Friday 4 March 2016

Habari iliotikisa magazeti na Blog wiki hii ni Umeya wa DAR

Wasomi wanena, kivuli cha Lowassa chaitesa CCM.
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.
Tangu kurudishwa kwa awamu ya pili ya mfumo wa vyama vingi nchini mwaka 1992 na uchaguzi wa kwanza wa mfumo huo kufanyika 1995, baadhi ya maeneo yalijulikana ni ngome za CCM na wapinzani hawakuwa na chao. 
Joto la uchaguzi wa mwaka 2015 kuanzia ndani ya vyama, lilifanya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kujitoa CCM na kujiunga na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa). 
Hatua hiyo ilizidisha joto hilo na matokeo yake vyama vya upinzani vikapata takribani wabunge 110 na takriban halmashauri 25, idadi ambayo haijawahi kufikiwa na vyama vya upinzani.  Baadhi ya Halamashauri ambazo hazijawahi kuwa chini ya upinzani na kutokana na nguvu ya Ukawa kwenye uchaguzi uliopita ilizichukua ni zile za Tanga mjini na Dar es Salaam kwa manispaa za Kinondoni na Ilala.Mbali na kuwa na madiwani wengi na kufanikiwa kuongoza Halmashauri za Ilala na Kinondoni, huku vikikosa Temeke, bado vyama vya CUF na Chadema ambavyo vyote viko chini ya Ukawa, vinaizidi CCM takribani madiwani 10 kwa jiji la Dar es Salaam, hivyo kuwapa uwezekano mkubwa wa kuongoza halmashauri ya jiji pia.
Wakati wa kampeni,  maeneo ambayo Lowassa aliweka nguvu kubwa kwa kufanya mikutano mingi ni pamoja na Dar es Salaam na Tanga mjini, matokeo yake Ukawa iliibuka na ushindi mkubwa.Baada ya mameya wa Ilala na Kinondoni kutangazwa na kwenda nyumbani kwa Lowassa kumshukuru, moja ya mitihani aliyowapa ni kuhakikisha jijini linakuwa la mfano kwenye maendeleo na kutumikia wananchi.
Miezi minne sasa baada ya uchaguzi mkuu, uchaguzi wa meya wa jiji la Dar es Salaam umekuwa na vitimbi vilivyofanya mpaka sasa uahirishwe mara tatu kutokana na sababu zisizoelezeka.
Kwa jiji la Tanga, upinzani wana madiwani 17 na CCM 12, hatua ambayo imesababisha halmashauri kushindwa kufanya kazi, baada ya CCM kushinda kiti cha umeya na upinzani kukataa kwa madai kwamba haki haikutendeka. Hali iko hivyo hivyo kwenye wilaya ya Kilombero ambako pia uchaguzi uliahirishwa mara kadhaa kabla ya kufanyika tena wiki hii na CCM kuibuka mshindi, licha ya upinzania kuwa na madiwani wengi. Hatua hiyo ilisababisha kuwapo malalamiko kwamba kuna mbinu chafu zilifanyika. 
Halmashauri zingine ambazo vyama vya Ukawa vilikuwa na madiwani wengi ni Kilimanjaro kwa wilaya za Hai, Rombo, Moshi,  Siha na manispaa ya Moshi.Mbeya ni jiji la Mbeya Mji Tunduma; Arusha- jiji la Arusha, Monduli na Arumeru; Manyara-Karatu na Mji Babati, Kagera-Manispaa ya Bukoba  na mji mdogo wa Kayanga.
Kwa upande wa Mtwara, vyama hivyo vilikuwa na madiwani wengi Tandahimba, Mtwara/Mikindani, Mji Newala, Lindi (Kilwa), Tanga (Jiji Tanga), Mara (Serengeti, Tarime  na Mji Tarime), Morogoro-Kilombero na Ifakara huku katika Mkoa wa Iringa kukiwa na madiwani wengi kwenye Manispaa ya Iringa. 
Mkoani Kigoma, Ujiji/ Kigoma inaongozwa na ACT –Wazalendo ambao si sehemu ya Ukawa. Kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana, halmashauri hiyo ilikuwa na madiwani wengi kutoka Chadema. Migogoro hiyo ambayo matokeo yake ni kukwama kwa shughuli za halmashauri husika, baadhi ya wadau wanasema wananchi ndio wanaoumia zaidi.
SAMIA ATABIRI MDORORO
Akizungumza na viongozi serikali na kisiasa jijini Tanga hivi karibuni, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, alisema serikali italazimika kuivunja halmashauri ya jiji hilo endapo mgogoro uliopo hautamalizwa haraka.
Kauli hiyo ilitokana na kushindwa kufanyika kwa vikao vya maendeleo  vya halimashauri hiyo kutokana na mgogoro wa kisisa baina ya CCM na vyama vinavyounda Ukawa, ambavyo ndivyo vyenye madiwani wengi, vikituhumu chama tawala kutumia mabavu kushinda uchaguzi.
 “Mpaka sasa jiji la Tanga hakuna uongozi uliosimama. Sasa hatuwezi kwenda kwa mwendo huu, wananchi wanahitaji maendeleo na kurudia uchaguzi hatuwezi ni gharama kubwa. Kilichobaki ni kuivunja halmashauri mpaka hapo muda wa kufanya uchaguzi kwa mujibu wa Katiba ya nchi utakapotimia, hivyo kwa maana nyingine kama itavunjwa serikali kuu ndiyo itasimamia shughuli za jiji hili.
“Jiji ni kioo cha mkoa mzima, sasa kama wazee hawatakaa kitako na viongozi kutafuta suluhu, basi hii mipango yenu yote ya kufufua viwanda itakuwa ndoto tu kwa sababu hapa mjini hakupo shwari na tunalitambua hilo,” alisema.
MEYA TANGA AANZA KUJUTA
Meya wa Jiji la Tanga,  Mustapha Mhina, aliliambia gazeti hili kuwa kuvunjwa kwa  halimashauri hiyo kutawaathiri zaidi wananchi ambao wanalitegemea zaidi Baraza la Madiwani katika usimamizi na utatuzi wa kero zinazowakabili.
Alipohojiwa na Nipashe, Mhina alisema kuvunjwa kwa Halmashauri kwa maana nyingine ni kutengua nafasi aliyo nayo diwani katika  usimamizi wa miradi, matumizi ya fedha na msukumo wa utetezi wa kero za wanachi kutoka kwa watendaji .
Alisema iwapo serikali itachukua uamuzi huo, haina budi kutambua kwamba watendaji watakuwa wasimamizi na wafanyaji wa uamuzi wowote, jambo ambalo wakiwapo wasio waaminifu huweza kutumia mwanya huo kujinufaisha badala ya kuwaondolea wananchi kero zinazowakabili.
Hata hivyo, aliwataka madiwani wa CUF kukubali kukaa kwenye meza ya mazungumzo ili kukamilisha ajenda zilizobaki wakati wa kikao kilichovunjika Desemba, mwaka jana, baada ya Msimamizi wa Uchaguzi kumtangaza mshindi wa nafasi ya Meya.
Kwa mujibu wa Mhina, ajenda zilizobaki ni pamoja na ile ya kuchagua kamati za kudumu za halmshauri, kupitisha ratiba za vikao, kupokea taarifa ya utendaji wa halmashauri katika kipindi madiwani walipokuwa kwenye uchaguzi na kusomewa taarifa ya serikali.
Alisema Baraza hilo halikufanya kikao rasmi kwa mujibu wa sheria na kanuni kwa kuwa mpaka sasa hakuna barua waliyoipokea kutoka kwa Mkurugenzi wa Jiji ya kuitwa kwenye kikao.
“Ukifuata kanuni na sheria ni kwamba kama Baraza litashindwa kukutana katika vikao vitatu litavunjwa. Lakini sisi hatujakaa hata kimoja, sasa niwaombe wenzetu waliangalie jambo hili kwa kina sana kuwa sisi ni wamoja na ni wana Tanga na kwamba kuna maisha baada ya siasa. 
Hao watakaovunja halmshauri hawawezi kuwa na uchungu kama tulio nao sisi,” alisema Mhina ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Nguvumali.
KIGOMA WACHANJA MBUGA
Wakati migogoro ikiendelea kwenye Halmashauri hizo, Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, alisema kutokana na amani kwenye Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma/Ujiji inayoongozwa na ACT-Wazalendo, tayari wameanza kufanya kazi za wananchi.
Zitto alisema pamoja na mambo mengine wamefanya mazungumzo na wadau balimbali na wana mpango wa kuanzisha bima ya afya kwa wananchi wote na mpango maalumu wa kuhakikisha wanaboresha elimu ili shule za jimbo hilo zisifanye vibaya kama ilivyokuwa kwenye mtihani uliopita wa kidato cha nne.
Alisema lengo ni kuhakikisha Kigoma/Ujiji inakuwa halmashauri ya mfano kwa kuleta maendeleo kwa wananchi wake.
Hali ya migogoro kwenye halmashauri hizi ni kama ile iliyokuwa Bukoba Mjini, awamu iliyopita kutokana na mgawanyiko ndani ya baraza la madiwani. Mgogoro huo ulisababishwa na aliyekuwa Meya, Anatory Amani na Mbunge, Balozi Khamis Kagasheki na ule wa Arusha ambao ulitengamaa baada ya miaka kadhaa.
Halmashari ya Manispaa ya Bukoba kwa takribani miaka mitano ilishindwa kufanya mradi wowote wa maendeleo, kutokana na kutofanyika kwa vikao ambavyo pamoja na mambo mengine vinatakiwa vipitishe bajeti za maendeleo.
Hali hiyo pia inanukia kwa jiji la Dar es Salaam ambalo mpaka sasa halijafanya chochote kutokana na kutokuwa na uongozi, Tanga na Kilombero hali ikiwa vivyo hivyo.
KILICHOWAPATA ARUSHA
Pia Arusha ilikuwa na mgogoro kwenye awamu iliyopita kutokana na Mbunge  wa sasa wa Arusha mjini, Godbless Lema, ambaye pia alikuwepo kipindi kilichopita, anasema mambo mengi yalikwama kutokana na mtafaruku huo.
"Kama mnakumbuka uchaguzi wa mwaka 2010 wakati wakimchagua Meya wa Jiji la Arusha,  kulitokea vurugu zilizosababisha mauaji ya watu wasio na hatia ubabe ukafanyika Meya akapatikana,  kila mtu alijua kilichofanyika na athari zake ni kubwa,” alisema.
“Kwa mtizamo huo vikao havikuwa na amani, madiwani walikuwa na migogoro, mambo ya msingi ya maendeleo ambayo yaliletwa na Chadema au CCM ili yajadiliwe yalikwama,” alisema.
Alisema athari zingine zinazotokana na migogoro hiyo ni kujengeka uadui baina ya wananchi na serikali yao kwa kuamini kuwa uamuzi wao wa kumchagua kiongozi fulani haujaheshimika.
Pia alisema athari nyingine ni vikao vya kujadili mambo ya maendeleo havifanyiki badala yake  kunakuwa na vile vya malumbano.
Pia alisema migogoro hiyo inaleta madhara kwa wafadhili kwa sababu kutoka uchaguzi mkuu uishe kinachoendelea baadhi ya majiji ni malumbano ya nani awe meya badala ya kuzungumzia maendeleo.
BUKOBA WALIVYOSOTA
Kutokana mgogoro wa madiwani wa Manispaa ya Bukoba katika  awamu iliyopita, miradi ya maendeleo haikutekelezwa kwa sababu vikao vilikuwa havifanyiki.
Manispaa hiyo ilitegemea kupata michango ya wahisani lakini haikutolewa kwa sababu waliposikia kuna migogoro walikimbia hivyo kutotimia kwa malengo waliyokuwa wamepanga kuyatekeleza.
WASOMI WALONGA 
Baadhi ya wasomi waliozungumza na gazeti hili, walisema athari za migogoro inayoendelea sasa itaonekana zaidi kwa wananchi.
Mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia, Dk. Kitojo Wetengere, alisema ni aibu kuwapo migogoro kwenye baadhi ya halmashauri ilhali kuna sheria zinazoongoza uchaguzi na mambo yote ya halmashauri.
Alisema uchaguzi wa Meya wa Halmashauri uko kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa lakini watu wachache wenye malengo yao binafsi wamekiuka taratibu hizo.
“Haiwezekani serikali iweke sheria, kanuni na taratibu lakini watu wachache ambao wameona kwa sababu wanazoamini wao, wavuruge uchaguzi na kuendelea kuwachwa,” alisema. 
Kuhusu athari ambazo zinatokana na kuahirishwa kwa uchaguzi huo, alisema ni watu kuathirika  kisaikolojia na kufikiria uchaguzi wa Meya na matukio yaliyotokea wakati wa uchaguzi mkuu wakati watu walishamaliza badala ya kufikiria shughuli za kufanya.
Alisema matokeo ya hayo ni kukaribisha makundi ya siasa kuanza kushamiri badala ya vijana kufikiria kufanya kazi na kusukuma  gurudumu la maendeleo.
Naye Mhadhiri wa Idara ya Sayansi za Siasa na Utawala kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Rasul Ahmed, alisema tatizo kubwa linalojitokeza ni vyama shiriki kutokukubali kushindwa.
“Sioni kama ni jambo la ajabu wajumbe wa chama fulani kumpigia kura wa chama kingine na akashinda uchaguzi huo, jambo ambalo wengi wanadhani haliwezekani na ndio sababu vyama havijajiandaa kushinda,” alisema.
Alisema bado hakuna ukomavu wa kisiasa kutokana na vurugu zilizotokea na kuahirishwa kwa uchaguzi katika Halmashauri za Kilombero, Tanga na Dar es Salaam.
Alisema vurugu ambazo zimetokea, zimeirudisha nyuma hatua tano demokrasia ya Tanzania na kusababisha wananchi kugawanyika kutokana na vyama vyao kuwaangusha.
Naye aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba, alisema tatizo kubwa linalojitokeza  Kilombero, Tanga, Dar es Salaam na Zanzibar ni kutokana na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutojiandaa kushindwa.
Alisema CCM haijakubali kuwa iko kwenye mfumo wa vyama vingi na kutokana na hali hiyo, chama chochote kinaweza kushika dola.
Alisema athari kubwa ambayo itatokea ni watu kuchoka na kuamua kufanya jambo lolote ambalo linaweza kuwa na athari kwa nchi.
Lipumba alimshauri Rais Dk. John Magufuli kuingilia kati ajenda ya kidemokrasia ambayo inamalizwa na watu wachache.
Alisema ni vyema pia akaagiza uchaguzi wa meya ufanyike na mshindi apatikane ambaye ataongoza katika halmashauri hiyo.
Habari hii imeandaliwa na Romana Mallya, Mary Geofrey, Dar,  Na Lulu George, Tanga na Lilian Lugakingira Bukoba.
CHANZO: NIPASHE

No comments: