Saturday, 3 May 2014

KALAMU YAAHMED RAJAB

Ahmed Rajab     Toleo la 350      30 Aprili 2014

KUNA uwezekano kwamba Tanzania inaendeshwa na mtu asiyejijuwa yeye ni nani. Uwezekano huo unatisha kwa sababu kiongozi asipojijuwa yeye ni nani inakuwa vigumu kwake kuzijuwa nguvu zake na udhaifu wake.Ili awe kiongozi bora na aliye imara ni muhimu aweze kuzitambua nguvu zake na pia udhaifu wake. Utambuzi huo ni moja ya sifa anazopaswa awe nazo kiongozi yeyote yule, hasa wa nchi.Historia inatufunza mengi kuhusu marais waliotangulia katika nchi mbalimbali na sifa walizokuwa nazo. Inatuonyesha, kwa mfano, kwamba wale waliokuwa marais wazuri walikuwa wakiwasikiliza na kuwaridhia wananchi wenzao. Walikuwa wakizingatia maslahi ya wananchi wote au ya wengi wao bila ya kuyapuuza ya wachache.Miongoni mwa sifa nyingine walizokuwa nazo ni uadilifu, ujasiri na uchapaji kazi.Waliweza kukata maamuzi na kuchukuwa hatua thabiti kwa manufaa ya wananchi wao na ya vizazi vijavyo.

Wananchi nao wakiwaamini marais wa sampuli hiyo. Sifa ya kuaminiwa na wananchi anaowaongoza ni moja ya sifa kubwa ambazo rais anahitaji awe nazo.Rais aliye bora anakuwa kila saa anakumbuka kwamba anakikalia kiti cha urais kwa lengo moja tu: kuwahudumia wananchi kwa haki na usawa. Hiyo ndiyo kazi yake. Si kujihudumia mwenyewe na marafiki zake au kukihudumia chama chake na wanachama wenzake.Fedheha iliyojianika wazi hivi karibuni katika Bunge Maalumu la Katiba haikuwaaibisha tu waliokuwa wakitukana matusi yasiyosemeka. Au wale waliojitokeza wazi na matamshi ya ubaguzi wa kikabila. Fedheha hiyo ilikuwa ni aibu kubwa pia kwa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Mwenyekiti wake ambaye ni Rais wa taifa.Historia itamlaumu Rais Jakaya Kikwete, akiwa Mwenyekiti wa CCM, kwa kushindwa kuwadhibiti watovu wa adabu wa chama chake katika Bunge hilo. Alichopaswa kufanya ni kuwachukulia hatua za kinidhamu hao wabunge wasio na heshima ambao ndio walioanza kutumia lugha chafu ya matusi na kueneza ubaguzi wa kikabila.Kushindwa kwake kunatufanya tuamini kwamba labda na yeye mwenyewe ama ameyafurahia hayo matusi au ameshindwa kuchukuwa hatua kwa sababu matusi na ubaguzi wa kikabila ni mambo yasiyopingana na sera za CCM. Au labda ameshindwa nguvu na vigogo wa CCM.
Kikwete ameshindwa pia kumchukulia hatua William Lukuvi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, kwa kauli za uchochezi kama vile kuwaambia Wakristo kanisani kwamba pakiwapo na Muungano wenye muundo wa shirikisho basi Zanzibar itajitangaza kuwa dola ya Kiislamu au alipokihusisha Chama cha Wananchi (CUF) na harakati za Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu.Hiyo ni mbinu ya propaganda ya hofu yenye shabaha ya kuwatisha walio ndani na nje ya Tanzania kwamba Muungano wa serikali tatu utaifanya Zanzibar iwe nchi ya hatari isiyokalika. Kuithibitisha hoja hiyo Lukuvi aliongeza kusema kwamba pendekezo la Serikali Tatu likipitishwa basi jeshi litaingilia kati na kuongoza nchi.Matamshi kama hayo ya kulitomeza jeshi liingilie siasa za nchi yalitolewa mara ya kwanza na Rais alipokuwa akilifungua Bunge la Katiba. Ni kauli ya kushangaza kabisa.
Ni kauli iliyoonyesha jinsi Rais alivyojisahau au asivyojijuwa yeye ni nani. Katika hotuba hiyo ya ufunguzi wa Bunge la Katiba alikuwa mara akitoa matamshi ya kutisha, mara akiiponda Tume ya Katiba aliyoiteua mwenyewe, mara akilitomeza jeshi.Labda inafaa tumkumbushe kutokana na historia ya mapinduzi ya kijeshi kwingineko duniani kwamba jeshi likitwaa madaraka yeye mwenyewe pamoja na marais wengine wastaafu walio hai wanaweza wakawa miongoni mwa wa mwanzo ‘watakaoshughulikiwa’ na wanajeshi. Na chama chake pamoja na vingine huenda vikenda na maji.Watawala wetu haweshi kujigamba kwamba Tanzania ni taifa la kidemokrasia lisilo na ubaguzi. Lakini ukweli halisi tuliushuhudia katika Bunge la Katiba pale baadhi ya wajumbe wa CCM, hasa kutoka Zanzibar, walipoushadidia ubaguzi bila ya haya.Mmojawao, Bibi Asha Bakari, alithubutu kusema kwamba CCM haitokubali kuyaacha madaraka Zanzibar kwani Serikali ya huko ilipatikana kwakupindua na si kwa karatasi.Nawengine wakiitaka watabidi waipindue.Ni maneno gani hayo ya kusemwa na kiongozi katika karne ya 21.Alichokuwa akisema ni kwamba potelea mbali uchaguzi kwani CCM huko Visiwani ikishindwa kwa kura haitoyaacha madaraka. Kwa hakika, mkereketwa huyo wa CCM alifurutu ada kwa matusi yake ya nguoni na matamshi ya kibaguzi.
Profesa Ibrahim Lipumba, mwenyekiti CUF, hakukosea alipowafananisha naInterahamwe wale waliokuwa wakileta mambo ya ubaguzi katika Bunge hilo. Lipumba alisema aliyoyasema kwa kulitahadharisha taifa kwani anaielewa historia ya mauaji ya halaiki ya Rwanda yaliochochewa na matamshi ya kibaguzi. Matamshi ya kibaguzi ndiyo yaliyowahamasisha wanamgambo wa Wahutu — Interahamwe — waliosababisha mauaji ya kimbari huko Rwanda.Sumu ya wabaguzi ni kali kushinda ile ya nyoka wa gangawiya. Hulka ya gangawiya ni kwamba hata kama hujamchokoza akikuona tu atakuandama mpaka akuue kwa sumu yake.Hakuna mwalimu bora wa fani ya siasa kushinda historia. Na historia inaonyesha kwamba mauaji ya kikabila yalizuka duniani pale watu walipoanza kujitafautisha baina ya “sisi” na “wale”.
Nilishtuka nilipomsikia mjumbe mmoja wa Bunge la Katiba wakati wa mjadala juu ya muundo wa Muungano akisema kwamba Wazanzibari wanaodai Muungano wa serikali tatu wanataka utawala wa wenye madevu kwa sababu “Sultani ana madevu”.Masikini roho yake, kwani hajui kwamba Sultan, Seyyid Sir Jamshid bin Abdallah, hafugi ndevu, si siku hizo alipokuwa akitawala na wala si sasa anavyoishi uhamishoni Portsmouth, Uingereza.Lakini tena hao wakorofi wa CCM katika Bunge la Katiba wamezoea kusema maneno kama hayo ya uongo na kutoa hoja za kitoto kutetea sera yao ya kutaka muundo wa Muungano wa serikali mbili uendelee. Kati ya hizo hoja za kitoto wanazozitoa ni eti wenye kutaka serikali tatu wana ajenda ya siri ya kuurejesha “utawala wa Waarabu” kwa kumrejesha Sultan Zanzibar.Inakirihisha kuwasikia viongozi na wanasiasa wengine wakuu wakisema maneno ya uzandiki kama hayo. Unafiki wao hujitokeza mara kwa mara tunapowaona wanafunga safari wakikimbilia Arabuni, hasa Oman, kwenda kuomba misaada.Pengine tungeweza kuwapuuza na uongo wao lau wasingekuwa wanatukana na kuliaibisha taifa au wasingekuwa wanachochea chuki za kikabila na kulihatarisha taifa.
Historia inatufunza jingine: kwamba chuki aina hizo aghalabu huwa ndizo chanzo cha cheche za moto utaoweza kuliteketeza taifa. Ndiyo maana ili kuliepusha janga hilo kuna haja ya Tanzania kutunga sheria za kumfanya mwenye kueneza chuki za kikabila awe ni mhalifu wa sheria. Asaa pakitungwa sheria za kuharamisha chuki za kikabila na ubaguzi wa kikabila taifa linaweza likanusurika na mauaji yenye kuchochewa na ukabila au ubaguzi wa aina yoyote.Mizozo ya kikabila na ya kidini imekuwa ni chanzo cha vita katika sehemu mbalimbali duniani. Hata hivyo, ni tabu kuelewa kwa nini ukabila au dini zikawa na uwezo wa kuleta mpasuko katika nchi, zikaweza kuivunjavunja nchi na kuwafanya watu waliokuwa majirani wakiishi pamoja kwa amani kwa muda mrefu waanze kutafuta mapanga na kuchinjana. Tumeyashuhudia hayo Rwanda, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Sudan, Sudan ya Kusini na hata Somalia.
Tuseme ni chuki za kale za kikabila au kuna kingine kinachosababisha mauaji ya kikabila? Nadhani labda sababu ni chuki za kikabila za wanasiasa kwa vile matamshi yao ya chuki yanaweza kuwahamasisha watu waanze kuchukiana na kubaguana kwa sababu ya kabila zao. Moto wa kikabila ukishaanza kuwashwa inakuwa tabu sana kuuzima.Rais anayejijuwa yeye ni nani na anayejiamini huwa hakubali kuwaona watu wa kaumu yake wakimharibia jina lake au la utawala wake. Ndiyo maana inashangaza na kusikitisha kwamba Rais Kikwete, ambaye mwakani atamaliza muhula wake wa mwisho wa urais, amewavumilia wajumbe wa CCM katika Bunge la Katiba waliokuwa wakitumia lugha ya kihuni katika vikao vya Bunge hilo. Labda kweli hajijui ni nani na ana nguvu gani.

No comments: