Thursday, 28 January 2016




Faida na hasara za CUF kushiriki uchaguzi wa marudio Zanzibar – Uchambuzi Maalum


Na. Julius Mtatiro

UTANGULIZI

Zanzibar imeshiriki uchaguzi wake wa tano wa kitaifa Jumapili ya tarehe 25 Oktoba 2015. Vituoni wananchi walipanga foleni na kupewa karatasi tano za kupigia kura, karatasi za udiwani, uwakilishi, ubunge, urais wa Zanzibar na Urais wa Muungano. Hiyo ni tofauti na kura tatu zilizopigwa Tanzania bara kwa madiwani, wabunge na rais.

Kwa mujibu wa taarifa aliyoitoa mgombea urais wa Zanzibar kupitia CUF/UKAWA, Maalim Seif Sharif Hamad; “…Hadi kufikia asubuhi ya tarehe 26 Oktoba, matokeo ya majimbo yote 53 ambayo yalifanya uchaguzi wa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi yalitangazwa na Wasimamizi wa Uchaguzi na kuwapatia shahada za kuchaguliwa wale wote walioshinda. Pia, uchaguzi wa madiwani ulikamilika na kupatiwa shahada katika Wadi zote zilizofanya uchaguzi…”.

Wakati tarehe 28 Oktoba siku ya mwisho kisheria kutangaza matokeo ya urais ikikaribia, mambo mengi yalijitokeza njiani. Mathalani tarehe 27 Oktoba Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Jecha Salum Jecha aliahirisha zoezi la kutangaza matokeo kwa madai ya kuwa na shinikizo la damu.

Siku ya tarehe 28 Oktoba ambayo kwa mujibu wa Sheria ndiyo ilikuwa siku ya mwisho ya kutangaza matokeo, Mwenyekiti huyo hakuonekana kabisa katika kituo cha kutangaza matokeo katika Hoteli ya Bwawani lakini baadaye aliibukia mahali kwingine na kutoa tangazo la kufuta matokeo ya uchaguzi.

Wakati Jecha anafuta uchaguzi na matokeo yake tarehe 28 Oktoba, tayari tume yake ilikuwa imeshatangaza matokeo ya kura za Urais kutoka katika majimbo 31 kati ya 54; na ilishakamilisha kujumlisha matokeo ya majimbo mengine 9 (ambayo ilikuwa bado haijayatangaza). Kwa maana hiyo, kazi ya kujumlisha na kuhakiki matokeo ya majimbo 40 kati ya majimbo 54 ilikuwa imekwishakamilika.

Ukisoma sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar na Katiba ya Zanzibar, hakuna kipengele hata kimoja kinachomruhusu Mwenyekiti huyo kujifanyia maamuzi yake na kuyatangaza lakini pia hakuna kifungu cha katiba kinachomruhusu Rais Shein kuendelea na madaraka baada ya kutimiza miaka mitano bila kibali cha Baraza la Wawakilishi.

Baada ya siku 57 (takribani miezi miwili) ya majadiliano na vikao vya Maalim Seif (kwa upande mmoja) akiwakilisha CUF na Rais Shein akiwa na Balozi Seif Ali Idd na marais wastaafu wa Zanzibar (kwa upande mwingine), hakuna muafaka uliopatikana. CCM imeendelea kushinikiza uchaguzi urudiwe na CUF imeendelea kudai matokeo yakamilishwe na mshindi atangazwe.

Tarehe 23 Januari 2016, yule yule aliyevuruga uchaguzi wa Zanzibar, Jecha Salum Jecha akajitokeza hadharani na kutangaza kuwa Uchaguzi wa Marudio lazima ufanyike na akaitaja tarehe 20 Machi 2016 kama tarehe rasmi ambayo uchaguzi huo utafanywa.

Tayari Chama Cha Wananchi CUF kimo kwenye tafakuri nzito inayoambatana na vikao vya kuamua ikiwa ishiriki kwenye uchaguzi huo wa marudio au la!

Uchambuzi huu unaangazia faida tano muhimu za CUF kushiriki kwenye uchaguzi huo na hasara tano za ushiriki wa chama hicho.

FAIDA 5 ZA CUF KUSHIRIKI MARUDIO YA UCHAGUZI ZANZIBAR;
Faida ya kwanza ya CUF kushiriki uchaguzi wa marudio wa Machi 20 ni “Kuionesha dunia ukomavu wa kisiasa hata mahali ilipoporwa haki”. ‘Ukifuatilia historia ya CUF kwenye siasa za Zanzibar lazima utajiridhisha kuwa chama hicho kimekuwa mstari wa mbele kuvumilia mawimbi ya kisiasa tangu mwaka 1995.

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wa kitaifa na kimataifa wanaeleza kwa ushahidi kuwa CUF haijawahi kushindwa uchaguzi Zanzibar hata mara moja. Inaonekana CUF hushinda uchaguzi lakini huzidiwa mbinu za “kidola” na wenzao na mara zote hizo CUF ilitumia busara kubwa zilizoendelea kulinda ustawi wa Zanzibar.

Busara hizo na utulivu wa CUF kwa miaka 20 sasa bado unaweza kuoneshwa na kukifanya chama hicho kiendelee kuwa miongoni mwa vyama vilivyokomaa na kujiongoza kwa busara kubwa barani Afrika.

Faida ya pili ambayo CUF itaipata kwa kushiriki uchaguzi wa tarehe 20 Machi 2016 ni “Kuepuka athari za CCM kujitwalia madaraka yote’. Ikumbukwe kuwa asili ya CCM katika chaguzi hata ndogo sana huwa ni mapambano ya kufa na kupona.

Ikiwa CUF haishiriki kwenye uchaguzi huo ni sawa na “kumuachia nyani shamba la mahindi” atakula mahindi atakavyo na bila kuzuiwa na mtu! Kwa uzoefu wa Zanzibar pia, CCM na CUF viliwahi kuingia kwenye mgogoro wa namna hiyo na CUF ilipokataa kushiriki kwenye uchaguzi ndipo CCM ikapata mwanya wa kufanya itakavyo, ikashinda majimbo yote na kuchukua uongozi wa nchi.

Faida ya tatu ya CUF kushiriki uchaguzi wa tarehe 20 Machi ni “Kuepuka CCM kuvitumia vyama dhaifu kuhalalisha matokeo ya uchaguzi”. Tayari zipo taarifa za wazi kwamba aliyekuwa mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya ADC, Hamad Rashid Mohamed anajipanga kwa nguvu kushiriki kwenye uchaguzi wa marudio bila kujali kwamba kuna uvunjifu mkubwa wa demokrasia umekwishafanyika.

Hamad Rashid anajua kuwa katiba ya Zanzibar inampa mwanya wa kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais kwani chama chake kinayo nafasi ya kupata ushindi wa pili hata kama ni kwa asilimia moja ya kura. Na kwa wanaomfahamu Hamad Radhid wanajua kwamba hashindwi kufanya analotaka linapokuja suala la kutafuta madaraka. Jambo hilo limeshaleta mgogoro wa wazi na kukivuruga chama cha ADC.

Vyama vingine kama AFP n.k navyo vinajipanga kushiriki kwenye uchaguzi wa marudio. Kutoshiriki kwa CUF kuna maana ya kuipa mwanya CCM kuvitumia vyama hivi kuhalalisha ubatili. Hali ya namna hii pia imewahi kutokea kwenye nchi kadhaa ikiwemo Burundi ambako pamoja na upinzani kususia uchaguzi ulio kinyume na katiba, chama tawala kiliendelea na uchaguzi na kikabaki madarakani.

Faida ya nne ni kwa CUF kushiriki uchaguzi wa marudio wa Machi 20 ni “Kuhakikisha wananchi wa Pemba na Unguja wanakuwa na uwakilishi thabiti”. Tunakubaliana kuwa tayari CUF ilikuwa imejijenga mno kwenye siasa za Zanzibar hivi karibuni.

Taarifa zinaonesha kuwa kati ya majimbo 54 ya uchaguzi CUF tayari ilishinda wawakilishi kwenye majimbo 27. Idadi hiyo ya ushindi inamaanisha chama hicho kinao mtaji mkubwa sana kwa siasa za uchaguzi wa mwaka 2020.

CUF ikiamua kushiriki uchaguzi huu bado itakuwa na uuwezo wa kushinda majimboyale 27 na huwenda kuongeza mengine mawili au matatu. Mipango binafsi ya maendeleo ya CUF kwa wananchi hasa katika visiwa vya Pemba itakwama ikiwa CCM itachukua majimbo yote kwani bajeti zinapaswa kupitishwa na Baraza la Wawakilishi na kutekelezwa na serikali.

Baraza likijaa wawakilishi wa CCM hawatatenda haki kwenye majimbo ambayo ni ngome za CUF kwa miaka mitano ijayo, kama sehemu ya kulipiza kisasi na kuishughulikia CUF.

Na faida ya tano ambao CUF itaipata ikiwa itafanya uamuzi wa kwenda kwenye uchaguzi wa tarehe 20 Machi ni “Kuiepusha Zanzibar na mgogoro mkubwa zaidi kuliko huu wa sasa”. Huko nyuma CUF ina kumbukumbu nzuri na migogoro iliyowahi kutokea na namna ilivyokuwa inatatuliwa.

Mgogoro mkubwa zaidi uliwahi kuwa ule wa mwaka 2001 ambapo zaidi ya wanachama 100 wa CUF walidaiwa kuuawa na vyombo vya ulinzi na usalama katika oparesheni maalum iliyoamriwa. Kama CUF ikiamua kurejea kwenye uchaguzi huo wa Machi itapata faida ya kuiepusha Zanzibar na machafuko makubwa kwani uzoefu unaonesha kuwa ni kawaida kwa upande wa pili “CCM” kuwa tayari kwa “lolote lile lije” inapofikia wakati chama hicho kikajua kuwa kuna kitisho cha wao kuondolewa madarakani kidemokrasia.

HASARA 5 ZA CUF KUSHIRIKI MARUDIO YA UCHAGUZI ZANZIBAR;

Hasara ya kwanza ambayo CUF itaipata kwa kushiriki kwenye uchaguzi ulioitishwa na Jecha wa ZEC ni “Kusaidia kubariki mchakato batili”. Wanasheria na wataalamu mbalimbali wamethibitisha kwamba mchakato wa uchaguzi wa Zanzibar uliofanyika tarehe 25 Oktoba 2015 ulikuwa huru, halali na wa haki.

Vyombo mbalimbali vya kimataifa, waangalizi wa uchaguzi wa ndani na nje ya nchi waliokuwa Zanzibar kufuatilia mchakato wa uchaguzi wamethibitisha kwenye ripoti zao kuwa uchaguzi ulikuwa huru na haki. Na hata nakala za matokeo yaliyotangazwa ngazi za chini kwenye udiwani, uwakilishi, ubunge, urais wa Zanzibar na ule wa Muungano zinaonesha hakukuwa na kasoro zozote.

Kilichofanywa na Jecha na “waliomtuma” ni “uhuni” wa hali ya juu na maamuzi yoyote ya CUF kushiriki uchaguzi wa marudio yatatafsiriwa na wadau wa demokrasia, utawala bora na haki duniani kama kukubali na kubariki tendo batili. Hii ni hasara kubwa sana kisiasa.

