Sunday 28 September 2014

POLE POLE ACHAMBUA JINSI CCM ILIVYOJICHIMBIA KABURI LAKE

Huzuni kubwa ninayopata kutokana na kupuuzwa kwa maoni ya wananchi ambayo mimi Polepole na wenzagu tulikuwepo walipoyatoa yananipa ujasiri zaidi na usiyo kifani, moyo mkuu na tumaini kwamba kuna tija katika kusimamia kweli. Nimeanza kusema hivi kwasababu hatimaye dhamira safi na ile mbaya zinaanza kuonekana bayana. Ninarudia kusema kwamba sasa wananchi wanaweza kuona chuya na mchele, kwa maana ya kile walichosema kiwemo katika Rasimu ya Warioba na ambacho Bunge Maalumu linapendekeza. Katika makala hii nitafafanua ni kwa namna gani Tanganyika imepotezwa na Zanzibar inahadaiwa.
Tanganyika unapotezwa tena
Rasimu ya Katiba inayopendekezwa inaondoa dhana ya usawa kati ya Tanganyika na Zanzibar. Zanzibar inaendelea kutambuliwa zaidi Kikatiba na inapewa mamlaka zaidi kwa mambo yake yasiyo ya Muungano, kitendo hiki ni kuikosea haki Tanganyika ambayo ni mshirika sawa na Zanzibar katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Tanganyika kataa kufichwa katika koti la Muungano, ni makosa kwa watu wachache kuifanya Tanganyika ndiyo iinuke kama Tanzania kwa maslahi yao binafsi. Kuna watu na makundi taasisi ambayo yananufaika katika Tanganyika iliyofichwa, isiyo na mwenyewe, isiyo na mwenye kuitizama, kuisimamia na kuiongoza. Kuna watu wanaona Tanganyika ukionekana bayana ubaya wao utawekwa bayana. Hata wahenga wa leo wanasema, mali bila daftari hupotea bila habari, Mali za Tanganyika zinafujwa kwa sababu hakuna daftari (Katiba ya Tanganyika) ambayo ingesimamia rasilimali za Tanganyika kama ambavyo Katiba ya Zanzibar inafanya katika Zanzibar ya leo.
Iko siku Mungu akinijaalia nitasema namna ambavyo kwa Tanganyika kufichwa wachache wananufaika isivyostahili, watu mmoja mmoja na makundi Taasisi, tena sasa hata makundi yanaongezeka kutoka yale ya kidesturi kuelekea kwa yale yasiyo ya kidesturi. Uwepo wa Tanganyika hauondoi uimara wa Jamhuri ya Muungano, ni sawa na uwepo wa California jimbo kubwa zaidi Marekani hakutishii kuondoa uwepo wa Nchi Moja imara duniani tena yenye Nchi Washirika 50.
Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa inaongeza ukiritimba wa kimadaraka katika gharama ya Tanganyika, hii siyo sawa hata kidogo. Rasimu ya Warioba inapendekeza Rais wa Tanzania na Makamu wake na Baraza lake la Mawaziri lisilozidi Mawaziri 15. Rasimu ya Bunge Maalumu inapendekeza Rais wa Tanzania mwenye Makamu watatu yaani Makamu wa Kwanza (mgombea mwenza) Makamu wa Pili ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Makamu wa Tatu ambaye ni Waziri Mkuu wa Tanzania. Rais huyu kama ambavyo anapendekezwa na Bunge Maalumu atakuwa na Baraza la Mawaziri wasiozidi 30, na kwa kuzingatia mjadala wa Bunge Maalumu unaoendelea inaonekana baadhi ya wajumbe wanapendekeza kusiwe na ukomo wa mawaziri. Mzigo huu ataubeba Tanganyika, na kwa sababu amevaa koti jipya la Muungano, atagharimia Muungano na atahangaika na mambo yake yasiyo ya Muungano. Huruma iko wapi?
Kwa sababu Watanganyika wengi mnaonekana mna ndoto ya urais wa Tanzania, mmeangukia katika mtego wa wanasiasa wenye maslahi binafsi kutoka Zanzibar na kwa maana hiyo wamewashika masikio. Mtu ambaye anautafuta urais wa Tanzania kwa kuwaangukia wanasiasa wa Zanzibar ili kupata kukubalika nao huyo hatufai, wananchi tumkatae Kabisa. Rais makini ni yule ambaye ana hofu ya Mungu, anasema kweli na anasema kweli tu hata kama ukweli huu hauwapendekezi wanasiasa wenzake katika chama chake na umma wa Watanzania kutoka Bara na Zanzibar. Wanasiasa wa Tanzania Bara hasa wale wa maslahi binafsi wautakao urais acheni kuwa wafungwa (captives) na mnisamehe kwa kusema ukweli usiofaa.
Najua wanasiasa wautakao urais wanapata pia mashinikizo kutoka taasisi ambazo ziko kizani na hazina desturi ya kukaa meza moja ya karamu na wanasiasa. Niwaonye wale mnaowapa mashinikizo wanasiasa, ole wenu maana historia kwa hakika itawaweka katika orodha ya watu wa kuaibishwa. Ninasema hivi kwasababu ninaanza kugundua kidogo kidogo kwamba mashinikizo ni kutoka vyama lakini inaonekana kutokana na uholela wetu na taasisi nyingine zinaanza kwenda kinyume na maadili yao na kuingilia kazi ya jukwaani, ole ninaitoa kwao!
Mnasingiziwa mnataka kuwa nchi mpya, hili silo kweli, mbona Zanzibar ilhali wakijua wao siyo nchi, waliandika katika Katiba yao mwaka 2010 kuwa wao ni nchi? Nani aliwakemea waziwazi? Na najua, pale walipopeleka ujumbe kwa faragha, majibu ya Wazanzibari yaliwamaliza kabisa na hatimaye hata leo Zanzibar ni nchi kwa mujibu wa Katiba yake. Usiri usiyo katika maslahi ya Taifa hustawisha uovu kama huu ambao Tanganyika inafanyiwa.
Mtapotezwa na mtalipa zaidi, ni kweli, hata sasa kwa Katiba ya Mwaka 1977 kuna vyanzo vitatu vya mapato ambavyo ni Kodi ya Mapato, Ushuru wa Bidhaa na Ushuru wa Forodha. Sisi tunajua kwa takribani miaka 30 Zanzibar imekataa mapato kutoka vyanzo hivi yanayokusanywa kutoka Zanzibar yasipelekwe kwa hazina ya Jamhuri ya Muungano kwa matumizi ya Muungano. Tafsiri yake ni kwamba Serikali ya Muungano imekuwa ikiwezeshwa na mapato kutoka Tanzania Bara pekee.
Nilidhani Bunge Maalumu lingeondoa utata huu ambao chanzo chake kilikuwa muundo wa Muungano wenyewe wa Serikali Mbili. Zanzibar wanasema hatuwezi kuchangia kama matumizi yanahusisha kwa pamoja mambo ya Muungano na yale yasiyo ya Muungano ya Tanzania Bara. Wazanzibari hawa wana hoja hapa, matokeo yake Bunge Maalumu na Kamati ya uandishi wamekwenda kurudisha yale yale yaliyotuletea mgogoro wa kikatiba ndani ya miaka 30 iliyopita.


Wamesema tena kwa sauti kuu hakuna Tanganyika bali kuna Jamhuri ya Muungano, ila Serikali ya Muungano itashughulika kila kitu cha Tanganyika. Tume ya Shelukindo au Tume ya Pamoja ya Fedha ilisema tofautisha mambo ya Muungano na mambo yasiyo ya Muungano ya Tanzania Bara kimapato na kimatumizi. Tumesema tena na tena huwezi kuachanisha mambo ya Muungano na yale yasiyo ya Muungano ya Tanzania Bara pasina kuipa Tanzania Bara Serikali yake na Bunge lake. Najiuliza je, kama tumeshindwa kufanya hivi kwa miaka takribani 30 na tumeshindwa kufanya hivyo licha ya kuwepo kwa kifungu cha Katiba kwa zaidi ya miaka 17, tumerudia yaleyale hivi kweli tuna nia ya kutatua kero na changamoto au tuna letu jambo?
Zanzibar unahadaiwa
Ndugu zangu Watanzania wenzangu niwaambieni tena bila kupepesa maneno hapa, kinachoandaliwa na Bunge Maalumu ukikitizama kitaalamu ni Katiba ya Tanganyika ambayo imepewa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hii ni Katiba ya Tanganyika na ushahidi ni namna ambayo imesheheneshwa mambo yasiyo ya Muungano kiasili ilhali tukijua mambo hayo ambayo wajumbe wa Bunge Maalumu wanayaita mambo ya wananchi hayawahusu wananchi wa Tanzania waishio Zanzibar. Hii ni hadaa kwenu Wazanzibari. Tarehe 27 Septemba wakati John Cheyo akitoa mchango wake kwa Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa, alikuwa akiwasihi wajumbe kutoka Zanzibar wasitukwamishie Katiba ya Jamhuri ya Muungano maana humo kuna mambo yetu, nikajiuliza, hivi ukisema mambo ya wananchi, je, Wazanzibar mnatoka nchi gani.?
Serikali ya Muungano na Tanganyika ndani, mkumbuke kero yenu kubwa ni Tanganyika kuvaa koti la Muungano, sasa niwakumbushe Tanganyika imepata koti jipya la Muungano na humo tumeweka mambo yetu yote ya wakulima, wafugaji, wavuvi, waalimu, vijana, tumejiwekea na taasisi na vyombo vyetu vya Tanganyika, tuna mpango wa kuimarisha Takukuru hata kama na ninyi mnayo ya kwenu, Tuna weka Baraza la Mitihani hata kama na ninyi mnalo la kwenu. Kwasasa tunaendelea kujadiliana pamoja na wajumbe kutoka Zanzibar namna bora ya kuweka mambo ya Tanganyika zaidi katika Katiba yetu ya Tanzania ambayo nanyi kwa jina ni yenu ila kwa mambo ya wananchi kwa hakika ni ya Tanganyika lakini wajumbe wa Bunge Maalumu kutoka pande zote wanawaomba muwasaidie kuipitisha tu ili faida iwe kwetu Tanganyika.
Si unajua Waziri Mkuu wa Tanzania hana Mamlaka ya Kikatiba Zanzibar, huyu tumeendelea kumtambua kama Waziri Mkuu wa Tanzania katika Rsimu ya Katiba ya Bunge Maalum hata kama kazi yake ni Tanzania Bara.
Bunge la Muungano na Tanganyika ndani, wanasiasa wa Tanzania Bara wakisukumwa na wale wenye maslahi binafsi kutoka Zanzibar wanapendelea Bunge liwe la Jamhuri ya Muungano hata kama zaidi ya asilimia 90 za kazi zake ni mambo ya Tanzania Bara. Katika mazungumzo ya hapa na pale nikiwa Dodoma nikang’amua kumbe ni jambo la kufa na kupona kwa Wazanzibar kuendelea kuwemo kwa kiwango cha sasa katika Bunge la Muungano na kama lilivyo, na mtu akaninong’oneza, wanaotaka muundo wa Bunge ubaki hivi ni baadhi ya wanasiasa kutoka Zanzibar. Sasa Zanzibar mtusaidie ili haki iwepo, kama mna nguvu hivyo na mnawapeleka mbio wagombea urais, fanyeni muujiza Watanganyika nao wapate Bunge Lao.
Kuhusu ustawi wa mambo ya wananchi, kwenye Rasimu ya Warioba tuliandika kwamba Tume ya Uhusiano na Uratibu mojawapo ya Jukumu lake katika Ibara ya 111(1)(b) ni “kusimamia, kuratibu na kuhakikisha kwamba kuna kuwiana kwa sera na sheria za nchi washirika kwa mambo yasiyo ya Muungano”. Haya yote yamefutwa, maana yake ustawi wa mambo ya wananchi umegawika kati ya Tanzania Bara na Zanzibar, na haya ndiyo tunasema siyo sawa, tunaligawa Taifa, siyo sawa.
Mmemkosa mbia wenu katika Muungano, na ninapenda Wazanzibari mjue hivyo, mbia wenu sasa ni Jamhuri ya Muungano kwa mujibu wa Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa. Ni kama vile watu wawili wakifungua kampuni, halafu mmoja akajenga mazingira na kuhodhi kampuni, siku yule mwingine akalalamika na cha kushangaza alijibiwa na kampuni badala ya mbia mwenzake. Ukifikia hali hiyo ujue hauko kikamilifu katika kampuni, na ukiona unadai uhuru wako wa kufanya mambo yako nje ya kampuni uje una hila ya kuivunja kampuni. Kampuni hii ni Tanzania na wabia wake waanzilishi ni Tanganyika na Zanzibar.

No comments: