Wednesday 26 November 2014

PINDA AINGIZWA KWENYA KUNDI LA MAFISADI


Waziri Mkuu Mizengo Pinda. 
WAZIRI MKUU
- Kamati imesema imejiridhisha pasipo mashaka kuwa, Waziri Mkuu, alikuwa ana taarifa zote kuhusiana na mchakato mzima wa kuchotwa fedha kutoka katika akaunti ya ESCROW.
-Kamati, kwa kuzingatia kielelezo namba 22, inathibitisha bila shaka kwamba, Waziri Mkuu alikuwa analijua jambo hili vizuri na kwamba aliridhia muamala huu ufanyike. Ndiyo maana katika maelezo yake ya
Bungeni mara kadhaa Waziri Mkuu alithibitisha kuwa fedha za Escrow hazikuwa fedha za Umma.
- Ripoti yasema ni jambo la kushangaza kuona kwamba, jambo kubwa na zito kama hili lingeweza kufanyika bila ya mamlaka za juu, hususan Mhe. Waziri Mkuu kufahamu.
-Yaongeza kuwa kwa uzito na unyeti wa jambo hili, vyovyote vile, Waziri Mkuu anapaswa kuwajibika kwa kauli zake na kwa kutokutekeleza wajibu wake wa kikatiba ipasavyo, ili kurejesha imani ya wananchi
kwa serikali yao na viongozi wao wa kisiasa.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Fredrick Werema.
MWANASHERIA MKUU
-Kamati imethibitisha kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali alitoa ushauri ulioipotosha Benki Kuu ya Tanzania kuhusiana na hukumu ya Jaji Utamwa J. Kwa kutumia madaraka yake vibaya, Mwanasheria Mkuu
wa Serikali aliagiza kodi ya Serikali yenye thamani ya shilingi 21 bilioni isilipwe 107
na hivyo kuikosesha Serikali mapato adhimu.
- Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kujua na kwa makusudi alilipotosha Bunge na Taifa kwamba mgogoro uliopelekea kufunguliwa kwa Akaunti ya
ESCROW ulikuwa ni mgogoro wa Wanahisa wa IPTL badala ya mgogoro kati ya TANESCO na IPTL. Kamati inapendekeza kuwa uteuzi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali utenguliwe mara moja na kisha
afikishwe mahakamani kwa matumizi mabaya ya Ofisi yaliyopelekea Serikali kupoteza mabilioni ya fedha.
Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo.
WAZIRI WA NISHATI NA MADINI
- Kamati imethibitisha kuwa Waziri wa Nishati na Madini amekuwa, mara kwa mara, akilipotosha Bunge tukufu na Taifa kwa ujumla kuhusiana na Fedha za Akaunti ya Tegeta ESCROW kwamba ndani ya
fedha hizo hakukuwa na fedha za umma. Hata mtu wa kawaida angeweza kujua kwamba washirika wa ‘Tegeta Escrow Account’ ni akina nani na masharti ya kutoka kwa fedha hizo kwenye akaunti ni yapi
kwa mujibu wa Mkataba wa uendeshaji wa akaunti hiyo.
-Hata hivyo, katika hali ya kushangaza, aidha kwa makusudi ama kwa sababu anazozijua vizuri zaidi mwenyewe, Waziri wa Nishati ananukuliwa kwenye kumbukumbu rasmi za Bunge, Kwa nguvu
kubwa na kwa kujiamini, akitetea uchotwaji wa fedha hizo kinyume na masharti ya Mkataba wa Escrow.
-Aidha, Kamati imebaini kuwa Waziri wa Nishati na Madini ndiye alikuwa dalali mkuu aliyewakutanisha Bwana Harbinder Singh Sethi na Bwana James Rugemalira, tena katika ofisi ya Umma; na
pengine hii ndiyo iliyokuwa sababu ya upotoshaji huu. Waziri wa Nishati na Madini alifanya udalali huo akijua dhahiri kuwa Bwana Sethi hana uhalali wa kisheria kufanya biashara kwa jina la IPTL.
-Iwapo Waziri wa Nishati na Madini angetimiza wajibu wake ipasavyo, Fedha za Tegeta ESCROW zisingelipwa kwa watu wasiohusika, na Nchi ingeweza kuokoa mabilioni yaliyopotea kama kodi za VAT,
Capital Gain Tax na Ushuru wa Stempu ambazo ni sawa na takribani shilingi bilioni 30.
-Kamati inapendekeza kuwa Mamlaka yake ya uteuzi itengue uteuzi wa Waziri wa Nishati na Madini kutokana sababu hizo zilizoelezwa.

NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI
-Kamati imethibitisha kuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini alisema uongo Bungeni kwa kutamka kauli ambazo zilizokuwa na lengo la kupotosha umma kuhusu akaunti ya Tegeta ESCROW ikiwemo kutoa
kauli ambazo zingeweza kusababisha Nchi kuingia kwenye mgogoro wa kidiplomasia na
nchi ya Uingereza.
-Kamati inapendekeza kuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini achukuliwe hatua kali za kinidhamu ikiwemo kutenguliwa uteuzi wake. Kamati pia inapendekeza kuwa Naibu Waziri huyu afikishwe mbele ya
Kamati ya Bunge ya Maadili ili aadhibiwe kama Mbunge kwa kusema uwongo Bungeni ili liwe fundisho kwa wabunge wengine kuhusiana na kauli wanazotoa ndani ya Bunge lako tukufu.

KATIBU MKUU WA WIZARA YA NISHATI NA MADINI
-Kamati imethibitisha kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini aliingia makubaliano ya kutoa fedha katika Akaunti ya Tegeta ESCROW bila kujiridhisha kikamilifu kuwa maamuzi ya hukumu ya ICSID 2 yalikuwa bado kutolewa na hivyo kusababisha fedha kutolewa bila kukokotoa upya gharama za ‘capacity charges’, jambo ambalo limesababisha kupoteza fedha za umma.
-Vile vile, Kamati imebaini kuwa, Katibu Mkuu hakufanya uchunguzi wa kina (due diligence) kujiridhisha uhalali wa Kampuni ya Mechmar kuuzwa kwa Piperlink na baadaye kuuzwa kwa PAP, na hivyo kusababisha fedha za akaunti ya Tegeta ESCROW kulipwa kwa asiyestahili na kinyume cha Mkataba wa akaunti ya Escrow.
-Kwa maana hiyo, Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini, pengine kwa uzembe wake ama kwa kukusudia kwa sababu anazozijua yeye mwenyewe zaidi, amesaidia uchotwaji na
hatimaye utakatishaji wa fedha haramu.
-Kamati pia imethibitisha uzembe wa hali ya juu uliofanywa na Katibu Mkuu huyo, kushindwa kujiridhisha kama masharti ya Sheria ya kodi ya Mapato Sura ya 333, Kifungu cha 90(2) yalitekelezwa. Kifungu hicho kimsingi kinaitaka mamlaka ya ‘approval’’ ya uhamishaji wa Makampuni kutotambua Kampuni mpaka kwanza kodi za uhamishaji ziwe zimelipwa na hati za malipo ya kodi zimetolewa na mamlaka ya kodi.

-Kamati inapendekeza kuwa uteuzi wa Katibu Mkuu huyu utenguliwe, na TAKUKURU wamfikishe mahakamani mara moja, kwa kuikosesha Serikali Mapato, matumizi mabaya ya ofisi na kusaidia utakatishaji wa fedha haramu

No comments: