Sunday 10 May 2015

MAELEZO YA KATIBU MKUU WA CUF NA MAKAMU WA KWANZA WA RAIS, MAALIM SEIF SHARIF HAMAD, KWENYE MKUTANO NA VYOMBO VYA HABARI DAR ES SALAAM SERENA HOTEL, MEI,10, 2015

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


Ndugu zangu Wahariri na Waandishi wa Habari,
Assalam Alaykum.  Awali ya yote, hatuna budi kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kutujaalia kukutana wakati huu katika eneo hili kwa ajili ya mkutano huu maalum na waandishi wa vyombo mbali mbali vya habari vya ndani na nje ya nchi.

Ndugu wanahabari, kama sote tujuavyo, mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi mkuu ambao umepangwa kufanyika tarehe 25 Oktoba, 2015 kama ilivyokwisha tangazwa na Tume za Uchaguzi.

Ndugu wanahabari, Uchaguzi wa mwaka huu ni Uchaguzi wa aina yake na wa kipekee kutokana na ukweli kwamba Watanzania sasa wameungana kutaka mabadiliko ya dhati na ya kweli na wamejiandaa kukiondoa madarakani Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho kimeisaliti dhamana kiliopewa kuwaongoza na badala yake kujikita katika ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka huku wakijinufaisha wao, familia na marafiki zao. Kwa upande wa Zanzibar, Wazanzibari wameamua kujiunga na wimbi la kihistoria la kudai na kupigania kurejesha Mamlaka Kamili ya Zanzibar chini ya Chama Cha Wananchi (CUF), kwa kuzingatia siasa za kistaarabu, demokrasia, umoja wa kitaifa na kuweka mbele maslahi mapana ya Taifa letu.
Hata hivyo, wakati nchi ikishuhudia vuguvugu hilo, Tume za Uchaguzi hapa nchini kwa maana ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) ambazo ndizo zilizopewa mamlaka kikatiba na kisheria kubeba dhamana ya kuendesha na kusimamia chaguzi katika nchi zetu zinaonekana bado zinashindwa kuachana na maradhi sugu yanayozikabili ya kutumiwa na CCM na wao kukubali kutumika kukandamiza maamuzi huru ya wananchi.
Leo hii, tumeamua kuwaita hapa kuzungumzia hali halisi ya utendaji wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) wakati tunaelekea katika uchaguzi mkuu wa 2015 na hasa tunapoelekea uandikishaji wa mwisho wa wapiga kura kabla ya uchaguzi huo, uandikishaji ambao umepangwa kuanza tarehe 16 Mei na kukamilika tarehe 28 Juni, mwaka huu.

Ndugu wanahabari, mbali na ukweli kwamba Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu utakuwa ni wa sita tangu kurejeshwa kwa mfumo wa siasa za vyama vingi nchini, dalili zote zinaoenesha kuwa hakuna nia ya dhati ya kustawisha demokrasia kupitia msingi wake muhimu, ambao ni uchaguzi, tulioamua kufanyika kila baada ya kipindi cha miaka mitano. Tunasema hayo kutokana na hadaa nyingi zilizojitokeza awali na wakati huu tunapojitayarisha kuingia katika uandikishaji wa mwisho wa wapiga kura katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura (DKWK).
Mtakumbuka kwamba chaguzi zote za Zanzibar kuanzia ule wa mwaka 1995, 2000, 2005 na ule 2010, ambao kwa kiasi ulikuwa huru lakini usio wa haki, zilikabiliwa na kukumbwa na kasoro kadhaa kubwa kama vile uandikishwaji wa wapiga kura zaidi ya mara moja, uandikishwaji wa wapiga kura wasio wakaazi katika eneo la uandikishwaji hasa vikosi vya ulinzi na usalama kwa upande wa Zanzibar, uandikishwaji wa wapiga kura walio chini ya umri na kunyimwa kwa baadhi ya wapiga kura haki yao ya msingi ya kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura. Pale yote haya yaliposhindwa kufikia lengo lililokusudiwa la kuipa ushindi haramu CCM kupitia wapiga kura haramu basi nguvu zilitumika na mwishowe matokeo ya uchaguzi kubadilishwa na kumtangaza aliyeshindwa kuwa mshindi.

Ndugu wanahabari, mnakumbuka vyema jinsi nchi yetu ilivyokumbwa na balaa na maafa yaliyosababishwa na kasoro hizi za Uchaguzi ambazo kwa kiasi kikubwa zinaratibiwa na wasaliti waliotanguliza mbele maslahi yao binafsi na kufanikishwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) iliyokubali kutumiwa kuhujumu, kudhalilisha na kukandamiza demokrasia nchini.

Kutokana na ukweli huo, ni vyema tukatambua kwamba mizozo yote ya kisiasa Zanzibar huanzishwa na kuchochewa na ukiukwaji wa sheria na taratibu za Uchaguzi zilizowekwa hasa kuanzia hatua ya uandikishwaji wa wapiga kura, uhesabuji wa kura hizo na utangazwaji wa matokeo ya uchaguzi
Matukio ya vitisho, vipigo na mauaji ya wananchi wasiokuwa na hatia yaliyotekelezwana Jeshi la Polisi tarehe 26 na 27 Januari, 2001 Unguja na Pemba na hatimaye nchi kuzalisha wakimbizi katika kambi za Shimoni na Dadaab, nchini Kenya ni sehemu ya matukio mabaya na kumbukumbu inayoumiza katika historia ya nchi yetu inayotokana na ukiukwaji wa Sheria za Uchaguzi hasa uandikishaji wa wapiga kura kunakofanywa kwa makusudi na Tume ya Uchaguzi kwa lengo la kuibeba na kuisaidia CCM.
Sote ni mashahidi wa jitihada kubwa zinazochukuliwa na zinazoendelea kuchukuliwa na CUF kila baada ya Uchaguzi Mkuu ili kuiepusha nchi na mawimbi mazito ya migogoro ya kisiasa, mipasuko ya kijamii na kuhuisha mahusiano ya kidiplomasia na mataifa washirika wa maendeleo kama ilivyoshuhudiwa miaka iliyopita kufuatia kuvurugwa kwa makusudi kwa chaguzi.

Ndugu wanahabari, kama nilivyokwisha kueleza, Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) imetangaza kuanza kwa zoezi la uandikishaji wa wapiga kura wapya katika maeneo mbali mbali ya Zanzibar kuanzia tarehe 16 Mei, 2015 na kumalizika tarehe 28 Juni, 2015. Hii ndio kusema kwamba hatua za awali za matayarisho kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2015 zimeanza.
Ni katika muktadha huu, wa kuwa na Tume iliyoamua kuendelea kutumiwa kuingiza nchi katika vurugu za makusudi kwa sababu tu ya kutaka kukiridhisha Chama Cha Mapinduzi ambacho hakitakiwi tena na wapiga kura, The Civic United Front (CUF-Chama Cha Wananchi) kimeamua kukuiteni wanahabari kwa lengo la kukuelezeni, na kupitia nyinyi kuwaeleza wananchi na dunia, juu ya mambo matatu yafuatayo:

1. Uchafu uliomo katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura la Zanzibar kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Kitengo cha Sera, Utafiti na Mafunzo cha CUF.

2. Mipango ya uchafuzi inayofanywa sasa ya kuyarudia yale yaliyofanywa katika uandikishaji wa wapiga kura uliopita katika uandikishaji wa wapiga kura wapya unaotarajiwa kuanza wiki ijayo.

3. Mpango wa kuchelewesha ukataji wa mipaka ya majimbo kwa shinikizo za Sekretarieti ya CCM Zanzibar.

4. Kutofanyiwa marekebisho Sekretarieti ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC).
Ndugu wanahabari, kwa hili la kwanza linalohusu Uchafu uliomo katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura la Zanzibar, ili muweze kujionea wenyewe na kwa ushahidi na vielelezo yale niliyoyataja kabla, naomba nimpe nafasi Mkuu wa Kitengo cha Sera, Utafiti na Mafunzo cha CUF, Mhe. Hassan Jani Masoud, awasilishe matokeo ya utafiti waliyoufanya katika Daftari hilo ambao unabainisha kuwepo kwa:
Wapiga Kura wenye Umri Mdogo;
Wapiga Kura walioandikishwa zaidi ya mara moja (Multiple Registration);
Wapiga Kura Waliokufa;
Wapiga kura ambao si wakaazi katika maeneo waliyojiandikisha (Mapandikizi);
Wapiga Kura waliotumia majina au picha ambazo sio zao;
Idadi ya wapiga kura iliyozidi katika utolewaji wa vipande vya Kura.

Ndugu wanahabari, kuhusiana na suala la pili, ambalo ni Mipango ya uchafuzi inayofanywa sasa ya kuyarudia yale yaliyofanywa katika uandikishaji wa wapiga kura uliopita katika uandikishaji wa wapiga kura wapya unaotarajiwa kuanza wiki ijayo, hivi tunavyozungumza kunaendelea zoezi kubwa la kuandaa wapiga kura haramu ili waweze kuja kuandikishwa. Maandalizi hayo yanahusisha Idara ya Usajili wa Wazanzibari ambayo ndiyo hutoa Vitambulisho vya Mzanzibari (ZAN IDs), Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya, Masheha, Sekretarieti ya ZEC na la kusikitisha zaidi , hata Vikosi vyetu vya Ulinzi na Usalama. Miongoni mwa mambo yanayofanyika ni pamoja na:

1. Kutumiwa Kambi ya JWTZ iliyopo Chukwani, kisiwani Unguja kuandikisha mamia ya vijana wakiwemo wengi ambao si Wazanzibari na kuwapatia Vitambulisho vya Mzanzibari (ZAN IDs) kwa ajili ya kuja kuandikishwa kama wapiga kura. Vijana hawa walikuwa wakipelekwa katika kambi hiyo kwa magari maalum kwa kipindi cha mwezi mmoja uliopita na kuanza wiki iliopita wameitwa na kuanza kupewa vitambulisho hivyo haramu. Miongoni mwao wamepatiwa vitambulisho vinavyoonesha anuani zao ni eneo la Darajani lakini wamepelekwa kambi ya JWTZ Chukwani kwenda kusajiliwa kwa siri.

2. Katika majimbo mbali mbali ya visiwa vya Unguja na Pemba kumeandikishwa vijana wanaofikia 20,000 na kupewa ZAN IDs ambao wamepangwa kuja kuandikishwa kama wapiga kura. Wengi kati ya vijana hawa wamehamishwa kutoka nje ya majimbo yao. Kwa mfano, kuna vijana 700 waliochukuliwa katika maeneo mbali mbali ya jimbo la Uzini na ambao wamepelekwa kusajiliwa katika jimbo la Bububu kisiwani Unguja, vijana wapatao 10,000 waliohamishwa kutoka Wilaya ya Kati Unguja na kusajiliwa katika majimbo ya Dimani na Mtoni katika Wilaya ya Magharibi Unguja na majimbo ya Chumbuni na Kwamtipura katika Wilaya ya Mjini Unguja. Pia kuna vijana 1,200 wamepatiwa ZAN IDs kwa ajili ya kuja kuandikishwa katika jimbo la Chonga na wengine 1,000 katika jimbo la Mkanyageni, kisiwani Pemba.

3. Katika Mkoa wa Kaskazini Unguja, watoto wadogo wa chini ya umri wa miaka 18 wengi wao wakiwa baina ya miaka 14 hadi 17 wamekuwa wakichukuliwa na kupelekwa kituo cha kusajili vitambulisho vya Mzanzibari kilichopo Gamba ambako wamepatiwa ZAN IDs na sasa wanasubiri kuandikishwa katika Daftari la Wapiga Kura. Jimbo la Tumbatu limekuwa likiongoza katika suala hili.

Ndugu wanahabari, suala la tatu linahusu ucheleweshaji wa ukataji wa mipaka ya majimbo ya uchaguzi chini ya usimamizi wa Sekretarieti ya ZEC. Kazi hii ilipaswa iwe imeshakamilika muda mrefu uliopita na Makamishna wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar walizunguka katika majimbo yote ya Unguja na Pemba na kuchukua maoni ya wananchi. Tunazo taarifa za kuaminika kabisa kwamba Tume ilikwisha kamilisha kazi hiyo kwa kuzingatia maoni yaliyotolewa na wananchi na ripoti ya mapendekezo kutayarishwa. Hata hivyo, kwa sababu mapendekezo hayo hayakukiridhidha Chama Cha Mapinduzi, mapendekezo hayo yaliwekwa upande na sasa CCM imeitumia Wizara ya Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ kuandaa mapendekezo mengine ambayo yameandaliwa kwa lengo la kupunguza majimbo katika maeneo yenye wafuasi wengi wa CUF na kuongeza majimbo kwenye maeneo yenye wafuasi wengi wa CCM. Hadi hii leo, Tume ya Uchaguzi imekuwa ikiahirisha kila mara kutangaza majimbo hayo kwa kusubiri maelekezo hayo ya CCM kupitia Wizara ya Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ.

Ndugu wanahabari, suala la nne na la mwisho linahusu marekebisho ya Sekretarieti ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar. Mtakumbuka kwamba wakati CUF ilipokubali kuridhia matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2010, ilimtaka Dk. Ali Mohamed Shein kusimamia mambo mawili, ambayo ni kuhakikisha Daftari la Wapiga Kura linahakikiwa na pia kufanya marekebisho ya Sekretarieti ya ZEC. Dk. Ali Mohamed Shein katika hotuba yake aliyoitoa wakati wa utangazwaji wa matokeo ya Uchaguzi, alikubali kuyafanyia kazi mambo hayo yote mawili ili kuondoa kasoro zilizopo katika utendaji na utekelezaji wa majukumu ya Tume hiyo. 

Hadi hivi tunavyozungumza, mabadiliko hayo hayajafanyika na Sekretarieti hiyo ya ZEC sasa inajiandaa tena kututumbukiza katika vurugu nyengine za uchaguzi mkuu wa 2015. Hata hizi hatua nilizozitaja hapo juu zinategemewa kufanikishwa kwa kuitumia Sekretarieti hii ambayo ndiyo imekuwa chanzo cha uchafuzi wa chaguzi zote za 1995, 2000, 2005 hadi 2010.

Kutokana na hali hiyo, The Civic United Front (CUF-Chama Cha Wananchi) kimeona kuna haja ya kuyaeleza haya mbele ya wananchi kupitia kwenu waandishi wa habari. Tukiwa ni sehemu ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar tumekuwa tukiyawasilisha kwa wenzetu lakini hadi sasa hatujaona hatua za maana na za dhati zenye lengo la kuyachukulia hatua. 

Tunaamini wakati umefika masuala haya yajulikane na wananchi na jumuiya ya kimataifa kwa ujumla na pia tunataka hatua zifuatazo zichukuliwe ili kuiepusha nchi na vurugu zinazoweza kutokea kwa kukiuka misingi ya katiba na sheria katika uendeshaji wa uchaguzi huru, wa haki na amani:

1. Wapiga kura haramu wote waliopatiwa vitambulisho vya Mzanzibari kinyume na sheria watakiwe kuvisalimisha vitambulisho hivyo na wasiandikishwe katika Daftari la Wapiga Kura.

2. Watu wote wenye haki ya kupatiwa ZAN IDs wapewe vitambulisho vyao kabla ya uandikishaji wa mwisho unaotarajiwa kuanza tarhe 16 Mei ili waweze kutumia haki yao ya kikatiba kujiandikisha na kupiga kura.

3. Vikosi vya Ulinzi na Usalama vikiwemo JWTZ na Idara Maalum za SMZ ziache kutumiwa kisiasa na kwenda kinyume na sheria zinazoongoza kazi zao ambazo zinakataza kujiingiza katika masuala ya kisiasa.

4. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ) awache kuwatumia Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Masheha katika kusajili wapiga kura haramu kwa kuwapatia ZAN IDs na wakati huo huo kuwakatalia wapiga kura halali haki ya kusajiliwa na kupatiwa ZAN IDs.

5. Idara ya Usajili wa Wazanzibari iache kutumika kisiasa kwa kusajili watu wasio Wazanzibari, watoto wadogo na watu wanaotoka nje ya majimbo yao kwa lengo tu la kukisaidia CCM.

6. Jeshi la Polisi lisikubali kutumiwa kinyume na sheria kuwalinda wapiga kura hao haramu wanapopelekwa kwenda kujiandikisha.

7. Daftari la Wapiga Kura lifanyiwe uhakiki kwa mfumo wa kielektroniki unaotumia bio-metric features ili kuwafuta waliosajiliwa zaidi ya mara moja na pia kuwaondoa waliofariki na watoto walio chini ya umri wa miaka 18.

8. Sekretarieti ya ZEC ifanyiwe marekebisho ili iwe ni Sekretarieti huru isiyojiegemeza kwenye Chama cha CCM.

9. ZEC ikatae kutumiwa na CCM katika suala la ukataji wa mipaka ya majimbo ya uchaguzi.

Mwisho kabisa, nitumie fursa hii kusema kwamba pamoja na matatizo ya uchaguzi mkuu wa 2010, tuliweza kuvuka salama kupitia misingi madhubuti ya maridhiano ambayo tuliyaasisi mimi na Rais mstaafu, Dk. Amani Karume. 

Maridhiano yale yalipaswa kuendelezwa ili tufikie hatua ya kufanya chaguzi huru, za haki na za amani na pia kujenga misingi madhubuti ya umoja na maelewano katika nchi yetu. Sisi tulifanya wajibu wetu. Ni imani yangu kwamba Rais Jakaya Kikwete na Rais Ali Mohamed Shein nao watafanya wajibu wao ili kuepuka kuturudisha kule tulikotoka. 

Naamini kwamba Zanzibar na Tanzania zinaweza kufikia mahala pa kufanya uchaguzi ulio huru, wa haki na amani na kuwa mfano katika Bara la Afrika. Niwakumbushe tu wenzangu kwamba wimbi la mabadiliko linapofikia wakati wake huwa halizuiliki tena. 

CCM isitarajie kuendelea kubakia madarakani kwa kutumia njia za hadaa, udanganyifu, hujuma, nguvu, ubabe na vitisho. Hii ni nchi yetu sote na kama alivyowahi kusema Rais Mstaafu Benjamin William Mkapa, CCM haina hatimiliki ya nchi hii. Hatuna budi kulitambua hilo na tushirikiane kuivusha salama nchi yetu katika uchaguzi mkuu huu na baada ya uchaguzi mkuu kwa kuheshimu matakwa ya wananchi.

Nawashukuru kwa kunisikiliza.
Ahsanteni sana.

No comments: