Wednesday 10 February 2016

Huwezi kuwa na uchaguzi huru bila tume huru ya uchaguzi.

Hivi karibuni tumemsikia Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya  Uchaguzi, Jaji Lubuva akieleza kuwa uhuru wa Tume unapimwa kwa jinsi Tume husika inavyoendesha uchaguzi bila kuingiliwa, na kwamba Tume yake ni huru kwa vile haijawahi kuingiliwa. Ni wazi kuwa kauli hii ni ya utetezi dhidi ya mtazamo wa wale wanaosisitiza kuwa bado Tanzania haina Tume Huru ya Uchaguzi na Tume iliyopo pamoja na Sheria za Uchaguzi vimesanifiwa kiulaghai ili kuwa muokozi wa kudumu wa Chama Tawala. Kauli hii pia imelenga kuokoa haiba na taadhima inayotegemewa kuwa nayo kwa mtu wa stahiki yake ili kujikosha na muonekano kuwa yeye ni mtumishi wa Chama Tawala kupitia Taasisi ya Umma inayotegemewa kutenda haki bila upendeleo.

Pamoja na kumuelewa hivyo, lakini kauli yake ile ni ya kisikitisha sana. Nasema hivi kwa sababu ukiachilia mambo mengineyo, siamini kama Jaji Lubuva haelewi kuwa uhuru wa Tume ya Uchaguzi unapimwa kwa vigezo maalum vilivyokubaliwa kimataifa. Na hivyo ni wazi kuwa kauli yake ile ililenga  kuwaondoa watu katika vigezo na vipimo na kuwapotosha kuwa uhuru wa Tume ni kutoingiliwa na kwamba Tume yake haiingiliwi katika kufanya maamuzi. Kabla hatujenda kwenye vigezo tuanze na hili la Tume kuingiliwa. Najiuliza sisi kama wananchi tuna fursa gani ya kujua usahihi na ukweli wa kauli kuwa Tume haiingiliwi?  Hili ni suala la kuthibitisha kiushahidi (evidential question)  Au tutosheke kwa sababu imesemwa na Mwenyekiti, ndio iwe kuntu? Pamoja na kupenda kuamini kuwa kuna umri katika maisha ya mwanadamu ambapo huwa tunategemewa tuwe wakweli lakini tumeona mengi ya kinyume chake na hivyo umri pia si kigezo cha kusema ukweli. Pengine lililo sahihi ni kuipima kauli yake na ushahidi wa kimazingira (circumstantial evidence) juu ya uendeshaji wa shughuli za Tume ili tuone kuwa akili zetu za kawaida zinatusukuma tuamini kuwa kweli Chombo hichi kiko huru na hufanya maamuzi kwa kufuata katiba na sheria bila utashi wa kisiasa. Tujiulize, hivi kwa nini kila uchao malalamiko yanazidi (badala ya kufifia) kuwa Tume sio huru ila ni Kitengo cha Uokozi cha Chama Tawala?

 Ukweli ni kuwa malalamiko ya msingi sio Tume kuingiliwa. Malalamiko ni kuwa Chama Tawala kupitia nguvu za Kiserikali katika kufanya uteuzi huwa zinawapandikiza watiifu, wafuasi na waumini wa Chama hicho kiasi ambacho kuaminiwa kwao ni kukubwa na hakutiliwi shaka na wala haitokei haja ya kuingiliwa kwavile wao ni sehemu yao na wanajua malengo yao na watatimiza wajibu wa kuyalinda kwa umahiri mkubwa bila hata kuingiliwa. Vipi utamuingilia kati mchezaji mwenzako wa Timu moja? Endapo wachezaji na muamuzi wote wanatoka Timu moja kuna haja ya muamuzi kuingiliwa? Si anajua kazi yake? Si atatimiza wajibu wake? Na hili hufanywa kwa usanifu na ubobezi wa hali ya juu. Halifanywi kiholela. Tumesahau? Si hivi karibuni tu tulimuona aliyekuwa Makamo Mwenyekiti wa Tume hiyo hiyo "iliyo huru" akiibuka hadharani na Kadi ya Chama Tawala akigombea uteuzi wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Tawala. Huyu pia aliwahi kuwa Makamo Mwenyekitu wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC.) Aliwahi pia kuwa Jaji Mkuu wa Zanzibar na Jaji Mkuu wa JMT. Nafasi ambazo kisheria na hata kimaadili hazimruhusu kuwa mwanachama wa Chama cha Siasa. Hivi huyu wakati huo akiwa madarakani alikuwa anategemewa kuingiliwa? Si anajielewa!!! Katika hali hii tuna uhakika gani kama na Mwenyekiti wa sasa wakati ukifika hatojaribu bahati yake naye?

Tumesahau? Aliyewahi kuwa Msajili wa Vyama vya Siasa Tanzania , Jaji Liundi , mara baada ya muda wake wa kuwa Msajili kumalizika alichomoa kadi yake ya Chama Tawala na kugombea uteuzi wa kuwa mgombea ubunge. Hivi huyu naye alitegemewa kuingiliwa. Si anajielewa yupo pale kwa malengo gani. Na orodha hii ni refu sana , tusijichoshe kwa hili. Itoshe kusema hoja hapa sio kuingiliwa, hoja ni kuwa watu wanapandikizwa kukitumikia Chama Tawala katika Taasisi kadhaa na huku wanafanya usanii kuwa wako huru hawaingiliwi. Hivi Mhariri wa gazeti la Chama  cha siasa huwa anaingiliwa kupewa maelekezo katika majukumu yake? Si anaelewa kazi zake kuwa ni kupiga propaganda ya kusukuma mbele maslahi ya Chama chao.

Tukirudi kwenye hoja ya msingi kuwa uhuru wa Tume haupimwi kwa kauli ya yoyote kuwa ama  Tume ni huru au si huru. Hili sio suala "subjective" . Uhuru wa Tume unapimwa kwa vigezo makhsusi.
Tume ya Uchaguzi ni chombo cha kufanya maamuzi. Vyombo hivi, kama ilivyo mahkama, huundwa kwa namna ambayo huaminiwa na wadau kuwa viko huru na haviwezi kuwa na upendeleo. Kwa hivyo kigezo cha kwanza na cha msingi ni namna gani UTEUZI wao unafanyika. Mchakato wa uteuzi unatakiwa uwe huru na wa haki, wa wazi na ulio shirikishi. Sasa Jaji Lubuva atueleze yeye binafsi yake anaridhika kuwa uteuzi wake na wa wajumbe wenzake umekidhi kigezo hicho? Waliteuliwa kwa uhuru na haki? Kwa utaratibu upi? Kwa nini ni wao na sio wengine. Wengine walipata fursa ya kuomba nafasi hizo? Kwa nini hawakupata? Jee uteuzi wao ulikuwa wa wazi (transparent) au mtu mmoja tu alijifungia na akaibuka na majina yake? Jee mchakato wa uteuzi ulikuwa shirikishi? Uteuzi huu ulishirikisha mamlaka na taasisi nyenginezo? Kwa mfano hata katika uteuzi wa Majaji , Mamlaka ya Uteuzi hupokea majina kutoka Taasisi nyenginezo kama Tume ya Utumishi wa Mahkama ambayo ina uwakilishi mpana wa wadau wa sekta ya sheria. Jee hilo lipo katika uteuzi wa Tume ? Yote hayapo. Na bado tuamini kuwa chombo hicho ni huru kweli!!!

Katika kuondokana na kasoro hii ya msingi Rasimu ya Katiba Mpya (maarufu kama Rasimu ya Warioba) ilipendekeza utaratibu wa wazi na ulio shirikishi katika uteuzi wa Tume. Kwanza Rasimu iliweka sifa za kitaaluma zinazotakiwa kwa Wajumbe. Ikaweka utaratibu kuwa kila aliye na sifa awe na uhuru wa kuomba  nafasi anayotaka. Ikaunda Kamati ya Uteuzi itayoshirikisha Majaji Wakuu na Maspika na wengineo. Baada ya uteuzi kufanyika ikaweka utaratibu wa Bunge kuwajadili na kuwathibisha. Hatimaye Rais kama Mkuu wa Nchi anafanya uteuzi. Na huu ni utaratibu unaofuatwa na Nchi kadhaa zilizowafiki dhamira ya kuwa na Tume Huru. Huwezi kuteuliwa kisirisiri  na mtu mmoja tu ambaye naye ni mgombea mtarajiwa, na Chama chake kina wagombea kwa chaguzi zote, halafu ukajitia hamnazo na ubabaifu ukasema uko huru huingiliwi. Upo msemo wa kisheria unaosema haki sio tu kuwa itendeke ila ionekane na kuridhisha kuwa haki imetendeka (Justice should not only be done but should be seen to be done) Ndio maana hata huko Mahkamani ni mwiko kwa Jaji au Hakimu kuamua kesi ambayo muhusika/mshtakiwa ana ujamaa au ukaribu naye. Sababu ni kuwa hata atende haki namna gani bado macho ya jamii yataona kuwa pale iliyotawala sio haki bali ni ule ukaribu au ujamaa. Uswahilini huwa tunasema Jaji Msomali, Mwendesha Mashtaka Msomali, Shahidi Msomali, Wakili wa Utetezi Msomali,  mashtaka yanayokukabili ni kukashifu mila za Kisomali, Mshtakiwa tu ndio Mswahili. Hapo hata haki itendeke namna gani bado hofu itatawala kuwa kulikuwa na upendeleo na haki haikutendeka. Hili halitoshi kumfanya Jaji muadilifu kutamka ukweli!!! Akasema "Kwamba ni kweli mimi binafsi siingiliwi lakini uteuzi wangu haujengi taswira ya kuwa niko huru; badala yake naonekana, tena kwa sababu za kweli, kuwa napendelea kwa vile mteuzi wangu naye ni mchezaji pia,  hivyo hata nikisema hilo sio goli na ukweli ni kuwa sio goli kweli, lakini mashaka ni kuwa nimeteuliwa na mchezaji mmoja peke yake". Hata ujasiri wa kuweka bayana hilo hatuna!!! Ujenzi wa jamii inayofuta haki inatulazimisha tuwe wakweli , angalau kwa vile vitu vya msingi kabisa, ambapo tunapovipiga chenga tunajivunia dharau mbele ya macho ya jamii. Tusiukwepe ukweli na kushadidia ubabaishaji na upotoshaji kwa kulinda maslahi binafsi ya muda mfupi. Itatuchukua miongo mingi kupiga hatua ndogo endapo wale waliopewa nafasi za ushawishi katika Taasisi zao wataamua kuwa vibaraka na mawakala wa mfumo ambao tunajua fika kuwa ni wa kuikandamiza demokrasia.

Kigezo chenginecho cha Tume Huru ni uhuru wa rasilimali fedha iliyonayo Tume husika. Tume ambayo kila uchao watendaji wake wanasota kwenye mabenchi ya Wizara ya Fedha na pengine hata Mwenyekiti naye ifike hadi kumuona Rais ili kufikisha kilio cha ukata, hiyo si Tume huru. Tume huru huwa na kasma yake na inakuwa na uhuru wa kifedha (financial independence) na haipigi magoti kwa yoyote. Hichi nacho ni kigezo muhimu cha uhuru wa Tume.

Kigezo chengine ni kuwa na wafanyakazi wake wenyewe wa kutosha na ikawa wanawajibika kwa Tume na wala sio Mamlaka nyengine, kusimamia shughuli za uchaguzi. Katika mazingira ambayo Tume inategemea wafanyakazi wa Serikali, ambao kimsingi ni watiifu kwa Serikali ya Chama kilicho madarakani, hasa ukizingatia mazingira ya kisiasa yanayotawala sekta ya utumishi wa umma, huwezi hujinasibu kuwa Tume hiyo ni huru na haiingiliwi.

Kigezo chengine cha uhuru wa Tume ni namna ambavyo Umma au wadau wako huru kuhoji matendo au maamuzi ya Tume. Tume iliyoundwa katika  misingi ya kuipa hifadhi na kinga na kuifanya iko juu ya kila kitu na haiwezikuhojiwa haiko huru bali inalemazwa na kubweteka kutokana na kiburi cha kuwa hamna anayeweza kuirudisha kwenye mstari. Tume ya Uchaguzi ya Taifa bado ni miongoni mwa Tume chache duniani ambazo maamuzi yake hayahojiwi popote. Ibara ya 74 (12) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania ya 1977  inasomeka hivi :

"Hakuna mahakama yoyote itakayokuwa na mamlaka ya  kuchunguza jambo lolote lililotendwa na Tume ya Uchaguzi katika kutekeleza madaraka yake kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii."
Kifungu kama hicho , neno kwa neno, kipo pia katika Ibara ya 119 (13) cha Katiba ya Zanzibar ya 1984.
Kigezo chengine cha uhuru wa Tume ni namna gani shughuli zote za Tume zinavyofanywa kwa uwazi (transparency) na kushirikisha  wadau wote (inclusivity)  wa masuala ya uchaguzi.

Kwa ufupi, suala la kama Tume ni huru au laa halitegemei kabisa kauli tata za wanaojitetea. Uhuru wa Tume ni suala "objective" na lina vigezo na taratibu zake katika kuliamua. Kwa mfano ukimleta mtaalam na kumpa kazi ya kutathmini uhuru wa Tume hatoshughulishwa na kauli za wahusika , yeye atachoangalia ni vigezo vya utaratibu wa uteuzi wa wajumbe na watendaji  wake, kinga waliyonayo wajumbe, uwazi katika shughuli zake, mazingira mepesi ya kuhoji matendo yake na maamuzi yake, uwezo na uhuru wa kujiendesha kifedha na kujitosheleza katika rasilimali watu na mengineyo na sio kauli za utashi za yoyote.

Awadh Ali Said.
Wakili, Mahkama Kuu Zanzibar.
Rais Mstaafu wa Chama cha Wanasheria Zanzibar.
Aliyekuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

No comments: