Sunday, 10 January 2016

Ccm na Uhuni wake wa Zanzibar

“USANII” WA ZANZIBAR UPIGWE MARUFUKU!

Na. Julius Mtatiro,

Kati ya mambo muhimu yanayojadiliwa sana hapa nchini kwa sasa ni “mgogoro wa kisiasa Zanzibar”. Mgogoro huu si wa kwanza kusikika, ni mgogoro wa mwendelezo wa migogoro mingi iliyowahi kutokea huko nyuma na yote ikihusisha suala la haki ya kidemokrasia inayotokana na maamuzi ya wananchi kwenye uchaguzi. Wakati sisi tunajadili suala la Zanzibar kama mgogoro, ukweli ni kuwa kinachoendelea Zanzibar ni zaidi ya mgogoro, ni suala kubwa kuliko mgogoro na naweza kuliita “sakata la demokrasia kuwekwa mfukoni”.

Unajua kuna tofauti ya “mgogoro” (conflict) na “ukiukwaji wa demokrasia” (breach of democracy). Mgogoro ni ile hali ya kutoelewana baina ya pande mbili lakini ukiukwaji wa demokrasia ni ile hali ya upande mmoja kuhodhi mamlaka ya kidemokrasia juu ya wananchi na yule waliyemchagua. Kwa mtizamo wangu, kuita kinachoendelea Zanzibar kama “mgogoro” ni kujaribu kuweka kichwa kwenye mchanga huku mwili mzima uko nje. Zanzibar kuna “ubakwaji” mkubwa wa demokrasia, kuna “uchakachuaji wa wazi wa haki za wananchi” juu ya nini wameamua katika masanduku ya kura na jambo hili ni vyema likaeleweka hivyo, kutambulishwa hivyo na kujulikana hivyo, hatuna cha kuficha.

Ukosefu wa utashi wa kisiasa unaopelekea hali ya sasa ni jambo lililolelewa kwa muda mrefu sana, ni jambo mtambuka na lina mambo mengi ndani yake. Kuna dhana za kipuuzi sana zinaendelea miongoni mwa watu wengi kuwa Zanzibar haiwezi kuwa salama chini ya CUF, zamani wengi walisema haiwezi kuwa salama chini ya “Mpemba” na kuna wahafidhina wa CCM wamelifanya suala la Zanzibar kuwa propaganda yao kubwa kuwa “CUF ikiongoza itaiuza Zanzibar Uarabuni – kwa waarabu” huku wengine wakienda mbali zaidi na kujaribu kudanganya kuwa Zanzibar itakuwa kisiwa cha ugaidi ikiwa itaongozwa na CUF.

Dhana zote hizi ni za uongo, tena uongo wa mchana, ni dhana za “kujitekenya na kujicheka” hazina mashiko wala uthibitisho wowote wa kisayansi. Ni dhana zinazojengwa kila kukicha ili kuendelea kuisaidia CCM kupata uhalali wa kuendelea kutawala Zanzibar na kuinyima CUF uhalali huohuo.

Tulipokuwa kwenye Bunge Maalum la Katiba, dhana hizi potofu na za makusudi zinazopikwa chini ya wahafidhina wa CCM hazikujificha, zilionekana waziwazi zimekua na sasa kuna watu wanalazimisha ziaminiwe. Mjumbe mmoja (jina simtaji japokuwa hata wanaotaka video zake kwenye mitandao wanaweza kujionea) hakusita kusimama hadharani na kutamka kuwa “Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilipatikana kwa mtutu wa bunduki chini ya ASP (sasa CCM) na kamwe haiwezi kutolewa kwa makaratasi kwenda chama kingine (CUF)”.

Wajumbe wengi wa BMK hasa kutoka CCM Zanzibar walisimama na kushangilia kauli ile (iliyotolewa na mwanamama), waliona fahari kwenye maneno yale na waliona wametolewa kimasomaso. Kauli za namna hii zilikuwa zinatolewa “LIVE” na watanzania wote wanasikia na kuona. Halafu leo hii watu wanaporwa ushindi wao sisi tunaita ‘mgogoro’. Demokrasia inabakwa, inawekwa mfukoni, inachezewa, sisi tunaita “mgogoro”.

Huwa mara kadhaa nakaa na kutafakari, wale wanaodhani kuwa ni lazima CCM iondoke madarakani Zanzibar “kwa mtutu wa bunduki” ni watu wanaoishi karne ipi? Ni watu wa aina gani hawa? Hawaoni mambo yanayoendelea huko kwenye mitutu ya bunduki? Burundi, Afrika ya Kati, Somalia, Iraq, Syria n.k.

Nakaa na kumtafakari mwanamama yule mhafidhina aliyekuwa anakaukwa koo kwenye BMK kuwa ati ‘nchi haitoki kwa makaratasi’ najaribu kuwaza mwanamama yule anaziweza bunduki, ikianza kazi ya bunduki pale Zanzibar yule atakuwepo kweli? Si yeye anao uwezo hata wa kukodi “Coastal” na kutoroka na familia yake, je mwana CCM mwenzake wa kawaida, mvuvi, atawezaje hata kupata boti ya kukodi?

Itoshe kusema kuwa hali ile ya Zanzibar na wahafidhina wa Zanzibar inatia “hasira” na ikiendekezwa siku moja Zanzibar itatumbukia kwenye mchafuko makubwa.

Nchi huwa zinaingia kwenye machafuko kwa hatua, huwa hayaji ghafla kwa sababu mwanadamu ana tabia ya “huruma na subira” ndiyo maana mnaweza kukaa kwenye jamii matajiri watano na masikini elfu moja na bado masikini wakaishi kirafiki na matajiri, bila kuwadhuru.

