Friday 11 December 2015

Tujiulize kwa nini jeshi lipo mitaani Zanzibar ?

Watu wanajiuliza kwa nini wanajeshi hao wametawanywa mitaani ilhali Bara wanajeshi wameondoshwa mitaani baada ya kumalizika uchaguzi mkuu?

Mwenye kuweza kuwatuliza wananchi wa Zanzibar kuhusu suala hilo ni yeye Magufuli akiwa Amiri Jeshi wa majeshi yote nchini kwa kuamrisha kwamba vikosi vilivyopelekwa Zanzibar virudishwe Bara.

Asipochukuwa hatua za kuyatatua matatizo hayo ya Zanzibar Magufuli atakuwa anajitafutia uhasama wa bure na wengi wa Wazanzibari wanaotaka utawala wa kisheria uheshimiwa Visiwani. Huu si wakati wa kujipatia maadui zaidi ya wale walio katika uongozi wa CCM.

Hao viongozi wa CCM waliokaa kimya na wanaokerwa na miondoko yake ya uongozi hawana hila ila waendelee na kimya chao na labda waendelee pia kumperemba Magufuli na kutamani ajikwae.

Magufuli atafanya kosa kubwa akikipuuza kimya cha wasiomtakia yeye, na taifa, mema. Kimya chao ni cha shari na ni cha hatari. Ajue namna ya kupambana na wenye kimya hicho.

Kwa sadfa, Nyerere alitanguliza kijitabu chake kilichoushambulia uongozi wa Mwinyi kwa shairi kuhusu ukimya lililoandikwa na malenga wa mwambao wa Kenya, Muyaka bin Haji Ghassany (1776-1840). Inafaa Magufuli ayakumbuke maneno ya ubeti wa mwanzo wa shairi hilo:

“Kimya mshindo mkuu, ndivyo wambavyo wavyele

Kimya chataka kumbuu, viunoni mtatile

Kimya msikidharau, nami sikidharawile

Kimya kina mambo mbele, tahadharini na kimya!”

Baruapepe: ahmed@ahmedrajab.com

Chanzo: Raia Mwema

No comments: