Aghalabu kazi ya mabunge ya kuidhinisha miungano ya nchi hutanguliwa na hatua ya kuwashirikisha wananchi kwa kuwauliza iwapo wanataka nchi zao ziungane. Hilo halikutendeka Tanganyika wala Zanzibar.
Wengi wanaamini kwamba Muungano wa Tanzania hauna uhalali wa kisheria kwa sababu Hati ya Muungano haikuidhinishwa na Baraza la Mapinduzi la Zanzibar licha ya Bunge la Tanganyika kufanya hivyo. Swali jingine linalosababisha utata wa Muungano ni: serikali ya Tanganyika iko wapi? Hivi ni kweli imetoweka? Wengi wanaamini kwamba si kweli; serikali ya Tanganyika ipo lakini imejificha. Hakika ya mambo ni kwamba serikali ya Tanzania ndiyo serikali ya Tanganyika.Inafaa pia kuuliza: ni nini kilichomsababisha muasisi mkuu wa Muungano, Mwalimu Julius Nyerere, amhimize mwenziwe Sheikh Abeid Amani Karume, Rais wa kwanza wa Zanzibar, aikubali rai ya kuziunganisha nchi zao?
Nakwa nini Nyerere alifanya papara ya kutayarisha Hati ya Muungano, tena kwa siri kubwa?
Majibu ya maswali hayo na mengine yenye kuhusika na Muungano wa Tanzania yamo kwenye nakala za nyaraka zilizo katika Maktaba ya Lyndon Baines Johnson huko Texas, Marekani. Nakala hizo ni za mawasiliano baina ya wizara ya mambo ya nje ya Marekani, mawaziri wa wizara hiyo, mabalozi, wanabalozi na majasusi wa Kimarekani waliokuwako Afrika Mashariki, London na Washington.Mmoja wa majasusi hao ni Frank Carlucci ambaye 1964 alikuwa balozi mdogo wa Marekani, Zanzibar. Carlucci baadaye alikuwa mkurugenzi wa Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) na waziri wa ulinzi chini ya Rais Ronald Reagan.
Wamarekani wengine walioandika barua au waliopeleka ujumbe wa maandishi ya simu (cables) walikuwa Dean Rusk aliyekuwa waziri wa mambo ya nje, George Ball (waziri mdogo wa mambo ya nje), Averell Harriman (waziri mwingine mdogo wa mambo ya nje), William Leonhart(Balozi wa Marekani nchini Tanganyika), William Attwood, (Balozi wa Marekani huko Kenya) na McGeorge Bundy, Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Rais Lyndon Johnson.
Yalipozuka Mapinduzi ya Zanzibar Januari 12, 1964 serikali ya Johnson ilikuwa hamkani. Haikusahau jinsi akina Fidel Castro, nduguye Raul, Camilo Cienfuegos na Che Guevara walivyompindua dikteta wa Cuba Fulgencio Batista na kuingia Havana Januari Mosi 1959.
Kilichozidi kuifadhaisha Marekani yalikuwa mahusiano yaliyochanua baina ya Cuba na Muungano wa Jamhuri za Kisoshalisti za Kisovieti uliokuwa hasimu mkubwa wa Marekani katika zama hizo za vita baridi. Marekani ilishtuka kuiona nchi jirani ikikumbatiana na Wakomunisti. Cuba ya kimapinduzi ikawa mwiba katika koo la Marekani.
Marekani ilizidi kushtuka miaka mitano baadaye watawala wapya wa Zanzibar walipokuwa na mahusiano mema na madola ya Kikomunisti, hasa Urusi, China na Ujerumani ya Mashariki (GDR). Zanzibar ya kimapinduzi nayo ikawa mwiba mwingine ulioichoma Marekani.
Kwa hakika Wamarekani waliingiwa na kiwewe kwa habari za uongo za kuwepo Wacuba Zanzibar. Kwa mfano, gazeti la New York Times la Januari 15, liliripoti kwenye ukurasa wake wa mbele kwamba Wamarekani waliokimbia Zanzibar walisema waliwaona wanajeshi waliokuwa wakizungumza Kihispania na waliovaa sare ya Cuba. Kumbe walikuwa vijana wa Umma Party waliofunzwa kijeshi Cuba.
Siku nne baadaye gazeti hilo likaonya kwamba “Zanzibar inakaribia kuwa Cuba ya Afrika” na likaeleza namna Cuba ilivyojiandaa kuchochea mapinduzi kwingineko Afrika.
Shirika la CIA nalo lilizidisha hofu kwa ripoti zake zilizotiwa chumvi za Wacuba kushiriki katika Mapinduzi ya Zanzibar.
Marekani ilizidi kuingiwa na wahka baada ya jeshi la Tanganyika kuasi Januari 20. Siku chache baadaye majeshi ya Kenya na Uganda nayo yaliiga. Serikali za nchi zote hizo tatu ziliomba msaada wa kijeshi kutoka Uingereza.
Wakuu wa Marekani pamoja na Rais Johnson mwenyewe waliishikilia Uingereza ipeleke majeshi Zanzibar kuwang’oa waliodhaniwa kuwa ni Wakomunisti waliomzunguka Karume.
Wamarekani waliwataja Abdulrahman Babu, Waziri wa Mambo ya Nje, Waziri Mkuu Abdallah Kassim Hanga, Waziri Hassan Nassor Moyo na Salim Rashid, Katibu wa Baraza la Mapinduzi. Uingereza ilikataa kuchukua hatua ya kijeshi Zanzibar. Wamarekani wakaudhika.
“Waingereza hawalishughulikii tatizo hili,” Bundy, Mshauri wa Usalama wa Taifa, alimlalamikia Rais Johnson mwanzoni mwa Februari.
Wamarekani hawakujuwa kwamba Uingereza ilikuwa na mkakati mwingine. Ikitaka kushirikiana na Nyerere na Karume ili kuwashinda nguvu hao waliokuwa wakidhaniwa kuwa Wakomunisti.
Wamarekani wakaanza kuwatia hofu viongozi wa Afrika ya Mashariki kwamba wakilala kanda yao nzima itatekwa na Wakomunisti.
Machi 6 Rusk, waziri wa mambo ya nje, aliwaandikia mabalozi wa Marekani Nairobi na Dar es Salaam akiwaamrisha wawasiliane haraka na Nyerere, Rais Jomo Kenyatta wa Kenya na Rais Milton Obote wa Uganda na wawaeleze jinsi Karume anavyofanya hatari kwa kumtegemea Babu.
Rusk aliwashauri mabalozi wawaombe marais hao wamsemeshe Karume afahamu hatari ya Babu kwa madaraka yake Karume na kwa usalama wa Zanzibar na wa Afrika ya Mashariki.
Rusk aliwauliza hao mabalozi “iwapo itasaidia kumtajia tena Nyerere rai ya kuunda shirikisho la Tanganyika na Zanzibar kwa dhamiri ya kuimarisha madaraka ya Karume na kuupunguza ushawishi wa Babu.”
Marekani ilijiandaa pia kuivamia kijeshi Zanzibar lau rai ya kuunda shirikisho hilo ingeshindikana. Iliuita mpango huo Zanzibar Action Plan (ZAP).
Carlucci akiwa Zanzibar alikuwa na mipango yake miwili ya kimaluuni. Kwanza alikuwa mbioni kuwafitinisha viongozi wa Afro-Shirazi Party na wa Umma Party. Na Machi 30 aliiandikia wizara ya nje Washington akishauri kwamba Marekani imhonge Karume ndege ya aina ya “helikopta ikiwa na rubani wa Kimarekani.”
Armando Estrada wa Idara ya Ujasusi ya Cuba - Dirección General De Inteligencia (DGI)– anawakumbuka Wazanzibari waliokuwa Cuba wakifunzwa mbinu za kupindua lakini mawasiliano nao yalikatika waliporudi kwao. Wakati huo Cuba haikuwa na ubalozi Zanzibar.
Katika Afrika ya Mashariki nzima Cuba ilikuwa na ubalozi Tanganyika tu, na ilikuwa na wanabalozi wachache. Juu ya hayo, ilizidi kuvuma kwamba kulikuwa Wacuba walioshiriki katika Mapinduzi ya Zanzibar.
Magazeti ya nchi za Magharibi yakiandika kuwa Wacuba walionekana, waliokuwa wamefuga madevu kama Castro na wakizungumza Kihispania. Walizitaja kauli mbiu zao, matamshi kama “Venceremos!” (Tutashinda).Uvumi huo uliwababaisha hata viongozi wa Cuba.Wakijuwa kwamba hawakuwako Wacuba Zanzibar lakini wakidhania kwamba labda kweli Cuba iliwafunza wapinduzi wa huko.
Siku chache baada ya Mapinduzi ya Zanzibar Jorge Serguera Balozi wa Cuba nchini Algeria alifunga safari kwenda Zanzibar kuitathmini hali ya mambo. Kutoka huko akafululiza kwenda Moscow kumuarifu Castro aliyekuwa ziarani kutoka Januari 13 hadi Januari 23.
Serguera anakumbuka kwamba Castro alimuuliza ikiwa kweli wanamapinduzi wa Zanzibar wakizungumza Kihispania.
Serguera alimjibu: “Ni kweli, Fidel.”
Castro akaendelea kumuuliza: “Ni kweli wanasema Patria o Muerte (Nchi yangu au kifo) Venceremos! (Tutashinda)?”
Serguera akamjibu: “Ni kweli, Fidel.”
Castro asitosheke, akaendelea kumuuliza:
“Ni kweli sisi ndio tuliowapa mafunzo (ya kupindua)?” Naye Serguera akamjibu: “Ni kweli, Fidel.”
Januari 15 Cuba iliitambua Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar lakini haikufungua ubalozi huko. Hatimaye mwishoni mwa Januari Marekani ilikiri kwamba Cuba haikushiriki katika Mapinduzi ya Zanzibar.Lakini Wamarekani hawakukoma.Wakaanza kuwaangaza Warusi, Wachina na Wajerumani wa Mashariki na misaada waliokuwa wanaipa Zanzibar.
Wamarekani walikuwa kama waliingiwa na kichaa. Carlucci akiwa Zanzibar alipeleka ujumbe wizara ya mambo ya nje Washington ukisema: “Zanzibar karibu itakuwa dola ya Kikomunisti…” Thomas Hughes, mkurugenzi wa Ofisi ya Ujasusi na Uchunguzi (Bureau of Intelligence and Research –INR-) iliyo katika wizara wa mambo ya nje, alikuwa akipenda kuikariri indhari ya Carlucci. Safari moja aliandika: “…Katika muda wa miezi sita Zanzibar inaweza kuwa taifa la kwanza la Kiafrika kufungamana na Ukomunisti.”
Siku mbili baada ya hapo Waingereza waliiarifu Marekani kwamba Nyerere ameweza kumshawishi Karume waziunganishe nchi zao katika shirikisho. Waingereza waliieleza Marekani kwamba kwa kuikumbatia Zanzibar “Tanganyika itaweza kuuzima moto wa kimapinduzi wa Zanzibar na kuyafunika majivu yake.”Siku ya pili George Ball, waziri mdogo wa mambo ya nje wa Marekani, aliuandikia Ubalozi wa Marekani Dar es Salaam akisema: “Wizara (ya mambo ya nje ya Marekani) iko tayari kuibariki na kuiunga mkono juhudi ya Tanganyika…hii…inaonyesha kuwa njia bora na yumkini ni uwezekano wa pekee wa kuibadili hali ya sasa ya Zanzibar inayotatanisha.” Aprili 22, 1964 Nyerere na Karume walitia saini Hati ya Muungano. Kwa mujibu wa Carlucci, “Karume akifikiria kwamba anaridhia shirikisho la nchi mbili zilizo huru.” Siku nne baadaye ikazaliwa Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Tanzania ya leo.
No comments:
Post a Comment