Tuesday 2 February 2016

Mazombi’wa CCM wadaiwa kufanya vurugu Unguja

Hali ilivyokuwa baada ya kuvunjwa vibanda
Hali ilivyokuwa baada ya kuvunjwa vibanda
Zanzibar. Watu wasiojulikana juzi walivamia maeneo ya Barabara ya Magogoni, Wilaya ya Mjini Unguja na kuvunja vibanda vya biashara, kuharibu mali na kupiga watu ovyo.Mmoja wa walioathirika katika tukio hilo, Shaaban Juma ambaye ni mmiliki wa banda la biashara ya matunda na kioski cha vocha za simu alisema licha banda lake kuharibiwa, aliporwa mali zake.“Nimevunjika moyo na nimechoka kabisa, nahisi kuishiwa nguvu maana hatujui wapi pa kukimbilia na nani wa kumpelekea kilio chetu cha dhuluma hii,” alisema.
Watu walioshuhudia tukio hilo, walisema watu hao maarufu kama ‘Mazombi’ wakiwa na bunduki, mapanga, mikuki na mashoka walivamia mitaa ya Magogoni na Msumbiji na kusababisha uharibifu mkubwa wa vibanda vya biashara na viwanda vya useremala.

“Tuliwaona walikuja na yaleyale magari ya vikosi ambayo yalikuwa yakirandaranda hapa tangu usiku wa saa mbili hivi,” alisema Omar Said Juma (34) mkazi wa Kwa Mtumwajeni. Waandishi wa habari waliofika eneo hilo jana walishuhudia milango kadhaa ya maduka ya biashara ikiwa imevunjwa, hujuma iliyodaiwa kutekelezwa na wahalifu hao.
“Tuliarifiwa na walinzi waliokuwepo wakati huo lakini tulikuwa hatuna la kufanya maana hao jamaa walikuwa ni kama Serikali nzima na kila aina ya silaha, alisema Mohamed Omar (46) mkazi wa Msumbiji ambaye alidai meza yake ya kufanyia biashara ilivunjwavunjwa.
“Huu sasa ni ukatili… hali inatisha,” alilalama Juma Hassan (25) mkazi wa Jang’ombe ambaye ni miongoni mwa walionusurika kipigo kwa kutimua mbio alipoona gari lenye sura ya kijeshi likisimama karibu naye na watu waliofunika nyuso kuanza kutembeza kipigo.
Mmoja wa wajumbe wa Shehia ya Nyerere, jirani na mitaa hiyo, Mussa Juma alisema amepata habari za mikasa hiyo lakini hakubaini mara moja nini kilitendeka. Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Mkadam Khamis Mkadam alisema aliarifiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Magharibi kwamba itatekeleza azma ya kubomoa mabanda yaliyopo katika maeneo yasiyohusika.
Zombie2
“Waliniarifu hivi karibuni kwamba wangelifanya hivyo kwani hilo ni eneo linalowahusu (halmashauri) ila sina habari juu ya hayo mabanda mengine ya biashara, sijaenda lakini tunafuatilia,” alisema.
Alipoulizwa kwa nini azma hiyo itekelezwe usiku alisema, “sasa hivi nakwenda Kibele (Wilaya ya Kati Unguja) lakini nikirudi tutafuatilia, tunaweza kuwasiliana.”
Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Magharibi, Mussa Mohamed alisema licha ya kuwa eneo hilo limo katika ramani yao lakini hadhani kuwa waliotekeleza hatua hiyo ni watu wa ofisi hiyo.
“Sikuwepo wakati huo lakini sijui zaidi ya hivyo nilivyosema ila tuache maana hii hali inatatanisha,” alisema Mussa.
Chanzo: Mwananchi

No comments: