Sitta amesoma shahada yake kwa miaka 7 kwa sababu mwaka 1966, wakati yuko mwaka wa pili na akiwa kiongozi wa wanafunzi UDSM, wanafunzi waligoma na kuandamana kupinga kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na kukatwa mishahara yao baada ya JKT. Hoja ya wanafunzi ilikuwa na mantiki kubwa, kwamba mbona vigogo wa serikali na wanasiasa wanalipwa mishahara minono na marupurupu makubwa?
Baada ya shinikizo hilo la wanafunzi Mwalimu Julius Nyerere alikubali kupunguza mshahara wake wa Sh4,000 bila kodi akaagiza pia mishahara ya mawaziri ipunguzwe kwa asilimia mbili. Miezi miwili baadaye akatangaza Azimio la Arusha (Februari 5, 1967) kuyapa uzito malalamiko ya wanafunzi hao.
Watukutu wawili – Sitta na Wilfred Mwabulambo (sasa marehemu) na wengine kadhaa – waliojitia wazimu na kutetea kile walichokiita haki zao, (haki za wakulima na wafanyakazi), walimshutumu Mwalimu Nyerere kwa maneno makali wakidai “…ni heri wakati wa ukoloni kuliko utawala wa Mwalimu”.
Mwalimu Nyerere alikasirika na kuwafukuza chuo wanafunzi wote 400 kwa kile alichokiita “kwenda kufunzwa adabu majumbani mwao”. Miezi kumi baadaye, baada ya Nyerere kushawishiwa na hasira kutulia akaamua kuwarudisha chuoni wanafunzi 392. Viongozi wa mgomo; Sitta na wenzake 7 walitiliwa ngumu, hawakurejeshwa chuoni.
Busara za viongozi wa chuo zilifanya Mwalimu aliliwe zaidi na kuandikiwa barua mbili maalumu na chuo zenye Kumb. Na. C3/Sa.13 ya 2/3/1967 na C3/Ss.13 ya 9/07/1967. Mwalimu alikubali kilio hicho na kuwaruhusu vijana hao wanane warudi kwa sharti kwamba wale watukutu wawili (Sitta na Mwabulambo) watandikwe viboko na “Mwalimu Nyerere” mwenyewe. Hii ndiyo ilikuwa pona ya Sitta ambaye alirejea UDSM na kuendelea na masomo kwa miaka kadhaa hadi alipohitimu mwaka 1971.
Wakati Sitta anarudi chuoni tayari alikuwa mwajiriwa wa Kampuni ya Mafuta ya “CALTEX OIL” kama Meneja wa Tawi (1967 – 1969) na mwaka 1969 – 1975 aliajiriwa na Shirika la Maendeleo la Taifa kama Katibu na Mkurugenzi wa Utawala. Baadaye mwaka 1976 Sitta aliamua kujiendeleza kielimu katika masuala ya Usimamizi nchini Uswisi kwenye Chuo Kikuu cha IMEDE ambako alihitimu Stashahada ya Juu ya Usimamizi mwaka huohuo 1976. Chini ya mfumo wa chama kimoja, Sitta amekuwa kiongozi wa juu wa CCM na serikali akiwa mbunge, mkuu wa mkoa na waziri katika nyakati tofauti na ameendelea kuwa mbunge na waziri katika mfumo wa vyama vingi.
Sitta amemuoa Margareth Simwanza Sitta na wana familia imara.
MBIO ZA UBUNGE
Enzi za chama kimoja 1975 - 1995 Sitta amekuwa mbunge wa Jimbo la Urambo (kabla halijagawanywa na kuwa Urambo Magharibi na Mashariki) na pia alifanikiwa kuwa waziri kwa nyakati tofauti. Kwa mfano wakati wa kipindi cha mwisho cha Mzee Mwinyi, Sitta alikuwa Waziri za Katiba na Sheria.
Enzi za chama kimoja 1975 - 1995 Sitta amekuwa mbunge wa Jimbo la Urambo (kabla halijagawanywa na kuwa Urambo Magharibi na Mashariki) na pia alifanikiwa kuwa waziri kwa nyakati tofauti. Kwa mfano wakati wa kipindi cha mwisho cha Mzee Mwinyi, Sitta alikuwa Waziri za Katiba na Sheria.
Mwaka 1995 Sitta aliingia kwenye mapambano mapya ya siasa za vyama vingi na kwa bahati mbaya akawa mmoja wa vigogo walioangushwa na wabunge wa NCCR. Mshindani wake mkuu alikuwa Msina Jacob Abraham. Msina alishinda kwa kura 10,788 dhidi ya 9,497 za Sitta.
Sitta alirudi tena kwenye jukwaa la siasa mwaka 2005 kwenye uchaguzi mkuu na aliwashinda wapinzani wake wakuu Lumatiliza Yotamu Lubungila wa NCCR na Wilson George Ntakamulenga wa CUF. Sitta alipata kura 28,660 (72.3%) na kurejesha heshima yake jimboni Urambo Mashariki. Kurudi kwa nguvu kulimpa nafasi ya kuwania na kuteuliwa na CCM kugombea uspika wa Bunge la Tanzania na akaliongoza Bunge la Tisa kwa mafanikio na changamoto nyingi.
Mwaka 2010 Sitta alishiriki tena uchaguzi Urambo Mashariki akawashinda wapinzani wake wakuu Msafiri Abdulrahmani Mtemelwa (Chadema) na Zombwe Lotto Edward (CUF) kwa kupata kura 19,947 (70.47%). Baada ya ushindi huo, Sitta alijaribu tena kuwania uspika bila mafanikio; utendaji wake wa kuiuma serikali na wakati mwingine kuipuliza kwenye Bunge la Tisa ulimfanya achukiwe na serikali.
Ilipoonekana ana nguvu akatengenezewa “chui wa karatasi” (mshindani), Andrew Chenge. Chenge naye akachukua fomu ya uspika ghafla, likatengenezwa ‘zengwe’ kuwa wagombea wote wana nguvu, hapo CCM ikapata mwanya wa kutamka kuwa haiwataki wote ili kuondoa mvutano. Sitta akapoteza ndoto za uspika na ukahamia kwa mwanamama Anne Makinda.
Rais Jakaya Kikwete alipotangaza Baraza la Mawaziri mwaka 2010 alimpa Sitta Wizara ya Afrika Mashariki kama Waziri, wadhifa aliodumu nao hadi mwaka huu mwanzoni alipobadilishwa na kupelekwa Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi.
MBIO ZA URAIS
Samuel John Sitta alianza mbio za urais “kimyakimya” tangu alipokuwa Spika wa Bunge la Tisa (2005 – 2010). Kuna nyakati alikuwa akitoa kauli zinazoashiria kuwa nchi inayumba na haina uongozi thabiti huku akionyesha kuwa nchi ina viongozi thabiti na hawajapewa uongozi mkuu wa nchi, akiwemo yeye.
Samuel John Sitta alianza mbio za urais “kimyakimya” tangu alipokuwa Spika wa Bunge la Tisa (2005 – 2010). Kuna nyakati alikuwa akitoa kauli zinazoashiria kuwa nchi inayumba na haina uongozi thabiti huku akionyesha kuwa nchi ina viongozi thabiti na hawajapewa uongozi mkuu wa nchi, akiwemo yeye.
Hata alipoliongoza Bunge la Katiba mwaka 2014, mara nyingi Sitta alionekana kama mtu mwenye shauku kubwa na urais na alipohojiwa, mara kwa mara, juu ya urais alionyesha ana ndoto hizo. Mara kadhaa, alilalamika kuwa wala rushwa wakubwa wanampiga vita kwa sababu ni msafi.
NGUVU YAKE
Sitta ni kiongozi mwajibikaji kwa namna moja. Majukumu mengi ambayo amekuwa akipewa anayasimamia hadi mwisho bila kujali athari zake. Alipokuwa Spika wa Bunge la Tisa alisimamia mabadiliko makubwa katika mfumo wa uendeshaji wa Bunge na kupunguza mtindo wa Serikali kulidhibiti, jambo ambalo lilimpa sifa kubwa.
Sitta ni kiongozi mwajibikaji kwa namna moja. Majukumu mengi ambayo amekuwa akipewa anayasimamia hadi mwisho bila kujali athari zake. Alipokuwa Spika wa Bunge la Tisa alisimamia mabadiliko makubwa katika mfumo wa uendeshaji wa Bunge na kupunguza mtindo wa Serikali kulidhibiti, jambo ambalo lilimpa sifa kubwa.
Na hata anapokabidhiwa mamlaka ya uwaziri amekuwa mtu anayethubutu bila kuogopa na uthubutu hakuuanza majuzi; aliuanza enzi zile za Mwalimu Nyerere miaka ya 1965 alipokuwa Rais wa Umoja wa Wanafunzi Tanzania na anakumbukwa kwa kauli yake ya “…ilikuwa afadhali wakati wa ukoloni”, akimshambulia Mwalimu Nyerere.
Sitta ni kiongozi mzoefu na ni mmoja wa watu waliopata kufanya kazi na marais wote wanne waliopata kuongoza Tanzania. Chini ya Nyerere na Mwinyi amekuwa Waziri wa Maendeleo, Waziri wa Kazi na Waziri wa Katiba na Sheria. Wakati wa Mkapa aliteuliwa kuongoza Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na wakati wa Kikwete ameshikilia Nyadhifa nyingi zaidi. Huu ni uzoefu wa kujivunia kwa mtu anayetaka kuongoza nchi.
UDHAIFU WAKE
Moja ya udhaifu mkubwa wa Sitta ni kutokuwa na uvumilivu. Wakati wa sakata la BUZWAGI kwenye Bunge la Tisa, aliwahi kuweka msimamo kuwa mtu yeyote ambaye ataendelea kupinga maamuzi ya Bunge ya kumsimamisha ubunge, Zitto Kabwe kwa miezi sita, kwenye magazeti na harakati nyingine, atafunguliwa mashtaka au kuchukuliwa hatua kali za kibunge. Huku ni kukosa uvumilivu kwa hali ya juu.
Moja ya udhaifu mkubwa wa Sitta ni kutokuwa na uvumilivu. Wakati wa sakata la BUZWAGI kwenye Bunge la Tisa, aliwahi kuweka msimamo kuwa mtu yeyote ambaye ataendelea kupinga maamuzi ya Bunge ya kumsimamisha ubunge, Zitto Kabwe kwa miezi sita, kwenye magazeti na harakati nyingine, atafunguliwa mashtaka au kuchukuliwa hatua kali za kibunge. Huku ni kukosa uvumilivu kwa hali ya juu.
Mwaka jana wakati anaongoza Bunge Maalumu la Katiba (BMK) aliwahi kuiomba Serikali ivichukulie hatua kali vyombo vya habari ambavyo vinaruhusu makongamano yanayopinga kuendelea kwa BMK akimshangaa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, kwa nini hajavifungia baadhi ya vyombo hivyo. Kauli hiyo ilionyesha ni namna gani kiongozi huyu anachokitaka yeye lazima kiwe hata kama kinavunja misingi ya demokrasia.
Sitta ana sura mbili, namaanisha kwamba ni “Mtata” sana. Wakati wa sakata la EPA alikataa lisiwasilishwe na kujadiliwa bungeni. Alikwenda mbali zaidi na kumtishia mbunge wa Karatu Dk Willibroad Slaa kwamba atamchukulia hatua za kimahakama kwa kutaka kujaribu kuwasilisha bungeni kile alichokiita “Nyaraka za Kughushi” achilia mbali ufisadi wa Buzwagi ambao ulisababisha Zitto asimamishwe ubunge.
Lilipokuja sakata la ufisadi wa Richmond, Sitta alifanya kila awezalo jambo lishughulikiwe ipasavyo. Kwanza, ilikuwa asafiri kwenda nje, akaagiza ripoti ya Richmond isiwasilishwe hadi arejee. Baadaye aliamua kubaki yeye mwenyewe na akasimama kidete hadi Edward Lowassa akaanguka. Lakini Sitta huyu ndiye alipinga kabisa kashfa za EPA na Buzwagi kushughulikiwa na Bunge na ndiye aliyeruhusu kashfa ya RICHMOND ishughulikiwe na chombo kile kile. “Double Standard!”
Hivi karibuni video moja ya mahojiano iliyowekwa mitandaoni na Shirika la Utangazaji la Sauti ya Amerika (VoA) imemwonesha Sitta akitamka kwa kujiamini kuwa mfumo wa Serikali tatu ukirudi Watanzania walioko nchini Oman watarejea Zanzibar kwa wingi na kuipindua Serikali. Sitta anatoa kauli hii nzito bila tahadhari kuwa inawaumiza watu ambao hawana lengo baya analowatupia. Misimamo ya namna hii “ya kuhisi” ina utata mkubwa kwa kiongozi mtarajiwa wa nchi na ni udhaifu uliopitiliza.
Udhaifu mwingine wa Sitta ulijidhihirisha wakati wa BMK. Pamoja na kukosekana maridhiano baina ya pande zilizokuwa zinasigana, bado aliapa kuendelea na kazi hiyo. Hata Rais Kikwete na viongozi wa Kituo cha Demokrasia (TCD) walipokutana Dodoma na kuamua mchakato wa katiba uendelee baada ya kura ya maoni, Sitta na wenzake waliendelea na msimamo wa kukamilisha safari ya Bunge hilo.
Katiba iliyozalishwa na Sitta na wenzake imeligawa taifa, mashirika mbalimbali yanaipinga, vyama vya siasa vikubwa vinaipinga na hata dini kuu katika nchi zinaipinga. Huu ni udhaifu mkubwa kwake pia, kama mtu aliyeongoza mchakato huo.
Pia, Sita ni mhubiri wa mambo asiyoyatenda. Wakati anajitanabaisha kama mtetezi wa kweli wa wanyonge alipokuwa Spika wa Bunge la Tisa, mwaka 2006 aliingia kwa ahadi ya kufanya kazi kwa kasi na viwango. Hata hivyo kuna jambo moja baya lilifanyika; alihusika kuboresha malipo ya wabunge na kuwa “kufuru” kiasi kwamba sasa ubunge ni kazi yenye neema kuu huku wafanyakazi wa serikali wakiendelea kulipwa pesa kiduchu hadi leo.
NINI KINAWEZA KUMFANYA APITISHWE
Moja ya mambo yanayoweza kumbeba Sitta katika kupenya mchujo wa CCM ni kukijua chama chake vizuri. Sitta ni mmoja wa vijana wa zamani waliokulia ndani ya TANU na baadaye CCM na amepata uzoefu wa kutosha katika awamu zote nne za uongozi wa nchi jambo linalomfanya awe kwenye nafasi ya kujua changamoto za taifa na labda namna ya kuzitatua.
Moja ya mambo yanayoweza kumbeba Sitta katika kupenya mchujo wa CCM ni kukijua chama chake vizuri. Sitta ni mmoja wa vijana wa zamani waliokulia ndani ya TANU na baadaye CCM na amepata uzoefu wa kutosha katika awamu zote nne za uongozi wa nchi jambo linalomfanya awe kwenye nafasi ya kujua changamoto za taifa na labda namna ya kuzitatua.
Pia, kwa kiasi kikubwa utendaji wake haujaambatana na kelele za kashfa kwenye maeneo mengi alikopita. Kuliwahi kuwa na wasiwasi juu ya mwenendo wake wakati alipoongoza TIC (Uteuzi wa Mkapa), lakini kelele zile hazikuthibitishwa ipasavyo; zilifunikwa. Kama CCM inahitaji wagombea wasio na kashfa za fedha za umma Sitta anaweza kuwa mmoja wao.
Kundi la Sitta ndani ya CCM katika kusaka urais halina nguvu kubwa, si kati ya makundi yanayosigana kweli kweli. Hali hiyo inamfanya abakie kama chaguo rahisi la kuikoa CCM ikiwa chama hicho kitazikimbia kambi kubwa za urais zilizo ndani ya yake lakini kikahitaji mtu mwenye uzoefu mkubwa. Jambo hili likitokea litaweza kumbeba Sitta.
NINI KINAWEZA KUMWANGUSHA
Moja ya mambo yanayoweza kumwangusha Sitta ni kutoaminika kwake. Sitta ni mwana CCM kindakindaki, lakini kilipoanzishwa Chama cha Jamii (CCJ) ambacho kilijizolea umaarufu mkubwa huku ikisemekana kitabeba makada nguli wa CCM, Sitta alitajwa kwenye orodha ya makada waliotuhumiwa.
Moja ya mambo yanayoweza kumwangusha Sitta ni kutoaminika kwake. Sitta ni mwana CCM kindakindaki, lakini kilipoanzishwa Chama cha Jamii (CCJ) ambacho kilijizolea umaarufu mkubwa huku ikisemekana kitabeba makada nguli wa CCM, Sitta alitajwa kwenye orodha ya makada waliotuhumiwa.
Pamoja na kukana kuhusishwa huko, aliyekuwa Mbunge wa Kishapu, Fred Mpendazoe katika kitabu chake “Tutashinda” alimtaja Sitta kuwa mwanzilishi wa CCJ. Aliwataja wengine kuwa ni Victor Mwambalaswa, Dk Harrison Mwakyembe, Nape Nnauye, Daniel Porokwa, yeye Mpendazoe na baadaye Paul Makonda.
Pia, alituhumiwa kuwa alitaka kujiunga Chadema ili agombee urais kupitia chama hicho na mipango yote ilikuwa imekamilika, lakini Sitta aliachana na mpango huu dakika za mwisho.
Kitu kingine kinachoweza kumwangusha ni kutokuwa na uhusiano mzuri na baadhi ya viongozi muhimu ndani ya CCM. Ndiyo maana alipoonekana kama mtu anayetishia mipango ya CCM alipokuwa Spika wa Bunge, iliwapasa wenzake wamdhibiti haraka ili asifikie ndoto hizo kwenye Bunge la Kumi. Kitendo cha kutengenezewa “chui wa karatasi” mwaka 2010 na hata (mwaka 2014 kwenye BMK) kinaonyesha kuwa kila mara anapotaka nafasi ya juu, wenzake wanamwekea vikwazo kwa sababu za kimahusiano.
ASIPOPITISHWA (MPANGO B)
Sitta amesikika mara kadhaa akitamka hadharani kuwa hatarudi kugombea ubunge Urambo na kwamba miaka 35 ya kazi hiyo inatosha kuwaachia wengine ili yeye atafute namna nyingine bora zaidi ya kuwatumikia wananchi.
Sitta amesikika mara kadhaa akitamka hadharani kuwa hatarudi kugombea ubunge Urambo na kwamba miaka 35 ya kazi hiyo inatosha kuwaachia wengine ili yeye atafute namna nyingine bora zaidi ya kuwatumikia wananchi.
Kwa sababu ni kiongozi mzoefu sana hapa nchini, mchango wake kwa taifa bado unahitajika katika masuala ya ushauri na uongozi wa ujumla katika maeneo magumu. Akiukosa urais kwa tiketi ya CCM anaweza kusaidia katika masuala mengine ikiwemo kwenye ujenzi wa chama chake ili kijiendeshe kwa misingi ya uwazi na uwajibikaji kwani hivi sasa hakiko kwenye misingi ya uanzishwaji wake.
HITIMISHO
Hakika, Sitta ana sifa mchanganyiko sana, ni kiongozi thabiti, anayethubutu, mchapakazi, mwadilifu, mtata na mwenye malengo makubwa ya kisiasa. Huenda bado chama chake hakijaelewa hasa dhamira yake itakuwaje akishika madaraka ya nchi.
Hakika, Sitta ana sifa mchanganyiko sana, ni kiongozi thabiti, anayethubutu, mchapakazi, mwadilifu, mtata na mwenye malengo makubwa ya kisiasa. Huenda bado chama chake hakijaelewa hasa dhamira yake itakuwaje akishika madaraka ya nchi.
Kwenye BMK alionyesha upungufu mwingi ambao ulishusha taswira yake kwa wananchi. Wakati yeye anachukulia uongozi wake kwenye BMK kama kiashiria cha ukomavu na uongozi wake thabiti, jamii inamtazama kinyume chake lakini kwa kumtendea haki ikimkumbuka kama kiongozi thabiti, kwa juhudi alizozifanya kwenye Bunge la Tisa, japokuwa juhudi zile zikifutwa na yaliyotokea kwenye mchakato wa katiba na BMK.
Wanasiasa wanaothubutu kama Sitta hawatabiriki, hubadilika kulingana na mazingira ilimradi mfumo uliopo uwabebe kwa wakati husika. Tunamtakia Samuel John Sitta kila la heri katika safari yake na ndoto kubwa alizonazo.
Julius Mtatiro ni Mchambuzi wa Masuala ya Kisiasa na Kijamii, ana uzoefu mkubwa wa uongozi wa kisiasa hapa Tanzania. Ana Cheti cha Juu cha Sarufi na Lugha, Shahada ya Sanaa “B.A” katika Elimu (Lugha, Siasa na Utawala), Shahada ya Uzamili ya Utawala na Uongozi (M.A) na ni mwanafunzi wa fani ya sheria (L LB) – Anapatikana kupitia +255787536759,(juliusmtatiro@yahoo.com) Uchambuzi na huu unatokana na utafiti na maoni binafsi ya mwandishi). (Uchambuzi huu umechapishwa na Gazeti la Mwanchi la Jumapili, 26 Aprili 2015).
No comments:
Post a Comment