Jina la James Lembeli siyo jipya kwenye medani za siasa. Huyu ni moja ya wanasiasa waliopata umaarufu mkubwa katika kipindi cha ndani ya miaka 10 alichokaa bungeni akiwakilisha Jimbo la Kahama kwa tiketi ya CCM.Kwa takriban wiki moja, jina hilo limeteka vyombo vya habari baada ya kukacha kugombea ubunge kupitia chama hicho tawala kilichomlea tangu akiwa kijana kabla ya juzi kuhamia Chadema, kisha kutangaza kuwania ubunge katika Jimbo la Kahama Mjini. Mwanasiasa huyo ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira hadi hapo Agosti 20, alichaguliwa kuwa Mbunge wa Kahama mwaka 2005 na kutetea kiti hicho mwaka 2010.
Lembeli ni moja ya wabunge wa CCM watakaokumbukwa katika Bunge la tisa na 10 kwa michango yake mingi ya kujenga na hata kuikosoa Serikali yake moja kwa moja katika masuala mbalimbali yaliyoonekana bayana kuathiri wananchi.Ni moja ya wabunge ambao walionekana waziwazi kuichukia rushwa na ufisadi na ndiyo sababu ya misingi aliyoitaja kumkimbiza CCM.Kwa nafasi yake hiyo ya kuongoza kamati inayojihusisha na masuala ya ardhi, maliasili na mazingira, Lembeli alionekana kuwa mkali kwa Serikali hasa katika migogoro ya ardhi, ujangili wa wanyamapori na usafirishaji wa magogo.
Ikumbukwe kuwa mwaka 2013 alikuwa injini kuu ya uchunguzi wa sakata la uvunjifu wa haki za binadamu la Operesheni Tokomeza Ujangili uliofanywa na kamati yake na kuitikisa Serikali ya Rais Jakaya Kikwete.
Matokeo ya uchunguzi huo yalisababisha aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha, Waziri wa Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi, Dk Mathayo David Mathayo na Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki kujiuzulu.
Mbali na safari yake ijayo ya ubunge wa kutegemea ridhaa ya Chadema, hatua ya Lembeli kuhamia katika chama hicho cha upinzani huenda ikaongeza harakati zake za kupambana na ufisadi na kuleta maendeleo.
No comments:
Post a Comment