Hasara ya pili ya dhahiri ambayo CUF itaipata ikishiriki uchaguzi wa marudio ni “Kuporwa ushindi”. Kwenye hili wala haihitajiki akili ya Chuo Kikuu kufikiri. Ni uzubaifu wa kiwango cha Shahada ya Uzamivu (PhD) kujidanganya kuwa CUF inaweza kushinda uchaguzi wa marudio, siyo kwamba wapiga kura walioichagua tarehe 25 Oktoba 2015 hawapo, la hasha, wapo tele!

Lakini uchaguzi huu wa marudio unafanywa kwa lengo moja tu “CCM ishinde”, itashindaje? hilo litajulikana wakati ZEC ile ile itakapokuwa inatangaza matokeo ya kumpa ushindi Dk. Shein. Moja ya sababu zilizofanya CCM ianguke Zanzibar kwenye uchaguzi wa Oktoba 25 ni kupoteza muda wake wote ikipambana kuokoa jahazi kwenye Urais wa Muungano na wabunge wa Muungano.

Hata kabla ya uchaguzi ule wa kitaifa wengi wetu tulijua CCM ikifanikiwa “kubana” urais wa Muungano, lazima “ingeliachia” uchaguzi wa Zanzibar, siyo kwa kupenda bali ni kwa sababu haiwezekani ikalinda kote kote kwa siku moja.

Hadi Jecha anaibuka tena kutangaza marudio ya uchaguzi tayari CCM imeshajipanga na inajua itakwenda kushinda namna gani. Kama CUF itafanya uamuzi wa kurudi kwenye uchaguzi huu itakuwa inaisindikiza CCM kwenye ushindi wa lazima.

Hasara ya tatu ambayo CUF itaipata ikiwa itashiriki uchaguzi wa marudio wa Machi 20 ni “Kupoteza uungwaji mkono wa wanachama kabla na baada ya kushindwa”. Kabla ya kushindwa ni tarehe za sasa hadi 19 Machi (siku moja kabla ya uchaguzi); Ikiwa CUF itafanya uamuzi kuwa inarejea kwenye uchaguzi bila shaka baadhi ya wanachama wake wapenzi watawaona viongozi wao kama “wasaliti wakubwa” na watu waliokosa misimamo.

Hadi kufikia CUF kupigiwa kura nyingi namna ile kwenye uchaguzi wa Oktoba 25 ilikuwa ni juhudi za wanachama, wapenzi na wananchi. Kama leo ushindi umeporwa halafu viongozi wanakaa vikaoni kuwaelekeza wanachama warejee kwenye uchaguzi, natabiri kuwa zaidi ya robo ya wanachama na wananchi wa kawaida ambao hukipigia kura chama hicho wataona hawakutendewa haki na hawatakwenda vituoni kupoteza muda.

Baada ya uchaguzi wakati ambapo CCM itakuwa imeshajitangaza CUF itabaki na majeraha makubwa na kazi ya kuwajenga upya wanachama, wapenzi, wafuasi na wananchi waliopigania Oktoba 25 itachukua hata nusu muongo.

Hasara ya tatu itakayojitokeza kwa CUF ikiwa itafanya uamuzi wa kurejea kwenye uchaguzi wa Machi 20 ni “Kulea kansa isiyopona hata kwenye chaguzi zijazo”. Katika siasa na sheria kila uamuzi unaofanyika unatengeneza mazingira ya uamuzi wa namna hiyo kufanyika mbele ya safari.

Kama mwanao anauawa na watu unaowajua kisha unaamua kuwasamehe na kutowachukulia hatua za kisheria, upo uwezekano mkubwa “wakaja kuua mwanao mwingine au ndugu yako”, hiyo ni kanuni ya asili. Kwa miongo takribani miwili CUF imekuwa mwathirika mkubwa wa siasa za Zanzibar na kila ilipojiingiza kwenye mazungumzo yoyote mwisho wa siku CCM ndiyo ilinufaika.

Mazungumzo ya kipekee ambayo yalifanikiwa ni yale ya Maalim Seif na Rais Karume ambayo yalizaa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (GNU). Ikiwa unaporwa uchaguzi ulioshinda kihalali halafu unarudi kwenye uchaguzi ulioitishwa kinyume cha katiba na sheria na tena unasimamiwa na “wavurugaji” wale wale, ina maana wewe unajiandalia mazingira yatakayokuathiri mbele ya safari – huko nako, waliokupora ukarudi kushiriki “haramu” zao wataendelea kukupora hata baada ya miaka 100. Dawa ya udhalimu ni kuukataa moja kwa moja na bila kupepesa macho. Ukiukubali lazima uwe tayari kupokea madhara yake.

Hasara ya tano kwa CUF ikiwa itaamua kurejea kwenye uchaguzi wa Machi 20 ni kujenga taswira ya “Kushirikiana na CCM kupora haki na maoni ya wananchi na kupoka utawala wa kidemokrasia”.

Kwa sababu CCM haina shida kuonekana kama chama kinachotumia dola na nguvu kuongoza, CUF ikishiriki uchaguzi itakuwa inajitengenezea tawira mbaya sana, taswira hii haitaisha leo au kesho, itadumu na itawavunja moyo wananchi waliokiunga mkono chama hicho – kwamba chama walichokiamini wakakipigia kura nyingi kikaporwa ushindi kimerudi na kushirikiana na waporaji kupoka demokrasia na sauti za wananchi kwa ajili labda ya wakubwa kugawana vyeo serikalini.

Hili ni jambo hatari zaidi kwa chama chochote cha siasa ambacho kina malengo ya muda mrefu.

HITIMISHO

Kiongozi mwandamizi wa Chama cha Republican atokaye jimbo la “Carolina Kaskazini” Bi. Virginia Foxx amewahi kusema “If we do not make tough decisions now, future Americans will have to make even tougher ones”. Kiswahili; (Kama hatufanyi maamuzi magumu hivi sasa, Wamarekani wa baadaye watalazimika hata kufanya maamuzi magumu zaidi).

Wosia wa mwanamama huyu unawakumbusha viongozi wa Tanzania na Zanzibar kwa ujumla kuwa kama hawatafanya maamuzi ya msingi na yanayoumiza kwa kiasi kinachopaswa kuwa sasa, huwenda Watanzania na Wazanzibari wa siku zijazo wakafanya maamuzi magumu zaidi.

Kumbe basi maamuzi ya sasa huathiri sana kizazi cha leo na kesho na leo yasipofanywa maamuzi magumu, tunajenga hatari kwa kesho ambako yanaweza kufanyika magumu zaidi na yenye athari kubwa zaidi.

Kwa sababu CCM ndiyo imeshikilia kila kitu Zanzibar (Mpini) na CUF haina madaraka na mamlaka juu ya Zanzibar, ni wakati muafaka sasa ikiwa CCM imeshindwa kufanya maamuzi ya kidemokrasia ili kuondoa hatari kubwa za mbele – CUF iwajibike kuchukua maamuzi magumu ili iondoe hatari kubwa zaidi zinazoweza kuikabili Zanzibar mbele ya safari.

Kazi ya kupambana na CCM ni sawa na kupambana na “mtu aliyejifunga mabomu ya kujitoa mhanga”, yeye yuko tayari kufa, wewe umevaa vikinga risasi, unamsogelea!

Nawatakia kila la heri CUF katika kufikia maamuzi ya vikao vya kitaifa juu ya jambo hili lakini watambue kuwa uamuzi wowote ule una faida na hasara zake – wao jukumu lao ni kufanya uamuzi sahihi kwa wakati sahihi.

Uchambuzi huu umechapishwa kwenye Gazeti la Mwananchi la Jumatano 27 Januari 2016 – Julius Mtatiro Simu: +255787536759, Tovuti:www.juliusmtatiro.com, Email; juliusmtatiro@yahoo.com).


No comments: