Wednesday 11 February 2015

Salim-ahmed Salim

Joseph Mihangwa
HATIMAYE ile ndoto ya kuunganisha Vyama vya Tanganyika African National Union [TANU] cha Tanganyika na Afro-Shirazi Party [ASP] cha Zanzibar, ikatimia; Februari tano5, 1977. Wazo la kwanza la kuvunja TANU na ASP lilitolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Septemba 1975 mjini Dar es Salaam katika kikao cha pamoja cha Kamati Kuu za TANU na ASP, zilipokutana kujadili suala la uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano.

Rais wa Awamu ya Pili Zanzibar, Sheikh Aboud Jumbe Mwinyi, alikubali wazo hilo kimsingi, lakini akasema chama chake kilihitaji muda zaidi kufikiria. Wazo hilo lilijadiliwa Bara na Visiwani hivi kwamba, mwaka mmoja baadaye, Oktoba 1976, Vyama hivyo viwili vikakubaliana kuungana. Chama kipya kilichozaliwa kiliitwa “Chama cha Mapinduzi” [CCM] bila kuwa na tafsiri ya Kiingereza, baada ya Wazanzibari kusimama kidete kwamba, wasingekubali bila neno “Mapinduzi” kuonekana kwenye jina la chama kipya ili kuendeleza historia ya Mapinduzi yaliyoleta uhuru wao, Januari 12, 1964.

Ilikuwa ushindi pia kwa Wazanzibari kushinikiza na kufanikiwa kwamba, chama kipya CCM, kizinduliwe Februari 5, 1977, mwezi na tarehe ya kuzaliwa kwa ASP, kilichotokana na Muungano wa Vyama vya African Association [AA] na Shirazi Association [SA], kuunda “Afro-Shirazi Party” – ASP. Kuundwa kwa CCM kulirekebisha Katiba ya Pili ya Muda [Second Interim Constitution] ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, kuipa Serikali ya Muungano kinadharia, mamlaka makubwa kwa mambo ya Nje, Ulinzi, Polisi, Mabenki, Biashara ya Nje na Mikopo, Kodi na Ushuru wa Forodha; lakini kivitendo, Zanzibar iliendelea kivyake kwa mambo hayo bila kujali Katiba wala matakwa ya Mkataba wa Muungano.


Hii ilionesha dhahiri kwamba Wazanzibari waliingia kwenye muungano na kuunganisha vyama shingo upande. Ikumbukwe, Baraza la Mapinduzi na ASP vilikuwa na kauli turufu kwa Serikali, Wazanzibari na kwa Muungano kiasi cha kuonekana kero kwa mustakabali wa Muungano hivi kwamba, kuunganishwa kwa TANU na ASP ilikuwa mkakati na mbinu muhimu kwa Mwalimu kuleta udhibiti na utulivu kwa Muungano Visiwani.

Kuanzia Februari 1977 hadi Aprili 1983, fungate ya CCM ilikuwa ya furaha; lakini pale Mwalimu Nyerere alipoleta pendekezo lingine la marekebisho ya Katiba, kuliibuka zahama na tafsiri hasi Visiwani juu ya Muungano, kwamba Mwalimu alikuwa na nia ya kuimeza Zanzibar.

Matokeo yake, Wazanzibari wakaanza kulalamika na kuelezea hisia zao kupitia vyombo vya habari, ikiwamo redio mashuhuri ya mafichoni “Kiroboto tapes”, iliyomwaga matusi na kashfa mbali mbali kwa Muungano, “Watanganyika” na kwa Rais wa Muungano. Kufuatia tafrani hiyo, na kwa kuzihurumia sauti za Wazanzibari, Jumbe aliomba mawazo ya Makatibu Wakuu wa Wizara zote Visiwani juu ya Muundo wa Muungano unaotakiwa, ambapo karibu wote walipendekeza Muundo wa Serikali Tatu ili kulinda maslahi ya Zanzibar ndani ya Muungano.

Kwa kuzingatia malalamiko hayo, Rais Jumbe alimrejesha kwao Tanzania Bara, aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Jaji Damian Lubuva [sasa Mwenyekiti, Tume ya Uchaguzi nchini – NEC]; badala yake akamwita na kumteua raia wa Ghana, Kway Swanzy, na kumpa uraia kwa njia ya usajili. Mwalimu Nyerere aliona Jumbe akiupa kisogo Muungano na kuamua kutumia umahiri wake kuokoa jahazi. Alijua vyema udhaifu wa Wazanzibari ulikuwa kwenye umoja dhaifu na utaifa legelege kuweza kufananishwa na mti usio na mizizi.

Itakumbukwa pia kwamba, katika kipindi cha fungate mpya ya CCM, Jumbe alikuwa mstari wa mbele katika kutetea Muungano, akawa kipenzi cha Mwalimu, aliyetumika kwa uhuru zaidi ikilinganishwa na enzi za utawala wa mkono wa chuma wa hayati Abeid Karume. Kwa sababu hiyo, Jumbe alijiona ni mrithi mtarajiwa wa Nyerere asiye na mpinzani kwenye Serikali ya Muungano. Na kwa sababu ya kuelekeza nguvu na juhudi kubwa kwenye Muungano kuliko nyumbani, alijitengenezea maadui wengi Visiwani kiasi cha kutuhumiwa “kaolewa Tanganyika” – Mji Mwema, Dar Es Salaam.

Kufikia mwishoni mwa 1983, Jumbe alikuwa amepoteza imani na “hadhi” kwa Wazanzibari na Wasaidizi wake wa karibu; uongozi wake ulijenga vikundi vyenye uhasama ndani ya Serikali. Ni kwa sababu hizi, Jumbe alipoonekana kutaka “kuchokoza” Muungano kwa mbinu za Kizanzibari, ilikuwa rahisi kwa Nyerere kumng’oa madarakani.

Hatimaye, saa ya kumng’oa Jumbe kwa kuthubutu kukanyaga “patakatifu” ikawadia, Januari 1984. Kwenye Kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa [NEC] ya CCM mjini Dodoma, kilichoitishwa kwa dharura kujadili agenda ya Jumbe “kuhoji uhalali wa Muungano” kwenye Mahakama Kuu; Jumbe alielezewa kuwa kiongozi dhaifu na msaliti; akavuliwa nyadhifa zote za kichama na kiserikali katika Jamhuri ya Muungano na Zanzibar.

Tetemeko hili la kisiasa liliwakumba pia Wasaidizi wake wa juu; wakiwamo Waziri Kiongozi, Ramadhan Haji; Waziri wa Nchi, Aboud Talib; na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa zamani, Wolfgang Dourado, akatiwa kuzuizini kwa miezi sita. Aliyekuwa Naibu Waziri wa Ulinzi, Seif Bakari, na ambaye alimtetea Jumbe kwenye NEC kufa na kupona lakini bila mafanikio, aliwekwa chini ya ulinzi Bara, na baada ya hapo alipelekwa Geita kuwa Mkuu wa Wilaya. Bakari alikuwa chaguo la Wazanzibari kumrithi na kuendeleza sera za Karume, kama Nyerere asingeingilia kati na kumteua Jumbe badala yake. Nafasi ya Jumbe ilichukuliwa na Ali Hassan Mwinyi; na Seif Shariff Hamad akateuliwa Waziri Kiongozi.

Kutunguliwa kwa Jumbe pamoja na Waziri Kiongozi wake mjini Dodoma, kulijenga hali ya kutoelewana miongoni mwa viongozi wa Zanzibar kwa kundi moja kuunga mkono hatua hiyo kama njia ya kuondoa vikwazo kuelekea maendeleo; na kundi jingine kuona kama mbinu ya kisiasa ya kujitwalia madaraka bila haki ili kuirejesha Zanzibar enzi za kabla ya ukoloni. Kwa sababu hii, uongozi wa Zanzibar uligawanyika kwa misingi ya “Washindi” na “Washindwa”, huku kundi la “Washindwa” likitupa lawama kwa Mwalimu kwa “kucheza mchezo mchafu”.

Mgawanyiko huu ulizaa makundi mawili: kundi lililofanikisha kung’olewa kwa Jumbe likijiita “The Frontliners” [Wanamstari wa mbele] kwa maendeleo ya Zanzibar, na lile lililopinga kung’olewa kwake likijiita “The Liberators” [Wakombozi], kwa maana ya wakombozi na walinzi wa Mapinduzi ya Zanzibar, huku likiapa kulipiza kisasi kutikisa “mhimili” – Nyerere.

Hatimaye muda wa kufanya hivyo ukawadia, pale Nyerere alipowauma sikio “wapendwa” wake kwamba, muda wake wa kung’atuka ukifika, angependelea Rais atoke Zanzibar. Mchakato wa kumpata mrithi ulipoanza, idadi ya wagombea ilidhibitiwa kuwa watatu tu: Ali Hassan Mwinyi, wakati huo akiwa Rais wa Zanzibar na Makamu Mwenyekiti wa CCM Taifa na pia Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano; Rashid Kawawa; na aliyekuwa Waziri Mkuu na Mwanadiplomasia wa Kimataifa, Salim Ahmed Salim.

Kati ya watatu hao, ni Kawawa pekee hakuwa Mzanzibari; kuingizwa kwake kulionekana ni mchezo wa karata wa kisiasa. Kufumba na kufumbua Mwalimu akaanzisha mchezo wa karata ya kisiasa kupitia NEC na Kamati Kuu [CC] ya CCM kumpata mrithi aliyemtaka.

NEC na CC ziligubikwa tangu mwanzo na makundi mawili hasimu, yenye kuwania ukuu kwenye siasa za Zanzibar. Kundi la “Frontliners” liliundwa na wanasiasa wa mrengo wa kimaendeleo na usasa, kama kina Salim Ahmed Salim, Seif Sharrif Hamad [Waziri Kiongozi], Adam Mwakanjuki, Isaac Sepetu, Shabaan Mloo, Ali Salim na Ali Haji Pandu, wote Wajumbe wa NEC.

Kundi la “Liberators”, watetezi wa sera za hayati Abeid Aman Karume, liliongozwa na Brigedia Abdullah Said Natepe; wengine wakiwa ni Ali Mzee, Hassan Nassoro Moyo, Mohamed Seif Khatib na Salmin Amour. Kundi hili liliendesha pia kampeni za kutolewa kizuizini kwa Seif Bakari na Hafidh Suleiman kwa “jeuri yao” ya kutetea Jumbe asing’olewe.

Kwenye “Liberators” walikuwamo pia Wanausalama na Wanajeshi wastaafu. Mashuhuri miongoni mwao walikuwa ni aliyekuwa Waziri Kiongozi enzi za Jumbe, Brigedia Ramadhan Haji na Brigedia Khamis Hemed. Kundi hili lilikuwa na chuki dhidi ya Salim tangu mwanzo.

Kwa mfano, mwaka 1982 wakati Salim alipoteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Natepe [wakati huo Waziri katika Ofisi ya Rais mwenye dhamana ya Usalama wa Taifa] na Ali Mzee [Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais], walikwenda kwa aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Moringe Sokoine, kudai walikuwa na maagizo kutoka kwa Jumbe na Seif Bakari kusimamisha uteuzi wa Salim. Walitoa sababu mbili: moja kwamba kulikuwa na makubaliano ya siri tangu enzi za Karume, kwamba Wanachama wa zamani wa Vyama vya Siasa Visiwani mbali na ASP, wasipewe uongozi wa juu wa kisiasa katika Serikali ya Mapinduzi wala Serikali ya Muungano.

Salim Ahmed Salim alikuwa mmoja wa Viongozi Wakuu wa Chama cha Umma Party, kilichoratibu kwa mafanikio Mapinduzi ya Januari 12, 1964. Kufuatia kuundwa kwa Serikali ya mseto wa Vyama vya Afro-Shirazi na Umma Party mwezi huo, aliteuliwa kuwa Balozi wa Zanzibar nchini Misri, akiwa na umri mdogo wa miaka 22 tu.

Sokoine hakukubali kumeza “upuuzi” huo, akawatimua Natepe na Mzee wasionekane mbele yake; nyota ya Salim ikazidi kung’ara. Na Sokoine alipofariki kwa ajali ya gari mwaka 1984, Mwalimu alimteua Salim kuwa mrithi wake. Kitendo hicho kilifanya “Liberators” wavimbe kwa hasira na chuki; wakaanzisha kampeni nzito Bara wakidai kwamba Salim hakuwa na ushawishi wa kisiasa Visiwani, na kwamba angeshirikiana na “Ma-Sheikh” wa Kiarabu wa Ghuba kurejesha ubepari nchini; wakijua kwamba Salim alikuwa Msoshalisti wa kutupa tangu enzi za ZNP na Umma Party kusababisha baadaye akose kushika nafasi ya Ukatibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa kura [moja tu] turufu [veto] ya Marekani katika kinyang’anyiro cha nafasi hiyo.

Hawakujua pia kuwa siasa na sera za Tanzania wakati huo, zilikuwa zimeanza kufungua milango kwa Mataifa ya Kiarabu. Kwa mfano, kwa mara ya kwanza, Saudi Arabia ilikuwa imefungua Ofisi ya Ubalozi Jijini Dar es Salaam; na vivyo hivyo kwa Tanzania katika nchi nyingi za Kiarabu.

Kuona hoja yao haikuwa na mashiko, wakageuza kibao kwamba, Salim alihusika katika kifo cha Karume, wakati wakijua kipindi hicho alikuwa Balozi nchi za nje, na kamwe jina lake halikuwamo katika orodha ya walioshitakiwa. Mkakati wa kumchafua Salim uliandaliwa na kusimamiwa kwa ustadi mkubwa na Nassoro Hassan Moyo kwa kushirikiana na Natepe na kuwashirikisha pia Ramadhan Haji, Ali Mzee na Aboud Talib.

Moyo aliratibu mkakati huo kwa kushirikisha pia Wajumbe wa NEC wa Bara, kwa kuunda kambi iliyoongozwa na hayati Paulo Bomani na Getrude Mongella. Nyerere alipendelea Salim amrithi; alijua pia hujuma aliyokuwa akifanyiwa na kambi ya “Liberators”, lakini hakutaka kuonesha kumpigia kampeni.

Mwinyi aliombwa na Kambi ya “Front liners” kumuunga mkono Salim siku ya uteuzi, wakadhani wamemshawishi vya kutosha asiingie kwenye kinyang’anyiro. Ahadi yake iligeuka “shubiri” kwao siku Kamati Kuu ilipokutana, Agosti 12, 1985 kuteua wagombea wa nafasi ya Rais wa Muungano na wa Zanzibar. Kawawa, kama ilivyotarajiwa, alijitoa katika kinyang’anyiro; Mwinyi na Salim wakatolewa nje ili wajadiliwe kwa faragha.

Ilivyotokea, majadiliano yalijikita kwenye “sifa” za Mwinyi pekee na Salim hakujadiliwa kabisa, pengine kwa kuona kwamba alikuwa na sifa zilizotakiwa na za ziada. “Liberators” hawakulazia damu “ukimya” huo juu ya Salim; huku Moyo na Natepe wakiongoza kwa hoja.

Akazungumza Getrude Mongella; kwamba, kumruka Mwinyi ambaye alikuwa Makamu wa Rais na pia Makamu wa Mwenyekiti wa CCM Taifa, ili kumteua Salim, kungetafsiriwa vibaya kisiasa nchini na kimataifa. Kwa mlio huo wa “ngekewa” ambao haukutarajiwa, Mwinyi akawa mteule pekee wa Kamati Kuu kugombea Urais. Alitarajiwa kujiengua kutekeleza ahadi yake, lakini hakutaka tena; badala yake akasema: “Kama hayo ndiyo matakwa ya wananchi, nakubali [uteuzi huu] kwa moyo mkunjufu”.

Nyerere, akiwa Mwenyekiti wa Kamati Kuu hiyo, hakupinga; “Liberators” wakashangilia na kucheza kufurahia ushindi. Lakini mambo hayakuwa laini kiasi hicho majina yalipopelekwa kwenye NEC, Agosti, 15, 1985 ambako kambi ya “Frontliners” ilipinga vikali uteuzi wa Kamati Kuu na kuungwa mkono na “msiri” na mshauri mkuu wa Nyerere, Mzee Thabit Kombo. Kombo hakutaka kuona Mwinyi akiondoka Visiwani kwa hofu ya kupotea kwa hali ya amani na utulivu aliyoijenga katika miezi 18 ya uongozi wake.

Sauti za kuzomea kutoka kwa Wajumbe wa Bara [waliopandikizwa] zikasikika. Khatib Hassan wa kundi la “Frontliners”, kwa ujasiri mkubwa, akamuunga mkono Kombo; mjadala mkali ulioishia bila kupata mshindi, ukaanza. Nyerere, aliyekuwa na kauli turufu, akaahirisha kikao na kuwaita pembeni kwa mazungumzo washauri wake wakuu, wakiwamo Mwinyi, Kawawa na Kombo.

Kufuatia mazungumzo hayo, Kombo, katika hali ya kushangaza, alikubali uteuzi wa Mwinyi. Na kufuatia hatua hiyo, Wajumbe walipiga kura ya “Ndiyo” au “Hapana” kwa Mwinyi, ambapo ni kura 14 tu zilimkataa kati ya Wajumbe 1,746 waliopiga kura. Kambi ya “Frontliners” ililipuka tena kwa nderemo na vifijo kwa ushindi, safari hii wakidai kufanya “Mapinduzi” makubwa kuliko yale ya 1964, wakiimba “Salim amekwisha”.

Moyo na marafiki walisherehekea “ushindi” huo kwa kucheza hadharani, huku Mongella akipiga filimbi kuwa ni yeye aliyependekeza jina la Mwinyi na Abdul Wakil kwa Urais Visiwani kwenye Kamati Kuu na hivyo “kuokoa jahazi”. Tunapotazama nyuma kuona kipindi cha miaka 10 [1985 – 1995] cha uongozi wa Rais Mwinyi kwa Jamhuri ya Muungano, na kipindi cha Rais Idris Abdul Wakil Nombe Visiwani; tuna kipi cha kujivunia kwa Muungano na kwa Zanzibar kwa “jahazi kuokolewa”?. Mambo yangefananaje kama matokeo yangekuwa ni kinyume chake?.

Chanzo: Raia Mwema

No comments: