Leo wajumbe wa Katiba 629 wamepiga kura kati yao 412 Kutoka Tanganyika na Waliotoka Zanzibar ni 217 Rasimu hii inahitaji wajumbe hawa 145 kutoka Zanzibar ndio ipate two third majority, Lakujiuliza kwa vile CUF ina wawakilishi 33 na Wabunge 25 , Chadema ina wanne na Leo wabunge Saba wamepiga kura saba za hapana kati ya wale 201 Lakujiuliza vipi Ukawa watakuja na number ya wajumbe 75 kuikosesha rasim u ya vitisenti kupata ridhaa ya Wazanzibari ?
Kinyume chake ni kuwa Rasimu ya Vijisenti imeelemea moja kwa moja kwenye mrengo wa siasa kali za kulia. Imechukuwa kila kitu kwenye Muungano na haikuacha lolote kwa nchi washirika. Na hapo panaifanya Zanzibar kufa dungu msooni, kwa kutumia maneno ya Arham Ali Nabwa. Inaambiwa mchezoni haimo na ilokwishakula iziteme.Mwandishi wa siku nyingi na mwanasheria wa Zanzibar, Ally Saleh, ambaye pia aliwahi kuwa mjumbe wa tume iliyokusanya na kuratibu maoni ya wananchi juu ya katiba mpya (Tume ya Warioba), anaandika hivi kwenye waraka wake kwa wabunge wa Zanzibar waliomo kwenye Bunge Maalum la Katiba.
“Si kweli, na si kweli kabisa, kuwa Katiba Inayopendekezwa ina maslahi na Zanzibar. Haina, haina katu, haina abadan, kamwe haina. Ni katiba ambayo inatuweka pabaya na pagumu zaidi na imeendelea kuyachukua mamlaka ya Zanzibar na kuyatia katika Muungano. Vipi Katiba hii itakuwa na maslahi na sisi (ikiwa) …. kundosha au kuukataa mfumo wa Shirikisho ina maana
(a) Zanzibar haiwezi kuwa na hadhi na haki sawa na Serikali ya Muungano, (
b) Tumejibakisha pale pale Zanzibar haina mshirika mwenziwe kwenye Muungano
, (c) Tumerudi pale pale mshirika wa Zanzibar ni Tanzania na kwa hivyo hakuna usawa
, (d) Tumeganda pale pale kuwa Tanganyika inasimamiwa na Serikali ya Muungano
, (e) Tumesalia papo kuwa Bunge la Muungano linatunga sheria za Tanganyika na tunajua kuwa sheria kama hizo hazina nguvu Zanzibar
, (f) Tumejizuga vile vile kumwita Waziri wa Muungano hata asiyesimamia jambo la Muungano kama kilimo bila ya kuwa na hadhi kama hiyo, (
g) Tumekwama pale pale Mahakama Kuu ya Tanganyika inaitwa ya Muungano, (
h) Tumejidanganya vile vile wafanyakazi wote wa Tanganyika wanabaki ni wa Muungano na wale wa Zanzibar mwisho wao ni Chumbe.”
Ally Saleh, kama nilivyo mimi, ni mliberali wa Muungano. Anataka Muungano ubakie ukiwa na mageuzi ya kimsingi. Anataka nguvu ya Serikali ya Muungano kwa mambo yasiyokuwa ya Muungano katika nchi washirika zipungue kama si kuondoka kabisa. Anataka mgawanyiko wa wazi wa ipi Tanganyika (kama nchi mshirika) na ipi Tanzania (kama Muungano wenyewe). Anataka hadhi na heshima ya Tanganyika, kwa upande mmoja, na Zanzibar, kwa upande mwengine, zitambulike na ziheshimike.
Rasimu ya Vijisenti inafanya kinyume chake na hapo ndipo unapolifanya kundi la mrengo wa siasa kali za kushoto ndani ya visiwa vya Zanzibar kuwa na nguvu kwenye hoja yake. Baada ya Rasimu hii, sasa ni rahisi zaidi kuushawishi umma kuamua dhidi ya Muungano kwa ujumla wake kuliko kuamua juu ya baadhi ya mambo na kuacha baadhi ya mengine ndani Muungano huo, kama ambavyo Rasimu ya Warioba ilikuwa imefanikiwa kuweka mizania.
Danganya-toto, kwa mfano, ya kumfanya rais wa Zanzibar kuwa makamu wa pili wa rais wa Tanzania, lakini wakati huo huo kuyapeleka madaraka ya Muungano kwa makamu wa kwanza na wa tatu (ambao si lazima wawe Wazanzibari na hata wakiwa hawawakilishi matashi ya Zanzibar kwenye Muungano) kumedhihirisha tu hoja ya wenye siasa kali za kushoto kuelekea Muungano, kwamba Dodoma haitapata usingizi hadi imalize kila alama ya uhuru, uwezo na hadhi ya Zanzibar.
Waliberali wa Kizanzibari wa Muungano – kama tulivyo mimi na Ally Saleh – ambao kila siku tuliamini kuwa njia ya kati na kati inawezekana kupitika kuelekea Muungano ’mzuri zaidi’ kati ya Tanganyika na Zanzibar, tumeambiwa na Rasimu ya Vijisenti kwamba hilo halipo wala haliwezekani kabisa. Tumekhiyarishwa baina ya kuisalimisha kabisa heshima ya nchi yetu au kuukataa kabisa Muungano na Tanganyika.
Wakati Rasimu hii imetunyima sisi waliberali tunachokitaka, na ambacho tunaamini ndicho pekee kinachoweza kuudumisha na kuunusuru Muungano, imewapa kila kitu wale wenye siasa kali za mrengo wa kulia, ambao mtazamo na siasa zao ni kuelekea nchi moja na serikali moja na ambao wala si waumini wa Muungano kwa dhati yake, bali Muungano kwa jina lake tu. Kwa dhati kabisa, kundi hili linaamini kuwa Zanzibar haipaswi hata kuishi kama sehemu muhimu na yenye upekee kwenye Muungano, bali inapaswa tu kuwa kama vile zilivyo Arusha, Tanga na Shinyanga.
Tuliokosa si sisi Waliberali tu, bali pia kundi jengine ambalo si dogo ndani ya visiwa vya Zanzibar ambalo liliivumilia mizania ya Rasimu ya Warioba licha ya kwamba haikuwapa kila wakitakacho – la siasa kali za kushoto kuelekea Muungano. Lile ambalo linaamini juu ya kutokuwepo kabisa kwa Muungano. Lakini kwa kuwa kundi hili lilitegemea sana matokeo hayo, halikushitushwa isipokuwa tu limethibitisha na kupata hoja ya kutusuta sisi wengine. Na kwa msingi huo, sasa linapata uhalali zaidi kuliko kundi la akina miye na Ally Saleh.
Matokeo yake ni kuwa Rasimu ya Vijisenti inatufanya na sisi waliberali tuangalie upya siasa zetu kuelekea Muungano kwa mara ya kwanza. Je, ni kweli hapa njia ya kati na kati kuelekea kwenye Muungano wa heshima, haki na usawa kama tulivyokuwa tukiamini siku zote? Je, nasi tuelemee kushoto kabisa au kulia kabisa?
Majibu ya maswali haya yametolewa kwa njia isiyo sahihi ndani ya Rasimu ya Vijisenti; na haitakuwa ajabu kwamba Rasimu hii, kwa hivyo, ndiyo itakayouvunjilia mbali Muungano huu uliodumu kwa nusu karne. Waswahili husema: “kheri i matumboni mwa shari!”
No comments:
Post a Comment