Saturday 23 May 2015

LISSU AWA MTETEZI WA WA MUUNGANO WA KUHESHIMIANA BUNGENI.

Ismail Jussa's photo.
MAONI YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO),
MHESHIMIWA TUNDU A.M. LISSU (MB.)
KUHUSU MPANGO NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA YA OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO) KWA MWAKA 2015/2016
(Kanuni ya 99(9) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, 2013)
UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika,
Huu ni mwaka wa mwisho wa maisha ya Bunge la Kumi ambalo umeliongoza tangu tulipokuchagua mwezi Novemba 2010. Hii ni kwa sababu kwa mujibu wa ibara ya 65 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977, “... maisha ya kila Bunge yatakuwa ni muda wa miaka mitano ... unaoanzia tarehe ambapo Bunge jipya limeitishwa kukutana kwa mara ya kwanza baada ya Uchaguzi Mkuu na kuisha tarehe ya kuvunjwa kwa Bunge kwa ajili ya kuwezesha Uchaguzi Mkuu mwingine wa kawaida kufanyika.”
Kipindi cha miaka mitano katika maisha ya chombo muhimu katika nchi kama Bunge ni muda muafaka kufanya tathmini ya kazi ambazo tumezifanya kama Wabunge na majukumu ambayo tumeyatekeleza. Si busara kujisemea ama kujisifu kwa kazi ambazo nimezifanya ndani ya Bunge lako tukufu na majukumu ambayo nimeyatekeleza kama Mbunge, Mnadhimu Mkuu na Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu kuhusu masuala ya Muungano na masuala ya Katiba na Sheria. Hilo ninawaachia wapiga kura na wananchi wangu wa Jimbo la Singida Mashariki – ambao leo wamewakilishwa vyema na viongozi mbali mbali wa chama chao cha ukombozi wa Kata zote za Jimbo letu – na wengine nje ya Jimbo ambao wanafaa zaidi kutoa hukumu juu ya utendaji wangu wa kazi za kibunge.
Kwa leo naomba tu niwashukuru kwa moyo wangu wote kwa kunipa heshima kubwa ya kuwatumikia wao na Watanzania wengine katika Bunge lako tukufu. Ni matumaini yangu kwamba imani yao kubwa kwangu katika miaka hii mitano ya maisha ya Bunge hili la Kumi haikuwa ya bure. Najua hawajasahau, lakini si vibaya kuwakumbusha makamanda wangu, kwamba huu ni mwaka wa kukamilisha ile kazi tuliyoianza Januari 2008, tukaifanya vizuri Oktoba, 2010 na kufaulu kwa kiwango cha kihistoria kilichoishangaza Tanzania mwezi Desemba ya mwaka jana.
MGAWANYO WA MAPATO YA MUUNGANO
Mheshimiwa Spika,
Katika Maoni yetu ya mwaka jana tuliliambia Bunge lako tukufu – kwa mchanganuo wa mgawanyo wa mapato mbali mbali ya Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar - kwamba “... Muungano huu ni kielelezo cha unyonyaji na ukandamizaji mkubwa ambao nchi ndogo ya Zanzibar imefanyiwa na nchi kubwa ya Tanganyika. Ni mfano wa jinsi ambavyo nchi moja kubwa ya Kiafrika i[me]weza kuigeuza nchi nyingine ndogo ya Kiafrika kuwa koloni lake.”
Tulionyesha kwenye Maoni yetu jinsi ambavyo kwa miaka mingi Zanzibar imepunjwa katika mgawanyo wa misaada na mikopo ya kibajeti inayopatikana kwa jina la Jamhuri ya Muungano. Ndio maana mwaka 2013 Kamati ya Kudumu ya Bunge lako tukufu ya Katiba, Sheria na Utawala iliishauri Serikali hii ya CCM kuangalia upya “utaratibu wa mgawanyo wa mapato yanayotokana na fedha zinazotoka kwa wafadhili....” Aidha, Kamati ilishauri kwamba “Serikali itolee uamuzi mapendekezo ya Tume ya Pamoja ya Fedha yaliyowasilishwa Serikalini tangu mwaka 2006 na kuwasilishwa tena mwaka 2010 kuhusu utaratibu wa mgao wa fedha za Serikali zote mbili.”
Serikali hii ya CCM ilijibu ushauri wa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala kwa kuahidi kwamba “Serikali zetu mbili bado zinaendelea kushughulikia mapendekezo yaliyotolewa na Tume ya Pamoja ya Fedha.” Ndio kusema kwamba karibu miaka kumi baada ya Tume ya Pamoja ya Fedha kupendekeza utaratibu mpya wa mgawanyo wa mapato ya Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar, bado Serikali hii sikivu inaendelea na ‘mchakato’ wa kushughulikia mapendekezo hayo!

MIKOPO YA MASHARTI NAFUU NA MISAADA YA KIBAJETI
Mheshimiwa Spika,
Katika kujibu ushauri wa Kamati, Serikali hii ya CCM ililiambia Bunge lako tukufu vile vile kwamba, kwa utaratibu ulivyo sasa, mgawo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa misaada na mikopo ya kibajeti inayotolewa na nchi wafadhili na mashirika ya kimataifa ni asilimia 4.5. Hata hivyo, tulionyesha – kwa kutumia takwimu zilizoletwa Bungeni na Waziri wa Fedha - kwamba hata kwa makadirio ya mwaka wa fedha 2013/2014, Zanzibar ilikuwa imetengewa asilimia 2.8 tu ya misaada na mikopo ya kibajeti iliyotoka kwa wafadhili wa nje. Kiasi hicho kilipungua hadi kufikia takriban asilimia 2.2 katika makadirio ya mwaka wa fedha 2014/2015.
Mheshimiwa Spika,
Kwa mujibu wa Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango na Bajeti Mwaka wa Fedha 2014/15 na Makadirio ya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2015/16 iliyowasilishwa mbele ya Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala ya Bunge lako tukufu na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais mwezi uliopita, kati ya shilingi bilioni 44.039 zilizoidhinishwa na Bunge mwaka jana kwa ajili ya kupelekwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kama mgawo wa Zanzibar wa misaada ya kibajeti na mikopo, ni shilingi bilioni 27.681 ndizo zilizopelekwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar hadi kufikia tarehe 31 Machi, 2015.
Kiasi hiki hakitofautiani sana na shilingi bilioni 27.190 za misaada ya kibajeti na mikopo zilizopelekwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika mwaka wa fedha 2014/15. Hata hivyo, uchunguzi wa kina wa Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango na Bajeti unaonyesha kwamba takwimu hizi za Serikali hii ya CCM zinapotosha ukweli wa hali halisi kwa kiasi kikubwa. Kwamba takwimu sahihi zinaonyesha kiasi kilichotolewa kama mgawo wa Zanzibar wa mikopo nafuu na misaada ya kibajeti ni kidogo kwa karibu mara tatu kiasi cha shilingi bilioni 27.681 kilichotajwa kwenye Taarifa.
Kwa mujibu wa aya ya 3.3.2(b) ya Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango na Bajeti:
“Ofisi (ya Makamu wa Rais – Muungano) imeratibu gawio la fedha la asilimia 4.5 kwenda Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ajili ya kusaidia kuendesha shughuli za kiuchumi na kijamii. Gawio hilo hujumuisha Misaada ya Kibajeti (GBS), fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo, faida ya Benki Kuu na Kodi ya Mishahara (PAYE). Hadi kufikia tarehe 31 Machi, 2015, [Serikali ya Mapinduzi Zanzibar] ilipokea shilingi 27,681,808,403/= kati ya shilingi 44,039,608,000/= zilizoidhinishwa na Bunge. Kati ya fedha hizo, shilingi 7,137,882,543/= ni Gawio la Kibajeti kwa [Serikali ya Mapinduzi Zanzibar] na shilingi 15,750,000,000/= ni fedha za Kodi ya Mishahara, shilingi 1,243,925,860/= ni fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo na shilingi 3,200,000,000/= ni gawio la faida ya Benki Kuu ya Tanzania. Aidha, [Serikali ya Mapinduzi Zanzibar] imepokea shilingi 350,000,000/= ikiwa ni deni la fedha zilizotumiwa na [Serikali ya Mapinduzi Zanzibar] wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya sherehe za miaka 50 ya Muungano.”
Kumbe, Mheshimiwa Spika, kile ambacho Serikali hii ya CCM hukieleza kila mwaka kuwa ni mgawo wa Zanzibar wa fedha misaada ya kibajeti na mikopo yenye masharti nafuu kinajumuisha pia fedha za ndani zinazojumuisha makato ya mishahara ya wafanyakazi, fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo na hata mchango wa sherehe za kitaifa kama Muungano! Kama mgawo halisi wa Zanzibar kutokana na misaada ya kibajeti na mikopo nafuu ni shilingi bilioni 7.137 kama inavyoonyeshwa kwenye Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango na Bajeti, maana yake ni kwamba kiasi kilichotolewa kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika mwaka huu wa fedha ni pungufu kwa takriban asilimia 74 ukilinganisha na fedha iliyotolewa mwaka jana, assuming takwimu za mwaka jana hazikuchakachuliwa kama za mwaka huu.
Mheshimiwa Spika,
Whether tunatumia takwimu zilizochakachuliwa zinazoonyesha Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imepata shilingi bilioni 27.681 kama mgawo wake wa misaada ya kibajeti na mikopo yenye masharti nafuu katika mwaka huu wa fedha, au takwimu zinazoonyesha kiasi halisi kuwa ni shilingi bilioni 7.137, nyaraka nyingine zilizowasilishwa Bungeni na Serikali hii ya CCM zinaashiria kwamba Zanzibar imeendelea kupunjwa mapato yake halali kwa sababu ya Muungano huu.
Katika Maelezo ya Waziri wa Fedha Mheshimiwa Saada Mkuya Salum (MB) Akiwasilisha Mapendekezo ya Mfumo wa Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka 2015/16 kwa Waheshimiwa Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dar es Salaam, mnamo tarehe 29 Aprili, 2015, Bunge lako tukufu liliambiwa kwamba “[h]adi kufikia Machi, 2015 kiasi cha shilingi bilioni 1,583 kilipokelewa ...” kama misaada ya kibajeti na mikopo nafuu kutoka kwa washirika wa maendeleo.
Kwa kutumia takwimu zilizochakachuliwa za shilingi bilioni 27.681, hii ina maana kwamba mgawo wa Zanzibar kutokana na fedha zilizotoka nchi za nje na taasisi za maendeleo za kimataifa ni takriban asilimia 1.7 tu, wakati Tanganyika imechukua shilingi bilioni 1,555.319, au asilimia 98.3 ya fedha zote zilizokuja mwaka huu wa fedha kwa jina la Tanzania. Kwa upande mwingine, kwa kutumia takwimu zinazoonyesha kiasi hali kuwa shilingi bilioni 7.137, mgawo wa Zanzibar wa misaada ya kibajeti na mikopo yenye masharti nafuu kwa mwaka huu ni asilimia 0.45 tu! Kiasi kilichobaki, yaani shilingi bilioni 1,575.863 au asilimia 99.55 ya fedha zote za misaada ya kibajeti na mikopo ya masharti nafuu imebaki Tanganyika!
Mheshimiwa Spika,
Kama Zanzibar ingepata mgawo wa asilimia 4.5 ambao tumekuwa tunauambiwa na Serikali hii ya CCM, basi Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ingepaswa kupokea jumla ya shilingi bilioni 71.235 kama fedha za misaada ya kibajeti na mikopo yenye masharti nafuu. Kwa sababu ya muundo wa Muungano kama ulivyo sasa, Zanzibar imepokea shilingi bilioni 7.137 kati ya shilingi bilioni 71.235 ya fedha zake halali katika mwaka huu wa fedha. Hii ni asilimia 10 tu ya fedha ambazo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ilipaswa kupokea kama misaada ya kibajeti na mikopo yenye masharti nafuu. Shilingi bilioni 64.098 au asilimia 90 ya fedha zilizobaki imechukuliwa na Serikali ya Tanganyika ambayo, kwa maneno ya Speaker Emeritus Msekwa, ndiyo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Spika,
Mapendekezo ya Serikali hii ya CCM kuhusu mgawo wa Zanzibar kwa misaada ya kibajeti na mikopo yenye masharti nafuu kwa mwaka unaokuja wa fedha 2015/16 hayana nafuu yoyote kwa Zanzibar. Kwa mujibu wa Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango na Bajeti, katika mwaka wa fedha 2015/16 “... mgao wa misaada na mikopo ya kibajeti kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ...” unakadiriwa kuwa shilingi bilioni 22.400. Katika kipindi hicho, kwa mujibu wa Maelezo ya Waziri wa Fedha, misaada ya kibajeti na mikopo ya masharti nafuu inayokadiriwa kuja kwa jina la Jamhuri ya Muungano itakuwa shilingi bilioni 1,888.178. Kwa maana hiyo, mgawo unaopendekezwa kwa Zanzibar ni takriban asilimia 1.9.
Kama Zanzibar ingepata mgawo wa asilimia 4.5 kama ambavyo imezungumzwa kwa miaka mingi na Serikali hii ya CCM, basi makadirio ya mgawo wake yangekuwa shilingi bilioni 84.968. Kwa hiyo, kwa mapendekezo haya, Zanzibar itapoteza kwa Tanganyika shilingi bilioni 62.568, au asilimia 73.6 ya fedha zake halali. Katika mazingira haya, na kwa takwimu hizi, ni watu wenye maslahi katika unyonyaji huu pekee ndio wanaoweza kubishia ukweli wa kauli ya Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamad, kwamba: “Mfumo (wa Muungano) uliopo sasa hauinufaishi Zanzibar na hivyo haukubaliki kwa Wazanzibari. Koti la Muungano kama lilivyo sasa linabana sana. Wakati umefika tushone koti jipya kwa mujibu wa mahitaji ya zama hizi.”
MISAADA ISIYOKUWA YA KIBAJETI NA MIKOPO YA KIBIASHARA
Mheshimiwa Spika,
Katika Maoni yetu ya mwaka jana tulionyesha kwamba “... hali ni mbaya zaidi kuhusiana na fedha za misaada na mikopo isiyokuwa ya kibajeti.” Katika eneo hili tulionyesha kwamba Zanzibar imekuwa haipati mgawo wowote wa fedha za nje kwa ajili ya miradi ya maendeleo zikijumuisha misaada na mikopo ya Basket Fund na misaada na mikopo ya miradi. Katika mwaka wa fedha 2013/14, fedha hizo zilikuwa takriban shilingi bilioni 2,692 na zote zilitumika kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya Tanganyika.
Maelezo ya Waziri wa Fedha yanaonyesha kwamba kwa mwaka wa fedha 2014/15, ‘mikopo na misaada ya miradi maendeleo’ ilikadiriwa kuwa shilingi bilioni 2,019.43. Ijapokuwa Maelezo hayo hayaonyeshi ni kiasi gani cha fedha hizo kilipatikana, ni wazi kwamba kiasi chochote kitakachokuwa kimepatikana kitakuwa kimetumika kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya Tanganyika.
Hali ni hiyo hiyo kwa ‘mikopo yenye masharti ya kibiashara’, ambayo, katika mwaka wa fedha 2014/15, ilikadiriwa kuwa shilingi bilioni 1,320. Maelezo ya Waziri wa Fedha yanasema: “Hadi kufikia Machi 2015, Serikali ilipokea mkopo wa dola milioni 300 (sawa na shilingi bilioni 514) kutoka Benki ya Maendeleo ya China (CDB).” Kama tulivyotabiri mwaka jana, kwa sababu ya muundo wa Muungano wetu, kwenye fedha hizi “Zanzibar hai[ku]pata kitu chochote.”
DHANA POTOFU
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu inaamini kwamba dhana iliyojengwa kwa muda mrefu na Serikali hii ya CCM kwamba Zanzibar ina haki ya kupatiwa mgawo - hata kama ni kwa kupunjwa sana – wa fedha za mikopo ya masharti nafuu na misaada ya kibajeti, lakini haina haki ya kupata mgawo wowote wa fedha za mikopo ya masharti ya kibiashara na misaada ya miradi ya maendeleo ni sababu kubwa ya dhuluma inayotendewa Zanzibar katika mgawo wa fedha na mapato mengine yanayokuja kwa jina la Jamhuri ya Muungano.
Dhana hii haina msingi wowote kikatiba na kisheria. Ukweli ni kwamba mgawanyo wa fedha na mapato ya Muungano ambao umejengwa kwa msingi wa dhana hii unakiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano na ni kinyume cha masharti ya Makubaliano ya Muungano ya mwaka 1964. Nyongeza ya Kwanza ya Katiba ambayo imeorodhesha Mambo ya Muungano inaonyesha kwamba ‘Mikopo na Biashara ya Nchi za Nje’ ; na ‘Mambo yote yanayohusika na sarafu na fedha kwa ajili ya malipo yoyote halali; ... fedha za kigeni na usimamizi juu ya mambo yanayohusika na fedha za kigeni’ ni mojawapo ya mambo 22 ya Muungano. Hali hii imekuwa hivyo tangu Makubaliano ya Muungano yaliposainiwa tarehe 22 Aprili, 1964.
Mheshimiwa Spika,
Katiba yetu haijatenganisha kati ya mikopo ya masharti nafuu – ambayo Zanzibar ina haki ya kupata mgawo – na mikopo yenye masharti ya kibiashara, ambayo Zanzibar haina haki ya kupatiwa mgawo. Mikopo ya masharti ya aina zote ni Mambo ya Muungano na Zanzibar ina haki, na imekuwa na haki tangu mwaka 1964, kwa mujibu wa Katiba, ya kupata mgawo wa mikopo hiyo.
Msimamo ni huo huo kwa misaada kutoka kwa washirika wa maendeleo. Katiba yetu haijatenganisha kati ya misaada ya kibajeti – ambayo Zanzibar inastahili kugawiwa - na ile isiyokuwa ya kibajeti, ambayo Zanzibar haistahili kupata mgawo. Kwa vile misaada yote inayotoka kwa washirika wa maendeleo inakuja kama fedha za kigeni, basi inaangukia katika kipengere cha Mambo ya Muungano kinachohusiana na ‘mambo yote yanayohusika na sarafu na fedha kwa ajili ya malipo yoyote halali ... fedha za kigeni na usimamizi juu ya mambo yote yanayohusika na fedha za kigeni.’ Kwa sababu hiyo, Zanzibar ilistahili, na bado inastahili, kupata mgawo wa fedha za misaada ya aina zote, iwe ya kibajeti ama isiyokuwa ya kibajeti.
MAAGIZO YA BUNGE YAMEPUUZWA
Mheshimiwa Spika,
Mwaka jana Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala ya Bunge lako tukufu ilitoa agizo kwamba “Serikali iweke utaratibu wa kutoa taarifa/elimu kwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wananchi kwa ujumla kuhusu namna na kiasi gani cha fedha Serikali ya Jamhuri ya Muungano inaichangia Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.” Aidha, Kamati iliagiza kwamba “taarifa kuhusu fedha zote zinazopelekwa Zanzibar kupitia Hazina au mamlaka yoyote, ziwasilishwe Ofisi ya Makamu wa Rais – Muungano kwa ajili ya kumbukumbu na kuujulisha umma wa Watanzania.”
Agizo hilo la Bunge lako tukufu halijatekelezwa. Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya Mwaka 2014/15 haina tofauti yoyote na Taarifa ambazo zimekuwa zikitolewa kila mwaka na Ofisi ya Makamu wa Rais. Kama ilivyokuwa mwaka jana na miaka mingine yote ya nyuma, Taarifa ya mwaka huu haionyeshi kiasi chochote cha fedha kilichotolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kutoka fungu la ‘mikopo na misaada ya miradi ya maendeleo’ ambayo sio ya kibajeti.
Taarifa ya mwaka huu haionyeshi fedha yoyote iliyotolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano kama mgawo wa Zanzibar kutoka kwenye fungu la ‘mikopo yenye masharti ya kibiashara.’ Na wala hakuna taarifa yoyote kuhusu ‘fedha zote zinazopelekwa Zanzibar kupitia Hazina au mamlaka yoyote’ ya Jamhuri ya Muungano. Kwa kifupi, agizo la Bunge lako tukufu limepuuzwa na Serikali hii sikivu ya CCM!
Badala yake, Mheshimiwa Spika, Serikali hii ya CCM imekuja na blah blah zake za miaka yote ili kuwapumbaza wajinga na kuwadanganya wasioelewa. Hivi ndivyo Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais anavyoelezea ‘Utekelezaji’ wa agizo hilo la Bunge: “Serikali ina utaratibu wa kutoa taarifa kuhusu fedha zinazopelekwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Bunge na machapisho mbali mbali kuhusu Muungano. Aidha, Ofisi ya Makamu wa Rais itaendelea kuhakikisha kuwa, taarifa hizo zinapatikana na kuwajulisha wananchi.”
Kwa heshima zote kwa Mheshimiwa Waziri wa Nchi, hoja sio kwamba Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala ilikuwa haijui kuwa Serikali ina utaratibu wa kutoa taarifa kwa Bunge kuhusu fedha zinazopelekwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Hoja ya msingi ni kwamba Kamati haikuridhika na utaratibu huo. Hoja ya msingi ni kwamba utaratibu wa sasa wa utoaji wa taarifa za fedha za Muungano na mgawanyo wake unaficha unyonyaji na dhuluma kubwa inayofanyiwa Zanzibar katika mgawanyo wa fedha na mapato mengine ya Muungano.
Mheshimiwa Spika,
Katika Maoni yetu ya mwaka jana, Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu iliitaka Serikali hii ya CCM “... ilete mbele ya Bunge lako tukufu takwimu za fedha zote zilizopokelewa na Serikali kama misaada na mikopo ya kibajeti kwa kipindi cha miaka kumi iliyopita na sehemu ya fedha hizo zilizolipwa kwa Zanzibar kama gawio lake katika kipindi hicho.” Kama tulivyosema katika Maoni yetu hayo, “takwimu hizo ni muhimu ili Watanzania, na hasa Wazanzibari, waweze kufahamu kama Zanzibar imekuwa ikipata sehemu yake halali ya mapato ya Jamhuri ya Muungano yanayotokana na misaada na mikopo ya kibajeti.”
Mheshimiwa Waziri wa Fedha alitoa ahadi kwa Bunge lako tukufu kwamba angeleta takwimu hizo. Hajafanya hivyo. Maelezo yake hayana takwimu zozote za mgawanyo wa mapato ya Muungano baina ya Tanganyika na Zanzibar za kipindi chochote. Katika mazingira haya, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni itasemehewa na wapenda haki wote kwa kuamini kwamba takwimu hizo zinafichwa kwa sababu zina ushahidi wa dhuluma kubwa ambayo Zanzibar na Wazanzibari wamefanyiwa na Serikali ya Tanganyika – ambayo ndiyo Serikali ya Jamhuri ya Muungano – kwa miaka yote ya Muungano huu. Kama maneno yetu haya sio ya kweli basi Serikali hii ya CCM na ithubutu kuthibitisha uongo wetu kwa kutoa takwimu za mgawanyo wa mapato yote ya Muungano ambazo Mheshimiwa Waziri wa Fedha aliahidi kuzileta Bungeni.
HISA ZA ZANZIBAR BODI YA SARAFU YA AFRIKA MASHARIKI
Mheshimiwa Spika,
Agizo lingine la Bunge lako tukufu ambalo limepuuzwa na Serikali hii ya CCM linahusu hisa za Zanzibar katika iliyokuwa Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki (East African Currency Board) ambayo ilivunjwa mwaka 1966 pale nchi wanachama wake zilipoanzisha Benki Kuu zao. Kwa sababu ya masuala ya sarafu na fedha kufanywa mambo ya Muungano kufuatia Makubaliano ya Muungano, hisa za Zanzibar zilichukuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano, yaani Serikali ya Tanganyika iliyovaa joho la Tanzania.
Suala la fedha za Zanzibar katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki limekuwa mojawapo ya ‘kero’ sugu za Muungano kwa sababu Serikali ya Jamhuri ya Muungano, aka Serikali ya Tanganyika imekataa kuirudishia Serikali ya Mapinduzi Zanzibar fedha zake halali. Visingizio vinavyotumiwa na Serikali hii ya CCM kukataa kurudisha fedha za Wazanzibari ni vingi na vimekuwa vinabadilika badilika kutegemea mazingira na wakati.
Kwa mfano, mwezi Januari 2013, Mheshimiwa Waziri wa Nchi alitoa kauli ifuatayo mbele ya Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala kuhusu suala hili: “Katika Kikao cha Kamati ya Pamoja ya [Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania] na [Serikali ya Mapinduzi Zanzibar] ya Kushughulikia Masuala ya Muungano kilichofanyika tarehe 14 Januari 2013 imeelezwa kwamba Mawaziri wa Fedha wa [Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania] na [Serikali ya Mapinduzi Zanzibar] wamepatiwa nyaraka maalum zenye taarifa za siri na wamekubaliana kujadili suala hili mwezi Februari, 2013 baada ya kuzipitia nyaraka hizo.”
Hata hivyo, baada ya mwaka huo kumalizika bila ufumbuzi wa suala hilo, mwaka jana Mheshimiwa Waziri wa Nchi alikuja na maelezo hayo hayo kuhusu fedha hizo za Zanzibar. Kwa maneno yake mwenyewe, hisa za Zanzibar katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki ni mojawapo ya “kero zilizobaki katika orodha ya mambo ya kutafutiwa ufumbuzi....” Kwa sababu hiyo, “... masuala ya Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki na mgawanyo wa faida ya Benki Kuu yapo katika ngazi ya Mawaziri wa Fedha wa (Serikali ya Jamhuri ya Muungano) na (Serikali ya Mapinduzi Zanzibar) kwa hatua za majadiliano.”
Mwaka huu Mheshimiwa Waziri wa Nchi amekuja na hadithi tofauti. Kwa mujibu wa Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango na Bajeti, Kamati iliagiza kwamba “Wajumbe wa Bunge la Katiba watumie fursa ya Bunge la Katiba kuzimaliza kero za hisa za Zanzibar zilizokuwa kwenye Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki....” Majibu ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi yanadhihirisha ubabaishaji mkubwa na ukwepaji hoja ambao umetumika kuendeleza dhuluma dhidi ya Zanzibar katika suala hili:
“Bunge la Katiba limejadili Rasimu ya Katiba, na maeneo mengi yenye changamoto za Muungano yameibuliwa na kujadiliwa kwa lengo la kuzitatua na mengine kuondolewa kwenye orodha ya mambo ya Muungano. Baadhi ya hoja zilizokuwepo ambazo zitapatiwa ufumbuzi kupitia Katiba Inayopendekezwa ni pamoja na suala la utafiti na uchimbaji wa mafuta na gesi asili, ambalo limeondolewa katika orodha ya mambo ya Muungano, ibara ya 74(3). Aidha, Katiba Inayopendekezwa imeimarisha utekelezaji wa masuala ya Muungano na utatuzi wa changamoto zake kwa kuunda Tume ya Uhusiano na Uratibu wa Mambo ya Muungano (Sura ya Tisa). Ni matumaini yetu kuwa, kupitia Tume hiyo changamoto za Muungano zilizopo zitapatiwa ufumbuzi na maamuzi yatakayopatikana yatatambulika kikatiba.”
Maneno haya yametoka katika sehemu ya Taarifa iliyoandikwa ‘Utekelezaji’, lakini Mheshimiwa Waziri wa Nchi hajasema neno hata moja kuhusu hisa za Zanzibar katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki, ambalo ndio lilikuwa agizo la Bunge! Hata hivyo, kwingineko katika Taarifa yake, Waziri wa Nchi amerudia majibu yake ya mwaka jana na mwaka juzi kuhusu suala hili: “Miongoni mwa masuala yanayofuatiliwa ni pamoja na Hisa za [Serikali ya Mapinduzi Zanzibar] zilizokuwa katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki na mgawanyo wa faida ya Benki Kuu....”
Majibu ya aina hii yanathibitisha wazi kwamba Serikali hii ya CCM haina nia wala uwezo wa kutatua kero za Muungano ambazo zimeisibu Zanzibar tangu mwaka 1964. Kwa vile yenyewe ni zao la Muungano huu wa kinyonyaji, CCM haiwezi kutatua kero hizi za Muungano na ikabaki salama. Ndio maana waasisi wake waliobaki – kama akina Mzee Hassan Nassoro Moyo – ambao wametambua dhuluma za Muungano huu kwa Zanzibar na kudiriki kuzizungumzia hadharani wanafukuzwa uanachama badala hoja zao kusikilizwa kwa makini na kujibiwa.
KATIBA INAYOPENDEKEZWA NA KUISHI KWA MATUMAINI!!!
Mheshimiwa Spika,
Baada ya Serikali hii ya CCM kushindwa kutatua ‘kero za Muungano’, sasa imepata kisingizio kingine cha kuwafanya Wazanzibari waendelee kuishi kwa matumaini: Katiba Inayopendekezwa. Hivyo basi, kwa mujibu wa Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango na Bajeti iliyowasilishwa na Mheshiniwa Waziri wa Nchi, “... Katiba Inayopendekezwa imeimarisha utekelezaji wa masuala ya Muungano na utatuzi wa changamoto zake kwa kuunda Tume ya Uhusiano na Uratibu wa Mambo ya Muungano.... Ni matumaini yetu kuwa, kupitia Tume hiyo changamoto za Muungano zilizopo zitapatiwa ufumbuzi na maamuzi yatakayopatikana yatatambulika kikatiba.”
Kwingineko katika Taarifa hiyo tunakumbushwa kwamba matumaini hayo yamejengwa katika msingi wa mchanga: “Kupitia mchakato wa kuandika Katiba mpya, changamoto nyingi za Muungano zimejadiliwa na baadhi ya hoja zilizokuwepo zitapatiwa ufumbuzi kupitia Katiba Inayopendekezwa baada ya kupitishwa.... Vile vile, uanzishwaji wa Tume ya Usimamizi na Uratibu wa Mambo ya Muungano ... itajenga misingi imara ya kikatiba ya utekelezaji wa mambo ya Muungano na kuyapa nguvu ya kisheria maamuzi mbali mbali yatakayotolewa na Tume hii.”
Mheshimiwa Spika,
Kwa wale wanaofikiria kwamba kuanzishwa kwa Tume ya Mambo ya Muungano - kama inavyopendekezwa na Katiba Inayopendekezwa – kutakuwa ni mwarobaini wa kero za Muungano, ni vyema wakatafakari historia ya zaidi ya miaka thelathini ya Tume nyingine iliyoanzishwa na Mabadiliko ya Tano ya Katiba ya sasa, yaani Tume ya Pamoja ya Fedha. Tume hiyo ilipewa jukumu, inter alia, la “kuchambua mapato na matumizi yanayotokana na, au yanayohusu utekelezaji wa Mambo ya Muungano na kutoa mapendekezo kwa Serikali mbili kuhusu mchango na mgawo wa kila mojawapo ya Serikali hizo.”
Baada ya kutamkwa na Katiba mwaka 1984, Tume ya Pamoja ya Fedha haikutungiwa ya kuitekeleza mpaka mwaka 1996; na baada ya hapo Tume yenyewe haikuteuliwa hadi mwaka 2003, karibu miaka ishirini baada ya kuundwa rasmi kikatiba. Na tangu kuteuliwa miaka kumi na mbili iliyopita, mapendekezo yake muhimu kuhusu mgawanyo wa fedha na mapato ya Muungano na uchangiaji wa gharama zake yamekuwa yakipuuzwa na Serikali hii ya CCM. Kwa mfano, mwezi Agosti, 2006, Tume hiyo iliandaa Mapendekezo ya Tume Kuhusu Vigezo vya Kugawana Mapato na Kuchangia Gharama za Muungano. Kwa mujibu wa waraka huo wa Tume, “... mapato yanayotokana na vyanzo vya Muungano yanakidhi matumizi ya Muungano na kuwa na ziada ya kutosha. Takwimu zinaonyesha kuwa kiasi kidogo cha mapato hayo kimekuwa kinagharimia matumizi ya Muungano.
Aidha, uchambuzi wa Tume ya Pamoja ya Fedha ulionyesha kuwa “... kiasi kikubwa cha ziada ya mapato ya Muungano kimekuwa kinatumika kugharimia mambo yasiyo ya Muungano.” Kwa sababu hizo, Tume ilipendekeza kwamba uwekwe utaratibu utakaowezesha kutenganisha mapato na matumizi ya Muungano na yasiyo ya Muungano. Siku kama ya leo mwaka jana, miaka nane baada ya Tume kutoa mapendekezo yake, Mheshimiwa Waziri wa Nchi aliliambia Bunge lako tukufu kwamba “Serikali zetu mbili bado zinaendelea kushughulikia mapendekezo yaliyotolewa na Tume ya Pamoja ya Fedha.”
Na kama inavyofahamika, hadi sasa Akaunti ya Pamoja ya Fedha “... ambamo kutawekwa fedha yote itakayochangwa na Serikali mbili... kwa madhumuni ya shughuli za Jamhuri ya Muungano kwa Mambo ya Muungano” haijafunguliwa, yapata miaka thelathini na moja baada ya kuamriwa hivyo na Katiba. Kutokana na kushindikana kufunguliwa huko, kwa miaka yote hii, bajeti ya Muungano imekuwa ndio bajeti ya Tanganyika, kinyume na maelekezo ya Katiba.
KURA YA MAONI HEWA!!!
Mheshimiwa Spika,
Kuna sababu nyingine zaidi ya historia ya Serikali hii ya CCM kushindwa kutatua kero za Muungano: hakuna uhakika wowote kwamba Katiba Inayopendekezwa itakuwa ndiyo Katiba Mpya ya Tanzania. Suala kubwa hapa ni je, kutakuwa na kura ya maoni kuhalalisha Katiba Inayopendekezwa? Kwa kauli za viongozi wote wa Serikali hii ya CCM, kuanzia Rais Jakaya Kikwete, Waziri Mkuu na Waziri wa Katiba na Sheria, jibu la swali hili ni ndio. Hata hivyo, viongozi hawa hawa ndio waliokuwa mstari wa mbele kuwaaminisha wananchi kwamba kura ya maoni ingefanyika tarehe 30 Aprili iliyopita, licha ya kila mwenye macho ya kuona na akili ya kufikiria kusema kwamba kura ya maoni kwa tarehe hiyo ilikuwa ni ndoto ya mchana!!!! Kwa sababu hiyo, kauli za viongozi hawa haziaminiki tena.
Kwa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu, hata kama Tume ya Uchaguzi itakamilisha jukumu lake la kuandikisha wapiga kura nchi nzima, bado hakutakuwa na uhakika wa kufanyika kwa kura ya maoni kuhalalisha Katiba Inayopendekezwa. Tatizo la msingi hapa ni matakwa ya Sheria ya Kura ya Maoni, 2013. Sheria hiyo imeweka utaratibu mgumu wa uendeshaji wa kura ya maoni, ambapo kila hatua inayotakiwa kuchukuliwa haiwezekani kuahirishwa wala kuongezewa muda.
Kwa mfano, ndani ya siku kumi na nne tangu tarehe ya kupokea Katiba Inayopendekezwa, Rais anatakiwa – kwa Amri iliyotangazwa katika Gazeti la Serikali na baada ya kushauriana na Rais wa Zanzibar – kuielekeza Tume ya Uchaguzi kuendesha kura ya maoni juu ya Katiba Inayopendekezwa. Amri ya kura ya maoni inatakiwa kufafanua kipindi cha kampeni na kipindi ambacho kura hiyo ya maoni inatakiwa kufanyika. Rais Kikwete alikwishatoa Amri kwa mujibu wa kifungu cha 4 cha Sheria ya Kura ya Maoni. Rais hana mamlaka yoyote, kwa mujibu wa Sheria hii, wa kutengua Amri yake au kutoa Amri mpya ili kuwezesha kura ya maoni kufanyika kwa tarehe nyingine tofauti na tarehe iliyotangazwa kwenye Amri ya kwanza.
Pili, ndani ya siku saba baada ya kuchapishwa kwa Katiba Inayopendekezwa, Tume inatakiwa kuandaa swali la kura ya maoni na kulichapisha katika Gazeti la Serikali. Na ndani ya siku kumi na nne baada ya kuchapisha swali hilo, Tume inatakiwa kutoa Taarifa ya kufanyika kwa kura ya maoni, itakayoeleza kipindi cha kuhamasisha na kuelimisha umma juu ya kura hiyo na siku ya kura ya maoni. Na kila msimamizi wa kura ya maoni anatakiwa, ndani ya siku ishirini na moja baada ya kuchapishwa kwa Taarifa ya Tume, kuwajulisha wananchi katika Jimbo lake la Uchaguzi kuhusu utaratibu wa kufanyika kwa kura ya maoni. Aidha, Tume inatakiwa kutoa elimu kwa umma juu ya Katiba Inayopendekezwa kwa muda wa siku sitini tangu Katiba Inayopendekezwa ilipochapishwa.
Tume ilikwishaandaa na kuchapisha swali la kura ya maoni na ilikwishatoa Taarifa ya kura ya maoni na ratiba yake nzima. Tume haina mamlaka yoyote, kwa mujibu wa Sheria ya Kura ya Maoni, ya kutengua Taarifa yake na kutoa Taarifa nyingine, au kuweka ratiba nyingine badala ya ratiba iliyokwishatolewa. Vile vile, Tume haiwezi kujiongezea muda wa kutoa elimu kwa umma juu ya Katiba Inayopendekezwa; au kujipa muda mwingine kwa vile muda uliowekwa na Sheria haukutumika ipasavyo. Kwa upande wao, wasimamizi wa kura ya maoni hawana mamlaka yoyote kisheria ya kuongeza au kuongezewa muda wa kutoa taarifa kwa umma chini ya kifungu cha 5(2) cha Sheria ya Kura ya Maoni.
Mheshimiwa Spika,
Tume ya Uchaguzi haina mamlaka yoyote kisheria kuongeza muda kwa mashirika yasiyokuwa ya kiserikali kuendesha elimu kwa umma juu ya Katiba Inayopendekezwa baada ya muda wa awali uliowekwa kwa ajili hiyo kupita. Kwa kifupi, Mheshimiwa Spika, hakuna uwezekano kisheria wa kurudia tena hatua zozote muhimu ambazo zilikwishachukuliwa kwa ajili ya kufanyika kwa kura ya maoni iliyokuwa imepangwa tarehe 30 Aprili, 2015. Hakuna uwezekano kisheria wa kuongeza muda kwa hatua zozote ambazo muda wake ulikwishapita.
Kwa sababu hizi, hakuna kufanyika kura ya maoni juu ya Katiba Inayopendekezwa kwa mujibu wa Sheria ya Kura ya Maoni kama ilivyo kwa sasa. Na hadi sasa, Serikali hii ya CCM haijaleta Muswada wowote wa marekebisho ya Sheria hiyo ili kuwezesha kufanyika kwa kura ya maoni siku za usoni. Kama ilivyokuwa kwa ahadi ya kura ya maoni ya tarehe 30 Aprili, Serikali hii ya CCM inadanganya Watanzania kuwa kutakuwa na kura ya maoni wakati kila mwenye akili timamu anajua hilo haliwezekani bila kwanza kuwa na mazingira wezeshi ya kisheria. Inataka Watanzania, hasa Wazanzibari ambao ndio wamekuwa victims wakubwa wa Muungano, waendelee kuishi kwa matumaini kwamba kero za Muungano zitatafutiwa dawa wakati hakuna dawa ya kero hizo bila mabadiliko ya muundo wa Muungano.
Mheshimiwa Spika,
Historia yote ya Muungano inathibitisha ukweli mmoja mkuu: ‘kero za Muungano’ – hasa uchangiaji wa gharama na mgawanyo wa mapato yake - zinatokana na muundo wa Muungano. Bila kutatua tatizo la muundo, kero hizo hazitatatuliwa na hatimaye Muungano wenyewe utakufa. Kabla ya kutishwa na ‘kuufyata’ Dodoma wakati wa Bunge Maalum, Baraza la Wawakilishi Zanzibar lilitambua ukweli huu. Kama lilivyoiambia Tume ya Mabadiliko ya Katiba, “rasilmali za Muungano ziwe ni milki ya pande mbili za Muungano; na rasilmali hizo ndio zitumike katika uendeshaji wa Mamlaka za Muungano. Ugawaji wa rasilmali ufanywe kwa uwiyano maalum utakaokubaliwa kwa pamoja na pande mbili za Muungano.”
HITIMISHO: MUUNGANO WA DHATI AU WA KIINI MACHO???
Mheshimiwa Spika,
Kwa yeyote mwenye macho ya kuona na akili ya kufanyia tafakuri juu ya Muungano, hawezi kukanusha maneno ya aliyekuwa Spika wa Bunge lako tukufu, Mheshimiwa Pius Msekwa, kwamba ‘Muungano huu ni kiini macho tu.’ Kauli hiyo ilitolewa na Speaker Emeritus Msekwa katika mada yake Hali ya Muungano aliyoiwasilisha katika semina juu ya Miaka Thelathini ya Muungano iliyofanyika Tanga mwaka 1994.
Speaker Emeritus Msekwa alisema kwamba, chini ya Muungano huu, Zanzibar ilikabidhi sehemu muhimu ya mamlaka yake (mahusiano ya nchi za nje, ulinzi na usalama, uraia, kodi na ushuru wa forodha, sarafu, nguvu kuu za kuendeshea uchumi na mengineyo) kwa Tanganyika; na kisha Tanganyika ikajigeuza jina na kujiita Jamhuri ya Muungano. Kwa maneno yake, “kwa jinsi mambo yalivyo sasa, Zanzibar inaonekana kama vile ni ‘invited guest’ (mgeni mwalikwa) katika Muungano huu.”
Ili kuthibitisha kwamba Speaker Emeritus Msekwa hakuwa anatunga hadithi za mambo yasiyokuwepo, mwaka huo huo, msomi mashuhuri wa Kiafrika, hayati Profesa Ali A. Mazrui aliandika katika gazeti The Sunday Nation la Kenya kwamba kwa sababu ya Muungano, Zanzibar imepoteza kila kitu chake muhimu, wakati Tanganyika imebadilika jina tu na kuwa Tanzania, huku ikiwa na mamlaka zaidi.
Mheshimiwa Spika,
Kauli za Speaker Emeritus Msekwa na Hayati Profesa Mazrui juu ya Muungano wetu zilikuwa za kweli mwaka 1994, na bado ni za kweli leo, yapata miaka ishirini na moja baadae. Muungano wetu umebakia ni wa jina tu. Ndio maana hata Baraza la Wawakilishi Zanzibar, katika maoni yake kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, lilitaka ‘kuwa na Muungano wa dhati’, yaani “... Muungano wa kweli, hata kama ni kwa maeneo machache, kwa dhati ya wanasiasa na Watanzania kwa ujumla.”
Kwa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Muungano ‘wa dhati’ na ‘wa kweli’ ni ule ambao kuna “... Mamlaka ya Zanzibar huru na Mamlaka ya Tanganyika huru ndani ya Muungano, (na) Mamlaka ya Muungano iwekwe wazi – maeneo yake, uwezo au nguvu zake, na utendaji wake. Mambo yote hayo yawekwe wazi na mipaka yake.” Kwa vile mambo haya hayapo kwa sasa, na hayajawahi kuwekwa wazi tangu mwaka 1964, ni wazi kwamba Muungano huu sio wa ‘kweli’ wala wa ‘dhati’ na, kwa maneno ya Speaker Emeritus Msekwa, ni kiini macho!
Mheshimiwa Spika,
Kwa kumalizia, tunaomba kurudia maneno tuliyoyasema katika Maoni yetu ya mwaka jana kuhusu mgawanyo wa fedha na mapato ya Muungano: “... [K]wa sababu ya Muungano huu, uhusiano kati ya Tanganyika na Zanzibar ni uhusiano wa kinyonyaji. Kwa sababu hiyo, huu ni uhusiano wa kikoloni. Ni uhusiano kati ya ‘himaya’ ya Tanganyika na ‘koloni’ lake la Zanzibar. Himaya za kikoloni huwa zinadhibiti masuala yote ya ulinzi na usalama, mambo ya nje na uhusiano wa kimataifa, uraia, kodi, fedha, sarafu na benki kuu ya makoloni yao. Na himaya za kikoloni huwa zinatumia nguvu na udhibiti wao wa masuala haya kuyanyonya makoloni yao kiuchumi, kuyadidimiza kijamii na kuyatawala kisiasa. Hivi ndivyo ambavyo imekuwa kwa mahuasiano kati ya Tanganyika na Zanzibar tangu kuzaliwa kwa Muungano huu tarehe 26 Aprili, 1964.”
Mheshimiwa Spika,
Kama kuna mwenye tafsiri tofauti na tafsiri hii ya takwimu za mgawanyo wa fedha na mapato ya Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar basi na aiweke hadharani tafsiri yake hiyo na kutukanusha.
---------------------------------------------------------------
Tundu Antiphas Mughwai Lissu (MB)
MSEMAJI & WAZIRI KIVULI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO)
KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI
19 MEI,2015

No comments: