DK. SHEIN HAJUI JINSI YA
KUKUMBUKWA DAIMA?
Dk. Mohamed Shein hajui jinsi ya kuandika historia isiyofutika. Hajui. Angekuwa anajua asingekuwa ameng’ang’ania kiti cha urais aliopoteza miezi mitatu iliyopita.
Katika mazingira tuliyomo, Dk. Shein aweza kusema na kutenda – kwamba:
1. Asilazimishwe kuwa rais Zanzibar wakati anajua kuwa hakushinda. Aachie.
2. Asichonganishwe na umma wa Zanzibar kwa kitu kinachopita; tena kwa kasi. Aachie.
3. Asifanywe kondoo wa kafara kwa madai ya kulinda umoja wa Chama Cha Mapinduzi (CCM). Aachie.
4. Asifanywe chanzo cha mfarakano mkuu na hata umwagaji damu; eti kwa kuwa analinda uhai wa CCM Visiwani. Aachie.
5. Asifanywe kinga ya wachochezi wa ubaguzi wa rangi na asili ya watokako. Aachie.
6. Asifanywe mjinga, mpuuzi na mroho wa madaraka; kumbe wanaomsukuma ndio wenye maslahi mapana; hata ya kifisadi. Aachie.
7. Asipoteze hadhi yake ya kisomo na utendaji katika kipindi chake chote cha uongozi; vyote vikaonekana kuwa si kitu. Aachie.
8. Asifanywe kuwa mtu asiye na uwezo wa kufikiri – kuona, kusikia na kutenda inavyopasa – kwa mtu mstaarabu na mweledi. Aachie.
9. Asifanane na walafi wa kale na kale wasemao hawawezi kuachia madaraka kwa madai kuwa hawajaona “mwingine anayefaa.” Upuunzi mtupu. Nani amewatafuta na kuwakosa. Aachie.
10. Asishindwe kuona mikono lukuki ya historia ikiwa imekunjuliwa, tayari kumpokea Dk. Shein na kumweka kwenye nafasi yake anayostahili na hata kuenziwa. Aachie.
11. Asikatae kushiriki kazi kuu ya kuepusha migogoro na hata vita; na papohapo kuwa balozi wa amani kutoka Tanzania, Afrika Mashariki na Afrika. Aachie.
12. Asipoteze nafasi hii adimu ya kuwa kiongozi mwingine katika Afrika asiyeenda kwa nguvu za ulafi na tamaa isiyoelezeka ya ufalme wa kisiasa – angalia: Uganda, Kongo, Burundi, Rwanda, Zimbabwe – wengi tu. Wanataka na wanajigamba kuwa watafia kwenye kidonda kama inzi. Aachie.
13. Afahamu kuwa siyo kila wakati mihula ya utawala wa kisiasa huenda kwa hesabu za miaka. Anaweza akaingia leo akatoka kesho – kwa sababu mbalimbali nje ya uwezo wake, uwezo wangu; na bado nchi ikaendelea kuwapo. Aachie.
14. Afahamu kuwa maisha ya watu wa Zanzibar na Tanganyika, ndio muhimu zaidi kuliko maslahi ya CCM, viongozi wake maslahi yake binafsi. Aachie.
15. Ajue kuwa atakuwa mtu huru; anayetembea kifua wazi, anayeheshimika na anayepigiwa mfano; kuliko kutumiwa kama chambo au kichocheo cha vurugu, mifarakano na hata ukimbizi na umwagaji damu (kama ilivyowahi kuwa). Aachie.
Tutamwona wa hekima, heshima; na jasiri atendaye kwa manufaa ya wananchi wake na taifa lake; hata dunia yake. Akatae kuwa mkuki wa kuchomea wanaotafuta mwafaka kwa njia iliyokubaliwa kitatiba na kisheria – Uchaguzi. Aitikie sauti ya wapigakura wa Zanzibar. Ndio waamuzi wa kweli na pekee. Aachie ngazi .
Tanzania ya wapenda amani na utulivu itambeba. Afrika itamuenzi. Historia itamwandalia makao ya furaha kwa uhai wake wote uliosalia. Hata baada ya kifo chake – na kwa imani yake – roho yake itawekwa mahali panapostahili – bila shaka karibu na watu wake ambao atakuwa amekatasa kusaliti.
Inawezekana. Huu ndio ufalme kuliko wa kinyang’au wa “sinzia nikumalize!” Dk. Shein upo?
No comments:
Post a Comment