Hii ni tabia ya mwanadamu, lakini tabia hiyo hubadilika pale madhila na manyanyaso yanapozidi kuwa makubwa, mwanadamu huweza kuwa katili kuliko mnyama anayekula nyama porini na huweza kufanya vitendo vya ajabu, mwanadamu si mtu mwenye subira pale anapokuwa amekosa mbinu ya kujinasua kwenye jambo ambalo anadhani ni haki yake, hapo huwa akifika ndipo unasikia “mtu kajilipua na mabomu” n.k. Mwanadamu anapokata tamaa hufanya lolote.

Uporwaji wa haki za kidemokrasia Zanzibar umechekewa sana, na kuna watu wanaamini kuwa Zanzibar itaendelea na matatizo hayo milele, ukweli ni kuwa lazima hatua zichukuliwe, wahafidhina wawekwe kando na Zanzibar iachwe ipige hatua.

Ni upuuzi wa hali ya juu kudhani kuwa kuna watu wana hati miliki na mamlaka na uongozi wa nchi na kwamba kuna watu hawana.

Zamani sana katika nchi nyingi mwanamke alichukuliwa kama kiumbe dhaifu na hata sensa zilipofanyika hakuhesabiwa, na wakati wa utumwa pia, mtumwa alionekana kama binadamu wa daraja la chini na hakupewa haki za msingi sawa na “bwana wake”, asingehesabiwa pia kwenye sensa na asingepiga kura kwenye uchaguzi kama ilivyokuwa kwa mwanamke (kwenye jamii nyingi), lakini kadri dunia ilivyokua ndivyo kila mtu alikubali kuwa mwanamke anao uwezo sana na mwanaume na anaweza kuwa kiongozi, anaweza kupiga kura na kupigiwa kura na anaweza hata kuendesha ndege.

Wakati dunia imeshakuwa na mtizamo mkubwa namna hii hata katika jinsia, kuna “wendawazimu” wachache pale Zanzibar wanaamini kuwa kuna wenzao “wanaume na wanawake” hawawezi kuongoza nchi na hawana haki ya kufanya hivyo. Ni kwa nini basi wawakokote watu hawa hadi kwenye uchaguzi wakashindane?

Kwa nini katiba ya Zanzibar isitengenezwe kwa namna ambayo itakiwezesha Chama Cha Mapinduzi peke yake kushiriki uchaguzi na kushinda na vyama vingine vikae pembeni? Kuna haja gani ya kushiriki uchaguzi wa mwaka 1995, 2000, 2005, 2010 na sasa 2015 kwa mfumo wa vyama vingi huku chama kimoja tu ndio kinajua “ni lazima kishinde”? Kwa nini haturudishi nchi kwenye mfumo wa chama kimoja?

Watu wakishapora uchaguzi ndipo wanaanzisha sababu za “kijinga” na “kuanzisha mazungumzo”. Yaani mnashiriki kwenye uchaguzi ambao mnajua mnaweza kushindwa, halafu mkishindwa mnakatalia madarakani kisha mnaanzisha “mazungumzo ya kutatua mgogoro”.

Kwamba unakuta vyama vinashiriki kwenye uchaguzi huku jengo la kutatulia mzozo linajengwa na viti vinanunuliwa na mapambo yanawekwa humo, mbinu za kupora uchaguzi kwa kura za wizi zikishindikana mnakimbia haraka kuharibu uchaguzi au kujitangaza kwa lazima ili mshikilie madaraka kwanza kisha muitane mezani na upande wa pili kuanza kutatua hicho kinachotwa “mgogoro”. Vitendo vya namna hii kama kuna mtu amekaa pembeni anaweza kuona kama “mchezo wa wendawazimu” au “vichaa’.

Haiwezekani watu wazima wenye akili timamu wakafanyiana vitendo vya namna hii, huku unashiriki uchaguzi huku unajenga msingi na kutengeneza akidi ya wajumbe wa kikao cha utatuzi wa mgogoro. Na tena hata kikao cha utatuzi wa mgogoro kinapofanyika unataka upewe ushindi wa mezani na kuendelea kuongoza, yaani wewe uko kwenye ‘win win situation’ muda wote.

Kwa namna siasa za Zanzibar zinavyozidi kuendekezwa ndivyo Wazanzibari kina mama na kina baba wanazidi kukata tamaa na kuwepo kwa mfumo wa demokrasia ya vyama vingi katika visiwa hivyo. Kinachotokea baada ya kukata tamaa ni kuingia katika machafuko ambayo nayo mwishoni hutatuliwa kwa meza za mazungumzo.

Ni wakati muafaka sasa kuiacha demokrasia ichukue mkondo wake na kutoendekeza vitendo vinavyoendelea Zanzibar katika kila uchaguzi, haki kuporwa na demokrasia kuwekwa mfukoni huku kumbi za kutatua kile kinachoitwa “mgogoro” zikiwa zimeshaandaliwa miezi kadhaa kabla ya uchaguzi, tuache “unafiki” huu ili Zanzibar ipige hatua. Na tukome kuita “ukiukwaji wa demokrasia” kama “mgogoro”.

Migogoro tusiingizie uchuro huu wa kutengeneza kutokana na “uroho wa madaraka uliopitiliza” na ulio tayari kuona watu wetu wanaingia kwenye vita ya wenyewe kwa wenyewe au wanaishi kwa uhasama na chuki ilimradi sisi tuko madarakani daima dumu, jambo ambalo kihistoria haliwezekani.

(juliusmtatiro.com).

No comments: