano na watendaji wa chama wanatusi na kushambulia watetezi wa rasimu ya katiba.Wamezoea kusingizia mambo yakiwemo ya kashfa kisiasa kwa vyama vya mageuzi na viongozi wake. Walishasema Chama cha Wananchi (CUF) ni cha kigaidi. Wakati huo kimeshika hatamu ya upinzani bungeni.

Chama kilikubalika kwelikweli Tanzania Bara, ikiwa ni muendelezo wa uungwaji mkono mkubwa Zanzibar.Watawala wakamtumia IGP Omari Mahita kuisokomeza. Akabeba mzigo wa wanasiasa na kutangaza kabla uchaguzi mkuu 2005, “CUF wameingiza sare za jeshi na silaha ili kufanya ugaidi wakati wa uchaguzi.”Watanzania walivyoshindwa kung’amua mbinu chafu ile, wakaingia mkenge na kumchagua Jakaya Kikwete. Walimbeza Profesa Ibrahim Lipumba, mchumi wa kimataifa, ambaye kwa weledi wake na kwa dhamira ya kweli, aliahidi atawafaa kuusuka uchumi.
Akifanya kampeni, Profesa Lipumba alisema kujenga uchumi nchini ni kazi nzito; na mzigo mzito hupewa Mnyamwezi; basi umemstahikia hasa baba wa Unyamwezini, Tabora. “Nichagueni Mnyamwezi, achaneni na mtani wangu Mkwere, huyu hawezi labda usanii.”Alisema Kikwete atawafaa Watanzania kama rais iwapo wanataka mtu wa kutokeza vizuri kwenye televisheni na kupokea wageni mashuhuri wa mataifa na taasisi za kimataifa na kanda. Hatamudu kuusuka uchumi ambao kuvurugika kwake kumechangiwa sana na ulegevu wa usimamizi wa raslimali. Nani msimamizi? Serikali ya CCM.
Si uongo, nafasi ile muhimu ya kupata rais mtendaji kwelikweli ikapotezwa. Haikuchukua muda rais mpya akasema akiwa ziarani ughaibuni, “… hata mimi nashangaa Tanzania ni masikini.” Walimuuliza sababu ya umasikini unaonuka ndani hazina ya raslimali.Hapo ndo Watanzania wakagutuka, “du… tumechagua vipi?” mmechagua vipi, leo? Majuto mjukuu.Kupitia CCM, watawala wanatafuta kura za kutosha ili kupitisha rasimu waitakayo ya katiba baada ya kuona UKAWA wamegoma kuitenga iliyofuata maoni ya wananchi. Hawazipati maana kibarua chake kinafanana na kumkiuka simba.
Safari hii hawakanushi yasemwayo. Wameongeza nguvu katika kupotosha ukweli wanaoujua. Hata taarifa zitokanazo na nyaraka halali serikalini, wanazipotosha.Wanasingizia wasohusika. Wanamsingizia ubaya hata mwenzao wa enzi – Jaji Joseph Warioba ambaye kwa kujua hakubali kuyumbishwa, wananuna na kumshambulia. Kisa? Amesimamia maoni ya wananchi. Waliamini atawaridhia watakayo yasiyoendana na alichoahidi Rais Kikwete – katiba inayotokana na maoni ya wananchi.
Wanamshambulia kama kitoto, Maalim Seif Shariff Hamad, wanaejua ni Makamu wa Kwanza wa Rais aliyeteuliwa kwa nguvu ya mabadiliko ya katiba waliyoyaridhia Wazanzibari kwa asilimia 66 kwa Kura ya Maoni ya 31 Julai 2010. Kijana wao Tau anasema, yeye hakuulizwa. Inamaana alipiga kura kibubusa?Wanarudia kasumba za miaka ya 47: Wakishinda uchaguzi, CUF watamuita Sultani Jemshid bin Abdalla, aje kuongoza. Hapo ndipo watavunja Muungano kupitia serikali zao tatu.
CCM wameongeza: Zikija serikali tatu, ya Shirikisho wanayoitaka CUF, itashindwa kujiendesha, haitakuwa na mapato, itashindwa kulipa majeshi mishahara, watagoma, wataipindua nchi.Matumizi mabaya ya akili. Wanatumia nguvu nyingi kushawishi wananchi eti serikali tatu gharama. Haya anayasema hata Mama Anna Tibaijuka, profesa wa uchumi: “Tanzania ni nchi masikini nawaambia tatu ni dhambi.”Akili si nywele. Mbona hawawaambii Watanzania serikali ya CCM imeshindwa kutumia raslimali tele za nchi kujenga uchumi? Wamekwama kuitimiza bajeti maana hawakusanyi kodi za kutosha. Hawawezi kuamua vyanzo vipya vya mapato huku wakisamehe matajiri kodi. Mamilioni wanazitafuna wao.
Ili kufanikisha upotofu wao, wamewajaza jazba wajumbe wao kutoka Zanzibar na kuangusha matusi, kejeli, masimango na propaganda chovu dhidi ya wakuu wa CUF. Wakaingia kichwa kichwa kutukana ndugu zao.Walewale waliopiga kelele wawakilishi waliposhiriki semina kuhusu katiba mpya, wakiwemo mawaziri wa CCM, leo wanatunisha mishipa ya shingo na kuyatemea mate yale waliyoyasema na wananchi kuyasikia kupitia Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC).Mawaziri kutoka CCM na wawakilishi wengine kupitia huko wameungana kutusi ukweli wanaoujua na waliousema kwa jazba karibuni tu. Nani alisema mawaziri wa SMZ wakienda vikaoni Bara wanaishia kunywa chai na kurudi mikono mitupu? Nani? Hamza Hassan Juma wa Kwamtipura; Makame Mshimba Mbarouk wa Kitope; Salmin Awadh Salmin wa Magomeni; Mohamedraza Hassanali Dharamsi wa Uzini. Ni CCM.Ismail Jussa Ladhu (Mji Mkongwe, CUF), alisaidia tu kutaja zilipo haki, fedha ambazo Serikali ya Muungano inainyima Zanzibar. Hizi ni haki zinazotokana na faida kibiashara katika taasisi za Muungano.Ni wao waliotaka watumwe kuzidai haki za Wazanzibari zilizozuiwa kwa ukorofi tu na Bara. Wakasema ebo, Zanzibar si koloni la Tanganyika. Ni CCM.
Raza ambaye kwa miaka 20 anasema kwa mfumo wa serikali moja Tanganyika itatawala minazi Zanzibar, na siyo watu, alimwambia Spika Pandu Ameir Kificho, mwenyekiti wa semina, “nipo tayari kuzidai haki hizo niteuwe na watu wachache na watendaji wa SMZ niende.”Mtindo wa serikali ya Muungano kuigomea Zanzibar haki zake ni miongoni mwa kero kuu za mfumo wa serikali mbili ambazo Tume ya Jaji Warioba imetumia kupendekeza mfumo wa serikali tatu.Wao wameona kuna mkwamo wa kizembe wa kutekeleza hata makubaliano yaliyofikiwa baada ya kuundwa Tume ya Pamoja ya Fedha (JFC) na Rais Benjamin Mkapa kutafiti gharama halisi za Muungano na utaratibu wa kugawana mapato.
Raza amezoea kusema, “Viongozi wa Zanzibar wasipokuwa imara na kuipenda nchi yao, itafika siku vyeti vya ndoa Wanzanzibari wavifuate Bara.”Ni CCM. Ni Dk. Mwinyihaji Makame Mwadini, waziri katika Ofisi ya Rais wa Zanzibar, aliyesema katiba mpya itambue mamlaka kamili ya Rais. Anapotaka kufanya maamuzi kwa maslahi ya Zanzibar, asilazimike kuomba ridhaa ya Serikali ya Muungano.Hakutaka serikali tatu, lakini hilo linawezekanaje penye mfumo anaouabudu? Rais kukopa, kupigiwa mizinga ziarani, kuteua balozi Mzanzibari. Chini ya mbili dhambi daktari.Wameyakana. Daktari huyu wa mazao ya mizizi anasema CUF wanataka serikali ya mkataba ili wapate “kiti chao” Umoja wa Mataifa, Benki Kuu yao, Mabalozi wao na hata pembejeo za kilimo zao.
“Serikali yao itakuja kuongozwa na Waarabu ili wauvunje Muungano… ndo wanachotaka tu hawa mheshimiwa mwenyekiti (wa Bunge la Katiba),” anasema.Mzee Ali Mohamed Ali (Nabwa), Mwenyeezi Mungu amrehemu, alisema wahafidhina haweshi kukanusha. Hapa wanapotosha. Bali Mzee Hassan Nassor Moyo, mwanasiasa mkongwe kuliko Mwinyihaji na wenzake, anasema, “Sitaki kuona makosa tuliyoyafanya sisi yaendelee kuumiza kizazi cha leo.” Haya, wananchi amueni.
Chanzo: Mawio

No comments: