Juma Duni Haji ni Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF) ngazi ya Taifa naalikua niWaziri wa Afya wa Serikali ya Zanzibarna sasani Waziri wa Miundo mbinu . Juma Duni alizaliwa Novemba 26, 1950, Zanzibar (Novemba mwaka huu anatimiza miaka 65).Alianza elimu katika Shule ya Msingi Mkwajuni mwaka 1959 hadi 1965 kisha akajiunga na Shule ya Sekondari Gamal Abdel Nassar (siku hizi inaitwa “Beit el Ras”) mwaka 1966 na kuhitimu mwaka 1969.
Duni aliendelea na sekondari ya juu (kidato cha tano na sita) katika Chuo cha Lumumba, Zanzibar kati ya mwaka 1970–1971. Wakati akisoma Sekondari ya Beit el-Ras na Sekondari ya Lumumba, alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa ASP.Duni alidahiliwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambako alisoma Shahada ya Sayansi katika Elimu (BSC Education) kati ya mwaka 1972 hadi 1975.Baada ya kuhitimu shahada ya kwanza, aliajiriwa kama mwalimu wa Sekondari ya Beit Al Ras, wakati huo ikiitwa Gamal Abdil Nassir (jina la Rais wa zamani wa Misri), na baada ya mwaka mmoja akahamishiwa Sekondari ya Lumumba na kufundisha kidato cha tano na sita na baadhi ya wanafunzi wake ni “magwiji” wa siasa za Zanzibar; Ismail Jussa, Thuwayba Kisasi na wengineo.
Mwaka 1978–1979, Duni alikwenda masomoni Uingereza, akasoma na kuhitimu Stashahada ya Juu ya Elimu katika Chuo Kikuu cha Reading na aliporejea alihamishiwa Ofisi Kuu ya Wizara ya Elimu na kupewa wadhifa wa Ofisa Mipango ya Elimu.Duni alipata mafunzo mengine muhimu ya kitaaluma nchini Nigeria mwaka 1980 juu ya Mipango ya Elimu na mwaka 1982 alipelekwa Japan kujifunza kwa kina Mipango ya Kiuchumi.Pia, Mwaka 1980 Rais Aboud Jumbe, alimteua Juma Duni kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mipango (Zanzibar) na baadaye kuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango (Executive Secretary Planning Commission).Duni alianza safari ya kisiasa kwa “kulazimishwa” mwaka 1984, baada ya serikali ya Muungano kutoa Waraka wa Serikali (white paper) na kutakiwa wananchi watoe maoni yao juu ya hali na matatizo ya Muungano.Makatibu wakuu wa Serikali ya Zanzibar ya wakati huo akiwemo yeye walitoa maoni dhidi ya muungano, uhuru huo wa kitaalamu uligeuzwa kuwa mchungu kwani walisingiziwa kwamba wamefanya kinyume na walivyoagizwa na baadhi yao wakapewa onyo kali na wengine wakateremshwa vyeo.
Duni aliteremshwa cheo kutoka wadhifa wa Katibu Mkuu hadi mwalimu wa kawaida kwa Tangazo la Rais, akatakiwa kwenda kufundisha Shule ya Mikunguni.Mwaka mmoja tangu aanze kufundisha Mikunguni akaambiwa anashiriki siasa hapo shuleni na kuwatia kasumba chafu wanafunzi wa shule hiyo na hivyo akahamishiwa Shule ya Lumumba.Baada ya muda mfupi huko Lumumba nako akahamishwa na kurudishwa Ofisi Kuu ya Elimu kama Ofisa Mipango wa Elimu. Akiwa Ofisa Mipango alituhumiwa kuwa anakwenda nyumbani kwa Maalim Seif Sharrif usiku wa manane kufanya siasa na ikaipasa serikali imhamishie Idara ya Ukaguzi.
Kwenye idara ya ukaguzi nako akaambiwa anafanya siasa kwa kutoka saa za kazi na kukaa kwenye vibaraza (vijiwe), akarejeshwa tena Ofisi Kuu na huko akaambiwa kwamba anaondoka kwenda Dar es Salaam bila kuaga kwa wakubwa zake na mara nyingi ameonekana usiku akifanya siasa na Marehemu Abrahman Babu (ambaye wala hakuwepo Zanzibar wakati huo).Wizara ilipomchoka na kukosa cha kumfanya ikamrejesha kwa Mkurugenzi Mkuu wa Utumishi ambaye hakuwa na kazi ya kumpa, sana sana alimwambia abaki nyumbani bila kazi kwa zaidi ya miezi sita.Baadaye, mkurugenzi wa utumishi akamrejesha tena Wizara ya Elimu baada ya Duni kuwauliza kosa lake na kushindwa kumueleza.Duni alipoona visa hivyo vinamuumiza na vinamchosha aliomba ruhusa ya likizo bila malipo kwenda kusoma, ombi ambalo nalo pia lilikataliwa na ndiyo akaamua mwenyewe kuondoka na kwenda kujisomesha kwa fedha zake Chuo Kikuu cha Manchester, Uingereza na kuhitimu stashahada ya Juu ya Biashara kati ya mwaka 1993-1994.Wakati alipofika Uingereza akatumiwa barua ya kuachishwa kazi na kupoteza haki zake zote za miaka 18 ya utumishi serikalini. Mwaka huo 1994 akiwa bado nchini Uingereza, akaunganisha tena kwa shahada ya uzamili/umahiri akibobea kwenye usimamizi wa Rasilimali Watu na kabla hajaihitimu akarejea nchini ili kusaidia upinzani kujipanga kiuchaguzi.
Moja kwa moja akajiunga na vuguvugu la uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi. Chama Cha Wananchi (CUF) kikamteua kuwa Mgombea mwenza wa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba wakati bado hajakamlisha shahada yake ya pili ya uongozi na utawala.Tangu ajiunge CUF ameshika nyadhifa mbalimbali kwa nyakati tofauti, amekuwa Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar na Mkurugenzi wa Uchumi na Fedha CUF Taifa mwaka 1999–2003, amekuwa Mkurugenzi wa Uchumi na Fedha CUF kati ya mwaka 1997-2010, amekuwa Naibu Katibu Mkuu CUF (Zanzibar) kuanzia mwaka 1999-2010, Amekuwa Mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi Taifa CUF Taifa kati ya mwaka 1999-2014.Hivi sasa yeye ni Makamu Mwenyekiti wa CUF, nafasi aliyochaguliwa mwaka 2014 na analazimika kuishikia hadi uchaguzi mwingine wa ndani ya chama chake utakapofanyika, mwaka 2019.
Mbio za ubunge
Juma Duni Haji si mgeni katika masuala ya “kibunge’ au ya kiuwakilishi. Mwaka 1997 aligombea nafasi ya Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar (Mwakilishi wa Zanzibar anafanya kazi kama za Mbunge wa Bunge la Tanzania) Jimbo la Mkunazini, akashinda na kuwa mwakilishi kuanzia mwaka 1997-2000.Mwaka 2009 aliteuliwa na Rais Amani Abeid Karume kuwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa mara ya pili, akakaa katika wadhifa huo hadi uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 ulipofanyika na kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar (SUK).Katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, Juma Duni aliteuliwa na Rais wa Zanzibar kuwa mwakilishi na kisha akateuliwa kuwa Waziri wa Afya wa Zanzibar, wadhifa ambao ameushikilia hadi sasa.
Mbio za urais
Juma Duni ni mmoja wa Watanzania ambao wamewania kuongoza taasisi ya urais kwa muda mrefu sana, japokuwa hajawahi kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini kwa vipindi takribani vitatu yeye amekuwa ni Mgombea Mwenza wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Amefanya hivyo kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 1995, mwaka 2005 na mwaka 2010, mara zote akiwa mgombea mwenza wa Profesa Ibrahim Lipumba wa CUF.Juma Duni ni mmoja wa wanasiasa ambao wanatajwa sana kuwa na sifa, uwezo, vigezo na kila sababu ya kuweza kuwa rais wa nchi. Nilipomuuliza mipango yake juu ya mawazo hayo ya wananchi juu yake alinieleza kuwa yeye ni mtumishi wa watu na kila mara alikotumwa alikwenda. Juma Duni alinivunja mbavu aliponiambia kuwa hata leo akiteuliwa kwenda kuongoza ‘kijiji au kitongoji’ ilimradi Watanzania wametaka hivyo, ataitikia wito.
Nguvu zake
Nguvu ya kwanza inayompa Juma Duni uwezo mkubwa wa kuongoza nchi ni elimu yake. Kiongozi huyu ana shahada mbili za Chuo Kikuu na Stashahada mbili za Juu kutoka katika Vyuo Vikuu vinavyoheshimika duniani.
Zaidi ya yote amechanganya taaluma akibobea kwenye masula ya sayansi, elimu, uchumi, Biashara na Usimamizi wa Rasilimali Watu. Ni wanasiasa wachache sana wenye upeo mkubwa katika taaluma zaidi ya mbili au tatu na taaluma hizi zinampa sifa na uwezo zaidi wa kuwa rais bora.Lakini jambo la pili ni uzoefu kazini, kiongozi huyu ameanza kazi kama mwalimu na kupanda hadi kuwa Katibu Mkuu wa Wizara na baadaye Waziri. Na hata ndani ya chama chake amepanda kutoka kuwa mwanachama wa kawaida, Naibu Katibu Mkuu hadi kuwa Makamu Mwenyekiti wa chama Taifa.Lakini jambo muhimu kuliko yote, Juma Duni ni mpigania haki mkongwe na mfungwa wa kisiasa ambaye hakuwahi kuogopa kifo wala mateso. Mwaka 1997 hadi 2000 (miaka minne), alikuwa miongoni mwa wanachama na viongozi wa CUF waliotuhumiwa “kutaka kuipindua serikali ya Zanzibar”, wakapewa kesi ya uhaini “Kesi Maarufu kwa jina la Machano Khamis Ali na wengine” na kukaa gerezani miaka minne kabla mahakama haijatoa hukumu ikisisitiza kuwa hakuna uwezekano wa serikali ya Zanzibar kupinduliwa kwa sababu iko chini ya Muungano.
Lakini pia mwaka 2001–2002 (zaidi ya mwaka mzima), Juma Duni alikuwa mmoja wa viongozi wa CUF waliobambikiziwa kesi ya kisiasa wakihusishwa na kumuua Askari Polisi aliyeuawa Pemba. Cha kushangaza ni kuwa, mauaji yale ya Pemba yalipofanyika, Juma Duni alikuwa yuko Unguja, lakini kamatakamata ilipoanza naye akawekwa kwenye orodha na kukaa gerezani bila sababu.Uthubutu na uimara wa Juma Duni katika kupita kwenye misukosuko mikubwa unamfanya awe mwanasiasa wa aina yake hapa Tanzania.Wanasiasa wengi huwa ni waoga kukabiliwa na changamoto za dola na kuhofia kukaa gerezani, wengi wa wanasiasa huona shida sana kukaa gerezani siku moja au wiki moja, achilia mbali mwezi.Juma Duni amekaa gerezani kwa kuonewa kwa miaka mitano, yeye pamoja na wenzake, waliitwa wahaini lakini walithubutu kuendelea na mapambano bila kurudi nyuma. Hii ni sifa ya kipekee.Na mwisho, Juma Duni ni Mtu wa kawaida sana. Ukipishana naye barabarani huwezo kujua kama ni waziri katika serikali au Makamu Mwenyekiti wa Chama kikubwa kama CUF.Wakati tuko Bunge Maalum la Katiba ungemkuta anatembea barabarani na kufanya manunuzi binafsi kwa mguu na akitoka huko akakutana na muuza muhogo, angejinunulia na kuanza kula polepole huku akiongea na vijana, hana makuu na ni mmoja wa viongozi ambao wanajali sana utu wa watu wa kawaida, kushirikiana na watu hao na kuwasaidia kimawazo na kifikra.
Udhaifu wake
Moja ya mambo ninayoyachukulia kama udhaifu wa Juma Duni ni ubishi kupita kiasi akiwa anadai jambo ambalo anadhani linapindishwa. Pamoja na kuwa viongozi hupaswa kudai haki sana lakini wanapaswa kutokuwa “ving’ang’anizi” wa kudai haki kiasi cha kunyima upande wa pili fursa ya kufanya maamuzi sahihi. Duni akitaka jambo lake lazima liwe na huenda hii siyo sifa muhimu kwa viongozi wa kisasa.Lakini jambo la pili ni tabia yake ya kuibua kauli tata na zinazoibua mijadala mikubwa na kuikwaza sana CCM ambayo chama chake kinashirikiana nayo katika serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar. CCM mara kadhaa wamesikika wakimshutuma Juma Duni kwa tabia yake ya kuwananga kama “masultani weusi”.Kauli hizi za Juma Duni zimewahi kugeuzwa na CCM wakasisitiza kuwa amewaeleza Wazanzibari kuwa “utawala wa mtu mweusi mwisho ni kesho”. Mmoja wa viongozi wa CCM ambao nimeongea naye ameniambia kuwa kauli zake zinawaudhi sana na kwamba si mfano sahihi. Nami kwa upande wangu nimeona kuwa zinaweza kuwa sababu ya CCM “kujifanya” wamechokozwa na wao wakaendeleza chokochoko ambazo mwisho wa siku haziiweki Zanzibar mahali sahihi, hasa katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Nini kitamfanya apitishwe
Jambo la kwanza linaloweza kuifanya CUF impitishe Juma Duni kuwa mgombea Urais wa chama hicho na baadaye Ukawa ni kwa sababu ya uzoefu wa ugombea mwenza wa kiti cha urais na mtu ambaye amezunguka sana katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar. Hilo pekee linatosha kabisa kumuamini na kumpa kazi hii kwa sababu ana uzoefu, uwezo, sifa na anajua namna ya kufanya mambo yaende.Lakini pili, naona Juma Duni akipitishwa kugombea urais wa Tanzania kwa tiketi ya CUF na baadaye Ukawa ikiwa mgombea urais wa Ukawa atapaswa kutoka Zanzibar. Nawaona wanasiasa wachache sana ndani ya upinzani kule Zanzibar, wenye uzoefu, haiba, elimu na uwezo wa kumfikia yeye ikiwa kweli nchi inahitaji kuwa na viongozi imara watakaoivusha.
Nini kinaweza kumwangusha?
Jambo moja litakalomkwamisha Juma Duni katika kupita kwenye chujio la CUF na Ukawa katika kusaka tiketi ya uongozi wa nchi ni ikiwa ataamua kugombea uwakilishi. Kama nilivyoeleza, Juma Duni kuna nyakati ni kiongozi mbishi sana na akiamua jambo lake analisimamia. Ikiwa ataamua kugombea Uwakilishi (Na nimeambiwa kuwa ameanza harakati hizo) ina maana hatapita kwenya mchujo wa kuchukua nafasi ya urais wa Tanzania kwa tiketi ya Ukawa.Lakini jambo la pili ambalo litamkwamisha kwenye mchujo ni la moja kwa moja. Ni hukumu ya yeye ni Mtanzania wa asili ya wapi. Hukumu hii inatokea pale ambapo CUF na labda Ukawa wataamua kuweka mgombea urais kutika upande wa Tanzania Bara, uwezekano wa Juma Duni kuwa rais wa Tanzania mwaka huu, utafikia tamati mahali hapo.
Asipopitishwa (Mpango B)
Namtazama Juma Duni katika mipango miwili ikiwa hatagombea urais wa Tanzania. Mpango wa kwanza ni kupewa fursa ya kuendeleza kazi aliyoifanya mwaka 1995, 2005 na 2010 ya kuwa mgombea mwenza wa urais wa Tanzania na mara hii nadhani akiungwa mkono na vyama vya Ukawa.Pili, ni kugombea uwakilishi ili kutafuta tiketi ya kuwahudumia zaidi wananchi na hata kuendelea kuwa waziri ikiwa Rais wa Zanzibar ajaye ataamua kumteua na ama kupewa jukumu la kuvaa viatu vya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu kule Zanzibar. Jambo hili litaweza kutokea ikiwa CUF ndiyo itakuwa “Kaka Mkubwa” katika serikali ya pamoja inayoendelea kikatiba upande wa Zanzibar.
Hitimisho
Hakika, tutakubaliana kuwa nchi hii ina viongozi wenye uwezo mkubwa sana na wanaweza kabisa kulivusha taifa ikiwa watapewa nafasi. Mmoja wa viongozi hao ni Juma Duni.Juma Duni ameniambia kuwa moja ya maumivu makubwa aliyowahi kuyapata katika siasa za nchi hii ni kushindwa kuonana na baba yake mzazi (Mzee Duni), akiwa gerezani. Mbaya zaidi, siku ambayo alikuwa amuone baba yake kwa mara ya mwisho, ilikuwa siku ambayo Duni na wenzake waliletwa mahakamani Vuga kusikiliza kesi ya uhaini.Baba yake Juma Duni, (Mzee Duni), aliomba msaada kwa askari wa FFU, ili amsalimie mwanaye ndani ya jengo la mahakama, na kwa bahati mbaya mzee yule alikua na matatizo ya usikivu (uzito wa kusikia) Askari mmoja akamuamrisha Mzee Duni aondoke mara moja, kwa sababu mzee yule hasikii vizuri hakumuelewa askari na akajaribu kuongeza hatua moja mbele, askari yule akampiga kofi zito mzee wa watu na kuanguka chini, hakuweza kumsogelea wala kumsalimu.
Tukio lile lilitokea huku Juma Duni akiona, ameniambia aliumia sana na kwa bahati mbaya, huo ndiyo ukawa mwisho wa Juma Duni kumuona mzee wake. Muda si mrefu Mzee Duni (baba) alifariki dunia mwanaye Juma Duni akiwa gerezani na hakuruhusiwa kumzika.Pamoja na mambo makubwa aliyopitia, Juma Duni ameendelea kuwa mtumishi wa Wazanzibari wote akisimamia majukumu yake kufa au kupona. Na yeye, namtakia kila lililo jema katika safari na ndoto zake kisiasa.
No comments:
Post a Comment