Tuesday, 28 April 2015

CCM wanataka kumbakiza JK hadi 2019

GODBLESS Lema-Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), amewasihi wananchi kuipigia kura ya ‘hapana’ Katiba inayopendekezwa, akidai kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kinataka kutumia udhaifu wa katiba hiyo kumbakiza Rais Jakaya Kikwete, madarakani hadi 2019.

Akihutumia mamia ya wafuasi wa Chadema mjini Shinyanga katika viwanja ya Mahakama ya Mwanzo, Lema ambaye pia ni Waziri Kivuli kwa Wizara ya Mambo ya Ndani, amewataka wananchi kujiandikisha kwa wingi katika daftari jipya la kudumu la wapiga kura ili kuikataa katiba hiyo mpya isipite.
Huku akishangiliwa na wananchi, mbunge huyo alinukuu kifungu cha katiba hiyo inayopendekezwa, akisema kuwa endapo itapita, Rais Kikwete na timu yake yote wataendelea kubaki madarakani mpaka pale kipindi cha mpito cha miaka minne kitakapokamilika. Lema aamesema “uhalali wa viongozi wa Jamhuri ya Muungano waliopo madarakani hivi sasa umeelezwa wazi ndani ya katiba inayopendekezwa kwenye ibara za 285, 286 na 288. Wananchi isomeni katiba mvielewe vifungu hivyo.”
Amesema hivi sasa viongozi wa CCM wanahangaika na kuwashinikiza watanzania kuipigia kura ya “ndiyo” katiba ili ipite na waweze kuendelea na nyadhifa zao. Kwamba, “dawa pekee ya kunusuru hali hiyo ni kupiga kwa wingi kura za “hapana.” Lema alinukuu ibara ya 285 ya katiba inayopendekezwa katika sehemu ya tatu ambayo inayozungumzia utumishi wa umma kuhusu kuendelea kuwepo kwa Rais kwamba ataendelea kushika madaraka hayo hadi kipindi cha mpito kimalizike. Ameongeza kuwa, ibara ya 288 katika kifungu kidogo cha (1) inaendelea kuwataja viongozi wengine watakaoendelea na nyadhifa zao mpaka pale katiba inayopendekezwa itakapoanza kutumika rasmi. 
“Viongozi haoni Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, mawaziri, naibu mawaziri, wabunge, majaji na watumishi wote wa umma katika serikali ya Jamhuri ya Muungano wataokuwa madarakani kabla ya kutumika kwa katiba hiyo, nyadhifa zao zitaendelea kutambulika,”amesema. Amefafanua kuwa CCM imeweka mtego ambao watanzania wengi hawajaubaini ili washawishike kuipigia kura ya “ndiyo” katiba hiyo na ikipita ndipo waelimishwe kwamba viongozi wote walioko madarakani watawajibika kuendelea na nyadhifa zao hadi pale kipindi cha mpito kitakapokamilika. “Ndugu zangu kwa kadri hali ilivyo, katiba hii ikipita na kurudishwa bungeni kwa hatua za mwisho ili ianze kutumika ikiwemo kutungiwa sheria mbalimbali ni wazi asilimia 90 ya wabunge wetu wa CCM, wataipitisha kwa kishindo ili wao wajipe fursa ya kuendelea kula nchi, kitu ambacho sisi tunakipinga,” amedai.

No comments: