Monday, 2 February 2015

MAJIMBO YA TEMEKE NA KIGAMBONI – HAPATOSHI MWEZI OKTOBA

Na. Julius Mtatiro, former CUF Deputy Sectary

Katika uchambuzi wa leo tutagusia majimbo mawili ambayo ni Temeke na Kigamboni. Majimbo haya yanatufungia rasmi mfululizo wa uchambuzi wa majimbo ya Mkoa wa Dar Es Salaam, kwani, katika makala mbili zilizopita (Jumamosi ya tarehe 10 na 17 Januari 2015) tulichambua majimbo mengine 6 ya Dar Es Salaam huku Temeke na Kigamboni vikibaki kuwa kiporo, “lakini kisichochacha”.
UTANGULIZI
Wilaya ya Temeke ni moja ya wilaya tatu za Mkoa wa Dar Es Salaam, ina eneo la kilomita za mraba 656; ipo upande wa kusini wa Mkoa wa Dar es Salaam, kwa upande wa mashariki inapakana na Bahari ya Hindi, kusini inapakana na Wilaya ya Mkuranga – Mkoa wa Pwani na upande wa kaskazini na magharibi inapakana na Manispaa ya Ilala.
Kwa mujibu wa Sensa ya Taifa ya mwaka 2012 Temeke ina jumla ya wakazi 1,368,881. Kati ya hao wanaume ni 669,056 na wanawake ni 699,825, huku ongezeko kubwa la wakazi, likitokana na harakati za kufufua uchumi pamoja na uhamiaji wa watu kutoka vijijini.
Temeke inamiliki eneo kubwa la biashara na viwanda ambapo kuna viwanda zaidi ya 200 vikubwa vikiwa zaidi ya 40 zaidi ya 160 vikiwa vya kati na vinachangia ajira kwa wakazi pamoja na wananchi wa wilaya za jirani.


JIMBO LA TEMEKE
Hili ni moja ya majimbo mawili yanayopatikana katika wilaya ya Temeke na ni moja kati ya majimbo yenye historia ya kufanya chaguzi nyingi mno hapa Tanzania. Uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi ulishuhudia jimbo hili likichukuliwa na CCM lakini ikipata upinzani mkubwa kutoka kwa vyama vingine.
Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995 kwa majimbo ya Dar Es Salaam ikiwemo Kigamboni ulifanyika tarehe 19 Novemba 1995, baada ya uchaguzi, wagombea wa NCCR na CUF walikata rufaa Mahakama Kuu dhidi ya mgombea wa CCM kwa sababu mgombea huyo alituhumiwa kutoa rushwa na makosa mengine. Mahakama kuu ilimkuta na hatia na kubatilisha matokeo ya jimbo la Temeke.
Baada ya uamuzi wa mahakama.
Uchaguzi wa marudio uliofanyika jimboni humo mwezi Oktoba mwaka 1996 ulikuwa na msisimko mkubwa baada ya gwiji la siasa za Tanzania wakati huo, Augustine Mrema (Ambaye alimtikisa Benjamin Mkapa katika urais mwaka 1995) kugombea Temeke kwa tiketi ya NCCR. Mrema alishinda kwa kura 54,840 = 59% dhidi ya Abdul Cisco Ntiro wa CCM aliyepata kura 33,113 = 36%.
Hata hivyo, kutokana na kutoelewana na viongozi na wabunge wenzie wa NCCR, Mrema aliamua kuhamia chama cha TLP na hivyo kukatisha kipindi chake cha ubunge katika jimbo la Temeke mwaka 1999 kwani kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania ya wakati huo na sasa, ukihama chama cha siasa unapoteza na nafasi ya uwakilishi kwa wakati huo.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) iliitisha uchaguzi mwingine, safari hii pia Mrema alijiandaa kugombea kwa tiketi ya TLP lakini Mahakama Kuu ya Tanzania ilizuia asigombee baada ya NCCR kumuwekea pingamizi.
Tarehe 11 Julai 1999 uchaguzi wa marudio ulifanyika na Matokeo yalilirudisha jimbo la Temeke mikononi mwa CCM baada ya John Kibasso wa CCM kupata ushindi wa kura 27,090, Tambwe Hizza wa CUF akiwa wa pili kwa kura 25,742, Abbas Mtemvu(Mbunge wa sasa wa CCM) akipata kura 14,701 (wakati huo akiwakilisha chama cha TLP) na Suleiman Hegga wa NCCR-Mageuzi alipata kura 866.
Uchaguzi mkuu uliofuatia, yaani mwezi Oktoba mwaka 2000, ulishuhudia ushindani mkubwa katika jimbo la Temeke. Chama Cha Wananchi CUF ambacho kilimsimamisha Tambwe Hizza (aliyekuwa moto wakati huo) kilipewa nafasi kubwa ya kushinda lakini mgawanyiko wa vyama vya upinzani ulisababisha mgombea wa CCM John Kibaso apate jumla ya kura 60,872 huku vyama 8 vya upinzani kwa ujumla (Ikiwemo CUF) vikipata kura 89,665 (nyingi kuliko za CCM) laini vikibwagwa na CCM ikipeta.
Mtanange wa mwaka 2005 ulizidi kuiweka CCM katika chati yake huku mgombea wa CUF Hizza Tambwe akipoteza umaarufu, lakini CCM mara hii inasaidiwa na umaarufu wa mgombea urais wake, Jakaya Mrisho Kikwete. Jumla ya vyama 6 vilisimamisha wagombea kwa uchaguzi wa mwaka 2005, matokeo rasmi yaliipa CCM ushindi wa asilimia 60 uliotokana na kura 103,545 huku CUF ikipata asilimia 27.5 zilizotokana na kura 47,448, CHAUSTA ikiwa ya tatu kwa kura 14,425 zilizoipa asilimia 8.4 na kisha vyama vingine vitatu CHADEMA, TLP na DP vikipata kura 5,762 (kwa ujumla) ambazo ni sawa na asilimia 3.4 ya kura zote.
Katika uchaguzi huu CCM ilimleta Zuberi Abasi Mtemvu (aliyewahi kugombea kupitia TLP katika jimbo hilohilo), CUF ikimrejesha Tambwe hiza na CHAUSTA ikimuweka Sheikh Fumba Jamanda.
Nusura jimbo la Temeke liende mikononi upinzani mwaka 2010, lakini kukosekana kwa maridhiano baina ya vyama vya upinzani kulipelekea CCM kupata ushindi huku vyama vikuu vya upinzani vikigawana kura.
Abasi Mtemvu safari hii akipoteza mvuto alishinda kwa asilimia 48.21 = kura 58,339 (akishuka kwa asilimia 12 kulingana na mwaka 2005), kura za CUF zilipungua kwa kiasi kikubwa, kutoka 47,448 mwaka 2005 hadi kura 28,877 = 23.86% mwaka 2010 huku mgombea wa CUF akiwa ni Limbu Kadawi Lucas (Muasisi wa chama cha ADC na sasa Mwenyekiti aliyesimamishwa wa ACT – Tanzania). Kura za CUF ziligawika sana baada ya CHADEMA kumsimamisha Ng’hilly Dickson Amos aliyekuwa wa tatu kwa kura 27,899 = 23.06%.
Wagombea wa vyama vingine 8 walipata asilimia 2.59 ya kura zote. Tutagundua kuwa, matokeo ya jimbo la Temeke kwa mwaka 2010 yangepeleka ushindi kwa upinzani kwa sababu kura za wagombea wa CUF, CHADEMA na vyama vingine 8 zinafanya upinzani kwa ujumla kuwa na asilimia 49.5 dhidi ya 48.21% za CCM.
Kwa vyovyote vile iwavyo, miaka 10 ya Abbas Mtemvu kuwa mbunge wa Temeke inaelekea ukingoni na naamini CCM haitamsimamisha tena kwa kuhofia nguvu ya UKAWA na hata kuchokwa kwambunge wao. Ikiwa CCM itamrudisha tena Mtemvu ina kila sababu ya kulipoteza jimbo la Temeke. Na hata ikileta mgombea mpya, nguvu ya UKAWA inaweza kuwa kubwa sana na ikabebwa na historia ya jimbo lenyewe kuwahi kuwa kitovu cha upinzani.
Lakini ushindi wa UKAWA utategemeana sana na aina ya mgombea atakayepeperusha bendera kwa sababu wapiga kura wa Temeke wanaweza wasifuate mkumbo wa upepo wa UKAWA na wakazingatia sifa za mgombea wa UKAWA atakayekuwepo ukilinganisha na zile za mgombea wa CCM. Ndiyo kusema kuwa, UKAWA ikimuweka mgombea dhaifu, isitegemee kubebwa na upepo wa mabadiliko labda tu itokee kwamba CCM nayo imesimamisha mgombea dhaifu. Kwa sababu hizi zote, jimbo la Temeke lina nafasi kubwa ya kwenda upinzani Oktoba mwaka huu.

JIMBO LA KIGAMBONI.
.




Jimbo la Kigamboni halikuwa nyuma kwenye siasa za mabadiliko, ni jimbo ambalo limewahi kuwa gumu kwa CCM na rahisi kwa upinzani na kuna wakati likawa tamu kwa CCM na chungu kwa upinzani na kwa ujumla hili ni jimbo gumu sana kama lilivyo lile la Temeke.
Katika uchaguzi wa mwaka 1995 mwezi Novemba ulioahirishwa kutoka Otoba 1995 kwa majimbo yote 7 ya Dar Es Salaam, CCM ilijipatia ushindi na kuliongoza jimbo hilo hadi mwaka 2000.
Vuguvugu la mabadiliko na kukua kwa Chama Cha Wananchi CUF nafasi ya NCCR ikipwaya, vilipelekea uchaguzi wa mwaka 2000 kuwa wenye ushindani mkali kati ya CCM na CUF na matokeo ya mwisho na rasmi yalimpa ushindi mgombea wa CUF Frank Magoba.
Kwa hiyo, kati ya majimbo ya Dar Es Salaam yaliyoonja ladha ya upinzani mapema na kwenye uchaguzi Mkuu wa jumla ni pamoja na jimbo la Kigamboni. Tafsiri ya hali hii ni kuwa, jimbo hili liko “flexible” katika chaguzi zijazo. Hata hivyo, Frank Magoba alijisalimisha CCM na kuwa mwanachama wa chama hicho alipomaliza kipindi chake cha ubunge wa Kigamboni, baadaye alikimbilia Mbeya Vijijini ili kugombea ubunge katika uchaguzi wa mwaka 2005 na kuangushwa kwenye kura za maoni ndani ya CCM.
Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 ulikuja na kimbunga cha umaarufu wa “JK” akiwa mgombea urais wa CCM na umaarufu huo uliibeba CCM kwa ujumla na kuwasaidia wagombea ubunge wa chama hicho. Hata hivyo, huu ni wakati ambapo mgombea wa CUF Prof. Ibrahim Lipumba alizidi kuwa na nguvu za kisiasa katika nchi na ilitarajiwa kwamba ukuaji wa CUF na mvuto na umaarufu wa Lipumba vingeisaidia CUF. Hali haikuwa hivyo wakati matokeo yanatangazwa kwa jimbo la Kigamboni, CCM ilifanikiwa kulitoa mikononi mwa CUF na kulirudisha kwenye himaya yake. Mwichumu Abdulrahman Msomi wa CCM aliwabwaga wagombea wengine.
Kiongozi huyu alipata kura 78,898 = 60.6% akifuatiwa na Bawji Mbwana Othman wa CUF aliyepata kura 45,671 = 35.1% huku wagombea wa vyama vingine 8 ikiwemo CHADEMA, wakipata asilimia 4.5 iliyotokana na kura 5,677
Mwaka 2010 uchaguzi mkuu ulikuwa na mabadiliko makubwa sana. Kushuka kwa umaarufu wa Kikwete, kasi ya kukubalika kwa CHADEMA katika maeneo mengi ya nchi n.k. Mara hii pia, CCM ilibadili mgombea na haikumleta Bi. Mwinchoum pale Kigamboni. Aliyepeperusha bendera ya CCM safari hii ni Dr. Ndungulile Faustine ambaye alipambana vikali na wagombea wa CUF na CHADEMA ambao waling’ara.
Sababu zilezile za kukosekana “UKAWA” mwaka 2010 ndizo ziliviponza vyama vya upinzani. Matokeo yanaonesha wananchi wengi walipiga kura CCM kwa sababu waliona kuna mvutano wa wazi kati ya vyama vya upinzani(hawa ni wale “undecided voters – wapiga kura wasiofanya maamuzi”) ambao kwa kawaida ni wengi.
Ushindi wa CCM katika jimbo la Kigamboni mwaka 2010 ulipungua kwa asilimia 10 ukilinganisha na mwaka 2005. Dr. Faustine Ndungulile aliipa CCM kura 53,389 dhidi ya kura 25,166 za Komu Maulidah Komu wa CHADEMA na kura 24,419 za Mustapha Ismail wa CUF. Vyama hivi vitatu na asilimia za ushindi wao katika mabano ni CCM (50.07%), CHADEMA (23.06%) na CUF (22.9%). Vyama vingine 9 vilivyoshiriki kwenye uchaguzi huo vikiwemo APPT Maendeleo kilichochukua nafasi ya nne na NCCR Mageuzi kilichochukua nafasi ya 7, vilipata jumla ya kura 2695 zilizofanikisha asilimia 2.52.
Uchaguzi wa mwaka 2010 kwa Kigamboni ulionesha dhahiri kuwa jimbo hilo linaweza kurudia historia yake ya kuongozwa na upinzani ikiwa vyama vya upinzani vyenye nguvu vitaweka mgombea mmoja. Uwepo wa UKAWA na kama itafanikiwa kuweka mgombea mmoja katika jimbo la Kigamboni mwezi Oktoba mwaka huu, kunaweza kumaanisha safari ya mwisho ya CCM kulichukua jimbo hilo. Kufanya vibaya kwa CCM katika masuala ya uanzishwaji wa mji mpya wa Kigamboni, madai mbalimbali ya wananchi kunyimwa haki zao katika mchakato huo kunaiweka CCM katika wakati mgumu kujitetea kwa wapiga kura. Inavyoelekea pia, katika kupunguza makali ya nguvu ya upinzani, itaipasa CCM kusaka mgombea mpya anayekubalika zaidi kuliko Ndugulile.
Pamoja na mgombea mpya, ukweli unabakia kuwa ikiwa UKAWA itapata mgombea thabiti, aliyejipanga, mwenye sifa, anayeuzika na atakayesaidiwa ipasavyo, jimbo hili la Kigamboni linaweza kuangukia mikononi mwa UKAWA.
Leo tumekamilisha rasmi uchambuzi wa majimbo yaliyopo mkoa wa Dar Es Salaam. Baada ya Dar Es Salaam, tutaanza kuchambua majimbo yaliyoko Mkoa wa Dodoma.
(Mchambuzi wa ukurasa huu ana uzoefu mkubwa wa masuala ya uongozi wa kisiasa ndani ya Tanzania. Ana shahada ya Uzamili ya Utawala na Uongozi (M.A) na ni mwanafunzi wa fani ya sheria (L LB) – Anapatikana kupitia +255787536759, majimboni2015@yahoo.com)
Uchambuzi huu wa majimbo unachapishwa na Gazeti la Mwananchi kila Jumatano na kila 




No comments: