TAARIFA YA WAJUMBE WAWILI WA TUME YA UCHAGUZI YA ZANZIBAR (ZEC) KWA WAANDISHI WA HABARI ILIYOTOLEWA LEO JUMAPILI TAREHE07/02/2016, LAMADA HOTEL - DAR ES SALAAM.
1.0 Utangulizi
Ndugu Waandishi wa habari,
Kwanza kabisa tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia kukutana hapa leo tukiwa katika hali hizi nzuri. Kisha tunawashukuru nyinyi, kwanza kwa kuitikia wito wetu wa kuhudhururia katika kikao hiki kwa siku ya leo, lakini pili ni kwa kuwa kwenu mstari wa mbele kuwapasha habari na kuwaelimisha wananchi juu ya taarifa muhimu kuhusu hali ya Zanzibar.
Sisi Ayoub Bakari Hamad na Nassor Khamis Mohammed ni Wajumbe wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kwa mihula miwili sasa. Muhula wa kwanza ulikua ni ule wa mwaka 2008 -2012 na muhula wa pili ni 2013 – 2018. Katika muhula ule wa mwanzo Tume iliongozwa na Mh. Khatibu Mwinchande, ambapo tuliendesha na kusimamia Kura ya Maoni ya 2010 na pia Uchaguzi Mkuu wa 2010 ambao ndio uliomuweka Dr. Ali Mohammed Sheni madarakani.
Ni vyema kukumbushia japo kwa uchache juu ya muundo wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ambayo ina wajumbe saba akiwemo Mwenyekiti. Kifungu cha 119 (1) cha katiba ya Zanzibar ya 1984 kinaeleza kuwa Mwenyekiti wa Tume atakua ni mtu mwenye sifa za kuwa Jaji wa Mahkama Kuu au ya Rufaa katika nchi yoyote ya Jumuiya ya Madola au mtu anayeheshimika katika jamii. Mjumbe mwengine atatoka miongoni mwa Majaji wa Mahkama Kuu. Mjumbe wa tatu atateuliwa na Rais kama atakavyoona inafaa. Wajumbe wawili watateuliwa kutokana na mapendekezo ya Kiongozi wa shughuli za Serikali kwenye Baraza la Wawakilishi na wajumbe wawili watateuliwa kutokana na mapendekezo ya Kiongozi wa Upinzani katika Baraza la Wawakilishi au iwapo hakuna Kiongozi huyo basi atashauriana na vyama vya siasa.
Muundo huu wa Tume umezingatia ushirikishaji wa vyama vyenye uwakilishi ndani ya Baraza la Wawakilishi au kutoka kwa vyama vya siasa. Vyama vya siasa kupewa nafasi katika Tume hii hakuifanyi Tume hii kuendeshwa kisiasa, kwani Wajumbe wake wote wanatakiwa kufuata Katiba na Sheria za Uchaguzi katika kuendesha shughuli za Tume bila ya kujali ni mlango gani uteuzi wao ulitokea.
Kifungu hicho cha 119 (10) cha Katiba ya Zanzibar pia kinazungumzia Akidi ya vikao vya Tume kuwa ni Mwenyekiti au Makamo Mwenyekiti na Wajumbe wengine wanne. Pia kinaeleza kuwa KILA uamuzi wa Tume ni LAZIMA uungwe mkono na Wajumbe waliowengi. Kwa hivyo maamuzi yoyote ya Tume ni yale tu yanayotokana na Kikao halali cha Tume.
2.0 YALIYOJIRI KATIKA UCHAGUZI WA TAREHE 25 OCTOBA, 2015
Ndugu waandishi wa habari,
Zanzibar pamekuwa na matukio mengi yanayotokana na Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, 2015. Kuna matukio yaliyotokea kabla ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar Mh. Jecha Salim Jecha kutangaza kuufuta Uchaguzi huo siku ya tarehe 28 Oktoba 2015 na kuna matukio baada ya kutangaza kuufuta Uchaguzi huo. Matukio hayo yamekua ni sinema isiyoisha na hivyo kuyafanya yavutie watu wengi, ndani na nje ya nchi yetu. Tunaamini kwamba tunao wajibu wa kuyaeleza na kuyatolea ufafanuzi kwa wananchi ili waweze kuelewa nini kilichotusibu na nini khatma ya Nchi yetu huko mbeleni.
Ndugu Waandishi wa habari,
Ni vyema mkaelewa kuwa sisi hatukuwahi hata mara moja kuzungumza na vyombo vya habari wakati wa ile Tume ya Mh. Mwinchande. Kwa mara ya kwanza tulitoka hadharani tarehe 28 Oktoba 2015 kuutangazia umma kuwa tangazo la kufuta Uchaguzi Mkuu na matokeo yake ni la Mwenyekiti peke yake na hivyo ni batili, kwani sisi kama Tume hatukukaa kikao chochote kufikia uamuzi huo. Leo itakua ni mara yetu ya pili kuja hadharani, tumeufikia uamuzi huu kwa kuzingatia sababu kuu tatu zifuatazo:-
1. Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, peke yake, amekuwa akitoa taarifa za ndani za Tume na baadhi ya wakati taarifa hizo zinashutumu baadhi ya Wajumbe kwa kukosa maadili juu ya dhamana walizopewa. Huu ni upotoshaji ambao tunaona sasa ni wakati muafaka kuusemea.
2. Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar sasa imewacha kuamua mambo kwa vigezo vya Katiba na Sheria, na badala yake inaamua kwa utashi wa kisiasa. Jambo hili halikubaliki katika chombo chochote kinachotakiwa kuchunga na kutoa HAKI.
3. Hali inaashiria kuwa tunakoelekea hali ya Zanzibar inazidi kuwa tete, hivyo tunao wajibu wa kueleza wazi msimamo wetu ili wananchi wauelewe na kama kuna hatua zakuchukuliwa na wahusika zichukuliwe mapema kabla ya kutokea kwa athari kubwa ambazo zinaweza kuepukika.
3.0 KIINI CHA MGOGORO
Ndugu Waandishi wa habari,
Siku ya Oktoba 25, 2015 ilikuwa siku ya kupiga kura. Wananchi walijitokeza kwa wingi, katika hali ya amani na utulivu kwenda kupiga kura. Baada ya hapo, wananchi walitoa nafasi kwa Tume ya Uchaguzi kuhesabu kura zao na hatimaye kutangaziwa matokeo yao kwa mujibu wa Sheria. Zoezi la kupiga kura, kuhesabu kura na kutangaza matokeo lilifanyika chini ya uangalizi wa mawakala wa vyama na hatimaye waliweka saini zao katika fomu husika. Kwa hivyo, kila Mgombea makini wa kila nafasi aliweza kujua matokeo yake ya Uchaguzi huo sio zaidi ya asubuhi ya tarehe 26 Oktoba 2015.
Siku ya 26 Oktoba, 2015 nyakati za mchana, Chama cha Mapinduzi kilileta barua kwa Tume ya Uchaguzi na nakla za barua hio kwa Wajumbe wote wa Tume kueleza malalamiko yao pamoja na kuitaka Tume iurejee Uchaguzi Mkuu wote. Wakati barua hio inaletwa kwa Tume, Tume ya Uchaguzi ilikuwa tayari imeshatangaza pamoja na kutoa vyeti kwa washindi wote wa nafasi za Uwakilishi pamoja na Udiwani zilizoshindaniwa kwa mujibu wa Sheria. Vile vile Tume ilishabandika kwenye kuta matokeo yote ya Urais katika ngazi ya vituo vya kupigia kura na ngazi ya majumuisho ya majimbo yote 54 ya Zanzibar. Siku ya tarehe 26 mchana, Tume ilikuwa imo katika shughuli ya kuhakiki na kuyatangaza matokeo ya Uraisi mbele ya Mawakala wa Wagombea Urais na Waangalizi wa Uchaguzi.
Malalamiko hayo ya Chama Cha Mapinduzi yalizingatiwa ipasavyo katika kikao cha Tume cha tarehe 26 Oktoba 2015. Baadae kazi ya kuhakiki na kutangaza maokeo ikaendelea. Siku ya tarehe 27 Oktoba 2015, asubuhi, Mwenyekiti aliitisha tena kikao na akaleta ajenda tatu zijadiliwe. Ajenda hizo ni:-
1. Kuijadili kwa mara nyengine barua ya malalamiko ya ccm ya tarehe 26 Oktoba 2015.
2. Kujadili taarifa alizozisikia mitaani kuwa kuna Mgombea wa Urais amejitangazia matokeo yake.
3. Kujadili tena taarifa ya Wajumbe wawili wa Tume waliokwenda Pemba kuchukua fomu za matokeo ya Urais.
Kikao kilikaa na kuamua maamuzi yafuatayo juu ya kila hoja:-
1. Juu ya malalamiko ya ccm, kikao kiliamua kuyatupilia mbali malalamiko hayo kwani ushahidi uliowasilishwa kuthibitisha malalamiko hayo ulikua ukihusiana na Uchaguzi wa Wawakilishi, ambao kimsingi ulishakamilika na haukuhusiana na Uchaguzi wa Rais.
2. Hoja ya kuwa kuna Mgombea alijitangazia matokeo ilitupiliwa mbali kwani Tume ilikubaliana kuwa hilo kama lipo basi ni kosa la jinai kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi na Tume haina mamlaka ya kuwapeleka watu Mahkamani.
3. Hoja ya Wajumbe waliokuja na fomu za matokeo kutoka Pemba, Tume iliamua kuwa Wajumbe hao wayataje matatizo waliyoyaona ili iyazingatie katika kila jimbo husika wakati wa kuhakiki matokeo ya jimbo hilo.
Ndugu Waandishi wa Habari,
Vikao vyote viwili tunavyovieleza hapa vilivyoongozwa na Mwenyekiti Jecha Salim Jecha na Makamishna SOTE tulihudhuria. Baada ya uamuzi huo wa busara wa Tume, Mwenyekiti aliendelea kukiongoza kikao kuhakiki matokeo ya Urais na kuyatangaza.
Siku ya 28 Oktoba, 2015 Mwenyekiti hakuhudhuria katika kikao chetu cha kufanya uhakiki wala hakuonekana kabisa katika ofisi zetu hapo Bwawani. Tume ikaamua kuendelea na kazi ya majumuisho chini Makamo Mwenyekiti wake Mh. Jaji Abdul–hakim Ameir Issa. Hapo kuna matukio mawili yalitokea.
1. Eneo la ofisi za Tume Bwawani lilizingirwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania na kuzuwia mtu yeyote kutoka nje au kuingia ndani ya eneo hilo.
2. Makamo Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, ambaye pia ni Jaji wa Mahkama Kuu ya Zanzibar, alichukuliwa na vyombo vya Dola na kupelekwa Makao Makuu ya Jeshi la Polisi – Ziwani. Tukio hili, liliifanya Tume kukosa uhalali wa kuendelea na kazi ya majumuisho kwa vile haikuwa na Mwenyekiti wala Makamo wake.
Wakati Wajumbe wengine sote tukiwa tunatafakari yanayotutokea, ndipo tulipopata taarifa kupitia vyombo vya habari vya Serikali kuwa Mwenyekiti Jecha Salim Jecha anatangaza kuufuta Uchaguzi Mkuu na matokeo yake yote. Maamuzi ambayo sisi sote hatukushiriki, hakutushauri na wala hakutuhadithia, ndio maana tunasisitiza kuwa yalikua ni maamuzi yake binafsi na kwamba yamekwenda kinyume na masharti ya Katiba ya Zanzibar kifungu cha 119 (10).
4.0 NINI KILIMSIBU MWENYEKITI?
Tarehe 1 Novemba 2015, Mwenyekiti aliitisha kikao cha Tume ya Uchaguzi ambacho kilihudhuriwa na Wajumbe wote wa Tume. Ajenda ya kikao hicho ilikua ni moja tu na alikuwa akiijua Mwenyekiti peke yake. Ilikua ni kuunga mkono tamko la Mwenyekiti alilolitoa tarehe 28 Oktoba 2015 la kufuta Uchaguzi Mkuu na Matokeo yake yote. Katika kikao hicho Mwenyyekiti alisema kuwa kuna mazigira ukifikishwa kusema uongo hupati dhambi katika uislamu. Pia kuna mazingira ukifikishwa kula nguruwe hupati dhambi katika uislamu. Pia alisema kuwa amefikia uamuzi huo baada ya kushauriana na “vyombo”.Hivyo Mwenyekiti aliwaomba wajumbe wamuunge mkono katika tamko hilo ili hatua za kuandaa Uchaguzi ziendelee. Kikao kilijadili ombi hilo na hatimaye maamuzi kwa njia ya kura yakafanyika kwa Wajumbe watatu kuunga mkono na Wajumbe watatu kukataa kuunga mkono tamko la kufuta Uchaguzi lililotolewa na Mwenyekiti. Kwa vile Tume iliamua kwa kura, ilipaswa kila Mjumbe kupiga kura yake, jambo la kushangaza ni kuwa Mwenyekiti mwenyewe hakupiga kura!
Tarehe 6 Novemba 2015, Mwenyekiti alitoa tangazo katika gazeti rasmi la Serikali Nambari 130 la “kufuta matokeo” ya Uchaguzi Mkuu. Mambo matatu yanafaa kuzingatiwa katika tangazo hilo:-
1. Tangazo linaeleza kuwa uamuzi huo wa kufuta ni uamuzi wa Tume wa tarehe 28 Oktoba 2015, wakati yeye anajua kuwa tarehe 28 Tume haikukaa kufanya maamuzi hayo na ndio maana akaitisha kikao tarehe 1 Novemba cha kutaka kuungwa mkono. Pia anaelewa kuwa yeye hakuhudhuria kikao cha uhakiki wa matokeo siku ya tarehe 28 Oktoba 2015. Kwa hivyo Mwenyekiti hakusema kweli katika Tangazo lake alilolichapisha kwenye Gazeti Rasmi la Serikali.
2. Tangazo la Mwenyekiti alilolitoa tarehe 28 Oktoba 2015 alitangaza kufuta Uchaguzi na matokeo yake yote, wakati tangazo la Gazeti Rasmi la Serikali ameeleza kuwa amefuta matokeo ya Uchaguzi. Kwa hivyo alichokifuta tarehe 28 Oktoba sicho alichokitangaza katika Gazeti Rasmi la Serikali.
3. Vifungu vyote alivyovinukuu vya Katiba ya Zanzibar na Sheria ya Uchaguzi katika tangazo lake la Gazeti Rasmi la Serikali, havihusiani kabisa na mamlaka ya yeye au Tume kufuta Uchaguzi wala matokeo ya Uchaguzi.
Tarehe 21 Januari, 2016 Tume ilikaa tena kikao na kujadili juu ya tarehe ya Uchaguzi wa “Marudio”. Baadhi ya Wajumbe waliamua kuwa tarehe 20 Machi 2016 iwe ndio siku ya Uchaguzi na baadhi walipinga kwa msingi ule ule kuwa, ikiwa ufutaji wa Uchaguzi ulikuwa ni batili kikatiba na kisheria, basi na kuitisha Uchaguzi mwengine pia itakua ni batili kwa tarehe yoyote itakayoamuliwa na Tume.
Ndugu waandishi wa Habari,
Sisi tulio mbele yenu hatuungi mkono Uchaguzi wa “marudio” kutokana na sababu zifuatazo;
· Katiba ya Zanzibar kifungu cha 119 (10) hakitoi nafasi kwa Mwenyekiti peke yake kufanya maamuzi kwa jina la Tume ya Uchaguzi. Hivyo maamuzi makubwa aliyoyafanya Mwenyekiti hayawezi kuchukuliwa kuwa ni maamuzi ya Tume ya Uchaguzi.
· Kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar, Uchaguzi Mkuu wa 2015 ulishakamilika katika ngazi ya Uwakilishi na Udiwani. Wateule katika nafasi hizo walishakabidhiwa vyeti vyao vilivyotolewa kuthibitisha ushindi wao. Katika hatua hiyo hakuna chombo chochote kinachoweza kubatilisha uchaguzi huo isipokuwa Mahkama Kuu baada ya kusikiliza shauri la kiuchaguzi lililopelekwa mbele yake. Wenye uwezo wa kupeleka shauri hilo Mahakamani wametajwa kwenye sheria ya uchaguzi, miongoni mwao si Mwenyekiti wala Tume ya Uchaguzi. Uchaguzi wa Uraisi haukulalamikiwa na Mgombea ye yote kati ya Wagombea 14 waliogombea nafasi hiyo. Matokeo yote ya kura zilizopigwa yalitolewa kwa Wagombea kupitia Mawakala wao. Tume ilikuwa inakamilisha uhakiki wa matokeo ili imtangaze Mshindi. Majimbo 31 yalihakikiwa na kutangazwa, Majimbo 9 yalihakikiwa na hayakuwahi kutangazwa na Majimbo 14 hayakuwahi kuhakikiwa na wala kutangazwa.
· Kurudia uchaguzi ni kuiweka nchi katika majaribu. Uwezekano mkubwa upo wa kutokea fujo na hata viongozi wa Serikali wameliona hilo na wamekua wakilitolea kauli mbali mbali mara kwa mara.
· Wakati Rais wa Jamuhuri anachukua hatua nzito za kuzuwia matumizi mabaya ya fedha za umma, tunaamini kuwa Nchi yenye uchumi mdogo kama Zanzibar kutumia fedha za Umma zaidi ya bilioni saba kwa kufanya Uchaguzi ambao ulishakamilika na matokeo yake yapo, ni matumizi mabaya zaidi kuwahi kutokea tokea Uchaguzi Mkuu ukamilike. Kutokana na utashi wa kisiasa ndani ya Tume imepelekea hata utaratibu wa manunuzi kufanywa kwa kutumia “hali ya dharura” na hivyo kuondoa uwazi na uwajibikaji katika manunuzi hayo. Hayo ni matumizi ya dharura katika mambo yasiyo kuwa ya dharura. · Hata kama Tume ya Uchaguzi ingekuwa na uwezo wa kisheria wa kufuta Uchaguzi, basi bado utaratibu wa maamuzi ungebaki kuwa kwa mujibu wa Katiba kama unavyoelezwa katika Katiba kifungu 119 (10), kwamba Maamuzi yote ya Tume ni lazima yaungwe mkono na zaidi ya nusu ya wajumbe. Katika hili hata hapo Mwenyeketi alipotaka kuungwa mkono na Wajumbe wa Tume katika kikao cha tarehe 01 Novemba 2015. Maamuzi hayo hayakuungwa mkono na wajumbe wengi.
· Maelezo yaliyotolewa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi juu ya kufuta Uchagzi wa tarehe 25 Octoba 2015, hayajaweza kumshawishi hata mtu wa kawaida kuamini kuwa kulikuwa na sababu za msingi za kuufuta uchaguzi ule, bado yamebaki masuala mengi kutoka kwa wananchi wakawaida, waangalizi, vyama vya siasa na wanaharakati wengine juu ya sababu hizo. Katika hali hii masuala mengi yanaibuka juu ya umakini wa Mwenyekiti si tu kwa Uchaguzi uliopita bali hata kwa Uchaguzi huo wa marudio. Mfano; Jee vyombo vile vilivyomshauri Mwenyekiti kufuta uchgauzi wa tarehe 25 octoba, haviwezi tena kumshauri Mwenyekiti kufanya jambo jengine lolote lisilo la kawaida kuelekea tarehe 20 Marchi?
· Kwa mujibu wa tangazo la Mwenyekiti ni kuwa uchaguzi huu utarudiwa ile hatua ya upigaji kura tu, hatua nyengine zote zitakuwa zile zile. Ikiwa kweli anaamini kuwa Uchaguzi ule umefutwa, kwanini huu usiwe Uchaguzi mpya? Kwa nini mchakato wake usianze mwanzo? Jee anakusudia kutumia hatua zilizobatilishwa katika kuhalalisha uchaguzi wa marudio? Huu ni ubakaji wa demokrasia na ni kituko kipya kisichopata kutokea katika tasnia ya Uchaguzi popote duniani, isipokua hapa Zanzibar tena mwaka huu.
· Kama Uchaguzi huo utafanyika, basi utatoa viongozi batili, watakao iongoza Nchi kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Ndugu Waandishi wa Habari,
Ni vyema mkaelewa kuwa hali iliopo kwenye Tume ya Uchaguzi katika kufanikisha Uchaguzi wa marudio sio shuwari. Kwani baada ya tangazo la Mwenyekiti la tarehe 28 Oktoba, Wajumbe wa Tume wamekuwa hawaafikiani katika mambo mengi. Msingi wa hilo ni kuwa Tume ya Uchaguzi imepoteza uhuru wake kwa kikundi cha watu nje ya Tume. Mwenyekiti wa Tume anaonekana kama vile ni mtu anaechukua maelekezo kutoka pahali na kisha kuyalazimisha katika Tume kwa mtindo wa kupiga kura. Kwakuwa ana wafuasi wengi basi huwa anashinda kila anapopigisha kura za kupitisha maamuzi ya Tume.
Tume inaonekana kukosa mashirikiano na wadau muhimu wa Uchaguzi, mfano; baadhi ya vyama vya siasa vimetangaza kususia uchaguzi, Mashirika ya Kimataifa ambayo yamekua yakiisaidia Tume kwa utaalamu na rasilimali yamekataa rasmi kuisaidia Tume katika kufanikisha Uchaguzi wa marudio.
Tume kwa utaratibu iliojiwekea katika Uchaguzi wa marudio, inalazimisha Wagombea ambao walithibitisha kugombea katika uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2015 kuwa Wagombea wa uchaguzi wa Machi 2016 bila ya ridhaa zao ambazo wanatakiwa wazithibitishe mbele ya Hakimu wa Mkoa au Jaji wa Mahkama Kuu.
Tume kuwekwa chini ya ulinzi wa Jeshi la Wananchi. Hii haitoi taswira nzuri kwa nchi yetu, kuwa eti inafanya Uchaguzi wa kidemokrasia, lakini ofisi za Tume zimezingirwa na Jeshi. Pia hali hii inawatia khofu wadau wa Uchaguzi kufika kwa uhuru katika ofisi za Tume Huru!!!
Pamoja na kuwa Tume ya Uchaguzi imeingiliwa mno na wanasiasa na hivyo kupelekea maamuzi yake mengi kuwa ni ya kisiasa, likwemo hili la marudio ya Uchaguzi, lakini bado ilipaswa kuelewa kuwa uendeshaji wa Uchaguzi ni lazima ufuate utaratibu wa kisheria. Hali ilivyo sasa ni kuwa Tume inaendelea kuvunja Sheria kila hatua katika mchakato wa kuendesha Uchaguzi, jambo ambalo wengine hatutaweza kulinyamazia.
5.0 HITIMISHO
1. Tumefikia pahali sasa kuwa matukio yote haya yamesababishwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar. Hivyo ni nafasi ya Mwenyekiti ajipime, ajitolee maamuzi magumu ili kuiepusha Nchi hii na janga linaloinyemelea.
2. Matakwa ya Katiba ya kutaka Mwenyekiti wa Tume awe ni mtu mwenye sifa za kuwa Jaji wa Mahkama Kuu au Mahkama ya Rufaa ya Nchi yoyote ya Jumuiya ya Madola yaangaliwe badala ya kufuata sifa za mtu ambae “Rais anaona anafaa”.
3. Tunatoa wito kwa wajumbe wenzetu wa Tume ya Uchaguzi kuachana na Uchaguzi wa marudio wa tarehe 20 Machi 2016 kwani jambo hili halina maslahi kwa nchi yetu. Sisi tusiwe sababu ya kuwa sehemu ya historia mbaya ya nchi yetu.
4. Kwa kuwa mchakato wa Uchaguzi wadau wake wakubwa ni vyama vya siasa na kwa hali ya Zanzibar hivi sasa ilivyo tunadhani kwamba iko haja ya kupatikana kwa mpatanishi wa kimataifa ambaye ataweza kuziweka pande mbili zinazotofautiana kisiasa katika meza ili kufikia suluhu itakayoridhiwa na wote.
Ahsanteni wa kutusikiliza.
Ayoub Bakari Hamad
Nassor Khamis Mohammed
No comments:
Post a Comment