Monday 12 January 2015

Miaka 51 ya Mapinduzi tumetoka wapi na tuko wapi ?

hini ya uongozi wa Karume, Zanzibar inatajwa kama nchi iliyokuwa ikipiga hatua nzuri hasa katika maendeleo ya uchumi kuliko nchi zote za Afrika Mashariki.Kwa mfano, ‘tarikhi’ ya Zanzibar inaonyesha wananchi walikuwa wakipata huduma za maji safi na salama, afya, chanjo na matibabu, kujengewa makazi bora na ya kisasa.Chini ya Serikali ya awamu kwanza kulikuwa na kasi ya ujenzi wa viwanda, karakana, mashirika ya Serikali. Usafirishaji wa mazao kama pilipili, mbata na karafuu nao ulikuwa juu na kuiwezesha Zanzibar kupata fedha za kigeni hatua iliyosaidia kuimarisha uchumi.Nyaraka mbalimbali zinaonyesha kuwa msingi wa Mapinduzi ulikuwa ni kuwatoa wananchi katika kadhia ya unyonge, uonevu, ukandamizaji wa haki na fursa. Pia kuwapatia huduma bora za jamii baada ya kuondoa utawala wa Kisultan uliohamia kutoka Oman.Baada ya Mapinduzi, ujenzi wa viwanda vya sigara, mvinyo, nguo, sukari, soda, viatu, maziwa, magodoro na vitu vya nyumbani, kulitanua wigo wa ajira kwa wananchi, huku kukiwa na kasi kubwa ya uzalishaji mazao shambani kutokana na Serikali kupeleka pembejeo na mbolea kwa wakulima.
 Hali ilivyo sasa
Kati ya mambo yaliyowasukuma Waafrika wa Zanzibar na kulazimika kukiunga mkono Chama cha Afro Shirazi Party ( ASP) ilikuwa ni tatizo la ardhi. Walowezi na mabebari wengi ndiyo waliokuwa wakimiliki na kuhodhi ardhi yenye rutuba.Awamu ya kwanza iligawa ardhi kwa wananchi, lakini hali ilivyo sasa ni sawa na ile iliyokuwa kabla ya Mapinduzi mwaka 2964.Mkurugenzi wa Mamlaka ya Uwekezaji na Vitega uchumi Zanzibar (ZIPA), Nassor Salum anasema hivi sasa Zanzibar inakabiliwa na tatizo kubwa la uwekezaji wa miradi hasa katika sekta ya utalii, kutokana na maeneo mengi ya fukwe hasa katika ukanda wa Mashariki kuchukuliwa na baadhi ya vigogo na watendaji serikalini.“Maeneo makubwa ya ardhi yamehodhiwa, kuzungushwa kuta bila ya kuendelezwa kwa maelezo kuwa yamekuwa yakiwekwa ili kusubiri matajiri wa nje na ndani na kuuzwa kwa bei ya juu,’’ anasema.
Elimu
Wakoloni walitoa elimu kwa misingi ya rangi, Waafrika waliwekwa kando. Miaka 51 ya mapinduzi wananchi hawaridhiki na hali ilivyo kwenye sekta hiyo.Ukweli ni kuwa elimu Zanzibar inaendeshwa kimatabaka. Wananchi walio wengi wanasomesha watoto wao katika shule za Serikali zinazokabiliwa na changamoto nyingi za kitaaluma. Watoto wa viongozi, matajiri wengi wanasoma shule binafsi zenye mazingira bora ya utoaji taaluma.

 Makazi
Kabla ya mapinduzi, nyumba nyingi za wananchi wenye asili ya Kiafrika, zilikuwa zikisikitisha. Zilijengwa kwa miti, udongo na kuezekwa kwa makuti au vipande vya madebe.Hali hiyo inatajwa kuwa moja ya sababu zilizowahamasisha wananchi kukiunga mkono Chama cha ASP, kilichofanikiwa kuuondosha utawala wa Kisultan uliokuwa ukilindwa na Waingereza.Hata hivyo, mara baada ya Mapinduzi, Serikali ya awamu ya kwanza, ilitimiza ahadi ya kuwapatia wananchi makazi bora kwa kuwajengea makazi bora. Mpango huo uliendelezwa na awamu zilizofuatia ingawa haukuwa na tija kubwa kwa wananchi wanyonge, kutokana na nyumba nyingi za gharama nafuu zilizojengwa kuhodhiwa na vigogo badala ya wananchi makabwela.
 Kilimo

Wananchi wanyonge kabla ya Mapinduzi walipata dhiki katika ufanyaji wa kazi za kilimo kutokana na ardhi kubwa kuhodhiwa na walowezi na matajiri.gi walilazimika kukodi ardhi kwa ajili ya kilimo na sehemu ya mazao waliopata walitakiwa kuwapa waliowakodisha ardhi.Yalikuwa ni madhila na mashaka makubwa yaliowakumba Waafrika. Mara baada ya Mapinduzi, Serikali iliwapa ekari tatu kwa ajili ya kuendesha shughuli za kilimo.Hata hivyo, leo kilimo kimedorora licha ya kuwa sehemu kubwa ya visiwa vya Unguja na Pemba kuna ardhi ya kutosha yenye rutuba. Kilimo hicho kwa sasa kinachangia asilimia 31 ya pato la Zanzibar.Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Kilimo, Serikali imekuwa ikitenga kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya bajeti ya mishahara badala ya bajeti ya miradi ya maendeleo.Taarifa zinaonyesha bajeti ya mwaka inayokwenda katika mishahara ni zaidi ya Sh12 bilioni, ilhali bajeti inayotengwa kwa maendeleo ni Sh1.5 bilioni. Kinachosikitisha ni kuwa wahisani ndio wanaoonekana kuwa na uchungu na kilimo kwa kutenga bajeti ya Sh8 bilioni kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
 Afya
Mchango wa Serikali katika kutoa huduma za afya baada ya miaka 51 ya Mapinduzi, hauridhishi hali inayosababisha Wizara ya Afya kuonekana ni tegemezi kwa wahisani.Kwa sababu ya udogo wa bajeti ya sekta ya afya, huduma nyingi zimezorota, huku idadi ya wagonjwa wanaolazimika kutibiwa nje ikiongezeka kila mwaka. Fedha nyingi zinatumika nje kwa ajili ya kuwatibia wagonjwa wa moyo na saratani, kwa kuwa nchi haina wataalamu bingwa wa magonjwa hayo na vifaa vya kisasa.Tunatekelezaje malengo ya Mapinduzi?
Ili Serikali ionekane ikitekeleza malengo ya Mapinduzi, haina budi kusimamia dhana ya usawa, haki na uwajibikaji.Kero tete za wananchi kama vile kushamiri kwa rushwa, kuuzwa kwa ardhi, elimu duni, huduma mbaya za afya, zinaweza kufikia kikomo ikiwa Serikali itaamua kuzifungia kibwebwe.Kukuza uchumi wa mtu mmojammoja na hata Taifa, hatuna budi kuwekeza katika elimu, kilimo, ufugaji, uvuvi na ujenzi wa viwanda.

No comments: