Friday 22 January 2016

Kwa la Zanzibar, Rais Magufuli hawezi kujifanya hahusiki.

Shamis Alkhatry's photo.
Kwa la Zanzibar, Rais Magufuli hawezi kujifanya hahusiki.
Na Awadh Ali Said.
Makala ya Mheshimiwa Pius Msekwa, Spika wa zamani wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hapana shaka kada mkubwa wa Chama tawala cha Mapinduzi (CCM), iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii katika siku za hivi karibuni inatoa wito wa kuwepo mjadala wa wazi juu ya madaraka ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusiana na masuala ya Zanzibar.
Kwenye makala hiyo, Msekwa ametoa hoja kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hana madaraka ya kuukwamua mkwamo wa kisiasa na kikatiba ambao ulichochewa na kinachosemekana kuwa ufutwaji wa Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar uliofanyika tarehe 25 Oktoba 2015. Sababu anayotoa ni kuwa Uchaguzi wa Zanzibar si suala la Muungano na kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hawezi kuingilia yale aliyoyaita "mambo ya ndani" ya Zanzibar; na kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ana madaraka kwa Zanzibar juu ya yale Mambo ya Muungano tu.
Baadaye anahimitimisha kuwa wale wanaomtarajia Rais huyo kuingilia kati na kuutatua mkwamo huo hawauelewi hasa muundo wa kipekee ya Muungano kati ya Zanzibar na Tanganyika na hilo, anasema, ndilo lililomsukuma atowe ufafanuzi ili watu wajielimishe juu ya muundo huo wa kipekee wa Muungano huu. Anaendelea kuwakumbusha watu wote juu ya umuhimu wa kuheshimu Katiba na kutoa indhari dhidi ya wale wote wanaomtolea Rais wito wa kuingilia kati, maana kufanya hivyo kutakuwa sawa na uvunjwaji wa Katiba.
Kwa kusoma hoja zake, unapata picha ya wazi kwamba kwa hakika Msekwa yuko kwenye mpango maalum ya kumkingia kifua Rais John Pombe Magufuli dhidi ya shinikizo la kimataifa ambalo limemuelemea. Msekwa analionesha suala la MCC kama mfano. Ninasikitika kwamba hoja anazozitoa zina upotoshaji mkubwa sana na zinakosa uhalali wowote wa kikatiba.
Lakini kabla ya kuuelezea upotoshaji wenyewe, ningelipenda kukubaliana naye kwenye nukta moja aliyoitoa; kwamba uchaguzi si suala la Muungano. Hii ni kweli kabisa na inathibitishwa kutokana na ukweli kwamba kila upande wa Muungano una sheria zake tafauti za uchaguzi (Sheria ya Uchaguzi Na. 11 ya Mwaka 1984 kwa Zanzibar na Sheria ya Uchaguzi Na. 1 ya Mwaka 1985 kwa chaguzi za Tanzania Bara na zile za Jamhuri ya Muungano) na kila upande wa Muungano una chombo chake wenyewe cha kusimamia chaguzi hizo (Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kwa Zanzibar na Tume ya Uchaguzi ya Taifa kwa chaguzi za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na za Tanzania Bara). Ni kutokana na ukweli huo, kwa hakika, ndio maana palizuka mjadala mkali kwenye Baraza la Wawakilishi mwaka jana baada ya kuwasilishwa kwa Sheria ya Kura ya Maoni iliyotungwa makhsusi kabisa kwa ajili ya kuipigia kura ya maoni Katiba Inayopendekezwa, hoja ikiwa vipi sheria juu ya uchaguzi/kura ya maoni iliyopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaweza kufanya kazi pia Zanzibar!
Wajumbe wa Baraza hilo kutokea Chama cha Wananchi (CUF) waliipinga sheria hiyo kwa msingi kwamba uchaguzi na kura ya maoni si mambo ya Muungano na, kwa hivyo, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania halikuwa na madaraka ya kuitanua hadi Zanzibar sheria yoyote liliyoitunga juu ya mambo yasiyo ya Muungano. Walihoji kwamba kura ya maoni si jambo la Muungano na kwamba Zanzibar ina sheria yake yenyewe juu ya uendeshaji wa kura ya maoni (Sheria ya Kura ya Maoni Na. 6 ya Mwaka 2010). Hadi leo, Tanzania Bara haina sheria yoyote juu ya uendeshaji wa kura ya maoni.
Kwa hivyo, hoja ya Msekwa ingelikuwa na maana na ya muafaka zaidi kwa wakati huo. Lakini hapo asingesema kwa kuwa sheria hiyo ilikuwa na manufaa kwenye lengo kubwa zaidi la kuyahodhi madaraka na mamlaka yote ya Zanzibar- kwa njia za hadaa - na kuyafanya kuwa mambo ya Muungano na hatimaye kuiacha Zanzibar pangu pakavu au bufuru tupu. Huu ni mradi wa muda mrefu ambao unaendelea kwa kasi maalum iliyopangwa. Hata hivyo, kwenye hili la mara hii Tanzania Bara inaelekea kuumia, ndio maana anatoa ufafanuzi huu wa kikatiba unaopotosha. Hapa nitaelezea kwa nini ufafanuzi wake unapotosha.
Kwanza, chaguzi zote za kisiasa nchini Tanzania ni miliki ya vyama vya siasa pekee. Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1997 na Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984, hakuna mtu yeyote anayeruhusiwa kugombea nafasi yoyote ya kisiasa nchini Tanzania mpaka awe mwanachama na awe amepitishwa na chama ambacho kina usajili wa kudumu. Masuala yanayohusiana na Usajili na Uendeshaji wa vyama vya siasa ni jambo la Muungano na, kwa hivyo, hayawezi kuachiwa Zanzibar kama suala lake la ndani kama anavyoliita Msekwa. Sheria iko wazi sana kwenye hili: vyama vya kisiasa lazima viwe vya kitaifa. Japokuwa tuna chaguzi tafauti Tanzania Bara na Zanzibar, lakini zote zinagombewa na vyama vile vile vya kisiasa ambavyo viko chini ya madaraka ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hilo linamtwisha kiongozi huyo jukumu la moja kwa moja kwa Zanzibar. Kwa hakika, hata kisiasa Rais Magufuli hawezi kujitenga kando na kinachofanywa na chama chake visiwani Zanzibar, maana ikiwa rais anadhibiti vyama vya kisiasa, basi pia anahusika na shughuli zote za vyama hivyo ukiwemo uchaguzi, ambao ndio sababu hasa ya vyama vya siasa kuwepo.
Pili, ingelisaidia sana kujuwa Msekwa anautafsiri vipi uchaguzi, kwa sababu uchaguzi ni mchanganyiko wa mambo mengi sana na sio upigaji kura pekee. Takribani shughuli zote za uchaguzi, kama vile usajili wapigakura, upigaji kampeni na mengineyo, zinakwenda sambamba na suala la amani na usalama. Ni pande mbili za sarafu moja na haziwezi kutenganishwa. Amani na Usalama ni jambo la Muungano na liko chini ya madaraka pekee na ya mwisho ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa mfano, jeshi lililoripotiwa kukikizingira Kituo cha Kutangazia Matokeo Bwawani lilikuwa chini ya amri ya Rais wa Muungano ambaye ni Amiri Jeshi Mkuu. Jeshi la Polisi lililoripotiwa kutoweka na Makamu Mwenyekiti wa ZEC (ambaye pia ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar) na kumuweka kizuizini kwa masaa kadhaa, liko chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano. Kwa hivyo, ni vigumu kuelewa ni vipi Rais kama huyo anaweza kutenganishwa na uchaguzi wa Zanzibar!!!
Tatu, uchaguzi kwenye dunia ya sasa ya kidemokrasia ni njia ya kujipatia heshima ya kimataifa na sifa mbele ya walimwengu. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndiye Mkuu wa Dola ambaye jukumu lake ni kuhakikisha kwamba taswira ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haichafuliwi kimataifa, ama iwe uchafuzi huo unatokana na jambo la Muungano au jambo lisilo la Muungano kutoka upande wowote wa Muungano huu. Tusisahau kwamba Mahusiano ya Kimataifa ni jambo la Muungano. Ikiwa heshima ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaathirika kimataifa, si hoja wala si kinga kuwa kilichopelekea hilo ni jambo lisilo la Muungano lililochimbukia Zanzibar.
Kwa ujumla, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ana majukumu matatu makubwa ya kikatiba: Mkuu wa Dola, Amiri Jeshi Mkuu na Kiongozi wa Serikali/Baraza la Mawaziri la Jamhuri ya Muungano. Kwenye majukumu yake mawili ya kwanza, ana dhamana kwa kila kinachotokea Zanzibar, ama kiwe cha Muungano au kiwe si cha Muungano. Katika majukumu hayo mawili HAKUNA MGAWANYIKO baina ya Mambo ya Muungano na Mambo yasiyo ya Muungano. Mgawanyiko unakuja kwenye jukumu la tatu tu.
Vile vile, kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa nafasi yake kama Amiri Jeshi Mkuu amekabidhiwa vyombo vyote vinavyohusika na usalama wa Dola. Ndiye mwenye dhamana ya Jeshi, Polisi na Usalama wa Taifa, dhamana ambayo inamuweka kwenye nafasi ya kipekee ya kuijuwa kila hatua inayochukuliwa kabla, wakati na baada ya uchaguzi visiwani Zanzibar. Hakuna hata mmoja mwengine mwenye njia za kuyajuwa majalada yote juu ya uchaguzi wa Zanzibar kuliko Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hiyo ndiyo sababu Rais huyo ana wajibu wa kisheria na kimaadili wa kuukwamua mkwamo wa Zanzibar; hawezi kuwa mpitanjia au mkando tu. Kinyume chake ni kuwa kama atachaguwa kujifanya hajali na hayamhusu, basi atakuwa anajiweka mwenyewe kwenye nafasi ya kuhusishwa na hujuma ya kiwango cha juu.
Kimakosa, Msekwa anajaribu kutumia Katiba kumkingia kifua Rais Magufuli dhidi ya miito ya kimataifa inayomtaka aingilie kati mgogoro visiwani Zanzibar kwa kutumia madaraka yake kama Mkuu wa Dola na Amiri Jeshi Mkuu. Jaribio lolote la kuiharibu njia ya kutoka kwenye mkwamo uliopo nyumbani na kuwa tayari kutatua migogoro ya nchi jirani, kama vile Burundi, visiwa vya Comoro na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, litaweza tu kutupa uwelewa usiopendeza wa aina ya uongozi tulionao.
Mwisho, ningelipenda kumalizia kwa kumnukuu Msekwa kwenye makala yake iliyochapishwa mwaka 1994 chini ya mada iliyosomeka "Historia Pambanuzi ya Mfumo wa Serikali Mbili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania" pale aliposema kwa usahihi kabisa kwamba:
"Athari ya jumla ya matamko haya ya Kirais ni kwamba Tanganyika kwa hakika iliamuriwa kutokuwepo, na Tanganyika ya zamani ikajipatia hapo hapo hadhi, madaraka na kazi za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambapo Zanzibar ikasalia kama Zanzibar. Ilikuwa ni aina ya mabadiliko ya kimiujiza ambapo ghafla Tanganyika iligeuzwa (kwa Sheria/Dikrii zilizonukuliwa hapo juu) kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; badala ya kubakia kuwa mshirika sawa wa Zanzibar kwenye Muungano huu mpya. Matokeo ya moja kwa moja ya Tanganyika kujichukulia hadhi na majukumu ya Jamhuri ya Muungano kisheria, ni kuwajibika kwake kubeba gharama zote za Muungano, na ndiyo maana inaichukulia Zanzibar kama MGENI MWALIKWA kwenye Muungano huu. Hali isiyokuwa ya kawaida hata kidogo ikawa imetengenezwa!"
Chini ya msingi wa kile kiitwacho Jukumu la Mwenyeji/Mkaliaji katika Sheria ya Madhara (Tort) , daima Mwenyeji au Mkaliaji ana wajibu wa kisheria wa kuhakikisha usalama wa mgeni wake. Sasa je, kwa kuzingatia hali iliyopo Zanzibar kwa muktadha wa nukuu hiyo hapo juu, hivi haitoshi kumbebesha MWENYEJI/MKALIAJI huyo wajibu wa kuhakikisha usalama wa MGENI wake?
TANBIHI: Mwandishi wa makala hii, Awadh Ali Said, ni Wakili wa Mahakama Kuu ya Zanzibar, Kamishna wa zamani wa Tume ya Mabadiliko ya Mpya na Rais wa zamani wa Chama cha Wanasheria cha Zanzibar.
Makala imetafsiriwa na Mohammed Ghassani kwa idhini ya Mwandishi.

No comments: