Sunday 29 May 2016

Hakuna wa kuzima nyota ya Maalim Seif



Majina matatu ya Idri Abdul-wakil Nombe, Seif Sharif Hamad na Salmin Amour Juma ndio yaliojadiliwa na Halmashauri kuu ya Taifa ya CCM-NEC ili kuteua mmoja wapo kuwa rais mpya atakaemrithi Mzee Ali Hassan Mwinyi. Mzee Idris Abdulwakil Nombe alikuwa wa mwanzo kuomba jina lake liondoshwe mezani kutokana na sababu za uzee. Maalim Seif Sharif Hamad alikuwa kijana na mwenye umaarufu zaidi ndani ya CCM pamoja na NEC hivyo kulikuwa na kila aina ya fursa kwake kushinda uteuzi kwa kura nyingi kulinganisha na Mzee Idris Abdul-wakil na Salmin Amour . Kwa mshangao mkubwa baada ya kura kuhesabiwa, NEC ilitangaza matokeo kuwa Mzee Idris ndie mshindi katika uteuzi. Hapa ndipo wakati mgumu kwa siasa za Zanzibar ulipoanza. Kwani hata mwanachama wa ngazi ya chini sana wa CCM alifahamu kama uchakachauaji ulifanyika kumuengua Maalim Seif. Wazanzibari walikasirishwa na maamuzi ya kibabe ya CCM yasioakisi ridhaa zao.
Kiasi cha asilimia 37 tu ya wananchi wa mkoa wa Mjini maghrib ndio walimpa Mzee Idris kura za “NDIO”. Kwa upande wa kisiwa cha Pemba takriban watu wote walipiga kura ya “HAPANA” kuonesha hasira zao na kutokukubaliana na uteuzi wa Mzee Idris.”. Wimbi la hasira za kukataliwa Mzee Idris Zanzibar likanza kushika kasi na hali ya hewa ya Zanzibar kisiasa ikachafuka kwa kiwango cha hali ya juu. Baada ya CCM kuona hali imekuwa ngumu , Maalim Seif akaanza kusingiziwa kuwa ndie aliyejenga mazingira ya Mzee Idris kukataliwa na wazanzibari kwa kujizolea kura za “HAPANA”. Kwa kuwa hali ya kisiasa ilikuwa ngumu mno, Maalim Seif hakuweza kuepukwa na kupuuzwa. Nyerere akamshawishi Mzee Idris amteue Maalim Seif kuwa waziri kiongozi wake. Wazee walioitwa wanamapinduzi walilipinga vikali pendekezo hilo la Nyerere na wakamshauri Mzee Idris kumteua Salmin Amour kuwa waziri kiongozi badala ya Maalim Seif. Hata hivyo baada ya mazungumzo ya hapa na pale ya kujengeana imani kati ya Mzee Idris na Maalim Seif, na kwa ajili ya kulipunguza jotokali la kisiasa lililikwishatanda Mzee Idris akamteua Maalim Seif kuwa waziri kiongozi.

Na Ahmed Omar
Na Ahmed Omar
Sababu kubwa iliyopelekea Mzee Idris kukataliwa kabisa ni vile kutoweka kwa yale matarajio ambayo wazanzibari wengi walikuwa wameyaweka kwa Maalim Seif. Kwa upande wapemba nao waliamini kuwa zamu ya rais kutoka katika jamii yao ilikuwa imeshafika kwani tokea kufanyika kwa Mapinduzi hadi kuifikia hapo tayari maraisi watatu wa Zanzibar ndani ya awamu tatu, Mzee Karume, Maalim Aboud Jumbe na Mzee Ali Hssan Mwinyi wamekuwa wameshateuliwa kuongoza Zanzibar wote kutoka kisiwa cha Unguja pekee. Hivyo wananchi was kisiwa cha Pemba nao walikuwa na hamu na shauku kubwa ya kuona raisi anaefuata wa awamu ya nne anatokea Pemba ili kuonyesha upande huo wa pili wa Zanzibar haukutengwa katika kushika wadhifa huo mkubwa wa uongozi wa nchi. Wakati mazingira magumu ya kampeni ya Mzee Idris yakiendelea kutawala huko Pemba, Nyerere aliamua kufunga safari na kwenda kujionea mwenyewe hali hiyo na hivyo kutumia wadhifa wake na busara kuituliza hali hiyo. Kwa kuwa Nyerere aliyafahamu wazi madai ya wapemba alizungumza hivi katika moja ya mikutano yake ya hadhara huko Pemba: “kwa kuwa nafahamu kiu yenu (Pemba nayo kutoa rais) tutajitahidi na nawaahidini tutaweka mazingatio makubwa katika madai yenu katika awamu inayofuata”. Katika kauli yake hiyo alimaanisha watu wa kisiwa cha Pemba hawana budi kuvuta subira na kuyaunga mkono mapendekezo ya CCM kwa awamu hiyo ya nne lakini aliwahahakishia watu wa Pemba kwamba katika awamu inayofuata, yaani awamu ya tano, rasi atakaezingatiwa na CCM bila shaka atakuwa ni kutoka Pemba.
Kwa kuwa Nyerere hakuwa mkweli katika ahadi hiyo aliamua kuitumia mbinu ya kikoloni ya wagawe utawale na ufitinishaji baina ya waunguja na wapemba. Aliporejea Unguja akitokea Pemba na alifanya mkutano ili kulizungumzia suala hilo hilo kwa watu wa kisiwa cha Unguja. Nyerere alidhihirisha unafiki wa hali ya juu kwa kuwaeleza watu wa Unguja maneno ambayo ni kinyume kabisa na yale aliyowaahidi wapemba. Alilifanya hivi kwa lengo la kuwaridhisha wanamapinduzi bila ya kujali kuzuka kwa mgawanyiko kati ya wananchi wa visiwa viwili vya Unguja na Pemba. Nyerere aliwaambia hivi watu wa Unguja: “Waangalie wapemba eti wanataka raisi atoke kwao, sasa ikiwa kila mmoja atataka raisi wake wenyewe, vipi tutaweza kuongoza nchi hii?”. Kuthibitisha kuwa Nyerere alifikia maamuzi hayo kwa kuwatii na kuwaridhisha waasisi, wanamapinduzi, baada ya maneno yake hayo, siku iliyofuata aliitisha mkutano na waasisi na kuzungumza nao huku akiwa na kiwango kikubwa cha hasira. Nyerere aliwalaumu waasisi kwa kusababisha yote yaliyotokea. Kwa kauli ya Nyerere katika kikao hicho matatizo yote hayo ya migawanyiko baina ya wapemba na waunguja katika kumpata raisi wa nne wa Zanzibar yalitokana na itikadi potofu ya waasisi iliyojengeka ya kuogopa vivuli vyao wenyewe, yaani Wapemba.
Kwa kuwa waasisi hawakuupenda uteuzi wa Maalim Seif kuwa waziri kiongozi wakaamua kuzidisha chuki na vita vyao dhidi yake. Kila aina ya tuhuma wakazitoa ili kumpotezea umaarufu Maalim Seif ndani ya Serikali. Moja ya tuhuma zilizowahi kutolewa ni suala la ubadhirifu wa fedha za umma uliowahi kufanywa na viongozi wa serikali wakati wa utawala wa Jumbe. Serikali ya Jumbe iliwahi kuanzisha mradi wa shamba la mifungo huko Tanzania bara. Bahati mbaya kulifanyika ubadhirifu mkubwa wa fedha za mradi huo. Baraza la wawakilishi liliunda kamati maalum kuchunguza suala hilo na ndipo baadhi ya wazee wanamapinduzi kuonekana kuhusika na ubadhirifu huo. Kwa kuwa waasisi hawakuwa na kawaida ya kuitwa wakosaji, yaani kila ovu walifanyalo wao ni sawa na halihitaji kuhojiwa ndipo walipozua madai kwamba ripoti ya kamati hiyo ilikuwa ni mpango wa Maalim Seif wa kuwavunjia heshima na kuwadhalilisha.
Jina la Maalim Seif likazidi kuwa baya miongoni mwa waasisi pale walipompikia tuhuma za kuwapendelea wapemba katika utowaji wa nafasi za masomo ya elimu ya juu. Wanamapinduzi walizua madai kwamba Maalim Seif anawapendelea wapemba wenzake na kuwatenga watoto wa kiunguja katika utowaji wa nafasi za masomo ya elimu ya juu. Hii inawezekana sana kuwa tatizo haikuwa upendeleo kwa wapemba bali ni mazoea ya utamaduni wa awali wa kuwanyima wapemba fursa kama hizo . Hivyo basi Maalim Seif alipoamua kuuondoa utamaduni huo na kuleta utamaduni mpya wa “ufaulu kwa vigezo na uwezo” ambao haujazoeleka kwa wanamapinduzi ndipo walipohisi kuwa wapemba walikua wakipendelewa. Katika kitabu cha Race, Revolution and Struggle for Human Rights in Zanzibar, Maalim Seif anasema hivi kuhusu suala hili:
“Ukweli ni kwamba baadhi ya wanafunzi wa kiunguja walikuwa na utamaduni wa maisha ya kudekezana na hawakuwa wakijishughulisha sana na kusoma. Wanafunzi wa kipemba kwa upande wao walijua njia yao pekee ya mafanikio ni kujishughulisha na kusoma. Hivyo basi wazee wa wanafunzi wa kipemba walihakikisha watoto wao wanasoma kwa juhudi kubwa. Kilichojitokeza ni kwamba wanafunzi wa kisiwani Pemba walikuwa wanapasi zaidi kuliko wanafunzi kutoka Unguja. Hata hivyo lakini nafasi za masomo zikitolewa kwa asilimia 50 kwa 50 baina ya Unguja na Pemba na baadhi ya wakati tulitowa asilimia 55 kwa Unguja na 45 kwa Pemba kusudi kutoa upendeleo kwa Unguja” (Burgess 2009).
Wanamapinduzi pia walimtuhumu Maalim Seif kwamba ana mpango wa kuurudisha utawala wa kisultani Zanzibar. Maalim Seif alitupiwa tuhuma nzito za kupokea amri kutoka kwa waarabu na hivyo Zanzibar kuendeshwa kutokea Oman. Sababu ya tuhuma hizi inawezekana kuwa ni ule uhusiano mzuri baina nchi za kiarabu na serikali ya Zanzibar ambao ulishamiri wakati wa uongozi wa Maalim Sharif. Katika kipindi cha utawala wa Maalim Seif Zanzibar ilifanikiwa kuimarisha uhusiano mzuri kati yake na serikali ya Oman. Katika ziara ya Maalim Seif nchini Oman akiwa waziri kiongozi, Sultan Qabous Bin Said alisema wazi kwamba ana kila sababu ya kuisaidia Zanzibar kwa kiwango kikubwa kwa kuwa ni wasomi wa kizanzibari waliokimbia wakati wa mapinduzi ndio walioijenga Oman bila ya serikali ya Oman kuchangia chochote katika elimu zao (Burgess 2009). Maalim Seif na Sultan Qabous waliahidiana mambo mengi ya maendeleo kwa Zanzibar kama vile ujenzi wa viwanja vya ndege, kutanua miradi ya maji na ujenzi wa barabara.
Mwisho wa mwaka wa 1987, Maalim Seif akiwa bado ni waziri kiongozi alikwenda London kwa ajili ya matibabu na kurejea wanzoni mwa mwaka 1988. Kwa kuwa habari za kufukuzwa serikalini zilikuwa zimeshaanza kuzagaa wazanzibari walijitokeza kwa wingi huko Unguja kumpokea kupitia mkutano mkubwa wa hadhara hivyo kuonyesha uungaji wao mkono kwake. Huko Pemba makaribisho yalikuwa makubwa zaidi na ya aina yake. Wananchi walijitokeza kwa wingi mno katika uwanja wa ndege wa Pemba. Mapokezi hayo ya Pemba yalifuatiwa na maandamano makubwa na mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Tibirinzi Chake Chake ambapo Maalim Seif alitumi nafasi hiyo kuwapa wazanzibari ahadi ambayo bado hajaivunja hali leo hii. Maalim Seif aliwaambia hivi wazanzibari:
“Sina cha kuwalipa kwa imani kubwa mliyonionesha hata hivyo nawaahidi kuwa nitakuwa pamoja nanyi pindipo nitakuwa ndani serikali au nje ya serikali. Nitakuwa pamoja na nyinyi nikiwa ndani ya chama au nje ya chama”.
Wakati wa Seif Sharif kutolewa serikalini ukawadia. Mzee Idris bila shaka alipokea maagizo hayo na hivyo kulazimika kuyatii. Ghafla Idris alitangaza kulifuta baraza zima la mawaziri huku jeshi likiwekwa katika hali ya ulinzi mkali na kuwa tayari kwa hali yeyote. Baada ya siku nne alitangaza baraza jipya ambapo jina la Maalim Seif Sharif halikurejea. Habari za kutolewa serikalini Maalim Seif zikazagaa kila kona a nchi. Mrithi wa nafasi ya waziri kiongozi ilipangwa kuwa ni Marehemu Dr Omar Ali Juma. Dr Omar aliposikia fununu za kutaka kufukuzwa Maalim Seif na alikwenda kumuona Maalim Seif na kumwambia kwamba kuna habari kwamba unataka kutolewa serikalini na baadae nafasi hiyo nipewe mimi lakini mimi sitokubali kwani nikikubali ni kuwagawa wazanzibari. Tarehe 18 Januari mwaka 1988 ndipo alipofutwa rasmi wadhifa wa waziri kiongozi na Dr Omar Ali Juma akachaguliwa kuwa waziri kiongozi mpya bila kuikataa kama alivyoahidi kabla.
Baada ya Maalim Seif kutolewa serikalini wazanzibari walighadhibika mno na fujo kadhaa kuzuka. Makundi kwa makundi ya wananchi wakarudisha kadi za CCM na wengine kuzichana. Wengine walitengeneza sanamu za Nyerere hususan huko Pemba na kuziharibu hadharani kuonyesha hasira zao. Baada ya matukio hayo CCM ikaunda kamati ya kuchunguza chanzo cha matukiuo hayo iliyokuwa chini ya Mzee Rashid Mfaume Kawawa. Kamati hiyo iliibuka na ripoti kwamba Maalim Seif na wenzake sita walikuwa wakiwahamasisha wananchi waikatae CCM kufuatia kutolewa kwake serikalini. Halkadhalika ripoti hiyo ilidai kwamba Maalim Seif na wenzake walikuwa wakiwahamasisha wananchi kuubeza na kuukataaa muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa madai kwamba ndio unaopelekea matatizo yote hayo na kudhalilishwa kwa Zanzibar na kugawiwa kwa wazanzibari.
Baada ya ripoti ya Kawawa kukamilika kikao cha NEC Dodoma kikaitishwa ambapo tuhuma dhidi ya Maalim Seif na wenzake zilijadiliwa na maamuzi dhidi yao kutolewa. Miongoni mwa tuhuma hizo ni hizi zifuatazo:
• Maalim Seif alipoteza uaminifu aliopewa na chama na hivyo kukisaliti chama kwa maslahi yake binafsi.
• Maalim Seif baada ya kutolewa serikalini, alishirikiana na wenzake sita katika kuwashajihisha wananchi kukikataa chama cha Mapinduzi na kuubeza Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
• Maalim Seif alikuwa pachikizi la waarabu na hivyo kuiendesha Zanzibar kwa kupokea amri kutokea Oman. Mmoja wa wajumbe wa kikao hicho, Jamal Ramadhan Nasibu alidai mbele ya kiakao hicho kwamba ana ushahidi wa rekodi ya sauti inayomnakili Maalim Seif akipokea maagizo kutoka kwa Sheikh Ali Muhsin Al-barwany, mmoja wa viongozi waandamizi wa serikali iliyopinduliwa.
Pamoja na ushahidi juu ya madai yote hayo kukosekana, Nyerere aliwataka Maalim Seif na wenzake kujiuzulu nafasi zote za uongozi wa chama walizokuwa nazo. Maalim Seif na wenzake walikataa kujiuzulu kwa kuwa hawakuyaona makosa yao baada ya kikao kushindwa kuyathibitisha. Kwa kutumia nguvu zake za uwenyekiti Nyerere alitamka kuwavua uongozi na uwanachama huku wajumbe wakinyanyua mikono kuashiria kuunga mkono uamuzi wa Nyerere. Tukio hili lilifanyika katika usiku wa mwezi 27 Ramadhani ambao kwa mujibu wa dini ya kiislamu usiku huo una uwezekano mkubwa wa kupatikana lailatul-qadr.
Mara tu Seif Sharif alipowasili kisiwani Pemba akitokea machinjioni Dodoma makundi kwa makundi ya watu walikuwa wakikusanyika wakiwa na hamu na shauku ya kumuona shujaa wao na kiongozi wao. Kufuatia mapenzi hayo nya watu kwa kiongozi wao wanaempenda, Maalim Seif akashtakiwa kwa kosa la kufanya mikutano haramu. Katika kitabu cha historia ya maisha yake Maalim Seif anasema:
“Tunaweza tukasema ilikuwa mikutano haramu, lakini kama nilivyowaahidi watu hata nikiwa nje ya chama nitakuwa pamoja nao basi sikuweza kuwakimbia. Kila nilipopita kuanzia Wete mpaka Chake ilibidi nisimame nizungumze na watu vijijini” .(Burgess 2009).
Serikali ilijaribu kwanza kutaka kumshtaki Maalim Seif kwa madai kwamba ameiba nyaraka za serikali lakini ilishindwa kuthibitisha madai hayo. Hapo tena ndipo mashtaka ya kuitisha mikutano haramu yalipotumika. Maalim Seif alifungwa jela kwa kipindi cha miezi 30 kuanzia mwezi wa Mei 1989 hadi mwezi wa Novemba mwaka 1991.
Alipotoka gerezani ndipo safari ndefu ya kuung’oa utawala wa kidhalimu wa CCM ikaanza. Safari hiyo ikaungwa mkono na wazanzibari walio wengi hadi kupata mafanikio makubwa kwa CCM kukataliwa na wazanzibari wote na hivyo kubaki madarakani kwa mtutu wa bunduki. Baada ya Maalim Seif kupata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa Oktoba 2015 na CCM kutumia mtutu wa bunduki kulazimisha kubakia madarakani bado wazanzibari wanaonesha imani na mapenzi yao makubwa kwa Maalim Seif.
Inasemekana Maalim Seif anatakiwa kufika polisi siku ya Ijumaa ya tarehe 27/05/2016 kwa ajili ya mahojiano. Kwakuwa kauli kadhaa zimesikika za viongozi wa CCM wakilitaka jeshi la polisi kumkamata Maalim kwa makosa ya kufanya mikutano haramu wakati wa ziara yake kisiwani Pemba basi kuna kila dalili kuwa wito huo wa polisi ni kutekeleza matakwa hayo ya viongozi wa CCM. Hata hivyo ikumbukwe mashtaka kama haya yalitumika baada ya dhulma ya mwaka 1988 pale wazanzibari wenyewe walipokuwa wakijikusanya na kumlaki Maalim Seif makundi kwa makundi pale alipotembelea vijijini. Hakuna tofauti na ziara ya wiki iliyopita kisiwani Pemba. Maalim Seif hakusanyi watu bali wazanzibari tunajikusanya wenyewe kwa shauku yetu ya kumuunga mkono na kumuonesha tuko pamoja nae pamoja na dhulma anazofanyiwa na watawala madikteta.

No comments: