Wednesday 18 June 2014

Kifo cha serikali ya ccm kinakaribia

TAREHE 4 mwezi huu Mbunge wa Kilosa (CCM), Mustapha Mkulo, aliamua kusimama bungeni na kukanusha tuhuma ambazo zimekuwa zinamkabili tangu wakati alipokuwa waziri wa fedha kabla ya kuachwa na Rais Kikwete mwaka 2012 pamoja na mawaziri wenzake waliokabiliwa na shutuma mbalimbali.Shutuma ambazo zilikuwa ametupiwa yeye wakati ule ni kuhusu uuzaji wa kiwanja Na. 10 barabara ya Julius Nyerere, cha Shirika Hodhi la Mali za Serikali (CHC). Kiliuzwa kwa kampuni ya Mohamed Enterprise Tanzania Limited (MeTL) inayomilikiwa na familia ya Mbunge wa Singida (Mjini) Mohamed Dewji. Aliyoyasema Mkulo bungeni yalikuwa ni marudio, kwa vile tayari alikuwa ameibuka katika jimbo lake la Kilosa na kukanusha tuhuma za kuuza kiwanja hicho. 
Akizungumza na wazee wa jimbo lake mwishoni mwa Mei mwaka huu, Mkulo aliwaambia ameamua kuweka bayana kutohusika katika mchakato wa uuzwaji kiwanja hicho, ili “historia yake na utumishi wake katika Taifa usihukumiwe kabla na baada ya kufa”.Mkulo alisema tuhuma hiyo inayodaiwa kuibuliwa kwenye ripoti ya mwaka 2010/2011 ya Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa Serikali (CAG) haimkabili yeye, aliongeza:
“Nimeamua kuyaweka wazi haya ili kila mmoja atambue hivyo na kama kuna mtu mwenye uhakika dhidi ya tuhuma hizo, anapaswa kwenda mbele zaidi kwa faida ya nchi”.
Hayo ni maneno mazito. Ndiyo maana najiuliza, kweli ripoti ya CAG haimkabili Mkulo kama anavyodai? Suali la pili ni, kwanini aibuke sasa na kujitetea miaka kama mitatu tangu alipotuhumiwa? Kwanini asijitetee wakati ule ule? Kwa mujibu wa matamshi yake, anasema ni kwa kuwa wakati ule hakupata “nafasi ya kujitetea”. Alisema alijaribu kuomba kutoa nafasi ya utetezi wake ndani ya Bunge, lakini kwa bahati mbaya hakupata nafasi mpaka alipotoka Hazina.Kwanini hakupata nafasi? Nani alimzuia? Waziri anayeshutumiwa haruhusiwi kujitetea mpaka baada ya miaka mitatu?
Sasa Mkulo ameamua kueleza kwamba kilichotokea ni bodi ya CHC, iliandika barua kwa Wizara ya Fedha kuomba ruhusa ya kuuza kiwanja hicho, na barua hiyo haikwenda kwa Waziri wa Fedha bali kwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo.
Akasema Msajili wa Hazina alifanya uchambuzi na kutoa maoni yake kwa Katibu Mkuu ambaye alipendekeza kwa Waziri wa Fedha nini kifanyike. Kisha Waziri “alitoa maelekezo kwamba kulikuwa na mapungufu makubwa katika mapendekezo ya Bodi na aliagiza ufanyike utaratibu wa kawaida kwa kufuata kanuni kumpata mtu ambaye angeweza kuuziwa kiwanja hicho”.
Mkulo akaongeza kuwa barua iliandikwa kwa CHC na ikagundulika kuwa mtu waliyemtaka kununua kiwanja hicho alishalipa nusu ya gharama ya kiwanja hicho.
“Walishauza kiwanja, hivyo walikuwa wanataka Waziri aidihinishe, sikuidhinisha. Nataka niseme ukweli, Katibu Mkuu hakuidhinisha na wala Msajili hakuidhinisha. Waliouza kiwanja walikuwa ni Mwenyekiti wa Bodi wakati huo na aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa Bodi,” alijitetea Mkulo.
Ndipo najiuliza, Mkulo alichukua hatua zipi za kinidhamu? Mbona ripoti, ushahidi na nyaraka zinasema vingine?
Kwa mfano, wakati ule Oktoba 2011 Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), Zitto Kabwe aliwaambia waandishi:
“Nina nakala ya barua inayoiagiza CHC kutekeleza maagizo ya Waziri ya kuuza kiwanja ….pia nina ushahidi wa mkutano wa waziri Mkulo na Mwenyekiti wa Bodi ya CHC katika Morogoro Hotel”
Zitto akasema uchunguzi ulifanywa na kampuni ya Ernest and Young iliyokabidhiwa kazi hiyo na CAG. Ripoti yao inasema Mkulo anastahili kujibu shutuma dhidi yake na Wizara yake.
Mkulo akakataa kudadisiwa na wakaguzi. Badala yake akaandika barua (TYC/B/70/2/03) tarehe 8 Oktoba 2011
Je, ni kweli Mkulo alikataa kuhojiwa na wakaguzi? Kama si kweli, kwanini wamsinginzie?
Ripotiya CAG ya mwaka 2010/2011 ilisema kuwa Wizara ya Fedha ilihusika moja kwa moja katika uuzaji wa kiwanja, ingawa Mkulo aliwahi kukataa jambo hilo. CAG pia alisema uuzaji huo ulipaswa usimamiwe na Bodi ya CHC, lakini kilichofanyika ni kuwa uamuzi wa utawala wa CHC ulishinikizwa ‘nje ya Bodi’.
Ripoti ya CAG pia ilisema kuwa barua walizoandikiana CHC, MeTL, Wizara ya Fedha na Msajili wa Hazina kuhusu uuzaji wa kiwanja zilidhihirisha kuwa Waziri wa Fedha na Msajili wake walihusika katika uuzaji huo.
CAG anaongeza kuwa si tu Bodi ya CHC haikuhusika katika uamuzi, bali kulikuwako na ukiukwaji kadhaa katika dili iliyofikiwa na MeTL. Hivyo, kampuni hiyo ililipa shilingi bilioni 2.046 kwa ajili ya kiwanja bila ya kufuata sheria na kanuni za uuzaji wa mali ya umma.
Najiuliza, je ripoti ya CAG ilikosewa? Nani mkweli, Zitto, CAG au Mkulo? Kwa kawaida ripoti ya GAC  huwa inawasilishwa bungeni ili ijadiliwe. Hapo hata Mkulo angepata fursa ya kutoa maoni yake badala ya kulalamika sasa kuwa hakupewa nafasi ya kujibu. Ni vizuri kama ripoti hiyo pia ingekabidhiwa rasmi kwa Takukuru ili uchunguzi ufanywe na hatua zichukuliwe.
Sakata hili la ununuzi wa kiwanja namba 10 lilikuwa na historia ndefu. Mwaka 1999 MeTL walipeleka ombi la kununua kiwanja hiki kwa tume ya kubinafsisha (wenyewe walikuwa wanaita ya Kurekebisha) Mashirika ya Umma (PSRC) na wakaahidi kulipa dola 300,000 lakini PSRC ikataka walipwe dola 500,000.
Baada ya hapo hakuna kilichofanyika hadharani hadi Mkulo alipokutana na uongozi wa MeTL Juni 8, 2010, siku chache kabla ya Baraza la Mawaziri kuvunjwa na kuingia kwenye mchakato wa Uchaguzi Mkuu.
Ndipo Mkulo alipoanzisha mchakato wa kumuuzia kiwanja MeTL kwa kuitisha mkutano kati yake, wakuu wa CHC na mwakilishi wa Msajili wa Hazina.
Baada ya hapo MeTL waliandika barua kwa msajili wa hazina (Kumb. Na.METL/PLOT/2010/10-06)  ya tarahe 20 Juni 2010 ikimweleza kuwa Waziri wa Fedha Mkulo alikuwa amekabidhi suala la kiwanja kwake (Msajili).
Baada ya barua hii ya MeTL, Msajili, kwa niaba ya Katibu Mkuu, aliandika barua (Kumb TYC/A/290/13) tarehe 5 Julai 2010, kwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa CHC akimtaka atekeleze yaliyomo katika barua ya MeTL. Je, barua hii ni ya kugushi?
Si rahisi, kwani Mkulo alipoona agizo lake halijatekelezwa kwa miezi mitatu, ilipofika tarehe 1 Oktoba 2010, Wizara ya Fedha, kupitia Msajili wa Hazina, iliandika barua (Kumb TYC/C/180/85/59).
Mimi ningeshangaa sana kama Mkulo hakuwa na habari yoyote kuhusu barua hii. Kwanini?
Ni kwa sababu kutokana na barua hii, katika ukaguzi maalumu uliofanywa na CAG ndani ya CHC, CAG alitaka kumhoji Mkulo hivyo akampigia simu kuomba nafasi ya kukutana naye, lakini mara tu alipopigiwa simu Mkulo aliruka kimanga.
Mara moja Mkulo aliandika barua tarehe 8 Oktoba (Na. TYC/B/70/2/03) na kuisaini yeye mwenyewe, huku akiigonga mihuri minne ya SIRI. Barua hiyo ilisema hivi:-
“Yah: Ukaguzi wa Consolidated Holding Corporation
“Tafadhali rejea mazungumzo yetu ya simu (UTOUH/MKULO) ya tarehe 07/10/2011 na ujumbe wa simu (SMS Message) wa tarehe 05/10/2011.
“Napenda kuthibisha niliyoyasema kwenye simu, “kwa maandishi” kwamba mimi kama “Waziri wa Fedha” sijawahi kutoa KIBALI kwa Mwenyekiti wa Bodi ya CHC, kumpa madaraka ya kuuza kiwanja au nyumba zinazomilikiwa au kutunzwa na CHC bila kufuata taratibu za zabuni au sheria ya manunuzi. Kama Mwenyekiti wa Bodi aliamuru Kaimu Mkurugenzi Mkuu na Bodi ya Wakurugenzi kuuza kiwanja cha Shirika bila kufuata taratibu za zabuni, alifanya hivyo kwa ridhaa yake mwenyewe na si kwa maagizo ya Waziri wa Fedha.
“Wizara ya Fedha ina utaratibu maalumu wa kushughulikia masuala yote yanayohusu mashirika ya umma. Kisheria huanzia kwa Msajili wa Hazina, kupitia kwa Katibu Mkuu – Hazina (PST/PMG) hadi kumfikia Waziri wa Fedha kwa uamuzi. Hivyo utaratibu uliotumiwa na Mwenyekiti wa Bodi na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa CHC ni kinyume na kanuni za utendaji kazi ndani ya Wizara ya Fedha na pia ni kinyume na kanuni za manunuzi.
“Nakushukuru sana kwa kunijulisha jambo zito ambalo sikuwa nikilifahamu. Natumaini kwa maelezo haya ya maandishi, ofisi yako sasa inaweza kukamilisha ukaguzi wa CHC.
“Mustafa Haid Mkulo (Mb.) Waziri wa Fedha.”
Je, nani mkweli, ni Mkulo au nyaraka rasmi zilizopo kwenye majadala ya serikali zinazoonyesha ushiriki wa Mkulo katika kushinikiza METL auziwe kiwanja?
Ripoti ya CAG ilisema Mkulo aliingilia mchakato wa uuzwaji wa kiwanja, lakini wizara yake ikakanusha ripoti hii. Nani mkweli?
Uuzwaji wa kiwanja cha serikali namba 10 umemuweka njia panda Mustafa Mkulo baada ya ripoti ya CAG kuonyesha kuwa uuzwaji huo, uliihusisha Wizara yake na ofisi ya Msajili wa Hazina.
Sehemu ya ripoti hiyo ya CAG inasema: “Matokeo ya ukaguzi maalumu yalibaini mambo yafuatayo: Ilionekana kuwa ofisi ya Msajili wa Hazina na Wizara ya Fedha zilihusika moja kwa moja katika uuzwaji wa kiwanja Na.10…….. kilichouzwa kwa MeTL, bila kuishirikisha Bodi ya Wakurugenzi ya CHC.”
Je, CAG alikosea?
Labda swali la msingi ni je, hatua gani zitachukuliwa baada ya shutuma hizo zilizomo katika ripoti ya CAG? Au ripoti hiyo itatiwa kapuni kama ilivyo kawaida kila mwaka baada ya kujadiliwa kwa jazba pale mjengoni?
Mara baada ya Rais Kikwete mwishoni mwa Mei 2012 kuwatosa mawaziri sita kati ya wanane waliokuwa wametajwa kwa kashfa mbalimbali katika ripoti ya CAG, kulikuwa na tetesi kuwa baadhi yao walikuwa mbioni kushitakiwa kortini.
“Habari kutoka ndani ya serikali” zilisema tayari maofisa wa serikali walikuwa wanaandaa makabrasha ya kuwafikisha mahakamani mawaziri hao pamoja na maofisa kadhaa.
Hizo ni habari zilizotangazwa mwaka 2012, mpaka sasa hakuna ishara kuwa kuna hatua zozote za kisheria zinazochukuliwa.
Amentius Liyumba aliyekuwa mkurugenzi wa utawala wa Benki Kuu (BoT) alishitakiwa kwa matumizi mabaya ya ofisi. Je, na mawaziri wanaoandamwa na kashfa nzito na ripoti chafu za CAG kwanini wapendelewe?
- See more at: http://raiamwema.co.tz/lini-mawaziri-waliotimuliwa-watachukuliwa-hatua-za-kisheria#sthash.70LSStIe.dpuf

No comments: